Tuesday, August 31, 2021

PROF. LUGHANO KUSILUKA ATEULIWA KUWA MWENYEKITI WA BARAZA LA VETERINARI TANZANIA

Profesa Lughano Kusiluka Mwenyekiti Mpya Baraza la Veterinari Tanzania.


Na Mwandishi Wetu 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemteua Profesa. Lughano Kusiluka kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Veterinari Tanzania.

Profesa Kusiluka ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anachukua nafasi hiyo iliyokuwa inashikiliwa na Profesa. Rudovick Kazwala ambaye muda wake umeisha.

Uteuzi huo utaanza rasmi kesho Septemba 1, 2021 kwa kipindi cha miaka minne (4).

 

WAHUDUMU WA AFYA SINGIDA KUTEMBEA NYUMBA KWA NYUMBA KUONDOA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith  Mahenge akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Wataalam wa afya wa Mkoa wa Singida kilichokuwa kinajadili tathmini na vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga kilichofanyika katika Ukumbi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni  mkoani Singida leo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick akizungumza kwenye kikao hicho.
 


Na Mwandishi Wetu, Manyoni.


WATOA huduma za afya katika ngazi za kata na vijiji wametakiwa kutembelea nyumba kwa nyumba ili kuwatambua mama wajawazito na watoto walioko maeneo hayo ili kuwapatia ushauri wa kiafya kwa kuwa hao ndio wateja wao.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith  Mahenge ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akifungua kikao kazi cha Wataalam wa afya wa Mkoa wa Singida kilichokuwa kinajadili tathmini na vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga kilichofanyika katika ukumbi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni  mkoani Singida.

Akifungua kikako hicho Dkt. Mahenge alisema kwamba bado kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza au kuondoa vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi pamoja na watoto wachanga endapo wataalamu wa afya ngazi ya kata na vijiji watatembelea nyumba kwa nyumba kuangalia uwepo wa watu hao na kuwapatia ushauri wa kwenda hospitali kwa wakati na kutumia lishe bora kwa afya ya mama na mtoto.

“Kutembelea  nyumba kwa nyumba kutasaidia kujua  idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya afya na ushauri katika eno husika, hii inatokana na ukweli kwamba wanawake wengi huchelewa kuanza kiliniki pindi wanapokuwa wajawazito na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua” alikaririwa Dkt. Mahenge.

Alisema Serikali  ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kujenga miundombinu wezeshi kwa sekta ya afya  ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti na idadi ya watumishi katika sekta hiyo ili kusogeza huduma na elimu ya afya  kwa wanachi.

Alisema ujenzi na uboreshwaji wa vituo vya afya ni mkakati wa Serikali wa kuondoa changamoto ya vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga.

Hata hivyo Dkt. Mahenge amebainisha kwamba  jumla ya vituo vya afya 15 na hospitali tatu (3) zimejengwa mkoani hapo ili kusaidia utoaji wa  huduma za dharura  kwa wazazi na watoto.

Aidha Mahenge amezitaka Halmashauri mkoani hapo kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kutolea huduma ya afya vinakuwa na mikakati ya kupunguza au kuondoa  vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi pamoja na changamoto ya vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika.

Pia amezitaka Halmashauri kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kutoka MSD na kwa mshitiri  hasa kwa bidhaa za mama na mtoto kama vile vifaa tiba vya kupimia wingi wa damu, kuhakikisha uwepo wa dawa za kuongeza damu katika vituo vyote pamoja na dawa  muhimu za kuzuia damu kutoka baada ya kujifungua na matibabu mengine muhimu katika kundi hili.

Awali Mganga Mkuu wa Mkoa Victorina Ludovick alisema lengo la kikao kazi hicho ni kujadili na kutathmini vifo vya kinamama vilivyosababishwa na uzazi vilivyotokea kwa muda wa miezi mitatu ya April hadi Juni 2021 ambapo kikao hicho kitatoa  suluhisho la namna ya kuzuia hali hiyo isiweze kujirudia.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kinategemewa kutoa mrejesho wa matukio kadhaa ya vifo vilivyojitokeza na kujadili mipango kazi ya Halmashuari  hizi kwa kipindi cha miezi mitatu na kuchukua hatua stahiki za kuboresha maeneo yenye changamoto, alisema Dkt.Victorina.

