Monday, May 31, 2021

SERIKALI SINGIDA YAKAMATA MALORI YENYE TANI 40 ZA MAZAO YASIYO LIPIWA USHURU

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili akikagua moja ya lori lililokamatwa na shehena ya maharage ambayo yanadaiwa kutolipiwa ushuru.

Mfanyabiashara wa maharage , Philipp Lehema akizungumza na Mkuu wa Wilaya Paskas Muragili baada ya kukamatwa kwa maharage hayo.

Mkaguzi wa mazao katika Kituo cha Njia Panda, Juma Athumani akitoa maelezo kwa  DC Muragili jinsi alivyo yakamata magari hayo.

Malori yaliyokamatwa na mzigo huo.

Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Hassan Ngoma  (katikati) akizungumzia tukio hilo.

DC Muragili  (kushoto) akizungumza na dereva Moses Zelothe ambaye gari lake lilikamatwa na mchele ambao haukulipiwa ushuru.
Diwani Mstaafu Hamisi Labu akiipongeza Serikali kwa kuyakamata magari hayo na kuwaomba wafanyabiashara kujenga tabia ya kulipa ushuru wa mazao pasipo shuruti.


Na Dotto Mwaibale, Singida



SERIKALI mkoani Singida imekamata malori matano yenye magunia ya mazao mchanganyiko zaidi ya tani 40 yaliyokuwa yakipitia mkoani hapa bila ya kuwa na nyaraka zozote za kulipia ushuru.

Kufuatia kukamatwa kwa shehena hiyo Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili aliagiza Wafanyabiashara hao  waliokuwa wakisafirisha shehena hiyo ya mazao  kutozwa faini ya sh.milioni 4.5 ukiwemo ushuru.

"Faini kwa Mfanyabiashara wa maharagwe, Philipp Lehema ni sh.milioni 4 na mwenzake Moses Zelothe ni sh.500,000." alisema Mulagiri.

Akifafanuaa kuhusu faini hizo Mulagiri alisema kwa kosa la kudanganya kuhusu ulipaji huo Lehema alitozwa faini ya sh.200,000 kwa kila gari kati ya manne  yaliyokuwa na mzigo huo na kutakiwa kulipa ushuru wa sh.3000 kwa magunia 1200.

Alisema  kwa mfanyabiashara Zelothe alitozwa faini ya sh. 200,000 kwa gari lake na sh. 300,000 kwa magunia 150 ya mchele ambayo hakuyalipia ushuru.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Muragili alisema shehena hiyo ya mazao aina ya maharage na mchele ilikuwa ikisafirishwa kutoka mkoani Kagera na Tabora kwenda Arusha.

Alisema shehena hiyo ilikamatwa ikisafirishwa kwenye malori matano,  manne yenye maharage yakiwa ya Lehema na lenye pumba na mchele likiwa la Zelothe.

Alitaja namba za malori hayo kuwa ni T 335 AWH, T 178 CBB, T 662 DTL, T 489 DUV na T 850 AFQ.

Alisema wafanyabiashara waliokamatwa wakisafirisha shehena hiyo walikuwa wakitumia stakabadhi za malipo ya maegesho ya magari wakati wakipakia mazao hayo kukwepa ushuru.

Mfanyabiashara Philipp Lehema ambaye alikuwa akisafirisha maharage hayo alikiri kusafirisha bidhaa hiyo kwa kutumia stakabadhi ya ushuru wa maegesho na ameshangaa kuona akikamatwa kwa madai ya kutolipa ushuru wakati yeye alifahamu ameshalipia ushuru huo kwa kutumia stakabadhi hizo.

Muragili alitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wafanyabiashara wenye tabia  ya kukwepa kulipa ushuru kwa visingizio mbalimbali na kwamba kwa Mkoa wa Singida hawatapita watakamatwa. 

