Wednesday, April 28, 2021

RC NCHIMBI ATAKA MANUFAA YA CHANJO YATANGAZWE

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikata Utepe kuzindua Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo kimkoa kwenye viwanja vya Kata ya Muhintiri, Tarafa ya Ihanja, Wilaya ya Ikungi jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Edward Mpogolo.

Nchimbi akizungumza na kuhamasisha akina mama kuzingatia kuwafikisha watoto kwenye Vituo vya Afya kwa wakati na kupata dozi ya chanjo kamilifu ili kuwahakikishia afya bora katika ukuaji wao.

Baadhi ya Wanawake wakifuatilia maadhimisho hayo.

Kaimu Mganga Mkuu wa MkoawaSingida, Ernest Mgeta akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akizungumza.

Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Singida, Jadili Mhanginonya (wa kwanza kushoto) na watendaji wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakifuatilia mfululizo wa matukio ya uzinduzi huo

Wauguzi wa Afya wakiwa wamejipanga kwa maandalizi ya uzinduzi watukio la Wiki ya Chanjo.

Maadhimisho yakiendelea.


Sherehe za uzinduzi huo zikiendelea.


Na Godwin Myovela, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amewataka Wataalamu wa Afya mkoani hapa kuchanganua na kuainisha hadharani ni kwa namna gani chanjo zinazotolewa zimekuwa na tija kwa jamii ili kuleta msukumo kwa watu kuzipenda, kuzithamini, kuziheshimu na kuendelea kuchanjwa.

Akizindua ‘Wiki ya Chanjo’ kimkoa, kwenye viwanja vya Kata ya Muhintiri, Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana, Nchimbi pamoja na mambo mengine, aliwataka wataalamu hao kufuatilia na kutangaza hadharani matokeo na mazao ya chanjo hizo katika uhalisia wa maisha ili watu wajue.

“Wataalamu msikae kimya tuelezeni mara kwa mara manufaa ya hizi chanjo ni kwa namna gani zimekuwa chanzo cha afya bora na akili timamu kwa ukuaji stahiki wa watoto wetu, vijana, jamii na taifa…tuelezeni zinavyochangia ongezeko la ufaulu mashuleni na manufaa yake kwa ukuaji wa uchumi,”alisema Nchimbi na kuongeza;

“Mkieleza vizuri ubora wa chanjo hizi kwa jamii na tukawaelewa-basi- ubora huo ndio utakuwa msukumo katika kuchochea zaidi kasi ya ongezeko la watumiaji wake.”

Hata hivyo alisisitiza haitakuwa na maana yoyote kama chanjo zinazotolewa hazitaenda sambamba na lishe bora, huku akitumia nafasi hiyo kuhamasisha jamii kuzingatia vyote kwa pamoja, ili kuleta ustawi wa afya ya jamii kwa matokeo ya Taifa bora.

Nchimbi alisema Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha juhudi zilizopo za utoaji wa chanjo zinakwenda sambamba na maboresho katika utoaji wa huduma nyingine za afya-ili kupunguza vifo visivyo vya lazima na kumlinda kila mtanzania dhidi ya maradhi ambukizi.

Katika hilo, aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata dozi nzima ya chanjo zinazotolewa kwenye Vituo vya Afya, kwa kuzingatia chanjo ni chanzo cha afya bora na kinga madhubuti dhidi ya magonjwa hatarishi.

Awali, akiwasilisha taarifa ya mkoa juu ya hali halisi ya utoaji wa huduma za chanjo kwa mwaka 2020, Kaimu Mganga Mkuu mkoani hapa, Ernest Mgeta alisema licha ya mafanikio katika utoaji wa huduma hiyo lakini bado kuna changamoto, ikiwemo ya wengi kutokamilisha dozi.

Mgeta alibainisha kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa chanjo huanza vizuri lakini hawakamilishi chanjo. Mathalani katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2020, jumla ya akinamama 8,646 hawakupata au kukamilisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa Pepopunda.

Ugonjwa huo ni rahisi kumpata mtoto atakayezaliwa kupitia mama ambaye hana kinga yake, na maambukizi hutokea ndani ya siku 28 tangu kuzaliwa kupitia kovu la kitovuni. Watoto wote ambao hupata vimelea vya Pepopunda huishia kufariki.

Mgeta alitaja changamoto nyingine kuwa ni kasumba hatarishi ya wazazi kuendelea kujifungulia nyumbani ambayo hupelekea watoto kukosa huduma za afya za awali, ikiwa ni pamoja na kupata chanjo dhidi ya Kifua Kikuu na Polio.

