Friday, March 31, 2023

SINGIDA YAJIDHATITI KUTUMIA MFUMO WA MSHITIRI KUPATA BIDHAA ZA AFYA

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya wakati akifungua mafunzo ya wawezeshaji wa Mfumo Mshitiri kutoka Halmashauri Saba za mkoa huo katika mkutano uliofanyika mjini hapa Machi 30, 2023. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick na kulia ni  Mwezeshaji wa kitaifa wa mfumo huo kutoka Wizara ya TAMISEMI, Emmanuel Mayunga,

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKOA  wa Singida umeendelea kujidhatiti na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia mfumo wa Mshitiri kwa bidhaa za afya zinazokosekana Bohari ya Dawa (MSD).

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati akifungua mafunzo ya wawezeshaji wa Mfumo Mshitiri kutoka Halmashauri Saba za mkoa huo ambazo ni Itigi, Iramba, Singida Manispaa, Ikungi, Manyoni, Singida DC na Mkalama.

“Kutokana na changamoto na kuibuka kwa hoja mbalimbali za ununuzi wa bidhaa za afya vituoni, Ofisi ya  Rais - TAMISEMI ilitoa waraka namba moja wa mwaka 2018 ambao ulielekeza matumizi ya washitiri teule wa mikoa katika ununuzi wa bidhaa za afya pale vituo vinapokosa bidhaa kutoka MSD,” alisema.

Serukamba alisema kuwa uwapo wa mfumo huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama ilivyoainishwa katika sura ya Tatu, sehemu ya 81 (i) na (aa).

Alibainisha kuwa upatikanaji dawa na vipimo vya kitabibu kwa uhakika katika kituo cha huduma za afya kwa kiasi kikubwa unaakisi ubora wa huduma zitolewazo na mahali husika.Hivyo, alitoa mwito kwa washiriki kuzingatia utekelezaji wa mwongozo wa mfumo huo ili waweze kuusimamia kikamilifu kwa ajili ya kuleta matokeo chanya yanayolenga kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.

Katika hatua nyingine, Mwezeshaji wa kitaifa kutoka Wizara ya TAMISEMI, Emmanuel Mayunga, alisema semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo washiriki ili wanapomaliza waweze kusimamia vema Mfumo huo kulingana na mwongozo na sheria za nchi

 Mfamasia Elikana Lubango, alisema mfumo Mshitiri ulianzishwa kwa mujibu washeria za ununuzi wa umma pamoja na mpango mkakati wa kisekta ili kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.Alisema Mfumo huo unasaidia wakati bidhaa za afya zinapohitajika kwa dharura kupatikana mara moja tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Wadauwa Sekta ya Afya wakiwa kwenye mafunzo hayo.
 

Tuesday, March 28, 2023

SUA KUJA NA MAPENDEKEZO YA SERA BORA ZA BIASHARA YA MAZAO YA KILIMO NA NYAMA PORI NCHINI.

Kaimu Rasi wa Ndaki ya Uchumi Kilimo na stadi za Biashara Dkt. Zena Mpenda akifungua warsha ya Wadau wa Mradi wa TRADE HUB kujadili matokeo ya utafiti. 

Na Amina Hezron,Morogoro 

WADAU wa zao la Soya kahawa miwa na nyama pori wametakiwa kushiriki kikamilifu kwenye kutoa mapendekezo  na maoni yao kwenye Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendeleo na Mazingira (TRADE Hub) ili matokeo yatakayopatikana yaweze kuinua tija ya mazao hayo nchini.

Hayo yameelezwa na Kaimu Rasi wa Ndaki ya Uchumi Kilimo na stadi za Biashara Dkt. Zena Mpendu aliyemuwakilisha Rasi wa Ndaki hiyo Dkt Damas Philip katika  warsha iliyoandaliwa na mradi huo ili kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti wao kwa wadau ili kupata maoni yao  juu ya namna bora ya kufanya biashara ya haki na endelevu.

Amewataka wadau hao kuzingatia kuwa tasnia hizo zinagusa kwa namna moja ama nyingine maisha na maendeleo ya wadau mbalimbali pamoja na uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla hivyo watumie fursa hiyo kwa makini kutoa maoni yao ya namna bora ya kuboresha biashara  katika tasnia hizo zote za Nyama pori na Mazao ya kilimo.

