Tuesday, March 30, 2021

ESTL YAKUTANA NA MAKUNDI MBALIMBALI NDANI YA JAMII KUJADILI NAMNA YA KUTOKOMEZA UKATILI NA UKEKETAJI SINGIDA


Mratibu wa mradi wa kutokomeza ukatili na ukeketaji kutoka Shirika la  la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL),   Annamaria Mashaka akitoa mafunzo mbele ya watu maarufu na Mangariba wastaafu, mafunzo yaliyofanyika jana katika Shule ya Sekondari Mungumaji.


Wakatikati mbele ni Mohamed Msafiri mtu maarufu, wa kwanza kulia ni Mwalimu Doris Pantaleo na kushoto ni Hamida Senge wote wakazi wa Kata ya Mungumaji wakifuatilia mafunzo.

Mmoja wa watoa elimu kutoka Shirika la ESTL,  Brigita Mwaka akitoa mafunzo kwa Vijana wa Mungumaji walio nje ya Shule..


 Afisa Ufatiliaji na tathimini  wa Shirika  lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL)Mkoa wa Singida, Philbert Swai, akielekeza jambo katika kikao hicho.


Na Dotto Mwaibale, Singida


SHIRIKA lisilo la kiserikali la Empower Society Transform Lives (ESTL)Mkoa wa Singida limekutana na makundi mbalimbali ya wakazi wa Kata ya Mungumaji kujadili namna ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Katika kuhakikisha ukatili wa Kijinsia unaisha, Shirika hilo limeandaa mpango kazi katika Mradi wake wa mwaka mmoja wa Kutokomeza ukatili na ukeketaji mkoani hapa Mradi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Finland nchini.

Mratibu wa Mradi huo Bi Annamaria Mashaka kutoka Shirika hilo la (ESTL) alisema katika jitihada za kutokomeza ukatili Shirika limelenga kuyafikia makundi mbalimbali ya wananchi wa Mkoa wa Singida ambayo ni Wanawake, Watoto wanaosoma shule za Msingi,Vijana walio nje ya Shule,Wakunga wa Jadi pamoja na watu maarufu.

Makundi mengine ambayo Shirika limelenga kuyafikia ni Mangariba wastaafu,Wahudumu wa afya ngazi ya jamii,Kamati za ulinzi wa Mwanamke na Mtoto ngazi zote pamoja na Viongozi wa Dini,na lengo ni kuongeza uelewa,kubadili mtazamo,mabadiliko ya tabia dhidi ya ukeketaji na mifumo ya aina mbalimbali za ukatili dhidi ya Watoto, Wasichana na Wanawake.

"Tumelenga kuyafikia makundi haya ili tuwape Elimu ya namna ya kutokomeza ukatili kwasababu haya makundi yanafikika moja kwa moja kwenye jamii hivyo wakipata hii Elimu tunaamini jamii itaelimika." alisema  Annamaria.

Alisema mpaka sasa tayari wameyafikia makundi hayo katika Kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Singida kutoa Elimu hiyo ambapo pia zoezi hilo linaendelea katika Manispaa ya Singida kwenye kata za Mungumaji,Kisaki,Unyambwa na Uhamaka.

Kwa upande wao Viongozi wa Dini katika mafunzo yao walishauru na kuhimizana kwenda kuwafundisha waumini wao masuala ya mahusiano na kubainisha athari zake kuliko kuogopa na kuficha ile hali Watoto wanajifunza kwenye Television na sehemu zingine ambazo wakati mwingine hazionyeshi athari zake,hivyo kupelekea Watoto kujiingiza kwenye ndoa za utotoni na mambo mengine.

Huku Katibu wa Baraza kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kata ya Mungumaji Juma Athuman akifikirisha Viongozi wa Dini hiyo kuangalia namna ya kubadilisha muda wa madarasa ya Watoto wanajifunza Madrisa saa za jioni kwani inapelekea Watoto hao kuingia kwenye vishawishi.

Washiriki wengine wameiomba Jamii kutambua ukatili wa Kijinsia upo hivyo kila mmoja anayonafursa kwa nafasi zao kushiriki kikamilifu katika kupinga na kutokomeza ukatili na ukeketaji mkoani hapa na hatimaye nchi kwa ujumla.

TIA YAOMBA KUIDHINISHIWA BAJETI YA BILIONI 46.4

Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala  wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania  (TIA)  Dkt. Modest Assenga, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mipango na bajeti ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 katika kikao cha tatu cha baraza kuu la nne la wafanyakazi wa taasisi hiyo kilichofanyika jana ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine  (SUA) mkoani Morogoro.

Meneja wa TIA Kampasi ya Mtwara, Criph Swallo, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (RAAWU) Mkoa wa Mbeya Martin Mnyili, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Picha ya pamoja ya washiriki wote wa kikao hicho.
 


Na Mwandishi Wetu, Morogoro


TAASISI ya Uhasibu Tanzania  (TIA) inaomba kuidhinishiwa  bajeti ya Sh.Bilioni 46.4 kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022 ili iweze kutekeleza mipango yake.

Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Modest Assenga wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mipango na bajeti ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Taarifa hiyo alikuwa akiitoa katika kikao cha tatu cha baraza kuu la nne la wafanyakazi wa taasisi hiyo kilichofanyika jana ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine  (SUA) mkoani Morogoro.

Dkt.Assenga alisema pamoja na mambo mengine kupitia bajeti hiyo wamepanga kuongeza udahili wa wanafunzi 24,866 ambapo katika kozi za cheti watakuwa 5,413, Diploma 9,267, Shahada 10,145 na kozi za Stashahada 40 jumla yao ikiwa ni 24,866.