Suala lingine lililojitokeza ni watoto kusitishwa kuhudhuria kliniki mapema na kushindwa kukamilisha dozi ya mwisho ya chanjo dhidi ya Surua, mathalani, katika kipindi cha mwaka jana jumla ya watoto 18,583 hawakufika kukamilisha dozi ya pili ya Surua-hali inayoleta tishio la mlipuko wa ugonjwa huo miongoni mwa jamii ya wana-Singida.

Akizungumzia kinga dhidi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa wanawake hususani kwa wasichana wenye umri wa miaka 14, Kaimu Mganga Mkuu alisema serikali tayari ina chanjo ya kuzuia ugonjwa huo unaosababisha kifo iliyoanza kutolewa tangu mwaka 2018, lakini hata hivyo bado mwitikio ni mdogo.

“Chanjo hii hutakiwa kutolewa mara mbili lakini mabinti wengi wamekuwa wakipata mara moja kutokana na gharama iliyopo. Kutokana na serikali kuinunua kwa gharama kubwa nayo hulazimika kutolewa kwa gharama ya shilingi elfu 60,” alisema Mgeta.

Hata hivyo, aliwahamasisha wazazi kujitokeza kuwapeleka watoto kwenye vituo vya afya, hususani wiki hii ya maadhimisho ya chanjo ili kuhakikisha zingatio la mahitaji ya kidozi linafikiwa kwa matokeo chanya ya kiafya, sambamba na kuepuka maradhi na vifo.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu yanasema “Chanjo Hutuweka Huru Pamoja, Kapate Chanjo” ikiwa na maana ya kama tutazingatia ipasavyo upatikanaji wa huduma hiyo basi ni dhahiri itatuweka huru bila ya kuwa na wasiwasi wa kuambukizana magonjwa.

Imeelezwa, kwa aliyechanja akakamilisha dozi yupo huru kutopata magonjwa ambayo yanasababishwa na milipuko na ambayo yanakingwa kwa chanjo. 

Tuesday, April 27, 2021

KAMATI YA MAKATIBU WAKUU YAANDAA MKAKATI KABAMBE WA KUBORESHA MICHEZO MASHULENI

 


Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zenye dhamana yaElimu,Michezo na TAMISEMI  wakiwa kwenye kikao kazi leo Aprili 27,2021 Jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa maelekezo ya Mawaziri wenye dhamana hizo hizo kwa lengo la   kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa masuala mbalimbali ya uimarishaji wa somo la Elimu kwa Michezo na Michezo katika shule za Msingi na Sekondari hapa nchini chini ya uenyekiti wa Prof.Riziki Shemdoe ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya  TAMISEMI.


Dkt. Hasssan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia eneo la Elimu ndugu  Gerard Mweli (kulia) wakihudhuria kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zenye dhamana ya Elimu, Michezo na TAMISEMI  wamefanya kikao kazi leoAprili 27,2021Jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa maelekezo ya Mawaziri wenye dhamana hizo hizo kwa lengo la   kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa masuala mbalimbali  yauimarishaji wa somo la Elimu kwa Michezo na Michezo katika shule za Msingi na Sekondari hapa nchini. Upande wa pili ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusufu Omary Singo

 

Na John Mapepele, Dodoma

Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zenye  dhamana ya Elimu, Michezo na TAMISEMI  wamefanya kikao kazi leo Aprili 27,2021 Jijini Dodoma kujadili  utekelezaji wa maelekezo ya Mawaziri  wenye dhamana hizo hizo kwa lengo la   kuandaa  Mkakati  wa Utekelezaji wa masuala  mbalimbali  ya uimarishaji wa somo la Elimu kwa Michezo na Michezo katika shule za Msingi na Sekondari  hapa nchini

Mwenyekiti wa Kikao hicho, Prof. Riziki  Shemdoe  ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI amesema  miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa  na kukamilika ni pamoja na   kuandaliwa kwa  mapendekezo ya uimarishaji wa ufundishaji wa somo la michezo shuleni na tahasusi zenye somo hilo kwa kidato cha tano  ambapo ameseme tahasusi hizo zitaanza kufundishwa katika mwaka huu wa masomo.

Pia rasimu ya Mpango Mkakati na Mikakati ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya  somo  la Elimu kwa michezo na michezo katika shule za Msingi na Sekondari  imeandaliwa ili  kuboresha  michezo mashuleni.

Kuhusu kuandaa kiunzi cha uendeshaji wa michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA  Prof. Shemdoe amesema  tayari  Kamati ya Wataalam imeshauri kuwa  kwa sasa  miongozo iliyopo itumike na kiunzi tayari kimeshaandaliwa kwa kuzingatia changamoto  zilizopo ambapo  kitajadiliwa  na wadau wote Juni mwaka huu wakati wa michezo ya UMISHUMTA NA UMISSETA na  kwa sasa tayari miongozo hiyo imeshatumwa kwenye  mikoa yote hapa nchini.