Aidha alibainisha kwamba bado kuna changamoto ya jamii yetu kwenye kupanga uzazi na pia vijana kupata  mimba wakiwa katika umri mdogo ambapo wengi wao hupoteza  maisha kwa kutokwa na damu vyingi wakati wa kujifungua. “Bado tuna changamoto ya ukusanyaji wa damu salama ambayo hutumika kuwasaidia kinamama na watoto wanapokuwa na uhitaji”. alisema Victorina.

Dkt. Victorina amewaomba wananchi wa mkoa huo kuendelea kuchangia damu ili iweze kuwasaidia wenye uhitaji.

Hata hivyo Mganga Mkuu amewataka wahudumu wa afya kuendelea kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wananchi kwa kuwa itawezesha kuwa na uzazi salama na pia ina mchango mkubwa katika kuzuia vifo vya kinamama vinavyosababishwa na uzazi.

Naye Emanueli Mlalange  Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Itigi na Mwenyekiti wa Waganga wakuu wa mkoa huo kwa niaba ya waganga  hao ameishukuru serikali kwa jitihada zake za kuongeza watumishi mkoani hapo na kuimarisha utoaji wa dawa katika vituo vya afya.

Aidha amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba madaktari watajitahidi kuhakikisha kwamba vifo vya kinamama na watoto wachanga vinapungua.

Monday, August 30, 2021

MHE. BASHUNGWA AWAPIGANIA WANAMICHEZO KUPATIWA CHANJO DAR

 

Waziri  wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa akizungumza

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa aliyevalia jezi ya timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) katikati  akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa mpira wa soka na wachezaji wa timu za taifa za wanawake (Twiga Stars na Tanzanite) alipowatembelea wakiwa mazoezini katika viwanja vya  Kidongo chekundu maarufu kama  JK Park jijini Dar es Salaam.


Na John Mapepele, WHUSM

 

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya leo Agosti 28, 2021 imeratibu zoezi la hiari la siku mbili kwa timu za Taifa za michezo na wadau wote wa michezo upatiwa chanjo ya Uviko-19 jijini Dar es Salaam ili kujikinga na ugonjwa huo.

 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa amesema makundi hayo yamependekezwa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia, pamoja na mambo mengine, umuhimu wao kwa jamii na ukweli kwamba kwa mazingira ya kazi zao, wako katika hatari ya kuambukizwa.

 

“Ninapenda tena leo kuendelea kusisitiza na kuhamasisha wanahabari, wanautamaduni, wasanii na wanamichezo wenzangu kuendelea kupata huduma ya chanjo. Sekta zetu zinahudumia wananchi na hivyo kulazimika kukutana na makundi ya watu mara kwa mara. Kutokana na hivyo tuna hatari kubwa ya kuambukizwa, ama sisi wenyenyewe au kuambukiza wananchi ambao ndio wadau wetu wakubwa tunaowapa huduma. Kwa vyovyote vile ni lazima tujikinge lakini pia tuwakinge wadau wetu”. Amefafanua  Mhe. Bashungwa

 

Amesema ili kufanikisha zoezi hilo vimefunguliwa vituo maalum ndani ya uwanja wa Mkapa na Uhuru vitakavyokuwa vikitoa huduma ya chanjo hiyo kuanzia saa 3 asubuhi kwa siku zote mbili  ili kutoa fursa kwa wadau wote kupata huduma ya chanjo.

 

Ameushukuru Uongozi wa Klabu ya Simba kwa kuwapa chanjo wachezaji wao.

Aidha, amepongeza Klabu ya Yanga ya kutumia wiki yao ya wananchi kuhamasisha na kupata chanjo na kulifanya zoezi hilo la uchanjaji kuwa miongoni mwa shughuli zao muhimu watakazo zifanya siku hiyo ambapo pia ametoa wito kwa vilabu vingine vya soka nchini kuhamasika na kuwapatia chanjo wachezaji na watumishi wao.

Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusuph Singo Omary amemhakikishia  Mhe. Waziri kuwa maandalizi yote ya zoezi la chanjo yamekamilika na tayari wadau mbalimbali wa michezo wamepongeza hatua ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea kuwapa kipaombele wadau ili wajikinge.