“Ni vizuri tunaposikiliza hizi mada zinazotolewa tuangalie inaelezea kweli ile hali halisi kwenye maeneo yetu ili tuweze kuboresha yale ambayo tumeyaona lakini pia tuweze sasa kuangalia mapendekezo yanayotoka tuone hayo mapendekezo yatafanyika yanawezekana ili tukitoka hapa tuwe na mapendekezo ambayo ni bora zaidi”, alisema Dkt. Zena.

Dkt. Zena ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikiboresha mara kwa mara Sheria, taratibu na Kanuni kuhakikisha kwamba biashara hizo hazisababishi ongezeko la uharibifu wa mazingira na upotevu wa baionuai hivyo ni muhimu kama wadau wa biashara kuhakikisha wanaingia kwenye mikataba ya kijani kwenye biashaa zao ili kuwe na biashara endelevu kwaajili ya watu na ulimwengu pia.

Akieleza malengo ya warsha hiyo Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA Prof. Japhet Kashaigili amesema kuwa ni kuwasilisha kwa wadau matokeo ya tafiti kadhaa ambazo mradi huo umeyapata ili wapate nafasi ya kuyajua, kuyajadili na kutoa mapendekezo ili kuona ni namna gani yanaweza kuchangia kwenye maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

“Lengo lingine la pili la warsha yetu hii na mradi ni kutengeneza mpango au njia itakayotupeleka nchi mahali fulani kuptia ufanyaji wa biashara yenye haki na endelevu nchini Tanzania lakini pia bidhaa zetu ziweze kuhimili ushindani kwenye masoko ya kimataifa na kukuza uchumi”, alifafanua Prof. Kashaigili.

Aidha amesema dhumuni kubwa linalobeba mradi huo ni kuhakikisha biashara ya mazao na nyama pori inakuwa ni injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi,Kuondoa umasikini na kama mbinu ya kutekeeleza maendeleo endelevu kama ilivyosisitizwa kwenye Mpango wa maendeleo endelevu bila kuchangia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa mradi huo Prof. Reuben Kadigi amesema warsha hiyo ya wadau ni muhimu sana katika kupata maoni na mapendekezo ambayo yatawasaidia watafiti kuweza kutengeneza andiko la sera ambalo litawasilishwa Serikalini ili kusaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Kila mchango wa mdau unaotolewa andika mahali kila ushauri andika ili mwisho wa siku tupate kitu kizuri kifupi cha kuwasilisha serikalini baada ya kufanya uchambuzi wa kina kulingana na matokeo tuliyoyapata maana mwisho wa siku hatuwezi kupeleka kwa watunga sera kitu kinacholeweka nawaweze kukifanyia kazi kwa ustawi wa biashara nchini”, alieleza Prof. Kadigi.

Kwa upande wake Dkt. Charles Malaki aliyemuwakilisha Kaimu Rasi wa Ndaki hiyo amewashukuru wadau waliojitokeza katika warsha hiyo na amewataka kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha matokeo ya tafiti hizo ili kuisaidia Serikali baadae kupata sera bora zitakazosaidia kuwa na uendelevu katika biashara ambayo inajali Mazingira,Nyama pori pamoja na watu.

Mradi wa Utafiti wa Biashara,Maendelo na Mazingira (TRADE Hub)ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na washirika wengine kutoka katika nchi kumi na tano  za Afrika, Asia, Uingereza na Brazil kuanzia Februari 2019 hadi Machi 2024.

