Monday, August 31, 2020

MAANDALIZI YA KUMPOKEA MGOMBEA URAIS WA CCM MKOANI SINGIDA YANAENDELEA

 

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Ahmed Kaburu, akionesha llani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)  ya mwaka 2020-2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kumpokea mgombea Urais wa chama hicho Dkt.John Magufuli ambaye anatarajia kuwasili mkoani hapa kesho.

Mabango yenye picha za mgombea huyo yakiwekwa Barabara Kuu ya Singida Dodoma. 


Watoto Ashiruna Athumani (kushoto) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Utemini mkoani hapa  na wadogo zake wakitazama picha ya mgombea huyo iliyoweka viwanja vya Bombadia.
Vijana wa Jeshi la Akiba wakisafisha eneo la uwanja utakapofanyika mkutano wa mgombea huyo.
Uwanja utakapofanyika mkutano huo.

Mabango yenye picha za mgombea huyo yakiwa yamewekwa Barabara Kuu ya Singida Dodoma. 


Mafundi wakiendelea na kazi ya kusimika Jukwaa utakapofanyika mkutano huo. 

 

Mafundi wakiendelea na kazi ya kusimika Jukwaa utakapofanyika mkutano huo.

Wajasiriamali wakichangamkia fursa ya mkutano huo kwa kuuza sare za chama hicho.


Na Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale, Singida.

MAANDALIZI ya kumpokea mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida Dkt John Pombe Magufuli yanaendelea kukamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandalizi hayo Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Ahmed Kaburu alisema maandalizi yanaendelea kukamilika ambapo kesho wanatarajia kumpokea Mgombea huyo mkoani hapa.

Kaburu alisema mgombea huyo ataongea na wananchi wa Mkoa huo kwenye viwanja vya Bombadia vilivyopo Manispaa ya Singida.

"Kesho majira ya saa nne asubuhi nawakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Singida mfike kwenye viwanja vya Bombadia kuja kumsikiliza Dkt John Pombe Magufuli mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chetu cha CCM." alisema kaburu.

Alisema pamoja na maandalizi yote mgombea huyo atahutubia wanachama na wananchi pamoja na kunadi ilani ya chama hicho ya mwaka 2020-2025 ambayo alisema imejaa shehena ya vitu vizuri,pia atapata fursa ya kuwatambulisha na kuwanadi wagombea nafasi ya ubunge katika majimbo nane ya mkoa huo.

Katika mkutano huo wamekaribishwa wazee maarufu, viongozi wa dini pamoja na wasanii mbalimbali watakaotoa burudani.

Sunday, August 30, 2020

MSITU WA MINYUGHE ULIOPO IKUNGI MKOANI SINGIDA UPO HATARINI KUTOWEKA

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, viongozi wa Kata ya Mwaru pamoja na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, wakati akikagua Msitu wa Minyughe ambao umevamiwa na kufanyika uharibifu mkubwa wa mazingira.
Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (katikati) na wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Kata ya Mwaru wakiangalia mkaa uliotelekezwa na wavamizi katika msitu huo.Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (katikati) akiwaonesha wajumbe wa kamati hiyo mkaa uliotaifishwa na Serikali baada ya kutelekezwa na wavamizi katika Msitu wa Minyughe wilayani humo mwishoni mwa wiki wakati akikagua msitu huo. Kulia ni Mshauri wa Jeshi la Akiba wa wilaya hiyo, Capteni Gabriel Chabimia na Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP)  Stephano Chaula.