Ametoa wito kwa Wasanii, Wanahabari na Wachezaji kwa hiari yao kujitokeza na kutumia fursa hii kipata chanjo ili kujikinga na kuwakinga wengine na ugonjwa wa UVIKO 19

WAZIRI MKUU AZINDUA MRADI WA MAJENGO MAPYA YA JESHI LA POLISI MKOA WA SINGIDA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili kushoto) akikata utepe kuzindua jengo jipya la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida leo. Wengine kutoka kushoto ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ASP) Stella Rutabihirwa, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Siro, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Christopher Kadio. (Picha zote  Dotto Mwaibale na Godwin Myovela)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizindua jengo jipya la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida.
Muonekano wa jengo hilo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili kulia) akikata utepe kuzindua jengo la Kikosi cha Kutuliza Ghasia  (FFU) Mkoa wa Singida. Wengine kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Siro, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ASP) Stella Rutabihirwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea Salamu ya Mkuu iliyoambatana na Wimbo wa Taifa kutoka 'Mounted Guard' ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia  (FFU) Mkoa wa Singida muda mfupi alipowasili Makao Makuu ya Kikosi hicho mkoani hapa kwa shughuli ya kuzindua moja ya jengo lake.


Muonekano ya jengo jipya la FFU Mkoa wa Singida.

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Hayupo pichani) akipokea salamu kutoka Kikosi cha Kutuliza Ghasia  (FFU) Mkoa wa Singida alipowasili kwa shughuli ya kuzindua moja ya jengo jipya la kikosi hicho.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akikagua mradi wa jengo la FFU Singida muda mfupi kabla ya kulizindua.

Askari wa FFU wakiwa kwenye maandalizi ya kumpokea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kabla ya kuwasili kuzindua jengo jipya la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida.

Afisa Mwandamizi kutoka Kampuni ya Biosustain mkoani Singida Abdulazizi Chaudhry na Wadau wengine mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi huo. 
Wakuu wa Wilaya wakiwa kwenye uzinduzi huo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagesa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye hafla hiyo. Kushoto ni Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida Diana Chilolo akiteta jambo na Mbunge wa Manyoni Mashariki Dkt.Pius Chaya.
 

Sunday, August 29, 2021

MAADHIMISHO YA KIMATAIFA YA MUZIKI DUNIANI KUZINDULIWA RASMI JIJINI ARUSHA.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel. 


Dotto Mwaibale, Arusha  


WANAMUZIKI wa Watanzania wanatarajia kuanza Maadhimisho ya Kimataifa  ya Muziki Duniani yatakayo zinduliwa rasmi kesho kutwa Septemba 1, 2021 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel alisema kesho kutwa yatazinduliwa rasmi maadhimisho hayo na kuwa mwezi Septemba wote Wanamuziki wa kada zote watashiriki kuhamasisha shughuli mbalimbali za  maendeleo.

"Kwa Dar es salaam Wanamuziki watakutana Makumbusho ya Taifa iliyopo Posta kuanzia Saa 4 asubuhi ambao watakuwa na jumbe mbalimbali za Kuhamasisha maendeleo ya muziki na kushiriki shughuli za ujenzi wa Taifa," alisema Joel.

Joel alisema kwa upande wa Arusha Wanamuziki watakutana katika Makumbusho ya Taifa na kwa Mkoa wa Mwanza  watakutana na Kufanya ziara ya Utalii wa Ndani na  kujionea vivutio vya utalii wa nchi yetu na kukitangaza Kisiwa cha Sanaane.

Alisema wamechagua Jiji la Arusha kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa maadhimisho hayo  Kimataifa kwa sababu Mkoa wa Arusha upo katikati ya Afrika pia una Historia kubwa ya nchi yetu ambapo Mhasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere alianzisha Azimio la Arusha katika mkoa huo na alitembea kwa miguu na viongozi wengine kuunga azimio hilo na kuwa  Arusha ndipo kilipo kiti na mti wa Mwalimu  Nyerere.

Alisema kesho kutwa Wanamuziki watakutana Makumbusho ya Azimio la Arusha kuanzia Saa 4 asubuhi na kuhamasisha shughuli za maendeleo na kufanya Utalii wa Utamaduni katika jiji la Arusha.