" Mwaka huu wa fedha 2021/2022 TIA tumedhamiria kuendelea kuboresha utoaji wa elimu bora kwa kuajiri walimu wenye sifa, kuboresha huduma ya mtandao ili kuwawezesha wanafunzi kujipatia "study materials" mbalimbali, kuboresha huduma za maktaba, kuwapatia wanafunzi mazoezi, majaribio na mitihani pamoja na kuwadhamini wahadhiri wanaojiunga na kozi za "PhD." alisema Assenga.

Dkt.Assenga alitaja maboresho mengine kuwa ni kuongeza vifaa vya kufundishia, kuimarisha kitengo cha utafiti, ushauri na machapisho, kuunga ushirikiano wa kimataifa na kukuza uhusiano na taasisi zingine ili kuongeza maendeleo katika masomo, utafiti na ushauri na kuboresha na kuimarisha kitengo cha ICT na Takwimu kwa kuboresha huduma za ICT.

Assenga alisema katika mwaka  wa fedha wa 2021/2022 TIA imejipanga kukusanya jumla ya Sh.30,968,287,171 kutoka vyanzo vyake vya ndani na St.14,292,406,574.00 ikiwa ni ruzuku kutoka Serikalini, ambapo Sh.11,292,406,574.00 ni kwa ajili ya mshahara na Sh.3,000,000,000 ikiwa ni ruzuku kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Monday, March 22, 2021

TAMUFO YAOMBOLEZA KIFO CHA DKT. JOHN MAGUFULI

 Katibu Mkuu wa  Umoja  Wanamuziki Tanzania  (TAMUFO) , Stella Joel

 


Na Dotto Mwaibale 


UMOJA wa Wanamuziki Tanzania  (TAMUFO) wametoa salamu za rambi rambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021katika Hospitali ya Mzela jijini Dar es Salaam. 

Salamu hizo za rambi rambi pia wamezitoa kwa Waziri Mkuu, viongozi mbalimbali, mjane wa marehemu Janeth Magufuli ,Rais wa Zanzibar na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel alisema kifo cha Rais Magufuli wamekipokea kwa mshituko  mkubwa na kuwa watamkumbuka  milele daima.

"Tunamshukuruaa Mungu kwa ajili ya maisha ya Rais Magufuli ambaye katika uongozi wake aliinua  Tasinia ya Muziki kwa kuwasaidia wasanii kwa kutatua  changamoto zao mbalimbali" alisema Joel.

Alisema Rais Magufuli alifanikiwa kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo kwa kuwa jali wanamuziki hao  upande wa kiafya kwa Kuwapatia Bima ya Afya ya NHIF kwa gharama nafuu kwa ajili ya vipimo na matibabu katika Hospitali za Serikali na za Binafsi.

Joel alisema alikuwa katika maandalizi ya  kufanya maboresho mengi  ili wanamuziki waweze Kufaidika na kazi zao.

" Hakika tutamkumbuka Magufuli  kwa mema mengi aliyoyafanya enzi za uhai wake kama  Rais wa Tanzania"alisema Joel.

Stella alisema kwa niaba ya TAMUFO ana mpongeza Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais  Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na kuwa wana amini atayaendeleza yale  yote ambayo Hayati Rais Magufuli aliyokuwa ameyaanzisha  ambapo wanatambua kwamba kazi hiyo walishirikiana Pamoja.

" Tunakuombea Rais Mama Samia Mungu awe pamoja naye katika kutekeleza yale yote na sisi wanamuziki tumepokea kwa furaha kwa kuapishwa na kuwa Rais wa kwanza Mwanamke katika nchi yetu." alisema Joel.

Sunday, March 21, 2021

TAASISI YA WaLOTa YA MKOANI SINGIDA YAMLILIA DKT. MAGUFULI


Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kuimarisha Maadili na Usaidizi kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi (WoLaoTa), Samwel Olesaitabau, akizungumza na waandishi wa habari  (hawapo pichani)  wakati akituma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea siku ya Jumatano majira ya saa 12:00 jioni  Machi, 17/2021, katika Hospitali Nzela Dar es Salaam.


 Na Dotto Mwaibale, Singida.


MTENDAJI  Mkuu Taasisi ya Uboreshaji Maadili kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi Tanzania (WoLaOTa), Samwel Olesaitabau ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea siku ya Jumatano majira ya saa 12:00 jioni  Machi, 17/2021, katika Hospitali Nzela Dar es Salaam.

Akitoa salamu hizo  mbele ya wanahabari mjini hapa, Olesaitabau alisema kuwa ni tukio lililoshtua wengi maeneo mbalimbali ya nchi, ni tukio lililoshtua watu wengi wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, ni tukio  lililokuja wakati ambapo watanzania wengi walianza kuwa na imani ya utawala wake, ni tukio  ambalo hata baadhi ya nchi rafiki duniani limewashtua sana, ni tukio ambalo limewaacha watu wengi kutoamini masikio yao.

Ni tukio lililobeba huzuni kubwa kwa watanzania walio wengi, ni tukio lililokatisha ndoto njema kwa nchi yetu na ni tukio ambalo litaendelea kugonga vichwa vya watanzania kwa kipindi kirefu.

 Alisema kwa niaba ya taasisi hiyo anatoa pole  kwa Mwalimu Janeth Magufuli na familia yake kwa kuondokewa na mwenzi wake.