Miti ikiwa imekatwa kwenye msitu huo.
Mjummbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Mwaru, Mohamed Mrisho (katikati) akielezea uharibu wa msitu huo.
Ulinzi ukiimarishwa wakati wa ukaguzi wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na mtoto Soud Seme anayeishi na wazazi wake ndani ya msitu huo.
Wajummbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Mwaru,wakimwaga mkaa uliohifadhiwa kwenye viroba na wavamizi wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida  ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Edward Mpogolo (kushoto) na wajumbe wa kamati hiyo na viongozi wa Kata ya Mwaru wakiangalia mkaa uliotelekezwa na wavamizi katika msitu huo.
Mhifadhi Misitu Wilaya ya  Ikungi (DFC), Wilson Pikoloti akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwaru, Mwinyimvua Midelo , akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha wa Kijiji cha Mwaru, Shabani Nyombe akizungumzia uharibifu wa msitu huo.
Mjummbe wa Kamati ya Huduma za Jamii wa Kijiji cha Mwaru, Johari Haji, akielezea uharibifu wa msitu huo.

Safari ya ukaguzi wa msitu huo ikiendelea.



Na Dotto Mwaibale, Singida.

HALI ya Msitu wa Minyughe uliopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imeendelea kuwa mbaya kutokana na wakazi wanaouzunguka kuuvamia kwa kukata miti hovyo na kuingiza mifugo bila ya kufuata taratibu.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo mwishoni mwa wiki ilitembelea na kujionea hali halisi na namna uvunaji wa mazao ya msitu huo ikiwemo ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa ukifanyika bila ya kufuata utaratibu wimbi kubwa la wahamiaji kutoka mikoa ya jirani wakihusishwa na uharibifu huo.

Msitu huo wenye ukubwa wa takribani hekta 230,000 upo katika Tarafa za Sepuka, Ihanja na Ikungi na kuundwa na vijiji 26 wilayani Ikungi.

Msitu huo ulianzishwa chini ya mradi wa LAMP (Land Management Programme) ukifadhiliwa na Shirika la Sida la Uswisi mwaka 2002.

Msitu huo una uoto wa asili wa miti jamii ya miombo na maeneo kidogo ya mbuga na uoto adimu wa vichaka vya Itigi (Itigi Thickets) huku ukiwa na wanyamapori na viumbe wengine wa aina mbalimbali ambao walifanya makazi ndani ya msitu huo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, viongozi wa Kata ya Mwaru pamoja na waandishi wa habari wakati akikagua msitu huo alisema lengo la kuuanzisha ilikuwa ni kutunza uoto wa asili na bioanuwai zilizokuwa hatarini kutoweka ikiwemo wanyamapori

Alitaja lengo lingine kuwa ni kutunza mazingira kwa ujumla na kupambana na hali ya kuenea kwa jangwa, kutunza rasilimali asili kwa kizazi kilichopo na kijacho pamoja na jamii kunufaika moja kwa moja na rasilimali misitu zilizopo.

Mpogolo alisema msitu huo ni nguzo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ukiungana na msitu wa mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi katika kuimarisha mvua zitokazo misitu ya Kongo.

"Msitu huu ni chanzo cha maji ya Ruaha Mkuu ( Internal Drainage) ukiunga pori la akiba la Rungwa, Muhesi na Kizigo lililopo Manyoni" alisema Mpogolo.

Alisema msitu huo ni kidaka maji ( Catchment Forest) kwa bonde la Wembere linaloweka uhai wa Ziwa Kitangiri na Eyasi.

Mpogolo alikamilisha kuzungumza na wajumbe hao na waandishi wa habari kwa kutoa maagizo ya kuwachukulia hatua watu wote waliovamia msitu huo kwa kujenga na kuingiza mifugo yao ambapo alitaka orodha yao ikiwa na kuondoka mara moja ndani ya msitu ndipo wafanye utaratibu wa kuomba upya kwa serikali ya kijiji.

"Haiwezekani kuingia kwenye hifadhi bila ya kufuata taratibu na kufanya uharibifu huu mkubwa, Serikali ya kijiji na kamati yangu ya ulinzi na usalama ni lazima tuhakikishe uhalibifu huu wa msitu haujirudii tena" alisema Mpogolo.

Alisema hali hiyo ikiachwa eneo hilo litakuwa jangwa na jamii inayoishi humo itapata matatizo ya maisha kwani hata madawa yatokanayo na miti ya asili hayata patikana.