 Mratibu wa Utafiti na Machapisho (SUA) ambaye pia ni mtafiti kwenye mradi huo Prof. Japhet Kashaigili akieleza malengo ya Warsha hiyo na kazi ambazo mradi huo umefanya hadi sasa.
Mkuu wa mradi wa TRADE HUB, Prof. Reuben Kadigi akitoa neno la ukaribisho kwa Wadau hao kutoka nchi nzima kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo.
 Dkt. Charles Malaki akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi na wadau.
 Picha ya pamoja ya washiriki wa warsha hiyo kutoka SUA na Mikoa mbalimbali ambao ni wadau wa Mazao ya Soya, Kahawa, Mpunga, Parachichi na wawakilishi wa Halmashauri na Makampuni yaliyo kwenye mnyororo wa thamani ya mazao hayo.
Wadau wa Mradi wa TRADE HUB wakifuatilia mawasilisho ya matokeo ya tafiti mbali mbali zilizofanywa kwenye mzao ya Soya, Kahawa,Parachichi,Miwa na Nyama Pori.
Mkutano ukiendelea.
Wadau wakiwa kwenye mkutano huo.
Wadau wa Mradi wa TRADE HUB wakifuatilia mawasilisho ya matokeo ya tafiti mbali mbali zilizofanywa kwenye mzao ya Soya, Kahawa,Parachichi,Miwa na Nyama Pori.
Wadau wa Mradi wa TRADE HUB wakifuatilia mawasilisho ya matokeo ya tafiti mbali mbali zilizofanywa kwenye mzao ya Soya, Kahawa,Parachichi,Miwa na Nyama Pori.
Mkutano ukiendelea.
 

Friday, March 17, 2023

RC SINGIDA ATAKA WANANCHI KULIPA BILI ZA MAJI KILA MWEZI ILI KUISAPOTI SUWASA GHARAMA ZA UENDESHAJI

Mkuu  wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (wa pili kushoto) na viongozi mbalimbali wakivuta pazia kuashiria uzinduzi 

wa mradi wa maji wa Kata ya Unyambwa uliogharimu zaidi ya Sh.Milioni 622 ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 6120 wa vijiji vya kata hiyo.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amehimiza watumiaji wa maji kulipa ankara za maji kila mwezi bila kulaza ili kuiwezesha Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) iweze kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji, matengenezo na sehemu ya uwekezaji. 

Serukamba ameyasema hayo leo Machi, 17,2023 wakati akizindua  mradi wa maji wa Kata ya Unyambwa uliogharimu zaidi ya Sh.Milioni 622 ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 6120. 

Serukamba alisema wananchi mbali na kulipa ankara za maji kwa wakati pia wajiepushe na vitendo vya wizi wa maji kwani jambo hilo linaongeza mzigo wa gharama  kwa SUWASA na wateja wake. 

Aidha, Serukamba alitaja mambo mengine ambayo yataweza kuisaidia SUWASA kuwa ni kutunza vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yote ya huduma, kutumia maji kwa uangalifu na kufuata taratibu zilizowekwa wakati wa kuomba maunganisho ya majisafi. 

Serukamba alitumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa wananchi wa Kijiji cha Unyambwa na uongozi wa kata hiyo hususani Diwani, Shabani Magwe kwa ushirikiano mkubwa ambao wameipatia SUWASA katika hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi huo ikiwemo utoaji wa maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya maji na kuomba ushirikiano huo uendelezwe hata wakati wa uendeshaji wa mradi kwa kuwa Unyambwa sasa ipo ndani ya Manispaa na wananchi wanahitaji miundombinu ya majisafi iwekwe majumbani mwao.

Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA, Sebastian Warioba alisema mradi huo wa ujenzi wa miundombinu ya maji Kata ya Unyambwa, ni mradi wa awamu ya pili baada ya mradi wa awamu ya kwanza kukamilika mwaka 2018.

Alisema mradi wa awamu ya kwanza ulihusisha uchimbaji wa kisima eneo la Unyambwa juu na uligharimu kiasi cha Sh. Milioni  45.

Warioba alisema mnamo mwaka 2019, Watalaamu kutoka Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kushirikiana na watalaamu kutoka SUWASA walikamilisha taarifa ya usanifu wa mradi wa maji katika Kata ya Unyambwa na taarifa iliwasilishwa Wizara ya Maji kwa maombi ya fedha za utekelezaji wa mradi huo na kuwa Wizaraya Maji kupitia Mfuko wa Maji (NWF) ilianza kutoa fedha za ujenzi wa mradi wa ujenzi miundombinu ya maji Kijiji cha Unyambwa mwaka 2021.

Aliongeza kuwa awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya maji katika kata hiyo ulianza Juni 1,2021 na ulitarajiwa kukamilika Septemba 01, 2021 na kueleza kuwa mradi huo haukukamilika kwa tarehe iliyokuwa imepangwa kutokana na fedha za mfuko wa maji kutolewa kwa awamu tofauti tofauti.

