Friday, March 22, 2024

WADAU WA MSD WAHIMIZWA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA TAKWIMU BIDHAA ZA AFYA

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauteri Kanoni,  akifungua kikao cha wadau na wateja wa Bohari ya Dawa (MSD),  Kanda ya Mtwara Machi 22, 2024.

...........................

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

WADAU wa Afya wa Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya  Mtwara wamehimizwa kusimamia matumizi sahihi ya takwimu za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, ili ziwawezeshe kufanya maamuzi sahihi juu ya bidhaa hizo katika maeneo yao.

Akifungua kikao cha wadau na wateja wa MSD kanda ya Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauteri Kanoni amesema uwepo wa takwimu sahihi unaiwezesha MSD kuagiza kwa usahihi bidhaa za afya na kuboresha upatikanaji wa bidhaa hizo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, amewashauri MSD kuhakikisha utaratibu wa vikao  vya mwaka vya wadau ni muhimu kwa pande zote mbili, yaani Bohari ya Dawa (MSD) yenyewe na wadau ili kwa pamoja kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya, kwa kujadili changamoto na kuzitafutia utatuzi.

Kwa upande wake Meneja wa MSD Kanda ya Mtwara Tea Malay ameeleza kuwa kwa sasa kanda ya MSD Mtwara inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 631, na inasambaza bidhaa za afya kila baada miezi miwili.

Naye Meneja Huduma kwa Wateja na Miradi Dkt. Pamella Sawa ameeleza kuwa vikao vya MSD na wadau wake kuanzia sasa vitakuwa endelevu kila mwaka.

MSD Kanda ya Mtwara inahudumia mikoa ya Lindi,Mtwara na Wilaya ya Tunduru.Meneja wa MSD Kanda ya Mtwara Tea Malay, akizungumza kwenye kikao hicho

Wadau wa MSD wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Wadau wa MSD Kanda ya Mtwara wakifuatilia mada kwenye kikao hicho.
Taswira ya kikao hicho.
 

Saturday, March 16, 2024

MAAFISA WATENDAJI WATAKIWA AJENDA YAO KUWA ANWANI ZA MAKAZI, KUHAKIKI TAARIFA ZA WANANCHI

Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Innocent Jacob akizungumza wakati wa siku ya pili ya mafunzo ya siku 14 kwa watendaji wa kata, mitaa, wenyeviti wa Serikali za mitaa na vijiji yanayohusu namna ya kukusanya taarifa za Anwani za Makazi  Manispaa ya Singida.

.........................

Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)

MAAFISA Watendaji wa Mitaa kote nchini wametakiwa katika vikao vyao vyote vya msingi ajenda yao kubwa iwe ni anwani za makazi pamoja na uhakiki wa taarifa za wananchi.

Ombi hilo limetolewa Machi 15, 2024 na Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Innocent Jacob wakati wa siku ya pili ya mafunzo ya siku 14 kwa watendaji wa kata, mitaa, wenyeviti wa Serikali za mitaa na vijiji yanayohusu namna ya kukusanya taarifa za Anwani za Makazi Manispaa ya Singida yaliyoanza Machi 14, 2024 ambayo yameandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuwa siku mbili kati ya hizo 14 zitatumika kwa ajili ya kuhakiki taarifa.  .

Jacob alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawzesha wenyeviti hao ili waweze kutoa taarifa kwa wanananchi za zoezi hilo ndani ya siku hizo na wananchi nao waweze kutoa za kwao kama NIDA, namba ya simu, Tin namba ya biashara na taarifa nyingine za majengo, makazi kama walivyoelekezwa watendaji wa mitaa jinsi ya kulifanya zoezi hilo.

"Watendaji wa mitaa ndio watakao kwenda kukusanya taarifa hizi kwa wakazi wao kwa sababu katika maeneo yote ya utawala wao ndio wahusika wakubwa na watashirikiana na wenyeviti wa mitaa kufanya kazi hiyo," alisema Jacob.

Alisema Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), kwa kushirikiana na TAMISEMI, wameandaa zoezi hilo kwa lengo la kuhakiki taarifa za makazi kwa awamu ya pili baada ya awali kufanyika kwa njia ya operesheni ambapo huenda kuna baadhi ya wakazi hawakuweza kupata fursa ya kuingia katika kanzidata ya Anwani za Makazi.