Mpogolo alitumia nafasi hiyo kuwaagiza viongozi wa halmashauri ya kijiji katika eneo hilo kuitisha mkutano utakaowakutanisha wavamizi hao na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ili kujua walipateje kibali cha kuingia kwenye hifadhi hiyo kwani yamekuwepo madai ya watu kuwa kuna baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vijiji vinavyozunguka msitu huo kuchukua fedha au ng'ombe kutoka kwa wafugaji hao na kuwagawia ardhi katika hifadhi.

Alisema kupitia mkutano huo watawabaini viongozi waliojihusisha kwa namna moja au nyingine kutoa maeneo kwenye hifadhi hiyo nao watachukuliwa hatua za kisheria huku wavamizi hao wakifanyiwa utaratibu na halmashauri wa kutafutiwa maeneo mengine ya kuishi na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji nje ya hifadhi. 

Aidha Mpogolo alisema mvamizi  atakaye kahidi hatua hizo za awali za mazungumzo na kuwasikiliza atachukuliwa hatua kali ikiwemo kuondolewa kwa nguvu ndani ya hifadhi hiyo.

 

Tuesday, August 25, 2020

RPC MKOA WA SINGIDA AFANYA MKUTANO NA VIONGOZI WA DINI KUZUNGUMZIA UCHAGUZI MKUU

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,  Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Sweetbert Njewike, akizungumza na viongozi wa dini na wadau wengine (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa  Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Veta mkoani hapa jana.

Baadhi ya viongozi wa dini waliokuwepo kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.


Mkuu wa Polisi Wilaya ya Singida, Florence Mwenda akiwa kwenye kikao hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,  Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Sweetbert Njewike, akisisitiza jambo kwa waandishi wahabari.
Viongozi wa dini wakichukua taarifa hiyo.


 Kikao kikiendelea.



 Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale, Singida.


KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Singida,  Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Sweetbet Njewike ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kujiepusha na makundi yanayolenga kuleta uvunjifu wa amani katika kipindi cha uchaguzi.


Kamanda Njewike alitoa rai hiyo jana alipokutana na viongozi wa dini mkoani hapa na wadau wengine katika makundi mbalimbali kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa  Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Veta.


Aliyataka makundi mbalimbali yakiwemo ya Vijana kutojiingiza kwenye makundi yanayolenga kuleta uvunjifu wa amani katika kipindi cha kampeni,wakati wa zoezi la kupiga kura na matokeo kwani jeshi la polisi limejipanga sawasawa.


"Askari watakuwepo kwenye maeneo yote kunakofanyika kampeni na kila kituo cha kupigia kura na sio kwamba watakuwepo kutisha wananchi hapana ni kuhakikisha wanalinda amani na usalama wa wananchi." alisema kamanda.


Njewike alisema maendeleo ambayo yapo mkoani hapa yanatokana na amani iliopo, hivyo amewaomba Viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao kuzingatia sheria na taratibu wasije wakajikuta wako mikononi mwa vyombo vya sheria.


"Mkiwahimiza na kuwafundisha waumini wenu kuacha dhambi wakiacha watakuwa wametii sheria za nchi." alisema Njewike.


Aidha aliwasisitiza viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na ambayo yamekwisha tolewa na tume ya uchaguzi ikiwemo muda wa kuanza na kumaliza kampeni.


Nao wadau na Viongozi wa dini walipongeza hatua hiyo huku wengine wakiomba maelekezo hayo yatolewe na maaskari kwenye makanisa na misikitini licha ya kuwepo wawakilishi ambao ni viongozi hao.


Kwa upande wake Sheikh Issa Nassoro alisema anaamini kiongozi wa dini akimfundisha kwa unyenyekevu mtu akiwemo mwanasiasa ukiukwaji wa sheria hautakuwepo.


"Wapo wanasiasa ambao dhamira zao ni kuwasaidia wananchi lakini pia tufahamu wapo ambao wanatumiwa na watu/nchi kuleta machafuko,ni wajibu wetu sisi viongozi kuwakemea watu wa namna hiyo." alisema sheikh Nassoro.