Joel alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanamuziki wote katika maeneo hayo kujitokeza kwa wingi ili kukamilisha jambo hilo.

MPANGO WA USIMAMIZI WA MAZINGIRA WILAYA ZA SINGIDA MBIONI KUKAMILIKA

Mratibu wa Sera kutoka Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM), Paul Chilewa, akizungumza katika kikao kilicho wakutanisha wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Kilimo, TAMISEMI, na Mashirika ya kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM, GIZ na Helvetas), ambacho kilifanyika juzi mkoani hapa lengo likiwa ni kutathmini na kuweka mikakati ya kuhakikisha ajenda ya 'Kilimo Himilivu' na 'Mabadiliko ya Tabianchi' vinaingizwa katika Mpango wa Mazingira wa miaka mitano ndani ya halmashauri za wilaya za Singida.

Washiriki wakiwa kwenye kikao hicho.

Mratibu wa Mradi wa Kilimo Himilivu cha Pamba kutoka GIZ kwa mkoa wa Singida, Leonard Mtama, akichangia jambo kwenye kikao hicho.

Kikao kikiendelea.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Mkalama,  Seleman Musunga, akizungumza kwenye kikao hicho.
Afisa Mazingira kutoka Wilaya ya Iramba, Yohana Dondi,akizungumza kwenye kikao hicho.

Washiriki wa kikao hicho wakiwa katika picha ya pamoja,




Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida.


WATAALAMU mbalimbali wamekutana kutathmini na kuweka mikakati ya kuhakikisha ajenda ya 'Kilimo Himilivu' na 'Mabadiliko ya Tabianchi' vinaingizwa katika Mpango wa Mazingira wa miaka mitano ndani ya halmashauri za wilaya za Singida ili kuwezesha kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kuongeza tija katika kilimo.

Kupitia kikao hicho wataalam hao kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Kilimo, TAMISEMI, na Mashirika ya kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM, GIZ na Helvetas), pamoja na mambo mengine, walijikita katika kuziwezesha halmashauri mkoani hapa kutengeneza mipango inayoweza kuratibu na kusimamia uharibifu wa mazingira kwenye maeneo yao.

Mratibu wa Sera kutoka Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai nchini (TOAM), Paul Chilewa, alisema wamekutanisha  wilaya nne za Manyoni, Ikungi, Iramba na Mkalama ndani ya mkoa wa Singida ili kuzisaidia kitaalamu kutengeneza mipango hiyo ambayo inakwenda kuanza kutumika katika kipindi cha miaka 5.

Alisema lengo la TOAM ni kuhakikisha kwenye mpango huo masuala yote ya Kilimo Himilivu  na Mabadiliko ya Tabianchi yanaingizwa kikamilifu ili kuongeza tija kwenye kilimo katika muktadha chanya wa ongezeko la uzalishaji, ubora na zaidi kuifanya ardhi kuwa endelevu kwa matumizi ya kizazi cha sasa na baadaye.

Chilewa ambaye anatoka kwenye shirika hilo ambalo ni mwamvuli wa mashirika yenye lengo la kuendeleza kilimo hai nchini alisema mathalani kama taifa litajikita kwenye kuzalisha zao la Pamba kwa mfumo wa 'Kilimo Hai' na kuweka sera madhubuti sio tu litapata faida kubwa lakini pia wananchi wote wanaolima zao hili na mengine ya chakula kwenye eneo hilo watakuwa na uhakika wa kupata ithibati ya kuuza mazao yao kwenye soko la dunia kutokana na matokeo ya ubora wake.

"Uzalishaji wa pamba ya kilimo hai kwenye maeneo mengine duniani zikiwemo nchi za Afghanistan na India kwasasa kuna changamoto,  hivyo kama tutazalisha pamba hii (Organic Cotton) tutapata faida kutokana na kuwa na mahitaji makubwa kwenye soko," alieleza Chilewa.

Alisema lengo la kikao hicho, pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha kunakuwa na mkakati ambao utahakikisha kilimo kinazingatia taratibu zote za kilimo himilivu kwenye mabadiliko ya tabianchi.