Alisema mradi huo umetekelezwa kwa kutumia watalaamu wa ndani wa SUWASA (SUWASA force account) na kuwa iwapo utekelezaji wake ungetumia utaratibu wa mkandarasi gharama ingekuwa zaidi ya Sh. Milioni  869.

Mwenyekiti wa Bodi SUWASA, Deocres Kamala alisema mradi huo utawasaidia watu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazolenga kuleta maendeleo katika Manispaa ya Singida, kama Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya maji mwaka huu inavyosema 'Kuongeza Kasi ya Mabadiliko Katika Sekta ya Maji kwa Maendeleo Endelevu ya Kiuchumi' na kuunga mkono jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru alisema mradi huo unakwenda kuwaondolea adha waliokuwa wakiipata wajawazito wakati wa kwenda kujifungua kwenye Zahanati ya kata hiyo kwani walilazimika kwenda na vidumu vya maji.


Mkuu  wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi huo wa maji. 

Mwenyekiti wa Bodi SUWASA, Deocres Kamala, akizungumza katika uzinduzi huo.
Kaimu Mkurugenzi, Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Richard Kasase akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA, Sebastian Warioba, akielezea mradi huo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru, akizungumza.
Wanawake wa Kaya ya Unyambwa wakiwakwenye uzinduziwa mradi huo.
Wanaume wakiwa kwenye hafla hiyo
Washiriki wa uzinduzi huo wakiserebuka wakati wakimsubiri mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Wanafunzi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Unyambwa, Ally Jingu.
Hafla ikiendelea.
Uzinduzi wa mradi huo ukiendelea.


 

KAMATI YA BUNGE PAC YARIDHISHWA MRADI WA KIWANDA CHA MIPIRA YA MIKONO CHA MSD

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya  Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Japhet Hasunga, akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa kiwanda cha mipira ya mikono cha Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Idofi-Makambako mkoani Njombe. 

Na Mwandishi Wetu, Njombe

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa kiwanda cha mipira ya mikono cha Bohari ya Dawa (MSD) kilichopo Idofi-Makambako mkoani Njombe na kuahidi kuishauri serikali kuongeza bajeti ya shilingi bilioni 12, kuwezesha mradi huo kukamiloka kuanza kazi ifikapo Julai mwaka huu.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Japhet Hasunga, amesema kamati imeishauri bodi ya Wadhamini MSD na Menejimenti kuwa wabunifu kufikia adhma ya serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kufikia  uchumi wa viwanda.

Amesema kutokana na tathimini ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha ujenzi wa kiwanda hicho umefikia asilimia 70, ambapo kamati imeona haja kwa hatua zilizobaki taasisi za udhibiti kuhakikisha zinashirikiana ipasavyo kuwezesha bidhaa zitakazozalishwa kukidhi viwango vya kimataifa.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Rosemary Silaa, ameeleza kuwa kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha asilimia 83 ya mahitaji ya mipira ya mikono nchini, ambapo, bodi itahakikisha inaisimamia ipasavyo MSD kufuata kanuni, taratibu na sheria.

Amesema wapo kwenye hatua za kutekeleza mkakati wa kampuni tanzu itakayosimamia shughuli nzima za uzalishaji na MSD kubaki na wajibu wake wa kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai,  aliwasilisha kwa kamati hiyo taarifa ya mradi na kuomba ongezeko la fedha  ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji ipasavyo mwezi Julai mwaka huu na kuwaomba wajumbe hao wa Kamati ya PAC kuwa mabalozi wa mradi huo


 Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai,  aliwasilisha kwa kamati hiyo taarifa ya mradi huo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Rosemary Silaa, akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo.
Muonekano wa kiwanda hicho kilichopo Idofi Makambako wilayani Njombe.
Muonekano wa mipira ya mikono inayotengenezwa na kiwandani hicho.
Viongozi wa MSD wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati hiyo.
 

Wednesday, March 15, 2023

MAFUNDI 1800 KUKUTANA KWENYE KONGAMANO MJINI IRINGA MACHI 17, 2023

Mafundi umeme wakiwajibika sehemu ya mafunzo.


Na Mwandishi Wetu, Iringa

ZAIDI ya mafundi 1800 wa aina mbalimbali wanatarajia kukutana pamoja katika kongamano kubwa litakalo fanyika Mjini Iringa lengo kubwa likiwa kupanua wigo wa ajira na kuongeza fursa kwenye kundi hilo muhimu kwenye jamii.