Wengine waliwataka wanasiasa na wananchi kufahamu kuwa kuna maisha baada ya kupita uchaguzi, hivyo wasije wakakatisha maisha yao kwa jambo ambalo ni la mda mfupi,huku wakiwaomba wanasiasa kuwa wastaarabu wanaponadi sera za vyama vyao ili kuepuka uvunjifu wa amani.


Monday, August 24, 2020

TAKUKURU WILAYA YA IKUNGI MKOANI SINGIDA YAOKOA NG'OMBE SABA NA SHAMBA LA EKARI 36

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (kushoto) akimkabidhi sh.150,000 mkazi ya Kitongoji cha Mfumbuwahumba, Jumanne Athumani ikiwa ni kurejeshewa haki yake na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo jana baada ya kudhurumiwa kwa njia ya kughushi nyaraka kwa kipindi cha miaka tisa. Katikati anaye shuhudia ni Mkuu wa TAKUKURU Ikungi, Erick Nyoni.

Mkuu wa TAKUKURU wa Wilaya ya Ikungi, Erick Nyoni akielezea tukio hilo kwa mkuu wa wilaya kabla ya makabidhiano.

Ng'ombe aliodhurumiwa Jumanne Athumani wakiwa nje ya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Igombwe kabla ya kukabidhiwa.
Baadhi ya wananchi na maafisa wa TAKUKURU waliofika kushuhudia makabidhiano hayo.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Igombwe, Benjamin Ntandu akizungumzia tukio hilo kwa kifupi wakati akimkaribisha Mkuu wa TAKUKURU wa Wilaya ya Ikungi, Erick Nyoni kulizungumzia tukio hilo.
Jumanne Athumani (katikati) akimshukuru mkuu wa wilaya hiyo baada ya kukabidhiwa ng'ombe na shamba lake.

Mlalamikiwa katika shauri hilo, Peter Joseph ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Igombwe akizungumzia mgogoro huo.

 Baadhi ya wananchi na maafisa wa TAKUKURU waliofika kushuhudia makabidhiano hayo.


Na Dotto Mwaibale, Singida


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imefanikiwa kuokoa ng'ombe saba wenye thamani ya sh.milioni 3.5 na shamba la ekari 36 mali ya Jumanne Athuman mkazi wa Kitongoji cha Mfumbuahumba Kijiji cha Germani Kata ya Igombwe wilayani humo.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo wakati wa kumkabidhi  ng'ombe hao pamoja na sh.150,000,  Mkuu wa TAKUKURU wa Wilaya hiyo, Erick Nyoni alisema mali hiyo ilikuwa ni ya Jumanne Athumani lakini kutokana na mgogoro wa ardhi kati yake na Peter Joseph ambao uliwafikisha baraza la ardhi la kata Joseph alifanikiwa kushinda kesi baada ya kudaiwa kughushi nyaraka ya kijiji ambayo ilikuwa ikionesha eneo hilo la mgogoro alikabidhiwa na Serikali ya kijiji cha Igombwe wakati sio kweli.

"Mlalamikaji Jumanne Athumani alipofika ofisini kwetu kulalamika tulifanya uchunguzi wa kina na kubaini ile nyaraka ilighushiwa na kupelekea baraza la ardhi kumpa ushindi na hata alipokata rufaa kwenda baraza la ardhi la wilaya pia lilimpa ushindi Peter Joseph" alisema Nyoni.

Kutokana na ushindi huo ilimlazimu Jumanne Athumani kuliachia eneo hilo la ekari 36 lakini kutokana na uchungu aliokuwa ilikuwa vigumu kwake kuondoka.

Nyoni alisema baada ya kuona hatoki kwenye eneo hilo Joseph alikwenda kumshitaki kwa madai kuwa amevamia ambapo alifungwa miaka miwili na baada ya kutoka gerezani alifunguliwa tena kesi ya madai ambayo ilisababisha ng'ombe wake tisa wachukuliwe na Peter Joseph.