Mkaguzi wa mazao katika Kituo hicho cha Njia Panda kilochopo wilayani humo,  Juma  Athumani alisema baada ya kuyakamata magari hayo wahusika wenye mzigo huo walijaribu kumshawishi hayaruhusu magari hayo lakini aliwakatalia kwa kuwa alijua kufanya hivyo ilikuwa ni kuikosesha Serikali mapato.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashid Mandoa amempongeza mkaguzi huyo na wenzake waliokuwa zamu siku hiyo kwa kuwa na moyo wa kizalendo na ameahidi kuwapa motisha.

Sunday, May 30, 2021

WFP YAKABIDHI MRADI WA BORESHA LISHE SINGIDA

Viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, wakiwa na kabrasha lenye maelezo ya Mradi wa Boresha Lishe baada ya kukabidhiwa rasmi mradi huo  katika Kijiji cha Sekeutoure Wilayani Singida jana. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri  hiyo, Eliya Digha, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Hassan  Ngoma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashid Mandoa, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Idara ya Afya Kitengo cha Lishe, Mariam Nakuwa, Mwenyekiti wa kijiji hicho Joshua Majengo na Afisa Lishe wa Wilaya hiyo, Neema Swai.


Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Hassan  Ngoma,akihutubia kwenye hafla hiyo.

Afisa Lishe kutoka WFP, Neema Shosho akizungumza kwenye hafla hiyo.
Wawezeshaji wakiwa na bidhaa zao walizozitengeneza kutokana na vyakula vya mbalimbali pamoja na nafaka.

Wananchi wa Kijiji cha Sekeutoure wakiwa kwenye hafla hiyo.

Wananchi wa Kijiji cha Sekeutoure wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wananchi wa Kijiji cha Sekeutoure wakiwa kwenye hafla hiyo.
        Mgeni rasmi Katibu wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma,akiserebuka pamoja na wakina mama.
Mgeni rasmi Katibu wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma akipata maelezo ya elimu ya utunzaji wa mazingira alipokuwa akitembelea mabanda wakati wa hafla hiyo.
Mgeni rasmi Katibu wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma (hayupo pichani) akipata maelezo kwenye banda la ufugaji wa wanyama wadogo.
Mgeni rasmi Katibu wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma  akipata maelezo ya jinsi ya kukausha mbogamboga kwa kutumia kaushio maalumu bila ya kuondoa viini lishe.
Mgeni rasmi Katibu wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma  akipata maelezo ya jinsi ya kutengeneza  vyakula vya aina mbalimbali. Kulia ni Meneja Mkuu wa Shirika la SEMA, Ivo Manyaku

.Mgeni rasmi Katibu wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma  akipata maelezo ya jinsi ya kutengeneza  Juisi kwa kutumia nafaka.
Mgeni rasmi Katibu wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma  akipata maelezo ya jinsi ya kutengeneza  Juisi kwa kutumia nafaka na matunda ya asili.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sekeutoure, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Afisa Lishe wa Wilaya hiyo, Neema Swai., akizungumza kwenye hafla hiyo.
. Mwenyekiti wa Kijiji cha Sekeutoure., Joshua Majengo.akizungumza kwenye hafla hiyo.

Burudani zikiendelea.
Viongozi wakiwa meza kuu.

 Mwenyekiti wa Halmashauri  hiyo, Eliya Digha, (kushoto)  na Meneja wa Shirika la SEMA, Ivo Manyaku (kulia) wakiserebuka  kwenye hafla hiyo. 


Kwaya ya Boresha Lishe ya Wakina Mama wa Kijiji cha Sekeutoure ikitoa burudani kwenye hafla hiyo.