Alitaja baadhi ya vitu ambavyo viliweza kusahulika kuwekwa kwenye kanzidata kuwa ni taarifa ya majengo, viwanja, majina katika vibao vya mitaa hivyo kurudiwa tena katika zoezi hilo la awamu ya pili la uhakiki.

Jacob alisema umuhimu wa Anwani za Makazi zitarahisisha utambuzi kwa wakazi wa eneo husika na kuweza kupata huduma mbalimbali kwa kufikiwa kiurahisi mahala walipo kwa kutumia programu tumizi kwa ajili ya umma inayoitwa NAPA ambayo inapakuliwa kupitia simu janja ambapo wananchi wote hapa nchini wakiwemo wa Manispaa ya Singida wataweza kuingia katika mfumo huo kwa kuandika NAPA Tanzania.

Alisema mafunzo hayo yanafanyika Manispaa ya Kigoma, Iringa na Singida na yatakuwa endelevu kwa kufanyika katika mikoa mingine.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Dkt. Adrianus Kalekezi alisema katika mafunzo hayo wataalamu wanaelekeza namna ya kuingiza taarifa katika mfumo wa Anwani za Makazi na kuwa hivi sasa wanauhisha taarifa za awali baada ya kazi hiyo kufanyika awamu ya kwanza.

Dkt. Kalekezi alisema suala hilo la Anwani za Makazi ni la muhimu katika manispaa hiyo kwani wananchi watapata huduma kwa urahisi na alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuilinda miundombinu ya Anwani za Makazi iliyowekwa kama vibao vinavyoonesha majina ya mitaa na barabara na kueleza kuwa ni lazima ilindwe ili waweze kunufaika na zoezi hilo kwani bila miundombinu hiyo inakuwa vigumu kwao kuelekezwa na kuitambua mitaa na barabara.  

Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwankoko, Habiba Juma akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo alisema zoezi hilo litawarahisishia kutoa huduma kwa wananchi na kupunguza gharama ya fedha na muda kutoka sehemu moja kwenda nyingine na wananchi wataweza kupata huduma kupitia anuani za makazi.Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka WHMTH, George Leonard, akitoa mafunzo kwa watendaji hao.Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka WHMTH, Janeth Peter , akiwajibika wakati wa  mafunzo hayo.Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Dkt. Adrianus Kalekezi, akizungumzia zoezi hilo.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwankoko, Habiba Juma akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo.
Wataalamu wa mfumo wa Anwani za Makazi wakiwa kwenye mafunzo hayo. Kushoto ni Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH), Innocent Jacob na aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Ufatiliaji Operesheni Anwani za Makazi Mkoa wa Singida ambaye pia ni Afisa TEHAMA, Athumani Simba. .
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Manispaa ya Singida, Abdillai Hussein akimshuru Rais Samia kwa kuwezesha mafunzo hayo kupitia wizara hiyo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.

Attachments area Preview YouTube video MAAFISA WATENDAJI WATAKIWA AJENDA YAO KUWA ANWANI ZA MAKAZI

Wednesday, March 13, 2024

SINGIDA HAWATAKI DAWA NA VIFAA TIBA VILIVYO CHINI YA KIWANGO

Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida, Stanslaus Choaji ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua mafunzo hayo.

...........................

Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)

MKOA wa Singida hautakuwa tayari kuwa dampo la matumizi ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambavyo havina havina ubora.

Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Singida, Stanslaus Choaji aliyasema hayo Machi 12, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wataalamu, wakaguzi na wafamasia wa Halmashauri za wilaya ambao wanakagua dawa, vifaa tiba na vitendanishi yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA)

 Choaji alisema jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya na kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wa Taifa.

"Hilo ni jukumu kubwa la Serikali na mtaona jinsi inavyofanya kila jitihada kadili itakavyowezekana kwa kutumia rasilimali mbalimbali ili kuwawezesha na kuona wananchi wanapata huduma bora za afya," alisema Choaji.