"Mkuu wa wilaya leo utamkabidhi ng'ombe saba,  sh.150,000 ya gharama za zile hukumu zilizotolewa pamoja na ekari zake 36 ndugu Athumani" alisema Nyoni.

Akimkabidhi ng'ombe hao Mpogolo alimshukuru mkuu wa TAKUKURU wa wilaya hiyo na wafanyakazi wenzake wote kwa kazi wanayoifanya wilayani humo ambapo katika kipindi kifupi wameweza kufanya kazi kubwa ya kurejesha haki za watu zilizopotea na fedha zilizochukuliwa na vyama vya msingi.

"Leo hii ni sehemu ya ishara kwani wamekwisha wahi kurejesha ng'ombe kama hawa katika Jimbo la Singida Mashariki na sasa wamerejesha ng'ombe saba, ekari 36 pamoja na uhuru wa ndugu Jumanne Athumani" alisema Mpogolo.

Mpogolo alisema mtoaji wa hukumu hiyo alitoa kwa haki baada ya kupata ushahidi ambao ulikuwa batili kwenye vyombo vya sheria.

Alisema  tuendelee kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuwa ndiye aliyeamua kuifanyia mabadiliko mapya  TAKUKURU na kuipa majukumu mengine ya ziada kwani tulizoea kuona wakishughulika na watu waliokuwa wakitoa  na kupokea rushwa lakini sasa inafanya kazi nyingi ya kutafuta haki hata kama mtu atakuwa aliipoteza kwa miaka mingi lengo likiwa ni kurudisha haki kwa watanzania.

Mpogolo alitumia fursa hiyo kuomba wahusika na jamii kwa ujumla kuangalia uhalali wa nyaraka mbalimbali zinazopelekwa mahakamani kwani zingine zinakuwa batili na kuweza kupindisha haki.

Jumanne Athumani akipokea ng'ombe hao aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa hatua mbalimbali za kuwasaidia wanyonge kwani katika kipindi cha miaka tisa alikuwa katika mateso makali baada ya kupokwa haki yake. 

Kwa upande wake Peter Joseph ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Igombwe aliyekuwepo kwenye makabidhiano hayo alikiri kuwepo kwa mgogoro wa ardhi dhidi yake na Athumani na kudai haki ilikuwa ni yake ila changamoto  iliyojitokeza ni wajumbe kughushi saini ndio kuliko sababisha  ipotee licha ya awali kupata ushindi. 

Joseph alimshukuru mkuu wa wilaya na TAKUKURU wilayani humo kwa kumaliza mgogoro huo na kusema jambo hilo halitajirudia tena na akashauri sasa kuanza kwenda kanisani kusali akimaanisha kutubu.

Sunday, August 23, 2020

ESTL YAWAKUTANISHA WADAU KUJADILI UUNDAJI KAMATI ZA KUPINGA MATUKIO YA UKATILI

Mtendaji Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la  Empower Society Transform Lives (ESTL), Joshua Ntandu, akizungumza katika kikao kilicho wakutanisha wadau mbalimbali wa Kata ya Kinyagigi katika Wilaya ya Singida Vijijini kwa ajili ya kuunda kamati za vijiji za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia mwishoni mwa wiki. Kutoka kulia ni  Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Veronika Mure na  Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kinyagigi, Nives Mapunda.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Veronika Mure, akizungumzia majukumu ya Mtakuwwa.
Wadau wakipitia mwongozo wa Mtakuwwa.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kinyagigi, Nives Mapunda, (katikati) akizungumza katika kikao hicho.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kinyagigi, Hamisi Mohamed, akizungumza katika kikao hicho.
Mwakilishi wa vijana wa kata hiyo, Alfred Mohamed, akizungumza kwenye kikao hicho.
 Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mitula, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Majadiliano yakifanyika.
Kiongozi wa Dini ya Kikristo, Emanuely Ng'eni, akizungumza kwenye kikao hicho.
 Mmoja wa Wajumbe wa kikao hicho, Jackline Alute akizungumza