"Hapa tupo kimkoa lakini TOAM kwa kushirikiana na wenzetu GIZ Tanzania, Helvetas na wadau wengine ndani ya wilaya hizi za mkoa wa Singida tunataka kuzisaidia halmashauri kutengeneza mpango huu na kuchukua hatua ya kuwa na miradi mbadala ikiwemo kupanda miti na kuanzisha mashamba darasa ya kujifunzia hizi teknolojia kwa ustawi na tija," anasema.

Hata hivyo Chilewa alishauri kuangalia baadhi ya teknolojia na shughuli nyingine za kibinadamu zinazotumika katika kilimo hususani suala la matumizi makubwa ya mbolea za viwandani ambayo kwa kiasi kikubwa zinachangia kufanya mazingira yasiwe himilivu.

Katika hilo, alisema Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa wingi wa mifugo, lakini kitu cha kushangaza wakulima wake walio wengi hawatumii hizo mbolea za mifugo hususani ng'ombe katika kurutubisha ardhi.

Alisema hata zile teknolojia na aina nyingine za mbolea ambazo zinaweza kurutubisha ardhi kwa kiwango cha kutoathiri- kwa maana ya kuifanya ardhi iendelee kuishi na kuzalisha nazo bado hazitiliwi mkazo wala kutumika ipasavyo.

Chilewa zaidi aliainisha baadhi ya viashiria vya uharibifu huo wa mazingira kuwa ni pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya maji, wingi wa mifugo isiyozingatia tija, ukataji miti hovyo na uchomaji mkaa sambamba na matumizi makubwa ya viuatilifu ambavyo vina athari kwa udongo na afya za watu

"Hivyo kusanyiko la wadau na wataalamu hawa linalenga kutengeneza mpango wa miaka 5 utakaojibu changamoto hizi kwa kizazi cha sasa na kijacho katika muktadha wa kuwa na ufugaji endelevu na kilimo endelevu ambavyo vitazingatia utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi," alisema Chilewa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kilimo Himilivu cha Pamba kutoka GIZ kwa mkoa wa Singida, Leonard Mtama, kupitia kikao hicho anasema lengo lao hasa ni kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

"GIZ tunaratibu tu hizi shughuli kwa pamoja na wenzetu wa TOAM, Helvetas, Tari, Kampuni ya Biosustain, Bodi ya Pamba na wadau wengine, lakini pia tunasimamia uboreshaji wa AMCOS kwa kushirikiana na Chuo cha Ushirika Moshi na tawi lake la Singida," alisema Mtama.

Alisema majukumu mengine ya shirika hilo, pamoja na mambo mengine, ni kuangalia kwa namna gani vikundi vya akinamama kupitia Helvetas vinaweza kujiongezea kipato kwa kuzalisha pamba hai na mazao mengine.

Kwa mujibu wa Mtama jukumu lingine la GIZ ni kuunganisha wazalishaji wadogo waliopo mkoa wa Singida na masoko ya ndani na nje lakini masharti ni kwamba mazao husika yatokane na kilimo hai.

"Hivyo sisi tunaratibu hayo mambo mawili uzalishaji wa mazao ya wakulima yaani pamba hai na mengine ya chakula kama Dengu, Choroko, alizeti na ufuta ili kuhakikisha uzalishaji wake unakuwa wa tija," anasema Mtama.

Katika hatua nyingine, alihimiza kuwa na azma ya pamoja ya kudumisha suala la ushirikiano kwa Idara, Taasisi na wadau wote kwenye kutunza mazingira huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kila mmoja kwa nafasi yake mahali alipo kuchukua hatua katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

"Unapotaka kufuga pia unapaswa kuangalia tija mfano badala ya kufuga ng'ombe 10 wenye kilo 50 kila mmoja ni bora ufuge kisasa ng'ombe mmoja mwenye kilo 500," alisisitiza Mtama.

Naye Afisa Maliasili na Mazingira mkoa wa Singida, Charles Kidua, alisema kama mkoa wamenufaika vilivyo na uwezeshaji wa wataalamu hao katika kutengeneza mipango hiyo ya usimamizi wa mazingira, na anaamini pale itakapoanza kutumika itasaidia kwenye usimamizi thabiti mazingira.

"Kikao hiki kimetuwezesha kutengeneza mipango mtambuka ya usimamizi mzuri wa mazingira kwenye eneo la misitu, kilimo, afya na maeneo mengine mengi kwa kuzingatia suala la mazingira ni jambo mtambuka," alisema Kidua. 