Mwakilishi wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Idara ya Afya Kitengo cha Lishe, Mariam Nakuwa,  akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashid Mandoa, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri  hiyo, Eliya Digha, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Wananchi wa Kijiji cha Seketoure wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi huku wakionesha furaha yao baada ya kukabidhiwa mradi huo.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida 


JUMLA ya Vijiji 85 katika Wilaya za Ikungi na Singida  vimenufaika na Mradi wa Boresha Lishe ambao umefadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) Serikali ya Watu wa Japani na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)

Mradi huo wa miaka mitano ambao umefikia tamati jana mkoani Singida ulitekelezwa na Serikali ya Tanzania pamoja na wadau watatu Shirika la Sustainable Environment Management Action (SEMA) Research Community and Organizational Development associate (RECODA) na Tanzania Partnership in Nutrition (PANITA) katika mikoa ya Dodoma na Singida.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mradi huo iliyofanyika jana Kijiji cha Sekeutoure Wilayani Singida mkoani hapa, Afisa Lishe kutoka WFP, Neema Shosho alisema mradi huo ulijikita katika maeneo matatu makubwa.

Alitaja eneo la kwanza kuwa ni kwenye vituo vya afya  ambavyo walikuwa wakivisaidia kwa kutoa unga wa lishe ambao ulitumika kwa ajili ya kuondoa udumavu pamoja na kutibu udumavu kwa watoto walio chini ya miaka miwili.

"Pia tulikuwa tukitoa elimu ya lishe katika vituo hivyo vya afya, upimaji na ushauri wa masuala ya lishe." alisema Shosho.

Shosho alisema kuwa mradi huo haujaishia kwenye vituo hivyo vya afya pekee pia upo kwenye ngazi ya jamii ambapo kwenye mikoa hiyo miwili kuna vijiji 124 ambavyo vimefikiwa na shughuli mbalimbali za lishe moja ya shughuli hizo ni elimu ya masuala ya lishe bora.

Alisema jamii imefundishwa juu ya vyakula mchanganyiko, unyonyeshaji kwa watoto na umuhimu wa siku 1000 kuanzia mimba inapotunga hadi mtoto atakapokuwa na miaka miwili.

Aidha Shosho alisema kuwa jamii pia imefundishwa namna ya uzalishaji wa chakula mchanganyiko ambapo mradi huo umewapatia mbegu na kulima vyakula hivyo.

Alisema mbali ya kuwapa mafunzo hayo pia walifundishwa namna ya kufuga wanyama wadogo kama sungura na ufugaji wa kuku.

Alisema jamii pia ilifundishwa namna ya kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa (VICOBA) ambavyo vinawasaidia kuhifadhi fedha zao  na kuongeza chakula chenye lishe kwenye kaya.

Alitaja suala lingine kuwa ni la usafi ambalo ni muhimu sana kwani mtu hawezi akawa na lishe bora bila ya kuwepo na usafi ambapo walifundishwa namna ya kutumia vyoo, unawaji wa mikono na teknolojia nyepesi ya kuwezesha kila kaya kuwa na kinawia mikono 'kibuyu chirizi' ambavyo vipo katika kaya iliyofikiwa na mradi huo.

Alisema pia wamewafusha jinsi ya kupika vyakula mchanganyiko na vya lishe bora kutoka kwenye vyakula asili vilivyopo katika maeneo yao yakiwemo matunda na mboga.

Shosho alitaja suala la mwisho kuwa ni la kuzijengea uwezo halmashauri ili ziweze kusimamia mradi huo baada ya kukabidhiwa kwa kusaidia katika vikao vyao kufuatilia shughuli hizo  ukizingatia miradi hiyo ni yao na ipo chini ya Serikali.

"Tunaomba mradi huu muutunze na kama itawezekana ziundwe sheria ndogo ndogo zitakazosaidia kuutunza ili uendelee kuwanufaisha wana Singida hususani katika halmashauri hizo." alisema Shosho.

Mwakilishi wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Idara ya Afya Kitengo cha Lishe, Mariam Nakuwa aliyashukuru mashirika yote na halmashauri zilizopitiwa na mradi huo na akaahidi juhudi zote ambazo zimewekezwa kwa  miaka mitano hazitapotea bure na kuwa Serikali itaendelea kuratibu na kusimamia masuala yote ya  lishe.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashid Mandoa ameahidi kuyaendeleza mambo yote yaliyofanywa na mashirika hayo kupitia mradi wa Boresha Lishe ambao waliwapa mawazo na wao wamekuwa wanufaika.