"Nimpe pole  Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuondokewa na Rais wake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  John  Magufuli,

nimpe pole  mama yetu Samia Suluhu Hassani kwa kuondokewa na mtu muhimu aliyekuwa mbele yake katika kuongoza nchi, nitoe pole kwa Waziri Mkuu na Baraza zima la Mawaziri kwa msiba huu mkubwa," alisema Olesaitabau.

Olesaitabau ametoa pole kwa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa kwa msiba huu mkubwa, nitoe pole nyingi kwa wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuondokewa na Mwenyekiti wao ndugu John Pombe Magufuli na kuwa jambo lililo kubwa sana watanzania waamini hili limetokea na hakuna jinsi zaidi ya sisi kuendeleza upendo kama alivyoanzisha Hayati John Magufuli.

Alisema watanzania tunapaswa kuamini kwamba, hii ni mipango ya Mungu, tumuombee ndugu yetu Magufuli ili awe mahali salama huko ahera huku tukijipa moyo mkuu na kuamini Mungu anajua atakapo tupeleka baada ya tukio hili.

"Tuendelee kumtukuza yeye John Magufuli kwa kutenda yale aliyoyataka yawe kabla ya umauti kumkuta.Tuombe sana Mungu atupe mbadala sahihi wa Hayati Magufuli.

Niwaombe watanzania kuacha kuhesabu mabaya ya ndugu yetu Magufuli, niwaombe watanzania wajue kwamba, hakuna binadamu aliyekamilika na wajue kwamba,ili mwanadamu akamilike lazima awe na dhaifu  zake, niwaombe wayazungumzie yale mazuri mengi aliyotenda mpendwa wetu Magufuli," alisema Olesaitabau.

Olesaitabau aliwaomba watanzania wayakabidhi yale madhaifu ya ndugu yetu hayati Magufuli kwa Mungu na kuyanena mazuri yake kila wakati ili roho yake ikae mahali salama huko Mbinguni na kuwa wakubali kwamba, mipango ya maisha yetu yapo kwa Mungu na hivyo tusimtafute mchawi bali tumuombee  John Joseph Magufuli apokelewe kwenye ufalme wa Mbingu.


YATAKAYOKUMBUKWA NA WATANZANIA KUHUSU HAYATI MAGUFULI;


 Olesaitabau alisema japo hawezi kuwasemea watu wengine lakini wao kama Taasisi inayo jali maadili mema kwenye utendaji wa kila siku kwa watendaji wa Serikali na Watumishi wa Umma wataendelea kumkumbuka Hayati John  Magufuli kwa mengi na baadhi ya mambo hayo ameyataja kuwa ni kama rais aliyekuwa na msimamo thabiti wa kusimamia kile anachoamini kwamba ni sahihi, kuamini kwamba Bara la Afrika linaweza kujitegemea kwa kutumia rasimali zao wenyewe, atakumbukwa kwa alama nyingi alizoacha kupitia utendaji wake, mfano.Barabara za juu, reli na hata bwawa kubwa la umeme la Rufiji na kadhalika.

Aidha, Olesaitabau alisema Magufuli atakumbukwa na watanzania maskini kwa kujitolea kwa nguvu zote kupambana na wabadhirifu wa mali ya umma, kuanzisha mfumo wa ukusanyaji KODI uliyoziba, kama sio kupunguza mianya ya Rushwa na Ufisadi, atakumbukwa kwa kuanzisha mfumo wa udhibiti wa rasilimali fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri kwa ajili ya maendeleo.

Olesaitabau ataja mambo mengine ambayo atakumbukwa ni kurudisha maadili mema katika Utumishi wa Umma na yeye mwenyewe kuwa mfano, kuthubutu na kufanikiwa kuleta Elimu Msingi Bure, kuwa Rais aliyependa kila Kiongozi kuwajibika kwa nafasi yake, Rais asiyeyumbishwa kwa haraka na kelele kuhusu alichodhamiria, Rais ambaye hayupo tayari kulalamika pale anapokutana na changamoto, atakumbukwa kama Rais ambaye alikuwa na sauti ya kiutawala na kuwafanya walio chini yake kutekeleza yale yaliyo ya faida kwa watanzania wanyonge. Atakumbukwa  kama Rais ambaye hapendi mtu wa chini kuonewa.Atakumbukwa kama Rais ambaye hakupenda wateule wake kutoa majibu ya ubabaishaji.

Alitaja mambo mengine atakayokumbukwa ni kiongozi aliyekuwa na kipaji cha kuhifadhi kumbukumbu kichwani, ni kiongozi aliyetoa nafasi ya kujirekebisha pale inapobidi kwa wateule wake kabla ya kuwaondoa kwenye nafasi zao, atakumbukwa  kama kiongozi aliyejua kwamba, uongozi ni gharama  na unahitaji kujitoa Muhanga, atakumbukwa kama Rais aliyeonyesha kwa vitendo maana ya uadilifu, atakumbukwa kwakutaka kufuata nyayo za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hasa katika suala la kujitegemea kamaTaifa, Magufuli atakumbukwa kama mtu aliyeamini kwamba,uongozi ni utumishi wa Mungu kama ilivyoandikwa na mtumishi wa Mungu Mathayo kupitia Sura 20:26-28 na maneno ya Mungu yanasema; ”Lakini kwenu isiwe hivyo ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote, na anaye taka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu ,na hivyo hivyo mwana wa Mungu hakuja kutumikiwa bali amekuja kutumika na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu.”