Saturday, August 28, 2021

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA YARIDHISHWA NA MIRADI SINGIDA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheriaya hiyo Najma Murtaza Giga (katikati) akizungumza na Wanachuo cha Ufundi Veta Mkoa wa Singida na wadau wengine baada ya Wajumbe wa kamati hiyo kutembelea chuo hicho jana. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida, Selemani Mwenda na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Jamal  Katundu.

Wajumbe wa kamati hiyo wakipata maelezo walipotembelea karakana ya mitambo mbalimbali chuo cha Veta Singida.
Wajumbe wa kamati hiyo wakinunua bidhaa za wajasiriamali waliowezeshwa na Serikali.
Wajumbe wa kamati hiyo wakipata maelezo walipotembelea banda la Mjasiriamali aliyetengeneza majiko kwa kutumia teknolojia ya udongo na mabati.
Wajumbe wa kamati hiyo wakipata maelezo walipotembelea SabaSaba Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu.
Afisa Vijana Mkoa wa Singida Frederick Ndahani akizungumza na Wanafunzi wa SabaSaba Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu wanaojifunza kushona nguo.
Wanafunzi wa SabaSaba Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu wakiwa kwenye hafla ya kuwapokea wajumbe hao.
Wanafunzi wa SabaSaba Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu wakiwa kwenye hafla ya kuwapokea wajumbe hao.
 Mkuu wa chuo hicho, Fatma Malenga akisoma taarifa ya chuo hicho kwa wajumbe wa kamati hiyo. 
Wanafunzi wa Chuo cha FDC wakiwa kwenye hafla ya kuwapokea wajumbe hao.
Wajumbe wa kamati hiyo wakitoka kukagua jengo la TEHAMA la Chuo cha FDC.
Wajumbe wa kamati hiyo wakikagua Ofisi ya  Udhibiti Ubora wa Shule Manispaa ya Singida.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida

 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imekagua na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya vijana iliyopo mkoani hapa.

Wakati huo huo Wajumbe wa kamati hiyo wamewataka vijana kuchangamkia fursa ya program ya kukuza ujuzi kwa vijana inayofadhiliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwani itawakomboa kiuchumi.

Ombi hilo limetolewa jana kwa nyakati tofauti na wajumbe wa kamati hiyo wakati wa ziara yao ya siku moja ya kukagua miradi ya maendeleo ya vijana iliyopo Manispaa ya Singida.

Wajumbe hao waliwasihi vijana hao kujikita zaidi kwenye mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kujiajiri na kuondokana na dhana ya kutaka kuajiriwa.

 Mafunzo wanayojifunza ni ya fani za umeme, ushonaji nguo, mapambo,useremala,ujenzi na kupaka rangi.

Miradi waliyoitembelea ni  ile ya vijana waliowezeshwa na Serikali  kupitia asilimia nne  ya mapato ya ndani.

Awali akitoa neno la utangulizi  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,Vijana na Watu Wenye Ulemavu,  Profesa Jamal  Katundu alisema nia ya kamati hiyo kwenda Singida ni kutokana na kazi nzuri ya miradi walioifanya kwa asilimia 100 na kupitishwa bila ya kukataliwa kufuatia usimamizi mzuri wa vikundi vya vijana mkoani hapa.

Katika ziara hiyo wajumbe hao walipata fursa ya kuzungumza na vijana wanaopata mafunzo mbalimbali ya ufundi katika vyuo vya Veta, FDC, na SabaSaba Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu Wenye Ulemavu  ambapo pia walitembelea miradi yote iliyozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru na kukagua bidhaa za vijana hao kwenye Maonyesho yaliyofanyika Chuo cha Veta yaliyo andaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliokuwa kwenye ziara hiyo ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu Profesa Jamal  Katundu na Mwenyekiti wa kamati hiyo Najma Murtaza Giga.

WAZAZI WAHIMIZWA KUZINGATIA LISHE BORA KWA WATOTO

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Juma Irando (katikati) pamoja na Katibu wa Chama cha Ushirika cha Wanawake, Nronga, Hellen Ussiri kwa pamoja wakinywa maziwa ikiwa ni ishara ya kuzindua Awamu ya Pili ya Unywaji wa maziwa Shuleni katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro jana.
Msajili wa Bodi ya Maziwa Dkt.George Msalya akizungumzia maendeleo ya tasnia ya maziwa kwenye uzinduzi huo.
    Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mmoja wa Maafisa wa Chama cha Ushirika cha Wanawake Nronga akigawa maziwa kwa Wanafunzi.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Asimwe Rwiguza (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa majokofu kwa wafanyabiashara.