Mwenyekiti wa Halmashauri  hiyo, Eliya Digha aliwahimiza wananchi wa Kijiji hicho kulima mahindi yenye rangi ya njano ambayo yanapatika kwenye kijiji hicho cha Seketoure na kuwa yana lishe na bei yake ni kubwa.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Joshua Majengo alisema baada ya kupata mafunzo hayo kupitia mradi huo udumavu na utapiamlo kwa watoto umepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na awali.

WAWEKEZAJI WAIOMBA SERIKALI KUDHIBITI UVAMIZI RANCHI ZA TAIFA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiongea na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fredy Lowassa (kushoto) walipokutana katika kikao kilichoandaliwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kilichofanyika jijini Dodoma jana. Mbunge huyo alikuwa ni miongoni  mwa Wawekezaji waliohudhuria kikao hicho.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Sehemu ya Wawekezaji waliohudhuria kikao kilichoandaliwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) jijini Dodoma jana. 
 



Na Mbaraka Kambona,

 

Wawekezaji wa muda mrefu katika Vitalu vya Ranchi za Taifa wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti uvamizi unaofanywa na baadhi ya Wananchi katika maeneo hayo kwani vitendo hivyo vimekuwa kikwazo kikubwa katika kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini. 

Wawekezaji walisema  hayo kwa Waziri wa Mifugo na  Uvuvi, Mashimba  Ndaki alipokutana nao katika kikao kilichoandaliwa na Kampuni za Ranchi za Taifa (NARCO)  kilichofanyika jijini Dodoma jana. 

Wakieleza changamoto wanazozipata katika uwekezaji wao walisema kuwa pamoja na mambo mengine, suala la Wananchi kuvamia maeneo yao waliyowekeza linakwamisha kufanya shughuli zao za kuendeleza ufugaji wa kisasa. 

Mwenyekiti wa Wawekezaji hao, Jackson Mwasonga alisema kuwa wavamizi wanakwamisha shughuli zao na kuna wakati wanalazimika kutoa hela kwa wavamizi hao ili waweze kuchunga mifugo yao katika maeneo wanayomiliki kihalali. 

"Mhe. Waziri inafika wakati tunatoa hela ili tuweze kuchunga na kunusuru mifugo yetu,uvamizi unatishia maisha yetu na mali zetu, tunaomba mtangaze wavamizi waondoke ili tuweze kufanya ufugaji unaohitajika kwa amani," alisema Mwasonga. 

Projestus Gamasho, Mwekezaji katika Ranchi ya Kitengule, Mkoani Kagera alisema ranchi hiyo kwa sasa imevamiwa na tembo zaidi ya Mia Sita (600) na wameharibu miundombinu yote huku akiiomba Serikali kutoa msaada wa haraka kuwaondoa tembo hao. 

Mwekezaj wa Ranchi ya Uvinza, Kigoma, Benard Katamba  alisema wavamizi katika Ranchi hiyo sio tu wamechukua maeneo yao,  wanaiba mifugo yao kila wakati jambo ambalo linawakatisha tamaa ya kuendelea na ufugaji. 

Sisi Wawekezaji wa Ranchi ya Uvinza tumevamiwa haswa, mpaka sasa nimeshaibiwa ng'ombe 25 na mbuzi 150 na sina matumaini yoyote ya kuwapata, kwa kweli tunaomba msaada wa Serikali," alisema Katamba. 

Kufuatia hali hiyo, Mwekezaji katika Ranchi ya Misenyi, Mkoani Kagera, Nestory Lugakingira akitoa ushauri kwa Serikali alisema kuwa ili waweze kuishi kwa amani Serikali ione uwezekano katika yale maeneo yaliyovamiwa yagawiwe kwa wavamizi hao na sehemu itakayobaki waitumie kuendeleza mifugo yao na kuepuka migogoro na wananchi hao. 

Akitoa ufafanuzi wa hoja za Wawekezaji hao, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema kuwa Serikali ipo pamoja na Wawekezaji hao na itachukua hatua kali kwa wale wote wanaovamia maeneo ya ranchi kinyume na Sheria. 