Aidha, suala la uundwaji wa Kamati ya kitaifa ya UMISHUMTA NA UMISSETA tayari imependekezwa na kukubalika kuundwa kwa Kamati ya Usimamizi itakayoundwa na wataalam wawili wawili kutoka kwenye kila Wizara ambapo imekubalika kuwa  pamoja na usimamizi, Kamati itatumia fursa hiyo kujifunza na kuangalia changamoto zilizopo kwenye uendeshaji wa michezo ya UMITASHUMTA  na UMISSETA kuandaa  mapendekezo yatakayojadiliwa  na wadau wote kwa ajili ya  maboresho zaidi.

Prof. Shemdoe amesema kuhusu mchakato wa maandalizi ya UMISHUMTA NA UMISSETA mwaka huu, tayari mikoa yote imeshaandikiwa barua ya taarifa na Mhe. Waziri Ofisi ya Rais –TAMISEMI na kwamba waratibu wa michezo wanakwenda kwenye ukaguzi wa viwanja na maeneo ya malazi na chakula kuanzia Aprili 28-30, mwaka huu. Pia Kamati ya wataalam inaendelea na ufuatiliaji wa Shule teule za michezo ili kuhakikisha kuwa michezo inafanyika kwenye kiwango kinachotakiwa.

Makatibu Wakuu walioshiriki  kwenye  kikao hiki ni pamoja Mwenyekiti wa kikao hicho, Prof. Riziki  Shemdoe  ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI,na Naibu wake  anayeshughulikia eneo la Elimu ndugu  Gerard Mweli, mwingine ni  Dkt. Hasssan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Dkt. Leonard Akwilapo  kutoka  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojioa pamoja na Watendaji mbalimbali kutoka  Wizara hizo.

Maelekezo  ya Mawaziri wenye dhamana ya elimu, Michezo na TAMISEMI yalitolewa wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika Februari 8, Mwaka huu.

MALARIA YAENDELEA KUWASAKAMA WATOTO MKOANI SINGIDA

p>

Afisa Afya katika Kituo cha Afya Sokoine mjini Singida, Malangwa Joseph Seni akimpima uzito mmoja wa watoto waliohudhuria Kliniki hiyo.

Bango lililobeba Kaulimbiu ya Siku ya Malaria Duniani mwaka huu likiwa mbele ya moja ya majengo ya Kituo cha Afya Sokoine mjini Singida.

Baadhi ya wateja wakisubiri kupata huduma ya  mama  baba na mtoto Kituo cha Afya Sokoine mjini Singida.


 Na Abby Nkungu, Singida 


IMEBAINIKA kuwa malaria bado ni tatizo kubwa linalosumbua watoto mkoani Singida kutokana na takwimu za idara ya afya kuonesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wanaougua ugonjwa huo na kwenda kupatiwa matibabu kwenye vituo vya huduma wana umri chini ya miaka mitano.

Hayo yalibaika juzi Aprili 25 mwaka huu Tanzania ilipoungana na Nchi nyingine Wanachama wa  Shirika la  Afya Duniani (WHO)  kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani chini ya kauli mbiu “Ziro Malaria inaanza na mimi–Nachukua hatua kuitokomeza”  

Taarifa ya idara ya afya  iliyotolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa  wa Singida, Dk Ernest Mugeta inaonesha kuwa kati ya wagonjwa 42,262 waliougua malaria kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana na kwenda  kutibiwa vituo mbalimbali vya huduma, 10,469 walikuwa ni watoto ambayo ni sawa na asilimia 33.

"Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, jumla ya watu 7,272 waliugua malaria na kwenda kutibiwa kwenye vituo mbalimbali vya huduma ambapo 2,581 sawa na  asilimia 35.5 walikuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano" alifafanua Dk Mugeta.  

Aidha, alitaja baadhi ya  sababu zinazochangia watoto kuendelea kusumbuliwa na malaria kuwa ni pamoja na  kinga  yao  ya mwili kuwa chini; hivyo kuwa rahisi zaidi kushambuliwa na ugonjwa huo na wazazi au walezi kutotumia ipasavyo vyandarua katika kuwakinga watoto wao dhidi ya mbu.

Hata hivyo, alisema kuwa Mkoa umeweka mikakati mbalimbali ya kutokomeza ugonjwa huo wa malaria, ikiwa ni pamoja na kuhimiza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu na kuangamiza mazalia ya mbu.

“Kwa mwaka 2020 tumeweza kugawa vyandarua 817,151 ngazi ya kaya kwa halmashauri za Ikungi, Iramba, Itigi, Manyoni na Mkalama na huduma ya chandarua Kliniki kwa wajawazito hudhurio la kwanza na watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja kwa kupata chanjo ya Surua/Rubella (MR 1) kwenye vituo huduma” alieleza Dk Mugeta.