Olesaitabau alisema Magufuli atakumbukwa kama kiongozi aliyekuwa na uwezo wa ubunifu kama alivyosema Mwanafalsafa mmoja wa uongozi aitwaye Steve Jobs miaka ya hivi karibu ninanaomba ninukuu;”Ubunifu ndiyo hutofautisha kiongozi na wafuasi wake,na kwavyovyote vile ukitaka kusonga mbele katika Ulimwengu wa sasa lazima uwe na kiongozi mbunifu” kama alivyokuwa Hayati Magufuli.


WITO


Olesaitabau ametoa wito kwa Watanzania tuendelee kushikamana zaidi na tuachanena yale yote yatakayo tugawa sisi kamaTaifa, niwaombe waliyopo kwenye Serikali hivi sasa waendelee kuchapakazi na kamwe wasilegeze kamba na kwa kufanya hivyo watanzania wataendelea kuwa mahali salama hata baada ya kifo cha Hayati John Pombe Magufuli.

"Nimuombe  Rais Mama Samia na Serikali yake asiache kusimamia yale mazuri yote aliyoanzisha mpendwa wetu hayati John Magufuli, kuendelea kusimamia ule mfumo wa ukusanyaji KODI kwa faida ya Watanzania, kuendelea kuziba ile mianya ya wizi wa mali ya Umma kama alivyofanya hayati Magufuli na kwa kufanyahivyo, atakuwa amemuenzi," alisema.

Katika hatua nyingine Olesaitabau amewaomba watanzania kumpa ushirikiano wa kutosha Mama Samia ili kazi yake ya kuongoza nchi iwe rahisi kwake . Na alihitimisha kutoa salamu hizo za rambirambi kwa kufuata maandiko matakatifu kutoka katika kitabu cha AYUBU; 1:21. Na maneno ya Mungu yanasema,” Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa jina lake LIHIMIDIWE MILELE”.

Saturday, March 20, 2021

UMOJA WA DINI MBALIMBALI MKOA WA SINGIDA WAOMBOLEZA KIFO CHA JPM


Mwenyekiti wa Umoja wa dini mbalimbali Mkoa wa Singida, Hamisi Kisuke, akisoma salamu za rambirambi za umoja huo mbele ya waandishi wa habari mjini hapa kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Alhaji Burhan Amri Mlau akisaini katika kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa Tanzania Dkt. John  Magufuli.

Alhaj Burhan amemuelezea Dkt. Magufuli kuwa ni mtu aliyetumia uwezo wake wote wa kielimu  kutafuta njia bora ya kuwatumikia watanzania na kuwainua kiuchumi.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida, Elisante John, akisaini katika kitabu hicho.




Mchungaji Rehema Gwao wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati , akisaini katika kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa Tanzania Dkt. John  Magufuli.

Viongozi wa dini wakisubiri kusaini katika kitabu hicho.

Mwenyekiti wa Istiqaama Tawi la Singida, Khalfan Salum Khalfan, akisaini katika kitabu hicho.


Viongozi hao wa dini wakiomba dua kumuombea Rais Magufuli.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, akisaini katika kitabu hicho.

Viongozi wa dini wakisubiri kusaini katika kitabu hicho.
Mchungaji Wilson Mkoma wa Kanisa la EAGT-Puma na Katibu CPCT Mkoa wa Singida akitoa salamu za rambirambi.


Mjumbe wa Baraza la Mashehe Mkoa wa Singida, Issa Nassoro (kushoto), akizungumzia jinsi alivyo mfahamu Rais Magufuli


.........................................................................
 .

UMOJA wa Dini mbalimbali mkoa wa Singida, umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea majira ya saa 12:00 jjionu, tarehe 17/03/2021, katika Hospitali Nzela Dar es Salaam.

Katika salamu zetu za rambirambi tunatoa pole kwa mama Mjane Janeth J.P.Magufuli), watoto wa marehemu, ndugu jamaa na marafiki, aliyekuwa makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na watanzania wenzetu, na afrika kwa ujumla.

Tunawaomba watanzania wote hususani walioko Mkoa wa Singida, kuwa na utulivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi kwa kuondokewa na mpendwa wetu, shujaa wa Afrika. tunaamini kuwa Mungu alitupa zawadi na ni Mungu huyu huyu ameamua kumtwaa kutoka katika maisha haya sasa na mapenzi yake. tunawasihi watanzania wote kuiombea nchi ili idumu katika upendo, amani, utulivu na mshikamano huku tukisahau tofauti ztu na kusonga mbele kuyaenzi na kuyaendeleza mazuri yote aliyotuachia. pia tumuombee rehema marehemu ili afike mbinguni salama.

RAI:

Tunatoa rai kwa wote wasioitakia mema nchi yetu waliokonndani na nje ya nchi kwamba wasifikirie kuwa kuondokewa na Rais ni fursa kwao kuharibu upendo, amani, utulivu na mshikamano uliojengwa na waasisi wetu kwa muda mrefu. Mungu atuepushe na wote wenye kulitakia mabaya Taifa letu. pia tunamuombea mama yetu mpendwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kama lilivyo jina lake: Samia mwenye kusikia, atakuwa msikivu kwa Mungu na kwa wanadamu. Suluhu - kufanya suluhu/upatanisho mahali ambapo hakuna amani na Hassan maana yake kutenda mema yote aliyoyaanzisha mtangulinzi wake. mungu amvuvie Roho wake na kumvika ujasiri, akasimame kiume kwa nguvu za Mungu kuliongoza Taifa hili pasipo hofu, mashaka wala tashwishi ya aina yoyote, maana Mwenyezi Mungu atakuwa naye siku zote za uongozi wake.