"Ninaelewa kwamba kuna maeneo ambayo Wananchi wanakaa na kuwaondoa itakuwa ni uvunjifu wa haki za binadamu, maeneo hayo tutayainisha na ili tuone kama tunataka kuendelea nayo au tukubali  maeneo hayo yawe na matumizi mengine," alisema Ndaki. 

Aidha, Ndaki alitumia fursa hiyo kuwahimiza Wawekezaji hao kuyatumia maeneo waliyowekeza kwa malengo yaliyokusudiwa huku akisema kuna baadhi ya Wawekezaji wamekuwa hawayatumii vizuri maeneo hayo jambo lililopelekea kuvamiwa. 

"Niwaombe kuanzia sasa mkayatumie maeneo hayo kwa malengo yaliyokusudiwa, mkafanye ufugaji wa kibiashara, mkifanya hivyo mtaweza kuainisha vizuri gharama za matumizi na faida mnayopata," alisisitiza Ndaki. 

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya NARCO, Paul Kimiti  alisema uvamizi unaoendelea unawaumiza Wawekezaji  na kuwakatisha tamaa huku akiiomba Serikali kuchukua hatua kudhibiti vitendo hivyo. 

Naiomba Serikali kuangalia uwezekano wa NARCO kuwa na Askari kama TANAPA, naamini watasaidia kudhibiti uvamizi huu kabla haujashamiri, na vitendo hivyo vitakoma," alisema Kimiti 

Lengo la kikao hicho kilichoandaliwa na NARCO ni kuongea na Wawekezaji hao kuhusu Tozo mpya ya pango ya kitalu itakayoanza kufanyakazi Julai 1, 2021 na kuwahimiza kuhuisha mikataba yao.


Saturday, May 29, 2021

WAZEE SINGIDA WAMPOKEA RASMI RC MAHENGE, WAAHIDI KUMPA USHIRIKIANO

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge, akizungumza na Wazee wa Manispaa ya Singida   kwa mara ya kwanza tangu ahamishiwe akitokea mkoani Dodoma katika kikao kilicho fanyika leo. Kulia ni .Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Wilaya  ya Singida, Ramadhan Maughu na kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi,akizungumza kwenye kikao hicho.


Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Wilaya  ya Singida, Ramadhan Maughu akizungumza kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Shabani Mkata, akizungumza kwenye kikao hicho. 
Kikao kikiendelea.
Baadhi ya Watumishi wa Manispaa ya Singida wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Mzee Shabani Mwangi, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mzee aliye jitambulisha kwa jina moja la Duki, akichangia jambo kwenye kikao hicho.



 Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida.


BARAZA la Wazee Mkoa wa Singida limempokea rasmi Mkuu mpya wa Mkoa, Dkt. Binilith Mahenge na kuahidi kumpa kila aina ya ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Dkt. Mahenge ambaye kabla ya hapo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma aliteuliwa na kuapishwa hivi karibuni kushika wadhifa huo kuchukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amestaafu.

Akizungumza na baraza hilo mkoani hapa, Dkt. Mahenge aliwaomba wazee hao kumpa ushirikiano ili kwa pamoja aweze kuongoza kwa ufanisi jahazi hilo lenye shabaha ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mageuzi ya kiuchumi ndani ya mkoa.

"Singida ina kila kitu chema. Tuna Hali ya hewa nzuri inayokubali kila aina ya mazao...alizeti, ufuta, dengu, korosho na tunafuga sana, lakini zaidi tuna viwanda vya kutosha vya kukamua mafuta ya zao la alizeti," alisema Mkuu wa Mkoa.

Alihimiza kila mtu kwa nafasi yake likiwemo kundi la vijana, watendaji na wananchi wote kuwajibika kwa kuchapa kazi ili kupunguza au kuondoa kabisa adha ya umasikini.