Akinamama mbalimbali walisema kuwa pamoja na juhudi hizo  za Serikali, bado kuna changamoto ya elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya chandarua  katika jamii pamoja na  imani  potofu.

“Kweli vyandarua watu wanapewa lakini ukienda  vijijini utakuta vingi vimezungushiwa kwenye uzio wa kufugia kuku au bustani za mboga. Baadhi wanadai  vinapunguza  nguvu za kiume na wengine eti wanaona ni sawa na kujifunika sanda” alisema mama Rose Ntandu.

Mwito  wao kwa wataalamu wa afya na wadau  wengine  wa mapambano dhidi ya Malaria ni kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii juu ya umuhimu wa kutumia chandarua na madhara yanayoweza kujitokeza iwapo wataugua malaria; hasa watoto walio chini ya miaka mitano.

Monday, April 26, 2021

SUA INAONGOZA KWA MAPAMBANO DHIDI YA VVU NA UKIMWI KWA VYUO VIKUU NCHINI

 Daktari Kiongozi wa Hospitali za SUA naMkuu wa idara za huduma za hospitali Dkt. Omari Kasuwi akifungua mafunzo hayo ya waelimishaji rika chuoni hapo.

Mratibu wa UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza SUA Dkt. Erhard Kapilima akitoa maelezo ya maengo ya mafunzo hayo kabla ya ufunguzi rasmi wa mafunzo kwa waelimishaji rika SUA.

Daktari Bingwa wa Wanawake na Uzazi ambaye pia ni Daktari kiongozi wa hospitali ya SUA upande wa Mazimbu Dkt. Elimwidimi Swai akitoa mada yake kuhusu UKIMWI na Virusivya Ukimwi VVU.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto Dkt. Graca Chotamawe akiwasilisha mada yake kuhusu sababu  zinazochangia maambukizi ya virusi vya ukimwi na takwimu za Ugonjwa huo.

Mratibuwa UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza SUA Dkt. Erhard Kapilima akitoa maelezo ya malengo ya mafunzo hayo kabla ya ufunguzi rasmi wa  mafunzo kwa waelimishajirika SUA.

Washiriki wa mafunzo hayo ya uelimishaji rika wakichangia na kufuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa  kwenye mafunzo hayo ya siku moja chuoni hapo. 















 Na Calvin Gwabara, Morogoro 


WANAFUNZI wa Chuo kikuu cha sokoine cha kilimo SUA waliopata nafasi ya kupata mafunzo ya uelimishaji rika chuoni hapo wametakiwa kuhakikishawana yatumia mafunzo hayo vyema kwa kutoa elimu kwa wenzao ilikusaidia kupunguza maambukizi ya Virusi vya ukimwi na magonjwa Sugu yasiyoambukiza chuoni.

Wito huo umetolewa na mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo Dkt. Omar Kasuwi ambaye ni Daktari kiongozi wa Hospitali za SUA yaliyofanyika chuoni hapo na kuwakutanisha wawakilishi wa wanafunzi kutoka kozi mbalimbali kutoka kampasi zote za SUA mkoani Morogoro.

“ Elimu hii mnayoipata nyinyi leo ya uelimishaji rika lengo lake kubwa ni nyinyi kuwa mabalozi kuhusu masuala ya ukimwi na magonjwa mengine sugu kwenyemaeneo yote mnayotoka iwe kwenye kozi zenu, mabweni yenu na hata kwenye kampasi mnazotoka ndio maana mafunzo hayo yamezingatia mchanganyiko mzuri ambao unagusa kila kona hivyo hakikisheni elimu hii mnaifikisha kwa wenzenu kokote mnakotoka ili kwapamoja tuchangie kwenye kuongeza uelewa kuhusu magonjwa haya” alisisitiza Dkt. Kasuwi.

Dkt. Kasuwi alisema kuwa pamoja na dhamira na uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na familia na serikali katika kuwapatia vijana elimu na ujuzi ili hatimae waweze kusaidia familia na taifakwa kucnagia kwenye maendeleo lakini ndoto hizo kwa wengine hufutika kutokana na athari zamaambukizi ya VVU/UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukiza (MSY).

Aidha ameongeza kuwa pamoja na hilo lakini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2017/2017 umeonyesha kuwa sehemu kubwa ya maambukizi mapya ya VVU yanatokea kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-23 kundi ambalo wengi wao wapo vyuoni na kwamba utafiti pia ulibaini wanafuinzi wa  vyuovikuu wako katika hatari zaidi ya kupata maambukizi.