RAIS SAMIA AANZA NA WAANDISHI WA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha uaminifu
 

Na John Mapepele, Dodoma

Tanzania imeandika historia ya kuwa na Rais mwanamke wa kwanza kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameapishwa rasmi tarehe 19 Machi, 2021 kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Mhe, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi, 2021.

 

Kwa Mujibu wa ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kijiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana namaradhi ya mwili au  kushindwa  kutekeleza kazi za rais, basi  Makamu wa Rais ataapishwa  na atakuwa Rais kwa muda  uliobaki katika kipindi cha miaka mitano.

 

Mara baada ya kula kiapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na majonzi mazito amezungumza kwa kifupi na kuanza kwa kutoa ratiba ya mazishi ya mwili wa aliyekuwa Rais, Mhe. John Pombe ambapo amesema kutakuwa na vituo vinne (Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Chato) vitakavyotumika kwa ajili ya kuagia ili wananchi wengi waweze kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao katika kipindi hiki kabla  ya mazishi rasmi tarehe 25 Machi 2021.

 

“Leo si siku nzuri ya kwangu kusema, kutokana na kidonda kikubwa moyoni na mzigo mzito nilionao. Nimekula kiapo katika mazingira tofauti, nimezoea kula kiapo katika mazingira tofauti, nimezoea kula kiapo katika hali ya nderemo na furaha lakini leo nimekula kiapo katika hali ya huzuni na masikitiko” amesisitiza Rais Samia Suluhu Hassan

 

Kama ilivyotarajiwa na watanzania wengi  kuhitaji faraja na matumaini kutoka kwa Rais huyu mpya baada ya  wimbi jeusi lililotanda ghafla baada ya jemedari na shujaa  mwanamapinduzi Dkt JPM  kuanguka, ndivyo ilivyokuwa baada ya Rais Samia kusoma hotuba yake fupi iliyosheheni mwanga wa matumaini mapya kwa Taifa iliyosisitiza  upendo, mshikamano na umoja kwenye kipindi hiki cha maombolezo.

 

“Katika kipindi hiki cha maombolezo, ni kipindi cha kuzika tofauti zetu, huu ni wakati wa kuwa wamoja, huu si wakati wa kutazama yaliyopita, huu si wakati wa kunyosheana vidole bali huu ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kuweka mbele nguvu kwa pamoja ili kujenga Tanzania ambayo Mheshimiwa Magufuli aliitamani, na zaidi sana tuungane kumwombea (hayati John Pombe Joseph Magufuli) alale pema peponi.” Amefafanua

  

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Samwel Malecela  amesema Taifa linapitia katika kipindi kigumu jambo la muhimu  ni kuendelea kushikamana  kama watanzania ili kupita kwenye kipindi hiki kwa umoja na upendo.

 

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro anaona kuwa pamoja na kuondokewa na Jemedari Mkuu hayati Dkt. John Pombe Magufuli Mungu ataivusha nchi yetu itaendelea kuwa imara.

 

“Taifa hili ni imara,Mungu amelipendelea sana, halikuwahi kuyumba wala kutetereka katika nyakati zote za changamoto; yalipotokea maasi ya kijeshi mwaka 1964, alipofariki Mzee Karume mwaka 1972, nyakati mbaya za njaa, nzige na vita ya Uganda miaka ya 1970 na 1980, alipofariki Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine mwaka 1984 na alipong’atuka madarakani na kufariki Muasisi na Baba wa taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tusiogope na tusitetereke, sisi ni taifa imara siku zote,nyakati zote” anaongeza Mtaturu.

 

Rais Samia ameyashukuru makundi ya watu mbalimbali kwa  kuendelea  kushikamana na Serikali yake, makundi hayo  ni pamoja na Chama cha Mapinduzi,viongozi wakuu wastaafu, vyombo vyote vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini.  

 

Pia kwa namna ya pekee amewashukuru Wasanii na Waandishi wa Habari kwa kuendelea kutumia taaluma zao katika kuwaunganisha watanzania kuwa kitu kimmoja wakati wote. Baadhi ya Wasanii wakongwe wa muziki na Waandishi wameonekana kuguswa sana na hotuba hii na kutoa ya moyoni:

 

“OOOh, No. ungekuwepo wakati tunaangalia hii hotuba ilibidi tukae tuangalie kwenye luninga, mimi binafsi nilikuwa ninanena kwa lugha nakumbuka nilikuwa nimezungukwa na vijana nikawamuru watulie kwa sababu  huu ndiyo wakati wa bwana, nikawambia Mungu alipotaka kuwakomboa Taifa la Israel toka kwenye nchi ya utumwa alimtumia mwanamke na kwamba aliweka hekima ndani ya mwanamke na wakati huu Mungu ameweka mwanamke kwa maana kuna jambo ambalo Mungu anataka kutuingiza” amesema Christina Shusho, mmoja wa waimbaji wakongwe wa nyimbo za Injili hapa nchini.

 

“Mimi napenda kwenda na neno la kinabii Mheshimiwa Rais Samia ametuheshimisha sana wasanii wa Tanzania maana kuna makundi mengi lakini sisi wasanii tumependelewa tumetajwa katika hotuba ya kwanza natambua makundi mengine yataendelea kutajwa” ameongeza Shusho.