Meneja wa FundiSmart, Fabian Mwiga amesema kongamano hilo litafanyika Machi 17, 2023 katika ukumbi wa Masiti, Manispaa ya Iringa.

Kiuhalisia, mafundi ni kati ya kundi lililoachwa pembeni licha ya kuwa vitu vingi zinavyoizunguka dunia vinatokana na uwepo wa fundi.

 “Tunawakutanisha mafundi mbalimbali bila kujali aina ya ufundi wao, mpaka sasa tunao mafundi 1800 waliojiandikisha,” amesema Mwiga.

Amesema kwenye kongamano hilo mafundi watapata fursa ya kujua umuhimu na thamani ya kazi yao, elimu ya afya na bima, fedha, sheria, akiba na huduma bora kwa wateja.

“Sekta ya ufundi ni nyeti na mafundi wanazo ndoto zao, sasa wanaweza kufikia ndoto zao ikiwa tutawaonyesha mlango wa kupita, FundiSmart imekuja kwa ajili hiyo,” amesema Mwiga.

Amesema kwa sababu kundi hilo limekuwa likilalamikiwa zaidi na wateja hasa kwenye suala la uaminifu, elimu kuhusu sheria na huduma kwa wateja itawasaidia zaidi.

Kwa upande wao baadhi ya mafunzi wamesema hakuna siku waliketi pamoja na kutambuliwa kama sekta nyeti.

‘Hata tukifanya kazi mtu anakulipa atakavyo bila kujali kazi kubwa unayofanya, naamini hii ni fursa kwetu kutambua kazi yetu na kuipatia kipaumbele,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo.

Fundi Washi akiwajibika.
Mafundi Washi wakiendelea na kazi.
Fundi magari akiwa kazini
Fundi Seremala, Joseph Msoffe wa mkoani Morogoro akitengeneza milango katika Workshop yake.
 

Sunday, March 12, 2023

TACAIDS YAWASILISHA TAARIFA KUHUSU MUUNDO NA MAJUKUMU YAKE KWA KAMATI YA BUNGE AFYA NA UKIMWI

   Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu, Mhe George Simbachawene  akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI walipokutana na TACAIDS wakati wa wasilisho la muundo na majukumu ya TACAIDS kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika Ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma, Leo Machi,12, 2023.

Na Nadhifa Omar, Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe.George Simbachawene amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kutoa ushirikiano unaostahiki kwa kamati ya Afya na masuala ya UKIMWI kutekeleza majukumu kwa kufuata miongozo,maoni na ushauri unaotolewa na kamati hiyo.

Kauli hiyo amaitoa leo Machi12 ,2023 baada ya Tume ya kudhibiti UKMWI Tanzania (TACAIDS) kuwasilisha Taarifa kuhusu muundo na majukumu yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika Ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma.

Awali akiwasilisha taarifa hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amesema TACAIDS ni Idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na imeanzishwa kwa mujibu wa sheria Na.22 ya mwaka 2001 na Marekebisho yake Na.6 ya mwaka 2015, sheria hiyo ni kwa ajili ya Tanzania Bara pekee. Zanzibar ipo Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).

Dkt. Maboko ameyataja majukumu ya TACAIDS kuwa ni kuandaa sera na miongozo kwa ajili ya mwitikio wa UKIMWI nchini pamoja na kusimamia athari zake, kusimamia mpango mkakati kwa ajili ya mipango ya programu za UKIMWI pamoja na masuala mtambuka yahusuyo virusi vya UKIMWI na UKIMWI.

Kujenga mahusiano ya kitaifa na kimataifa kwa watu wote wenye UKIMWI kwa kufanya uratibu wa masuala ya UKIMWI,kutafuta raslimali fedha ,kuzigawa na kuzifuatilia katika programu za Mwitikio wa UKIMWI,kusambaza taarifa kuhusu UKIMWI na madhara yake na programu za kuzuia na kudhibiti.

Kukuza tafiti ,upashanaji taarifa na kutunza kumbukumbu zinazohusiana na udhibiti wa UKIMWI nchini,kukuza uraghibishi na utoaji wa elimu kwa ngazi ya juu kuhusu kuzuia na kudhibiti UKIMWI, kufuatilia na kutathimini shughuli zote za UKIMWI zinazotekelezwa nchini.