Na Dotto Mwaibale, Singida


SHIRIKA lisilo la kiserikali la  Empower Society Transform Lives (ESTL)limewakutanisha wadau mbalimbali wa Kata ya Kinyagigi katika Wilaya ya Singida Vijijini kwa ajili ya kuunda kamati za vijiji za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

Wadau waliokutanishwa na shirika hilo ili kupata mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuunda kamati hiyo ni wakunga wa jadi, walimu wa afya mashuleni, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, waganga wa tiba asilia, mangariba na watu wenye mahitaji maalumu.

Kikao hicho kilicho keti mwishoni mwa wiki katika kata hiyo kililenga kuunda kamati za vijiji zitakazokuwa zikifuatilia vitendo vya ukatili katika wilaya hiyo pamoja na kupitia mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA 2017/18 hadi 2021/22.

Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Joshua  Ntandu alisema shughuli hiyo inafanyika kwa ufadhili wa Ubalozi wa Finland Dar es Salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Singida vijijini kwa kutekeleza mradi huo katika Kata tano ambazo ni Maghojoa, Mwasauya, Merya, Munghunga na Kinyagigi.

Alisema shughuli ambazo kamati hiyo itazifanya kwa kushirikiana na shirika hilo ni kukutana na kina mama wanaohudhuria kliniki na kuwapa mafunzo, kutoa mafunzo kwa viongozi wa dini, vijana walio nje ya shule,wanafunzi mashuleni na kuimarisha klabu za wanafunzi (KLABU JUU) 

Alitaja shughuli nyingine ni kuandaa midahalo ya wazi ya kujadili namna ya kutokomeza mila potofu na kufanya mikutano ya hadhara. 

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Veronika Mure alisema majukumu ya kamati hiyo nikuhakikisha utekelezaji wa mpango kazi huo na shughuli za hutoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi unaendana na mikataba ya Kikanda na Kimataifa ya haki na ustawi wa Wanawake na Watoto pamoja na Sera, Sheria na Miongozo ya Serikali. 

Washiriki wa kikao hicho walisema vitendo vya ukeketaji na matukio ya ukatili wa kijinsia bado ni changamoto na kwamba maovu hayo hufanyika kwa siri kubwa.

“Matukio ya vitendo vya ukeketaji na ukatili wa kijinsia bado vinafanyika na kibaya zaidi watuhumiwa wakikamatwa na kufikishwa polisi au mahakamani huachiwa hivyo kuleta sintofahamu miongoni mwa jamii" alisema mmoja wa wajumbe hao Jackline Alute. 

Alute alisema suala la ukeketaji, mimba na ndoa za umri mdogo yamekuwa ni matukio ya kawaida na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa hata baada ya kumbaini mtuhumiwa walalamikaji na ndugu wa mtuhumiwa hukutana na kuyamaliza kiaina.

Katika kikao hicho wajumbe hao walijifunza mbinu za kuibua vitendo vya ukatili wa kijinsia na jinsi ya utoaji wa taarifa kwa vyombo husika kwa kushirikiana na ESTL.

Washiriki hao walipata fursa ya kukaa katika makundi na kutengeneza mpango kazi  utakaowaongoza katika kutekeleza majukumu yao dhidi ya vita ya matukio ya ukatili wa kijinsia na ukeketaji ambapo kila baada ya miezi mitatu watakuwa wakifanya kikao cha tathmini.

“Lengo la mpango kazi wetu huu ni kutusaidia kuanza kuibua matukio yote ya ukatili, kuhamasisha jamii kuacha kufanya vitendo hivyo na kufanya ufuatiliaji na hatimaye kutoa taarifa kwa MTAKUWWA na kwenye mfumo wa Tehama uliobuniwa na ESTL  ili kutoa taarifa za matukio ya ukatili kwa kutumia namba 0710567003, “ alisema Alfred Mohamed.