 

Kuhusu kifo cha Dkt. Magufuli Shusho amesema hayati Rais Magufuli  hakuona haya kumtambulisha Mungu wake katika kila hatua aliyopita pamoja na nafasi aliyokuwa nayo:

 ” kuna watu ambao tunampenda Mungu tunamjua Mungu tunapokuwa chini, tukiinuliwa hivi kama  mimi wa bwana Yesu asifiwe unakuta vinapungua kwa sababu ya position niliyoipata lakini Mheshimiwa Rais JPM hakumwacha kumsema Mungu wake wakati yeye ndiye alikuwa kiongozi Mkuu namba moja katika nchi yetu”.

 

Mwanamuziki Nguli nchni, Mrisho Mpoto amesema Wasanii na Wanamuziki wataendelea kumkumbuka Dkt. Magufuli kwa kuwa hakuwabagua, kila msanii alimfanya sawa na mwingine kiasi cha kumfanya kila msanii ajione anapendwa na Rais JPM.

 

“Utakumbuka  mtindo wake wa kuwavisha kofia yake alijitahidi sana kwa kadiri alivyoweza kufanya hivyo kwa kila msanii, mimi binafsi aliwahi hata kunitambulisha kuwa ni mwanamuziki  bora kabisa na  yeye ni shabiki wangu na kwenda mbali zaidi kwa kuimba  baadhi ya nyimbo zangu mbele ya umati wa  watu” amesema Mpoto kwa furaha

 

Mwandishi wa Habari wa kujitegemea Dotto Mwaibale amesema falsafa ya Dkt. Magufuli ya kuenzi lugha ya Kiswahili duniani umewafanya hata Viongozi wakuu barani afrika kufikiria kuanza Kiswahili kama lugha rasmi katika nchi hizo.

 

Mwandishi wa Makala haya ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anapatikana katika: jmapepele1@ gmail.com au 0784441180

Friday, March 19, 2021

KANISA LA ABC LAMPONGEZA MAMA SAMIA, LAMLILIA JPM

Askofu Kiongozi wa Kanisa la ABC, Flaston Ndabila


Na Dotto Mwaibale


ASKOFU Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Center (ABC) la Tabata  Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo wamempongeza  Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Sita wa Tanzania.

Mbali na pongezi hizo Askofu Ndabila ametumia nafasi hiyo kumpa pole Rais Samia Suluhu Hassani kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli kilichotokea jana Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.

Wengine waliyopewa pole ni mjane wa marehemu Janeth Magufuli, viongozi mbalimbali na watanzania wote kwa ujumla.

Ndabila akimzungumzia Hayati Rais John Magufuli alisema watanzania watamkumbuka kwa mambo yote ya maendeleo aliyofanya.

"Kila ninapofikiria mambo ambayo Mungu alimpa neema Rais wetu Magufuli kuyatenda nakumbuka vile Bwana yetu Kristo alivyo kuwa akifanya kazi zake hapa duniani." alisema Ndabila.

Ndabila akimtolea mfano Yesu  wakati akifanya kazi zake za kitume yalitokea mabishano mengi kati yake na waandishi , wanasheria, mafarisayo na masadukayo. 

" Kwa kuwa mtindo wake Yesu  wa kufanya kazi ulitofautiana kabisa na mazoea yao wengine walimtuhumu hafuati taratibu na desturi zao ambazo zilikuwa ni kinyume na mazoea yao ambapo aliokota fimbo na kuwapa mkong'oto na kupindua meza zao walipokuwa wakifanya biashara haramu hekaluni wakati alisaidia watu siku ya sabato na kuponya huku akiwaambia wale aliowaponya wabebe magodoro waende zao kumbe walikuwa  wakikwazika." alisema.

Ndabila alisema Yesu aliwajibu watu hao waliokuwa wakishindana naye kuwa kazi za mtu humshuhudia, kazi za mtu humsadikisha kwa watu. kazi za mtu humuaminisha mtu.

Alisema Rais wetu Magufuli ambaye Mungu amemtwaa alituaminisha ya kwamba kazi anazozifanya anazifanya kwa kumtanguliza Mungu na kuwa mafanikio yake yanatokana na  kumuweka  Mungu mbele.

" Magufuli aliwaaminisha watanzania kumwamini Mungu kwa kila kazi wazifanyazo na kuwa wakati wote alikuwa upande wake" alisema Ndabila.

 Alisema kitendo hicho cha kuwaaminisha kiliwapa wepesi wa kufundisha neno la Mungu na kuwa kazi hizo zilipokuwa zikifanyika alimrudishia Mungu utukufu.

Alisema maaskofu watamkumbuka  Magufuli kwa kuwapa  ari ya  kazi  baada ya kuona kiongozi wao ambaye ni mkuu wa nchi akimtanguliza Mungu kwa vitendo na ameondoka huku kazi zake zikiwa zinahubiri na kushuhudia.

Ndabila   alisema Rais Magufuli atakumbukwa kwa kazi kubwa alizozifanya katika kipindi chake kifupi cha uongozi wake.

" Kazi  aliyofanya   ni ya kutukuka ukiangalia hapa Dar es Salaam na mikoani ni mahali  gani utaenda usione mabadiliko kuanzia barabara, madaraja ya juu kuanzia Tazara na Ubungo" alisema.

Ndabila alisema mbali ya kazi hizo amejenga stendi kuu za mabasi za kisasa katika ya mikoa ya Simiyu,Morogoro, Korogwe Tanga, Kibaha na Dodoma pamoja na vituo vya afya, Hospitali na shule ukiachilia mbali miradi mikubwa kama  Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Reli, ununuzi wa vivuko kwa ajili ya usafiri wa majini, ndege na mingine. 