Dkt. Mahenge pamoja na kumshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumkabidhi mkoa huo kikubwa alisisitiza ushirikiano hususani kwenye nyanja ya kuinua sekta ya kilimo-na hasa zao la alizeti.

Alisema anatarajia kuona mtazamo chanya katika mageuzi makubwa ya kilimo cha alizeti katika muktadha wa kuleta utajiri kwa kila mtu, kaya, jamii,  lakini pia kuigeuza Singida kuwa kimbilio la soko kama sehemu ya jitihada zilizopo katika kukabiliana na changamoto ya kitaifa ya uhaba wa mafuta ya kula.

Akieleza hali halisi ya zao hilo mkoani hapa kwa sasa, alisema changamoto kubwa inayokwamisha ustawi wake kwanza ni uhaba wa mbegu bora, lakini pia wakulima wengi wamekosa utaalamu stahiki kujua kanuni za kilimo chake.

Mahenge alisema kwa ushirikiano na watendaji wake waliopo watahakikisha wanaongeza nguvu katika eneo hilo na lingine la kutoa utambuzi kwa mkulima kumuwezesha kufanya Uchaguzi sahihi wa mbegu zinazotoa kiwango cha juu cha mafuta na zinazohimili magonjwa yatokanayo na visumbufu vya wadudu.

Katika hilo, mkakati mwingine uliopo ndani ya ofisi yake kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Taasisi mbalimbali za kilimo ni kuhakikisha mbegu hizo zinaanza kupatikana kwa wingi na kuwafikia wakulima kwa gharama nafuu.

"Tatizo lililopo ukilinganisha na mazao mengine alizeti haina Bodi ya uratibu na usimamizi ndio mana hata kasi ya ukuaji wake haiendi kwa ufanisi," alisema Dkt. Mahenge na akaongeza;

"Wakulima wengi wanapopeleka zao hili sokoni wanaonekana kama wamepunjwa sababu kubwa ni mbegu kukosa sifa na ubora wa kutoa mafuta mengi." 

Alisema, mathalani, mbegu bora ya alizeti ijulikanayo kama Hysun 33 ambayo hukomaa kati ya siku 90 na 110 kwa uwezo wa kutoa gunia 16 hadi 22 kwa heka, sawa na uwiano wa lita 29 hadi 31 bei yake bado ipo juu na wakulima wengi wanashindwa kumudu.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo uliobeba hotuba hiyo iliyoashiria mikakati, matarajio na mwelekeo wa vipaumbele kadhaa kwa niaba ya wazee, Mwenyekiti wa Baraza hilo Ramadhan Maughu alimhakikishia Mkuu wa Mkoa ushirikiano wa hali ya juu katika azma iliyopo ya kubadilii sura ya kiuchumi ya mkoa.

""Karibu sana Singida wazee wote mbele yako wamekukubali na wamekupokea tutakupa kila aina ya ushirikiano, mana hatukuzoea wala kuwahi kuitwa na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa yeyote..kwa utambuzi huu inaonyesha umelelewa vizuri," alisema Mwenyekiti huyo.

Friday, May 28, 2021

RC MAHENGE AJILIPUA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO KUBWA YA MBEGU ZA ALIZETI SINGIDA, ATOA MWELEKEO WA SINGIDA MPYA AKIZUNGUMZA NA VIONGOZI WA DINI

 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge, akizungumza na viongozi wa dini mkoani hapa  kwa mara ya kwanza tangu ahamishiwe akitokea mkoani Dodoma katika kikao kilicho fanyika leo Kulia ni .Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi  Pascas Muragili na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi.
Padre Thomas Mangi wa Kanisa Katoliki (RC)
Viongozi wa dini wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea..
Kikao kikiendelea.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye kikao hicho.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waisalaamu (BAKWATA)  Manispaa ya Singida, Hamisi Kisuke, akizungumza kwenye kikao hicho.


Kaimu Sheikhe wa  Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akizungumza kwenye kikao hicho.
Katibu wa Baraza Kuu la Waisalaamu (BAKWATA)  Mkoa wa Singida, Sheikhe, Burhani Mlau, akizungumza kwenye kikao hicho.