Dkt. Kasuwi ameendelea kusema kuwa mwaka 2013 serikali ilifanya tathimini ili kubaini iwapo mikakati ya kudhibiti UKIMWI iliyokuwepo imeleta mafanikio yaliyokusudiwa hasa kwa watumishi wa Umma na matokeo hayo ya utafiti yalibainisha kuwa UKIMWI na MSY yalichangia sana kwenye vifo hivyo na kuathiri utendaji katika utumishi waUmma.

Daktari huyo kiongozi wa Hospitali za SUA aliesema utafiti huo ulipelekea Serikali kutoa waraka namba 2 wa mwaka 2014 uliowataka waajiri wote kuweka mikakati na kusimamia mikakati  yaudhibiti wa UKIMWI na MSY sehemu za kazi ilikupunguza athari zake.

Dkt. Kasuwi amebainisha kuwa tangu kuanza mapambano dhidi ya magonjwa hayo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimeendelea kuwa kinara katika mipango na mikakati ya utekelezaji wa waraka na maagizo hayo ya Serikali miongoni mwa vyuo vikuu vyote nchini na ameahidi kuendelea na jitihada hizo ilikuhakikisha wanafunzi na wafanyakazi wote wanakuwa salama wakati wote ili kutimiza ndoto zao nakutimiza malengo ya kila mfanyakazi ili kuleta maendeleo.

Awali akizungumza kuhusu mafunzo hayo kwa waelimishaji rika chuoni hapo Mratibu wa UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukiza SUA Dkt. Erhard Kapilima alisema sababu kuu mbili za mafunzo hayo  kwanza nikutekeleza maelekezo ya waraka huo namba mbili wa Serikali kuhusu usimamizi wa magonjwa hayo, lakini miaka michache iliyopita magonjwa hayo yameongezeka kwa kasi  nahiyo imetokana na kulegalega kwa mkazo kwenye kutoa elimu na kusimamia magonjwa hayo hivyo kufundisha waelimishaji rika kutasaidia kuongeza uelewa kwa jamii ya wanafunzi.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yameanza kwa jamii ya wanafunzi chuoni hapo lakini zoezi lingine kama hilo litafanyika pia kwa watumishi wa SUA watakaochaguliwa kulingana na maeneo yao ya kazi ili pia wapewe mafunzo na kupata waelimishaji rika hao kila kona ya chuo ili kuwe na nguvu ya pamoja ya kutoa elimu na kupunguza maambukizi ya magonjwa hayo na elimu kwani haiwezi kuwarahisi kutoa mafunzo kwa wanafunzi wote na wafanyakazi wote wa chuo.

Dkt. Kapilima ameongeza kuwa mafunzo hayo kwa wanafunzi yamekuwa ya kitolewa kila mwaka kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili  ilikusaidia kuziba pengo la wale wanaomaliza mwaka  watatu na kukifanya chuo kuendelea kuwa na waelimishaji rika wakutoka kila mwaka chuoni hapo na kusaidia mapambano ya kuyakabili magonjwa hayo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa SUA Heath Club, Musa Katyeka alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa muhimu sana kwao  kamawanafunzi kwani yamewasaidia kuwapatia wataalamuwengi wa kujitolea kutoa elimu kwa wanafunzi wenzao chuoni hapo juu ya magonjwa hayo na hivyo kuchangia kupunguza maambukizi miongoni mwao.

Kyateka ameongeza kuwa wao kama wanafunzi kila mwaka wanapata wanafunzi wengine wapya chuoni wengine wakiwa na umri mdogo hivyo ni muhimu kuwa na mafunzo ya aina hiyo ilikusaidia kupata idadi ya kutosha kuhudumia idadi kubwa ya wanafunzi wenzao kwenye mambo ya msingi ya namna ya kujikinga na maambukizi ili wawezekufikia ndoto zao na kuchangia kwenye maendeleo ya taifa.

Katika mafunzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa na SUA kupitia idara ya  huduma za hospitali mada mbalimbali zilifundishwa kwenye mafunzo hayo na madaktari bingwa wa magonjwa hayo pamoja na kupata shuhuda za watu mbalimbali wanaoishi na VVU mkoani Morogoro ambao nao walitapata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi hao.