Thursday, March 18, 2021

VIJANA SINGIDA WAMLILIA RAIS DR. JOHN MAGUFULI

Kaimu Afisa Vijana  Mkoa wa Singida Frederick Ndahani.
Mwanaharakati wa masuala ya kijamii  Mkoa  wa Singida, Stella Mwagowa
Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung'unyi  wilayani  Ikungi mkoani hapa, Yahaya Njiku.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida


 VIJANA mkoani hapa wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za  kifo cha Rais Dkt. John Magufuli kilichotokea Jana. 

Akizungumza na waandishi  wa habari mkoani hapa jana kwa niaba ya vijana hao Kaimu Afisa Vijana  Mkoa wa Singida Frederick Ndahani alisema   watamkumbuka  Rais Magufuli kwa kuwafundisha  kuwa wazalendo wa Taifa letu.

"  Vijana na  baadhi ya watanzania tulikosa uzalendo lakini Magufuli akatuhasa na kutusihi tuwe wazalendo."  alisema Ndahani.

Ndahani alisema kuonesha jinsi  alivyo  kuwa akiwapenda  vijana  alitoa  nafasi nyingi za uongozi  wakiwemo wakuu wa wilaya, mikoa na baadhi  yao  aliwateua  kuwa  mawaziri.

Alisema aliwateua vijana kwa sababu aliamini wanao uwezo wa kusimamia mambo kwa uchungu kwa kuwa wao ni nguvu ya Taifa.

Aidha Ndahhani  alisema  Rais Magufuli  amefariki akiwa ametujengea uchumi wa viwanda na kutufikisha katika uchumi wa kati sambamba na elimu bure kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.

Alisema kwa niaba  ya  vijana wa  mkoa  huu wanatoa pole kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Wabunge, viongozi wote na watanzania wote kwa msiba huu mkubwa na kuwa  wanamuomba mrithi wake  Mungu amjalie aendeleze yale yote mazuri aliyoyacha.

Mwanaharakati wa masuala ya kijamii kwa ujumla mkoani hapa Stellah Mwagowa alisema  Rais Magufuli aliwaaminisha  vijana kuwa wanaweza kwani  hapo awali hawakuweza kudhubutu kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi mbalimbali.

"Magufuli alijenga misingi kwa vijana kugombea nafasi mbalimbali  ambapo katika Bunge la 12 wapo wengi  tofauti na miaka mingine"alisema Mwagowa.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung'unyi  wilayani  Ikungi mkoani hapa, Yahaya Njiku alisema Rais Magufuli ametuachia alama na vitu ambavyo tutakapo kuwa tunaviangalia hatutaweza kumsahau kutokana na kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambao utawasaidia vijana kupata ajira na wananchi kupata umeme wa uhakika.

Njiku alitaja miradi mingine aliyoianzisha kuwa ni reli ya kisasa,  madaraja makubwa jijini Mwanza na Dar-es-saalamu, kununua vivuko kwa ajili  ya  usafiri wa majini  pamoja  na usafiri wa anga

Wednesday, March 17, 2021

UPATIKANA WA MAJI SAFI NA SALAMA WILAYANI MKALAMA SINGIDA KUONGEZEKA

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati kulia)  Mhandisi Jackson Masaka na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji,  Rosemary Rwebugisa ( katikati kushoto) wakifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Maji uliopo Kata ya Nduguti Wilayani humo jana kwenye maadhimisho ya wiki ya Maji.

Wananchi na viongozi wakishangilia wa uzinduzi wa mradi huo wa maji.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Lucy Boniphace akimtwisha ndoo mkazi wa Kata ya Nduguti baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo.
Maadhimisho hayo yakiendelea.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara Kata ya Nduguti yalipo fanyika maadhimisho hayo.
 


Na Mwandishi Wetu, Singida.


HALI ya upatikanaji wa Maji safi na salama katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia 76.8% kutoka 65.8% ya sasa baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kuchimba na kukarabati visima katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Meneja wa wakala huo (RUWASA) Wilaya Mhandisi Antidius Muchunguzi alitoa taarifa hiyo jana kwenye maadhimisho ya wiki ya maji wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji uliopo Kata ya Nduguti ukiwa ni miongoni mwa miradi inayoendelea na iliyotekelezwa katika Vijiji mbalimbali wilayani humo.

Mhandisi Muchunguzi alisema kwa sasa hali ya upatikanaji wa Maji katika Wilaya hiyo ni 65.8% lakini baada ya kukamilika Miradi ya Vijiji vya Kinyangiri,Ibaga,Kinyambuli,Mpambala,Ikolo,Lyelembo,Nkungi,Ipuli na Malaja hali ya upatikanaji wa Maji utafikia 76.8%

"RUWASA Wilaya ya Mkalama inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali vijiji, mingine tunakarabati na mingine tunachimba visima katika vijiji vya Nkungi,Ipuli na Malaja." alisema  Muchunguzi.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kuzindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jackson Masaka aliziagiza kamati za Maji na wananchi kwa ujumla kuitunza miradi hiyo ili iwe endelevu.

"Miradi hii ili iwe endelevu inahitaji usimamizi wa karibu.Wananchi mshiriki katika ulinzi wa miundombinu ya Miradi ya Maji na kushiriki kupanda Miti kwenye Vyanzo vya Maji." alisema Masaka.

Aidha ameagiza RUWASA na kamati za maji za vijiji kuhakikisha maji hayapotei huku fedha zinazotokana na ankara za maji akitaka zitumike katika kukarabati miundombinu.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji Rosemary Rwebugisa,  aliwaagiza wananchi pamoja na kutunza miradi hiyo na vyanzo vyote vya maji ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji,kulipa Ankara kwa wakati ili huduma ziendelee kutolewa.