Alisema kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na Serikali wakaguzi hao na watendaji kwenye eneo lao wanaweza kuonesha jinsi ambavyo wanashiriki kwenye hizo jitihada za Serikali kwa kutekeleza majukumu hayo kama vile inavyotakiwa.

Choaji alisema majukumu ya wataalamu hao ni ya msingi kwa sababu yanahusisha maisha ya binadamu hivyo kutekeleza jukumu hilo la kusaidia binadamu ni  kutekeleza jukumu la Mungu aliye tuumba.

Alisema kutenda tofauti na majukumu hayo na kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyotumika na binadamu ni kwenda kinyume kabisa na kusudio la Mungu la kumuumba binadamu na mifugo ambayo nayo ni viumbe hai.

Aliwaomba kufanya kaguzi zao kwa kuzingatia kanuni na maadili kwa lengo la kulinda afya za jamii  na kuwahakikishi uwepo wa bidhaa salama

"Tusingependa sisi Mkoa wa Singida tuwe na changamoto ya matumizi ya vifaa hivyo ambavyo havina sifa," alisema Choaji.

Kwa upande wake Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa alisema kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanalinda afya ya jamii kwa kuhakikisha bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi ni bora salama na zenye ufanisi.

Alisema ili jukumu hilo liweze kutekelezeka kwa kuzingatia ukubwa na upana wa nchi yetu yenye halmashauri za wilaya na   mikoa mingi takribani 26 kwa upande wa Tanzania Bara TDMA kwa kuzingatia uchache wa watumishi wake waliona haitakuwa rahisi kufika kila kona ya nchi ndipo kanuni ya kukasimu baadhi ya majukumu na madaraka ya TMDA iliandaliwa na kupitishwa ili majukumu hayo yaweze kukasimiwa kwa halmashauri za wilaya.

Alisema majukumu hayo yamepelekwa katika halmashauri  hizo ili ziweze kusaidia kufanya baadhi ya majukumu ya TMDA kwa kufanya ukaguzi na kuhakikisha wanafuatilia bidhaa ziwe bora na salama katika soko pia kufanya usajili wa maeneo ya kutolea huduma ambayo yapo chini ya TMDA.

"Leo tumewaalika wakaguzi kutoka halmashauri saba za Mkoa wa Singida tumejumuika kwa pamoja ili tuweze kupeana ABC jinsi ya kufanya kazi hizo ambazo zimekasimiwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa tupo hapa na wataalamu wakaguzi wa  mifugo, wafamasia, wataalamu wa maabara na dawa na wote hawa wanahusika kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha hizo bidhaa zinawafikia walengwa ambao ni wananchi.

Washiriki wa mafunzo hayo Upendo Kiula ambaye ni Mratibu wa Huduma za Maabara kutoka Wilaya ya Itigi na Alfred Rwamtoga Mfamasia kutoka Wilaya ya Manyoni wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kwani yamewajengea uwezo wa kukagua na kutambua bidhaa ambazo hazina ubora.Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa pamoja na mambo mengine akizungumzia kuhusu baadhi ya majukumu ya TMDA kukasimishwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa TAMISEMI.

Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa akiwaelekeza jambo washiriki wa mafunzo hayo.

Mshiriki wa mafunzo hayo Upendo Kiula ambaye ni Mratibu wa Huduma za Maabara kutoka Wilaya ya Itigi, akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo.

Mshiriki wa mafunzo hayo Alfred Rwamtoga Mfamasia kutoka Wilaya ya Manyoni akizungumza kuhusu mafunzo hayo


Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Taswira ya mafunzo hayo.

Afisa wa TMDA, Neema Debwe akichukua moja ya matukio wakati wa mafunzo hayo. 

Mafunzo yakiendelea.Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo hayo na mgeni rasmi

Saturday, March 9, 2024

DSE, WADAU WANG’ARISHA HAFLA YA ‘PIGA KENGELE’ KWA USAWA WA KIJINSIA 2024

Mkurugenzi wa Uwekezaji ndani ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji Aristides Mbwasi (wa tatu kushoto) ambaye alimuwakilisha Waziri wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa mgeni rasmi, akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa yaliyofanyika Machi 8, 2028 jijini Dar es Salaam.