SERIKALI YAMALIZA MGOGORO WA ARDHI BAINA YA WANANCHI NA NARCO KIGOMA

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mpeta ambapo alieleleza kuwa zaidi ya Ekari Elfu Kumi na Nne (14000) zitegwe kutoka katika Ranchi ya Uvinza na zigawiwe kwa wananchi wanaoishi katika eneo la Mwandulubhantu na Kazaroho ili wazitumie kwa makazi na shughuli nyingine za kimaendeleo. Waziri Ndaki alitembelea Wilaya ya Uvinza iliyopo Mkoani Kigoma jana na kufanya maamuzi hayo kwa lengo la kumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu kati ya wananchi hao na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akiagana na mmoja kati ya Wazee wanaoishi katika Kijiji cha Mpeta aliyejitokeza kuhudhuria mkutano wa Waziri huyo na Wananchi wa Kijiji hicho uliofanyika Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma jana. Katika Mkutano huo, Waziri Ndaki aliamua Ekari zaidi ya Elfu Nane (8000) zimegwe kutoka katika Ranchi ya Uvinza ili wakabidhiwe wananchi wanaoishi katika eneo la Mwandulubhantu lililopo katika kijiji cha Mpeta ili wazitumie kwa makazi na shughuli nyingine za maendeleo.

Wananchi wa Kijiji cha Mpeta wakiagana kwa furaha na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati kulia) muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa Waziri huyo na Wananchi wa Kijiji cha Mpeta uliofanyika Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma jana.


 

Na Mbaraka Kambona, Kigoma

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutenga Ekari Elfu Kumi na Tano (15000) na wazigawe kwa Wananchi wa Vijiji viwili vya Mpeta na Chakulu vilivyopo Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma ili kutatua mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya wananchi hao na Kampuni hiyo. 

Ndaki alitoa maelekezo hayo jana katika ziara yake Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma kwa lengo kutatua mgogoro huo ardhi kufuatia wananchi wa vijiji hivyo kuvamia maeneo ya Ranchi ya Uvinza na kuishi humo kinyume na taratibu. 

Akiongea na wananchi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti, Waziri Ndaki alisema kuwa Serikali imeamua kufikia maamuzi hayo ili wananchi hao waweze kujikita katika shughuli za maendeleo na kuachana na migogoro ya kila siku ambayo haina tija yoyote. 

“Hatupendi tuendelee na migogoro kwenye maeneo yetu, tunataka tumalize migogoro ili tuanze kufanya shughuli za maendeleo, kila mwananchi afanye shughuli yake bila bughudha yoyote,” alisema Ndaki. 

Aliongeza kuwa baada ya ugawaji wa maeneo hayo kukamilika Mkuu wa Wilaya ya Uvinza na timu yake watakwenda kufanya tathmini katika maeneo hayo na kuyafanyia mchakato wa kuyarasimisha ili kuwa Kijiji au Kitongoji. 

Alisisitiza kuwa pamoja na wananchi hao kuvunja Sheria, Serikali imeangalia maslahi mapana na ndio maana imeamua kutoa sehemu ya eneo katika ranchi hiyo ili wananchi hao waweze kuishi kwa utulivu na kuendelea na shughuli zao huku akiwaonya kuwa wasijaribu tena kuingia katika ranchi hiyo baada ya kugawa ekari hizo na atakayefanya hivyo anatafuta kesi. 

“Ranchi ni eneo la kufugia mifugo na sio eneo la kuishi watu au kulima humo, atakayejaribu kuingia tena ananitafuta kesi, tumewapa maeneo hayo ili mkae humo, atakayetaka kufuga aje sisi tutampa eneo la kukodisha kwa bei ya Serikali ili aweze kufuga kisasa, kulima malisho na kuongeza tija ya mifugo yake,” alisisitiza Ndaki. 

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko baada ya kumshukuru Waziri Ndaki kwa uamuzi huo naye aliwasisitiza wananchi hao kutoendelea kuvamia maeneo ya ranchi hiyo ili kuepukana na migogoro isiyo na tija na badala yake watumie maeneo hayo waliyopewa kujiletea maendeleo yao. 

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chakulu, Mohamed Baswage aliishukuru Serikali kwa tamko hilo la kuwapa eneo wananchi wa Kijiji hicho huku akisema kuwa uamuzi huo utawasaidia wao kusukuma maendeleo yao kwa pamoja wakishirikiana na Serikali.

Saturday, April 24, 2021

SERIKALI KUJA NA MKAKATI ENDELEVU KUDHIBITI UVUVI HARAMU NCHINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akizungumza na Wavuvi wa Mwalo wa Kibirizi ambapo alisema kuwa Serikali ipo katika mipango ya kuandaa mkakati shirikishi na endelevu wa kupambana na uvuvi haramu nchini. Ndaki alifanya Mkutano na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliopo Mkoani Kigoma jana.


    Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) Katika Mkutano wa Waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma jana.


      Mchakataji Mazao ya Uvuvi, Prisca Steven akitoa kero zinazowashumbua Wachakataji wa Mazao ya Uvuvi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) katika mkutano wa waziri huyo na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika mwalo wa Kibirizi uliofanyika Mkoani Kigoma jana.


