Na Selemani Msuya
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na
Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ametoa rai kwa wananchi, kampuni za sekta
binafsi na umma, taasisi za serikali kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza
katika hatifungani ya kijani au “Green Bond” ya Benki ya CRDB.
Profesa Kitila ametoa raia hiyo leo wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Hatifungani ya Kijani uliofanyika katika Hoteli ya Serena
jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu wa kada mbalimbali wa ndani na nje
ya nchi.
Amesema uamuzi wa Benki ya CRDB kuja na hatifungani
hiyo ya kijani na kutoa fursa kwa wananchi na taasisi mbalimbali kununua hisa
na fedha zitakazopatikana kuelekezwa kwenye miradi ya mazingira ni wa kuigwa na
taasisi nyingine kwani unaenda kusaidia serikali kutekeleza miradi mingi.
Kitila amesema serikali ina mipango mingi ya
kuhakikisha miradi ya kuzuia uharibifu wa mazingira unaosababishwa mabadiliko
ya tabianchi kutokea, hivyo ujio wa Kijani Bond ni wazi kuwa lengo hilo
litaweza kutumia.
"Kijani Bond inaenda kugusa miradi ya
mazingira, afya, elimu, maji na mingine mingi, hivyo nichukue nafasi hizi
kuziomba taasisi zingine za kifedha na zisizo za kifedha kuunga mkono juhudi
hizo za CRDB," amesema.
Waziri huyo amesema ujio wa hatifungani hiyo ya
kijani sio tu kwamba unanufaisha miradi tajwa, ila hata wawekezaji wenyewe
ambapo benki imeweka bayana kuwa itatoa riba ya zaidi ya asilimia 10.2 kwa kila
mwekezaji ambaye atawekeza kuanzia shilingi 500,000 ndani ya siku 37 kuanzia
leo.
Amesema Serikali itatoa ushirikiano na taasisi
yoyote ambayo itajikita kwenye uwekezaji ambao unagusa jamii, kwa kuwa lengo
lake ni kuongeza ajira na kipato kwa wananchi na nchi kwa ujumla.
"CRDB inafanya kile ambacho sisi
tunakipigania kuongeza ajira, kipato na kuitangaza nchi, leo hii wapo hadi
Burundi, DR Congo na hili la hatifungani ya kijani linaenda kugusa dunia kwa
ujumla," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mkuu wa CRDB,
Abdulmajid Nsekela amesema fedha ambazo zitapatikana kupitia hatifungani ya
kijani zitatumika kufanikisha miradi yenye mrengo wa kuhifadhi mazingira hali
ambayo itaifanya Tanzania iendane na mikakati ya dunia ya kupambana na
mabadiliko ya tabianchi.
"Agosti 18, 2023 ilikuwa siku moja ya siku
za furaha sana kwa Benki ya CRDB baada ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana (CMSA) kutupa idhini ya kuuza hatifungani ya kwanza ya kijani Tanzania
na kubwa zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Lakini naweza kusema leo tupo katika kilele cha
furaha kwa kuwa sasa tunakwenda kuaza kuunza hatifungani za kijani nawaomba
Watanzania na wasio watanzania kuchangamkia fursa hii," amesema.
Nsekela amesema kamilika kwa mchakato huu
ulioanza mapema mwaka jana ni mafanikio makubwa kwao kwani wataalamu wao wa
ndani na nje ya Benki yetu walilazimika kufanya kazi usiku na mchana
kukamilisha taratibu za kikanuni na kisheria.
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema jitihada hizi
zisingefaa kitu kama si ushirikiano ambao tulipata kutoka CMSA ambao
hawakuchoka kuwapa miongozo mpaka leo hii wanaanza kuiuza hatifungani yao.
"Kufanikiwa kuanza kuuza hatifungani hii
kubwa zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni heshima kwa nchi yetu
kwa kuwa Benki ya CRDB ni benki ya kizalendo inayomilikwa na Mtanzania mmoja
mmoja, Serikali pamoja na taasisi zake. Na hili linaendelea kudhihirisha kuwa
taasisi zetu zina uwezo wa kufanya mambo makubwa katika ulingo wa
kimataifa,"amesisitiza.
Nsekela amesema msukumo wa benki hiyo kuuza
hatifungani ya kijani umejikita katika ushiriki wao wa kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi ambayo yameleta athari duniani kote.
"Kwa kutambua umuhimu na mahitaji yaliyopo, Benki ya CRDB iliona ni muhimu kutafuta vyanzo vipya vya fedha ili kuwezesha miradi hii ndipo lilipopatikana wazo la hatifungani ya kijani.
Hatifungani hii ambayo CMSA imetupa idhini ya
kuiuza ina thamani ya dola milioni 300 za Marekani sawa na takribani shilingi
bilioni 780 za Tanzania ambayo kama nilivyosema awali hii ni kubwa zaidi kuwahi
kutolewa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara," amesema.
Amesema hatifungani hii itakayoorodheshwa katika
Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na Soko la Hisa London yaani London Stock
Exchange (LSE), wanatarajia kuiuza kwa awamu na katika awamu hii ya kwanza
mauzo yanaanza leo, Agosti 31, 2023 na yatadumu kwa siku 37 mpaka Septemba 6 na
matarajio ni kukusanya Shilingi Bilioni 55.
Nsekela amesema kufanikiwa kuuzwa kwa hatifungani
hiyo kutakwenda kuiongezea uwezo mkubwa Benki
kuwezesha wawekezaji ambao miradi yao katika namna moja au nyingine
inasaidia katika utunzaji wa mazingira.
Amesema hili ni eneo ambalo wameshuhudia mataifa
mengi duniani yanawekeza huko ambapo hapa Afrika tayari nchi kama Afrika
Kusini, Ghana, Nigeria na Kenya tayari wamepiga hatua kubwa.
Akizungumzia umuhimu wa Watanzania kuwekeza
katika hatifungani ya kijani Nsekela amesema ambapo kiwango cha chini ni
shilingi 500,000.
"Sambamba na hilo, hatifungani hii ya kijani
ni uwekezaji ambao una uhakika wa kukulipa au kwa lugha ya kigeni wanasema
“risk free investment”. Kupitia uwekezaji wa hatifungani ya kijani ya Benki ya
CRDB, muwekezaji atakua na uhakika wa kupata riba ya asilimia 10.25 ambayo ni
biashara chache sana ambazo unaweza kuzifanya na ukawa na uhakika wa kupata
kiasi hiki tena bila kujali mazingira ya biashara yatakuaje," amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Alhaj Ali Lawi
amesema benki hiyo itaendelea kuboresha huduma zake, ili kuhakikisha kila
anayepata huduma ananufaika.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama
amesema kinachofanywa na CRDB ni cha kuigwa na kila taasisi ya kifedha kwani
kina faida kwa jamii kwa ujumla.
Mkama amesema ili Tanzania iweze kuendelea ni
jukumu la kila taasisi kuja na bunifu mbalimbali za kuwezesha jamii nzima
inashiriki kwenye uchumi.
"CMSA tupo tayari kushirikiana na taasisi yoyote ambayo itakuja na wazo ambalo linataka kuwakwamua wananchi na nchi kwa ujumla, CRDB imeonesha njia tuiunge mkono benki yetu kwa kununua hisa za hatifungani ya kijani,"amesema.