Aidha ameongeza kuwa shughuli nyingine ni Kuratibu shughuli zote za UKIMWI na kuzisimamia kwa mujibu wa mkakati wa Taifa wa UKIMWI, kwa kushirikiana na sekta binafsi husika kuwezesha juhudi za upatikanaji wa tiba na kuhamasisha upatikanaji wa tiba na matunzo na chanjo.

Jukumu lingine ni kuhamasisha haki na wajibu kwa watu wanaoishi na VVU ,kuhamasisha WAVIU kuishi kwa matumaini na kushauri serikali kuhusu masuala yote yanayohusu kuzuia na kudhibiti UKIMWI ,kutambua vikwazo katika utekelezaji wa kuzuia na kudhibiti katika sera na programu ,kusimamia shughuli zote zinazohusiana na kuzuia na kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI,pamoja na kushirikiana na sekta nyingine husika,kufanya shughuli nyingine za kuzuia na kudhibiti VVU na UKIMWI.

Dkt. Maboko amesema utekelezaji wa majukumu ya TACAIDS unaongozwa na sera ,sheria ,kanuni ,mikakati na miongozo ikiwa ni pamoja na sheria ya tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania Na,22 ya mwaka 2001na marekebisho yake Na6 ya mwaka 2015,Sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001.

Mwongozo wa uraghibishi na mabadiliko ya tabia,Mwongozo wa VVu na UKIMWI  na magonjwa sugu yasiyoambukiza, mwongozo wa kusshughulikia makundi maalum kuhusu UKIMWI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ,mwongozo wa jinsia na UKIMWI

,Mwongozo wa UKIMWI na haki za binadamu ,Mwongozo wa kufundishia kamati za kudhibiti UKIMWI ngazi za Halmashauri,kata na vijiji, pamoja na mwongozo wa kuunda kamati za kudhibiti UKIMWI kwenye mikoa,mwongozo wa kuunda kamati za kudhibti UKIMWI kwenye Halmashauri.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe Stanslaus Nyongo iliipongeza TACAIDS kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kudhibiti na kupunguza maambukizi ya VVU nchini na kuagiza kuendelea kufanyia kazi ushauri na maekezo yaliyotolewa na kamati hiyo,ikiwa ni pamoja na kufanya ufatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya kamati za kudhibiti UKIMWI ngazi za chini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Stanslaus Nyongo akizungumza na wajumbe pamoja na watendaji wa TACAIDS na Ofisi ya Waziri Mkuu waliohdhuria kikao cha kamati hiyo walipokutana leo jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt Leonard Maboko akiwasilisha Muundo, na Majukumu ya TACAIDS kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakati wakikaokilichfanyika leo jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene na Katibu Mkuu Dkt. Jimmy Yonaz (kulia) wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt Leonard Maboko alipokuwa anawasilisha Muundo na Majukumu kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Seif Salum Seif akichangia wakati wa kikao cha kamati hiyo na TACAIDS kuhusu kubadilisha jumbe zinazotumika kwenye vibao vya ujenzi vinavyo tumia maneno ya Unyanyapaa.

Mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya  na masuala ya UKIMWI Mhe Hassan Mtega akichangia wakati wa kikao cha kamati hiyo umuhimu wa TACAIDS kufatilia utekelezaji wa majukumu ya kamati za UKIMWI za ngazi za chini. 

Friday, March 10, 2023

KATAMBI: HALMASHAURI ACHENI URASIMU MIKOPO MNAYOTOA KWA VIJANA, WANAWAKE NA WALEMAVU

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akiwa ameshika keki maalumu aliyoandaliwa na Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye Ulemavu Sabasaba-Singida  wakati wa ziara yake mkoani hapa ya kukagua shughuli mbalimbali zilizo chini ya wizara yake.