        Sehemu ya Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi wakifuatilia matukio yanayoendelea  katika Mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki na Wavuvi hao uliofanyika Mkoani Kigoma jana.

         


        Na Mbaraka Kambona, Kigoma

         

        Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ipo katika mpango wa kuwa na mkakati endelevu wa kudhibiti uvuvi haramu na kuachana na utaratibu wa kuendesha oparesheni za muda mfupi. 

        Ndaki alisema hayo wakati akizungumza na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Kibirizi ulipo katika Ziwa Tanganyika Mkoani Kigoma jana. 

        Akizungumza na wavuvi hao Ndaki alisema kuwa lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuwa na udhibiti wa uvuvi haramu ambao utakuwa endelevu utakaoshirikisha wahusika wenyewe wanaofanya shughuli za uvuvi na viongozi wa eneo husika kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya hadi Mkoa. 

        “Tunataka kuja na mkakati endelevu wa namna ya kudhibiti uvuvi haramu, tuusike sote, kuanzia Wataalamu, Viongozi wa ngazi zote na wananchi wanaohusika na uvuvi wenyewe,” alisema Ndaki. 

        “Uvuvi haramu unatishia rasilimali zetu za uvuvi, tusiulee, tuwashirikishe wahusika ili waone kuwa uvuvi haramu ni kitu kisichokubalika”. 

        Kwa Mujibu wa Ndaki anasema walichokigundua katika mkakati wa kutumia oparesheni za muda mfupi ni kwamba matokea yanakuwa ya muda mfupi na operesheni hizo zikiisha matukio ya uvuvi haramu yanaendelea tena kwa sababu operesheni hizo zinahusisha wataalamu kutoka Wizarani na sio wahusika wenyewe wa eneo husika. 

        ‘‘Ulinzi wa rasilimali za uvuvi sio jukumu la watu wa makao makuu peke yake, ni jukumu letu sote, tuone umuhimu wa kutunza rasilimali zetu na wote tukubaliane kuwa uvuvi haramu haukubaliki na tukikukamata sheria itachukua mkondo wake,” alisisitiza Ndaki. 

        Kuhusu baadhi ya viongozi wanaolalamikiwa kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu alisema kuwa kiongozi au mtaalamu yeyote mwenye dhamana ya masuala ya uvuvi atakayepatikana kuhusika na vitendo vya uvuvi haramu na yeye atakuwa haramu na atashughulikiwa kama wahalifu wengine. 

        Aliongeza kuwa kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia masuala ya uvuvi na eneo lake linafanya uvuvi haramu, wataanza kumchukulia hatua huyo kiongozi na wengine wote watakaokuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine kwa kutokuwajibika kwao. 

        Ndaki alisema kuwa hatalegeza nati hasa linapokuja suala la uvuvi haramu na kuwataka wananchi na viongozi wa ngazi zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita uvuvi haramu huku akiwahimiza kuwafichua wale wote wanaohusika na vitendo vya uvuvi haramu katika maeneo yao.

         

        BODI YAPONGEZA KASI YA TANROADS, TARURA MKOANI SINGIDA



        Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi (kulia) ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Singida akifungua kikao hicho kilichofanyika jana mkoani hapa. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba na Katibu Tawala wa mkoa huo, Dkt. Angelina Katambi.

        Meneja wa  Wakala wa Barabara  Nchini (TANROADS) Mkoa wa Singida , Mhandisi Matari Masige akielezea  utekelezaji wa mipango ya matengenezo ya barabara hadi kufikia Deseba 30, 2020. 

        Makamu Mwenyekiti wa kikao hicho. ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo,  akichangia jambo kwenye kikao hicho.

        Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba, akizungumzia mafanikio makubwa yaliyofanywa na Tanroads na Tarura ya kutengeneza barabara katika mkoa huo.

        Baadhi ya wabunge wakiwa katika kikao hicho,. Kutoka kushoto ni Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Masare, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Gwau na Mbunge wa Singida mjini, Musa Sima.

        Mratibu wa Mkoa wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Nchini (TARURA) Mhandisi Boniface Magani, akielezea  utekelezaji wa mipango ya matengenezo ya barabara hadi kufikia Deseba 30, 2020. 
        Mbunge wa Manyoni Mashariki, Dkt. Pius Chaya akichangia jambo kwenye kikao hicho kwa kuwapongeza Tanroad na Tarura kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutengeneza barabara na kufika kwa wakati eneo lenye changamoto baada ya kupewa taarifa.
        Mwenyekiti wa wabunge wote wa Mkoa wa Singida ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akizungumzia kazi kubwa iliyofanywa na Tanroad na Tarura ya kutengeneza barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
        Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima akichangia jambo kwenye kikao hicho.
        Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega akizungumza kwenye kikao hicho.
        Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Hussen Simba, akizungumza kwenye kikao hicho.


        Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Abubakar Muna, alichangia jambo kwenye kikao hicho kwa niaba ya mbunge huyo.
        Washiriki kutoka wilaya zote za Mkoa wa Singida wakiwa kwenye kikao hicho. Kushoto ni Kaimu Afisa maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani.

        Wabunge wakiwa kwenye kikao hicho.

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu, akichangia jambo kwenye kikao hicho.

        Wakuu wa Wilaya wakishiriki kwenye kikao hicho.

         Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Jumanne Mlagaza, akizungumza kwenye kikao hicho.

        Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
        Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida , Eliya Digha, akichangia jambo kwenye kikao hicho.


        Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ali Mwanga, akichangia jambo kwenye kikao hicho.




        Godwin Myovela na Doto Mwaibale, Singida.


        WAJUMBE wa Bodi ya Barabara mkoani hapa wamepongeza kasi ya matengenezo ya barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kuwataka kutobweteka, badala yake waharakishe kukamilisha barabara na madaraja muhimu kwa ukuaji wa uchumi, ili kupunguza kero na kuchagiza maendeleo mkoani hapa.

        Wakichangia kwa nyakati tofauti kwenye kikao hicho jana, pamoja na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na wakala hizo, waliwataka kuongeza usimamizi wa karibu kwa wazabuni ili kuongeza ufanisi.

        Pia ufinyu wa bajeti katika utekelezaji wa miradi mipya na ile ya umaliziaji ikiwemo barabara na madaraja bado ni changamoto jambo linalopelekea kupunguza ari na ustawi wa kiuchumi kwa wanasingida.

        Aidha, wamependekeza miradi inayojengwa na wakala hizo iende sambamba na uwekaji wa taa za barabarani ili kuwawezesha wajasiriamali kufanya biashara zao hadi usiku.

        Sambamba na hilo, wajumbe hao wameomba kuwapo kwa ukaguzi na matengenezo ya kawaida ya barabara mara kwa mara ili kuongeza tija na uimara badala ya kusubiri wakati wa majanga.

        "Nawapongeza sana wenzetu hawa wa Tanroads na Tarula pamoja na fedha ndogo wanazopata lakini wanajitahidi sana...naamini wakipata fedha za kutosha watafanya makubwa kuliko haya," alisema Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu.

        Akiwasilisha utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara kuanzia Julai hadi Desemba 2020, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Singida, Mhandisi Matari Masige alisema mpaka sasa sehemu kubwa ya mtandao mkoani hapa inapitika.

        "Kwa ujumla asilimia 62.7 ya barabara zote zipo katika hali nzuri, asilimia 27.9 zina hali ya wastani na asilimia 9.4 zina hali mbaya," alisema.

        Masige alisema kutokana mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana na baadhi ya barabara kupandishwa daraja kutoka wilaya kuwa za mkoa imepelekea baadhi kuwa katika hali mbaya na juhudi za matengenezo zinaendelea.

        Alizitaja barabara hizo kuwa ni Iyumbu Magereza yenye kilometa 123.7, Sepuka Mgungira kilometa kilometa 89.6 na Soweto Kisiriri Chemchem kilometa 43.3.

        Hata hivyo Masige alisema matengenezo ya kawaida kwa barabara kuu hadi mwezi Desemba 2020 yametekelezwa kwa asilimia 53 kikazi na asilimia 2.1 kifedha.

        "Kwa upande wa barabara za mkoa kwa matengenezo ya kawaida utekelezaji wake umefikia asilimia 77.7 kikazi na asilimia 45.3 kifedha," alisema Mhandisi Masige.

        Tanroads Mkoa wa Singida unahudumia jumla ya kilometa 1,727.6 za barabara Kuu na zile za Mkoa. Kati ya hizo, kilometa 484.2 ni lami sawa na asilimia 28 na sehemu iliyobaki yenye urefu wa km. 1,243.4 sawa na asilimia 72 ni changarawe.

        Kwa upande wake, Mratibu wa Tarura mkoani hapa, Mhandisi Boniface Magani alisema hali ya barabara zake mkoani hapa nayo imeendelea kuimarika.

        "Kwa sasa hali ya barabara inaridhisha ambapo asilimia 43.21 ya barabara hizo sehemu kubwa inapitika baada ya kufanyiwa matengenezo," alisema.

        Magani alisema Tarura Mkoa wa Singida una mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 5,669.412 ambazo zimeingia katika mfumo wa 'Droma.' (Neno la Kigiriki likimanisha miundombinu ya barabara).

        Alisema kati ya hizo barabara za wilaya zina jumla ya kilometa 1946.082, barabara za mjazio kilometa 2860.147 na zile za wananchi ni kilometa 863.183.