Rwebugisa alisema Wizara haitafikia malengo yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji na salama kama miundombinu ya miradi iliyotekelezwa haitatunzwa.

WANUFAIKA WA TASAF IRAMBA MKOANI SINGIDA WAOMBA WATAALAMU WA KILIMO NA MIFUGO

Mnufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) wilayani Iramba mkoani Singida, Magreth  Peter akiswaga ng'ombe wake aliowapata baada ya kuwezeshwa na mpango huo..
Mnufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)  Magreth  Peter (kushoto) mkazi wa Kijiji cha Kengege akizungumza na viongozi wa kijiji hicho pamoja na maafisa habari kutoka TASAF makao makuu waliomtembelea kujua mafanikio yake na changamoto alizo nazo.
Mnufaika wa mpango huo, Ukende  Kidyusi akiwa na wajukuu zake mbele ya nyumba yake ya kisasa aliyoijenga baada ya kuwezeshwa na TASAF.
Mnufaika wa mpango huo, Joyce Mpugi akiwa na mume wake mbele ya nyumba yao ya kisasa waliyoijenga baada ya kuwezeshwa na TASAF huku wakiwa na kuku ambao ni zao lililotokana na mpango huo..
Nyumba ya tembe iliyo kuwa ikitumiwa na Mariam Danford na wazazi wake kabla ya kujengwa nyumba yao ya kisasa.
Hii ni nyumba ya kisasa ya wazazi wake  Mariam Danford baada ya kuwezeshwa ma TASAF.
 Mariam Danford (kulia) akizungumzia mafanikio waliyopata kutoka TASAF.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kijiji cha Kengege, Edward Mdende akizungumzia jinsi TASAF ilivyo wawezesha kulifanyia matengezo  lambo la maji ambalo linawasaidia katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Betha Simon akizungumzia faida za lambo hilo.
Mratibu wa TASAF wilayani humo, Adamu Msangi akizungumzia utekeleza wa mpango huo. 



Na Dotto Mwaibale, Iramba


WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) wilayani Iramba mkoani hapa wameomba kutembelewa mara kwa mara na wataalamu wa kilimo, mifugo na biashara ili waweze kuwasaidia  kupata faida badala ya  hasara.

Maombi hayo yametolewa jana kwa nyakati tofauti na wanufaika hao wa Kijiji cha Kengege wakati wakizungumza na waandishi wa habari na maofisa wa mfuko huo ambao wapo katika ziara ya kuwatembelea ili kujua mafanikio na changamoto walizo nazo.

Mnufaika wa mpango huo Magreth Peter ambaye hujishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji wa nguruwe na ng"ombe alisema changamoto kubwa waliyonayo ni kukosa wataalamu wa kuwapa elimu ya ufugaji na kilimo pamoja na  biashara.

"Tunashindwa kupiga hatua kutokana na kupata matunda kidogo yatokanayo na kazi zetu kwa sababu ya kukosa wataalamu hao ambao hapa kwangu walifika mwaka juzi na hawajarudi tena" alisema Peter.

Aidha Peter alisema kutokuwa na elimu ya biashara kumechangia kwa kiwango kikubwa kuuza mifugo yao kwa bei ya chini kupitia walanguzi na madalali akitolea mfano alipouza nguruwe wake 11 kwa sh.milioni 1.8 tu.

Mnufaika mwingine Ukende Kidyusi anaye jishughulisha  na kilimo na ufugaji kazi zilizo msaidia kujenga nyumba ya kisasa baada ya kuwezeshwa na TASAF anasema elimu ndogo wanayopata kutoka kwa wataalamu hao wanayoitoa kwenye mikutano ya hadhara bila ya kufika zilipo shughuli hizo zina warudisha nyuma licha ya TASAF kuwa na maono mazuri ya kuziinua kaya Masikini.

Mratibu wa TASAF wilaya hiyo Adamu Msangi alisema mara kwa mara wanapokutana na  wataalamu hao katika mikutano ya kiutendaji  wamekuwa wakihimiza kuwatembelea walengwa wa mradi huo kwa ajili ya kujua changamoto zao za kilimo na ufugaji ili kuzipatia ufumbuzi haraka.

Akizungumzia utekeleza wa mpango huo alisema halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha sh. 7,716,971,481 kutoka Serikali kuu ambapo kwa  mwaka 2014/ 2020 wametumia sh.5,049,115,890 kwa ajili ya uhaulishaji fedha za ruzuku na utimizaji wa masharti ya afya na elimu. 

Alisema kwa mwaka 2016/2020 walitumia sh.2,032,809,000 kwa  ajira  ya muda mfupi.

Aidha Msangi aliongeza kuwa mwaka 2018/2020 walitumia sh.300,750,000 kwa ajili ya kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ulimi na athari za ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana walio ndani ya mfumo wa shule  (Timiza malengo)

Alisema mwaka  2018/2020 walitumia sh.23,963,500 kwa ajili ya kuwawesha wananchi kiuchumi na kuwa mwaka huo huo walitumia sh.170,304,091 kutoa kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana walio nje ya mfumo wa shule (Timiza male ngo)

Wanufaika wengine wa mpango huo ni Joyce Mpugi ambaye anajishughulisha na kilimo, ufugaji wa kuku, mbuzi na ng'ombe, Ukende  Kidyusi na Mariam Danford ambapo wote kwa pamoja wamefanikiwa kuondoka kwenye nyumba za matembe walizokuwa wakiishi  baada ya kujenga za kisasa.