. Godwin Myovela, Dar es Salaam

MAELFU ya wanawake nchini jana wamejitokeza kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake (8 Machi 2024) huku Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikitumia siku hii vilivyo kufanya tathmini ya hali ya usawa wa kijinsia, sambamba na kuongeza hamasa juu ya uelewa wa pamoja wa dhana hiyo kupitia mpango wa ‘Ring the Bell for Gender Equality’ (piga kengele kwa usawa wa kijinsia).

Mlio huo wa kengele wa kimataifa, ikiwemo Tanzania, unalenga kuleta umakini kwa jukumu muhimu ambalo taasisi na makampuni mbalimbali zinaweza kutekeleza katika kukuza dhana ya usawa wa kijinsia, ili kutimiza matakwa ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, sambamba na kuongeza ufahamu wa Kanuni za Uwezeshaji Wanawake (WEPs).

DSE imekuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango wa ‘Ring the Bell’ kwa kushirikiana na UN Global Compact Network Tanzania, UN Women, International Finance Corporation (IFC) na Shirikisho la Soko la Dunia, kwa azma ya kukuza dhana ya usawa wa kijinsia katika nyanja zote.

Akizungumza katika hafla hiyo jijini hapa, iliyobebwa na kaulimbiu “Wekeza kwa Wanawake: Kuharakisha Maendeleo,  Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Mary Mniwasa, alisema kuwekeza kwa wanawake katika nyanja mbalimbali kusichukuliwe kama ni jukumu la kijamii pekee; bali ni uwekezaji thabiti wa kibiashara wenye busara.

Mniwasa alisema utafiti unaonesha taasisi na kampuni nyingi ambazo zimejumuisha wanawake kwenye timu zao za uongozi huibuka kidedea kwa kuwashinda wenzao katika masuala ya ubunifu, faida na uendelevu, hivyo kwa kutumia talanta na mitazamo ya wanawake, dirisha la fursa mpya mbalimbali linafunguka-na hatimaye kupelekea ukuaji na uvumbuzi ambao unanufaisha sio tu wenye hisa bali jamii.

“Leo tunapotafakari hatua tulizopiga kuelekea usawa wa kijinsia pia tunapaswa kutambua kazi ambayo bado ipo mbele yetu. Bado wanawake wanaendelea kukabiliwa na vikwazo katika kupata mitaji, nafasi za uongozi na fursa sawa katika sehemu za kazi..ni muhimu kuongeza juhudi ili kusawazisha na kuunda mazingira ambayo kila mwanamke anaweza kustawi na kufanikiwa,” alisema Mniwasa na kuongeza:

Kama viongozi katika sekta za fedha na maeneo mengine, bado tuna fursa za kipekee na wajibu wa kuleta mabadiliko, hususani kwa kuwekeza katika mipango inayosaidia wajasiriamali wanawake, sanjari na kuhamasisha masuala ya usawa wa kijinsia kupitia vikao vya bodi mbalimbali za maamuzi, ili kwa pamoja tuweze kufikia mustakabali wenye mafanikio, jumuishi na endelevu kwa wote.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Uwekezaji ndani ya wizara hiyo Aristides Mbwasi, alisema lengo la Maendeleo Endelevu (SDG 5) na kipaumbele mtambuka katika ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030 ni kufikia usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake na wasichana wote.

Alisema bado kuna baadhi ya wanawake wananyimwa fursa ya kupata huduma za afya, wanakabiliana na vikwazo vya elimu na wengine wapo katika hatari ya kubaguliwa kwenye nyanja za kisiasa na kiuchumi, na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

”Kwa kuzingatia ajenda tuliyonayo ya maendeleo endelevu tunayo fursa ya kusahihisha makosa haya na kutanguliza afya, elimu, haki na ustawi wa wasichana na wanawake kila mahali…na msukumo huu wa usawa unapaswa kutambuliwa sio tu kama haki ya binadamu lakini kama msukumo wa maendeleo,”   alisema.  Maadhimisho hayo yakiendelea.

Picha zikipigwa wakati wa maadhimisho hayo.

Wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Baadhi ya wadau wakiwa katika picha ya pamoja na waandaaji wa maadhimisho hayo.