Na Mbaraka Kambona, Kilimanjaro


WAZAZI nchini wamehimizwa kuweka mkazo katika kuwapatia watoto wao lishe bora ikiwemo kuhakikisha wanakunywa maziwa kila wakati ili kuwafanya wawe na afya nzuri itakayowasaidia kufanya vizuri katika masomo yao. 

Rai hiyo ilitolewa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Asimwe Rwiguza wakati akizindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Unywaji Maziwa Shuleni uliyofanyika Mkoani Kilimanjaro Agosti 27, 2021.

Wakati akizindua kampeni hiyo Dkt. Rwiguza alisema kuwa jukumu la lishe lipo mikononi mwa wazazi hivyo ni muhimu wakajitahidi kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kugharamia lishe ya watoto  wao.

"Natoa wito kwa wazazi wote nchini kuona umuhimu wa kuwapa maziwa watoto,  faida za unywaji wa maziwa kwa watoto zinafahamika sitaki kuzirudia hapa, maziwa yatawajenga, watakuwa na akili na kuwasaidia kufanya vizuri katika masomo yao," alisema Dkt. Rwiguza.

Aliongeza kuwa uzinduzi huo wa awamu ya pili uwe chachu kwa jamii kuhakikisha watoto wao wanakunywa maziwa ya kutosha na zile changamoto zilizoonekana wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika awamu ya kwanza zishughulikiwe ili mafanikio yaweze kupatikana.

Naye,  Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dkt. George Msalya alisema kuwa kufuatia uzinduzi wa kampeni hiyo ni muhimu sasa kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa maziwa ili kufanya maziwa hayo kupatikana kwa wingi na wakati wote hatua ambayo itawawezesha wawekezaji  kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.

"Maziwa yanayoingia katika mfumo rasmi wa uchakataji katika Viwanda vyetu ni chini ya asilimia 3 ya maziwa yote yanayozalishwa hapa nchini, hiyo ni asilimia ndogo ukilinganisha na nchi za wenzetu, hivyo ni muhimu kuhamasisha wawekezaji ili kukuza tasnia hii ya maziwa nchini," alisema Dkt. Msalya.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Ushirika cha Wanawake, Nronga, kinachojishughulisha na uchakataji wa Maziwa Mkoani Kilimanjaro, Hellen Ussiri alisema kuwa baada ya Serikali kutoa tamko la uhamasishaji wa unywaji wa maziwa shule bado kumekuwa na mwamko mdogo hivyo Chama hicho kimefanya jitihada za kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni.

"Kiwanda cha Nronga kitasambaza maziwa kwa shule 10  za msingi zilizopo katika Wilaya ya Hai zenye jumla ya Wanafunzi 6151 ili kuendelea kutoa hamasa ya Unywaji wa maziwa kwa watoto," alisema Ussiri.

Aidha, alitoa rai kwa wadau mbalimbali wa biashara  pamoja na wazazi kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizo ili walau adhma ya kuwapatia watoto wa shule maziwa mara mbili kwa wiki iweze kufanikiwa. 

Friday, August 27, 2021

SHIRIKA LA POSTA MKOANI SINGIDA LAFUNGUA PAZIA MASHINDANO MBALIMBALI KUELEKEA KILELE CHA SIKU YA POSTA OKTOBA 9, 2021

Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Singida, Joseph Mutatina akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi kompyuta tano zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Singida Mussa Sima kwa ajili ya Shule ya Msingi Nyerere mjini hapa jana.


Diwani wa Kata ya Mghanga Manispaa ya Singida, Vellerian Kimambo akizungumza wakati akikabidhi kompyuta hizo.

Wanafunzi wa shule hiyo wakiwa kwenye hafla ya kukabidhiwa kompyuta hizo.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Charles Ngowi akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Kata ya Mghanga, Issa Mwanja akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Hamisi Karage akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Makabidhiano ya kompyuta hizo yakifanyika.


Viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule hiyo baadaya hafla hiyo.

Walimu wa shule hiyo, wazazi, pamoja na viongozi mbalimbali wakiwa katika picha yapamoja baada ya kumpokea msaada wa kompyuta hizo.

.

Na Godwin Myovela, Singida.

SHIRIKA la Posta nchini kupitia Ofisi yake ya Mkoa wa Singida limetangaza mashindano mbalimbali yatakayojikita katika kuonyesha ubunifu wa matumizi ya Tehama katika muktadha wa matumizi ya kidijitali kuelekea kilele cha Siku ya Posta Duniani itakayoadhimishwa Oktoba 9, 2021.

Pamoja na mambo mengine, Shirika hilo limeandaa mashindano ya uandishi wa barua kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, wabunifu bora wa TEHAMA, uandishi wa Makala Kwa Wanahabari, uandishi wa Insha kwa Wasanii na Wanamichezo na ubunifu wa video inayotumia vibonzo bora.

Akizungumza mkoani hapa jana wakati akishiriki kwenye hafla ya kukabidhi Kompyuta zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini Mussa Sima kwa ufadhili wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenye Shule ya Msingi Nyerere iliyopo Manispaa ya Singida, Meneja wa Posta Mkoa wa Singida Joseph Mutatina alihamasisha wadau mbalimbali kujitokeza na kushiriki. 

"Washindi watakabidhiwa fedha taslimu na zawadi nyingine mbalimbali ifikapo Oktoba 9 mwaka huu ikiwa ni katika kuadhimisha kilele cha Posta Duniani sherehe ambazo kitaifa zitafanyika Dodoma. Nawasihi mjitokeze kwa wingi maana mwisho wa mashindano haya ni ifikapo Septemba 20 mwaka huu," alisema Mutatina.

Kwa Mkoa wa Singida, Shirika la Posta ambalo lipo chini ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari mpaka sasa lina ofisi kamili 4 zilizopo Singida Mjini, Kiomboi Halmashauri ya Iramba, Manyoni na Itigi ambazo zimeendelea kufanya vizuri kwenye utoaji wa huduma za kupokea, kusafirisha na kusambaza barua, vifurushi na vipeto.

Mutatina alizitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na usafirishaji wa barua kwa njia ya haraka (EMS) ndani na nje ya nchi, usafirishaji mizigo mikubwa, kutoa huduma ya masanduku ya barua ikiwemo kwa kutumia TEHAMA ya Posta Kiganjani na huduma ya uwakala wa fedha.

Shirika hilo ambalo lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 19 ya mwaka 1993 na kuanza kazi rasmi Januari Mosi, 1994 huduma zake nyingine ni usafirishaji wa fedha kwa njia ya 'Posta Cash', Uwakala wa Bima ikiwemo Shirika la Bima nchini na Shirika la Bima Zanzibar.

Meneja Mutatina pamoja na mambo mengine alisema huduma za uuzaji wa hisa za makampuni mbalimbali, ulipaji wa wastaafu, huduma ya Bodi ya Mikopo na Baraza la Mitihani Kwa maana ya maulizo, kupokea maombi ya mikopo na kuyasafirisha kwenda Bodi sanjari na Baraza la Mitihani maulizo na kusajili watahiniwa vyote vinafanywa ndani ya shirika hilo.

"Posta tunagusa kila mahali, pia tuna huduma za Duka Mtandao, Intaneti Cafe, tunakodisha majengo kwa huduma mbalimbali na zaidi tuna mfumo wa kufuatilia barua au kifurushi kilichotumwa kupitia Mtandao kujua kimefikia wapi au kimepokelewa na nani," alisisitiza Meneja.

Kwa huduma za usafirishaji wa barua, vifurushi, vipeto na mizigo yote kuanzia bahasha mpaka Tani 30 imeelezwa kwamba utaratibu wa safari zake Kwa kuanzia Singida kuelekea Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kigoma hufanyika kila siku majira ya jioni.

"Magari yetu ya Dar es Salaam hupitia miji ya Manyoni, Dodoma na Morogoro, na yale ya Mwanza hupitia njia ya Shinyanga, na Kigoma hupitia miji ya Nzega, Tabora, Urambo hadi Kigoma," alisema Mutatina.