Mchungaji Wilson Mkoma kuoka Kanisa la EAGT, akizungumza kwenye kikao hicho.
Jaji Mstaafu, Fatuma Masengi,akizungumza kwenye kikao hicho.
Kasisi Joseph Kense wa Kanisa la Anglikana, akizungumza kwenye kikao hicho.
Abdurahaman Hassan Naibu Amri wa Mkoa Jamaat Ansaari Sunna, akizungumza kwenye kikao hicho.


 

Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida.



MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Dini mbalimbali, ambapo pamoja na kuwaomba ushirikiano, alitumia jukwaa hilo kueleza mipango, mikakati na mwelekeo wa singida mpya katika muktadha chanya wa maendeleo.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika ofisini kwake mkoani hapa, Dkt. Mahenge pamoja na mambo mengine, aliwataka viongozi hao wa dini kumpa ushirikiano wa kutosha hususani kwenye eneo la kuongeza tija ya kilimo cha alizeti ili kuokoa fedha nyingi zinazotumiwa na serikali kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

"Nadhani tuanze na mkakati wa haraka wa kushusha gharama ya mbegu ya alizeti. Mbegu zinazozaa vizuri na kutoa mafuta mengi bei yake haikamatiki ipo juu sana," alisema Mkuu wa Mkoa.

Akifafanua hilo, alisema kama serikali na wadau watashirikiana katika kushusha gharama ya mbegu hiyo basi ni dhahiri mkoa huo ambao jiografia yake ni rafiki kwa zao hilo itakuwa ni jawabu la kupunguza au kumaliza kabisa changamoto iliyopo ya upungufu wa mafuta ya kula.

Alisema kwa sasa nchi inaagiza takribani Tani laki 5 za mafuta ya kula kila mwaka jambo linalogharimu na kuleta mtikisiko wa uchumi, na alisisitiza katika kuepusha hilo lisiendelee mkoa wa Singida haukwepeki.

"Naomba viongozi wangu wa dini mtuunge mkono nguvu kubwa ielekezwe kwenye ongezeko la uzalishaji wa alizeti,..sababu soko la mafuta ya kula ni la uhakika, na viwanda tunavyo vya kutosha. Suala la hii changamoto ya mbegu na agronomia tunaendelea kushughulika nayo kama mkoa ili kuwezesha viwanda kuwa na malighafi ya kutosha," alisema Dkt. Mahenge.

Hata hivyo alipongeza juhudi kubwa za aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Rehema Nchimbi kwa namna alivyosimamia uzalishaji wa zao la korosho na ameahidi kuendeleza zaidi zao hilo kwa ustawi wa uchumi wa wana-singida.

Katika hilo, Mkuu huyo wa Mkoa alihamasisha jamii kujenga utamaduni wa kula vyakula vinavyozalishwa ndani ya nchi ikiwemo korosho, dengu na ufuta ili kupanua zaidi wigo wa soko la ndani kuliko kutegemea soko la nje.

Awali, wakichangia hotuba yake kwa nyakati tofauti, mbali ya kupongeza mkakati mzuri wa serikali uliopo, hususani kwenye eneo la ongezeko la tija ya zao la alizeti, jukwaa hilo lilimsihi Dkt. Mahenge kuweka mkazo katika kuimarisha huduma za afya, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, ukosefu wa dawa hospitalini, sanjari na kupandisha zaidi ufaulu kwenye sekta ya elimu.

Aidha, walimtaka aharakishe umaliziaji wa miradi ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa iliyopo, Stendi Kuu ya abiria, umeme, maji na miundombinu ya barabara ambayo kasi yake sio ya kuridhisha na imegeuka kero kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine, walimtaka afuatilie serikalini kujua nini hasa kimekwamisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege Singida, mkoa ambao ni wa kimkakati na upo jirani zaidi na makao makuu ya nchi huku tayari hatua za usanifu na upembuzi yakinifu kabla ya kuanza ujenzi wa Uwanja huo vilikwishafanyika.