Na Dotto Mwaibale, Singida

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, amezitaka Halmashauri za Wilaya na Manispaa nchini kuacha urasimu wa kutoa fedha zilizotolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu zinazotokana na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri hizo.
Katambi alitoa maagizo hayo juzi katika ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa inayotokana na asilimia 10 za mapato ya halmashauri wakati akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi mkoani hapa.
Hatua ya Katambi kutoa maagizo hayo ilifuatia baada ya Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana Chapa Kazi, Mwanahamisi Omari, kulalanikia kucheleweshewa kupatiwa fedha za kulipia tripu 50 za mchanga wanaotumia kufyatua matofali baada ya halmashauri hiyo kuwapa mkopo wa Sh. Milioni 25.
“ Mheshimiwa Naibu Waziri tunachangamoto kubwa ambayo inatukwamisha na kushindwa kuendelea na ufyatuaji wa matofali fedha yetu tuliopewa awali imekwisha sasa ni siku ya tatu kila tukienda pale halmashauri tunapigwa danadana hasa pale ofisi ya Maendeleo ya Jamii mara tunaambiwa hela hizo zitatolewa mpaka mhandisi aje kwenye mradi kuhakikisha kama mchanga huo upo, mara tumsubiri mkurugenzi jambo ambalo linatuchelewesha,” alisema Omari.
Katambi baada ya kupokea malalamiko hayo akazitaka halmashauri zote kuacha kufanya urasimu huo ukizingatia kuwa fedha hizo zinatolewa na halmashauri kwa lengo la kuyasaidia makundi hayo na unapojitokeza urasimu huo unarudisha nyuma maendeleo ya walengwa hao.
Aidha, Katambi aliagiza taasisi zote za Serikali zinapotekeleza miradi ikiwemo ya maji na ujenzi wa madarasa na miundombinu mbalimbali itoe kazi hizo kwa kununua matofali, vifaa vya chuma  na vifaa vingine kutoka katika vikundi hivyo ili vikuze mitaji yao.
Katambi alisema taasisi hizo zinapofanya sherehe zao hasa katika mikoa ambayo ina vyuo vya ufundi ziwe zinakwenda kununua keki, upambaji na sare zinazotengezwa na wanafunzi wa vyuo hivyo zikiwemo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na bendera ya Taifa ili kuviinua kiuchumi badala ya kwenda kuagiza nje.
Aliwaomba wataalamu waliopo inapotekelezwa miradi hiyo kujenga tabia ya kuvitembelea vikundi hivyo na kutoa elimu ya namna ya matumizi ya fedha hizo jambo litakalosaidia kupata bidhaa bora zinazozalishwa pamoja na kuondoa matumizi mabaya ya fedha zilizotolewa kwenye vikundi.
Akizungumzia kukua kiuchumi kwa vyuo hivyo, aliwataka walengwa hao kuondoa dhana ya kuwa wajasiriamali badala yake wawe wafanyabiashara wa kati na hata kufikia hatua ya kufungua makampuni yao makubwa kutokana na kazi zao wanazo zifanya na kuziomba halmashauri kutoa maeneo kwa bei nafuu kwa makundi hayo ili wajenge ofisi zao na kufungua viwanda.
Katambi pia aliziagiza halamashauri kuviongezea vikundi vinavyofanya vizuri kurejesha mikopo inayokopeshwa akikitolea mafano kikundi cha vijana cha St.Vidicon Manyoni Computer Workshop ambacho kilianzishwa Julai 2020 chini ya umoja wa mafundi wenye ujuzi wa fani mbalimbali waliokubaliana kufanya kazi kwa kushirikiana.
Aliongeza kuwa wanafunzi wanaopata fursa ya mafunzo ya miezi mitatu yanayowezeshwa bure na Ofisi ya Waziri Mkuu wanapomaliza mafunzo yao halmashauri iwe inawapa mikopo kwa ajili ya kufungua viwanda vidogo vidogo badala ya kukaa mitaani na ujuzi wao.
Katika ziara hiyo Katambi alitembelea miradi ya vijana hao katika wilaya za Manyoni, Ikungi, Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa watu wenye Ulemavu Sabasaba kilichopo Manispaa ya Singida, Shamba Kitalu Nyumba lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida Ilongero na kukagua ujenzi wa ukumbi wa CCM unaojengwa wilayani Manyoni.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akimlisha keki mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akisalimiana na Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani mara alipowasili wilayani Manyoni kuanza ziara yake hiyo juzi mkoani hapa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi,  akikagua ujenzi wa ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni.
Ukaguzi wa ukumbi huo ukiendelea. Kushoto ni Mjumbe wa Halimashauri Kuu CCM Wilaya ya Manyoni, Mjumbe wa Baraza  UVCCM Mkoa wa Singida na Mjumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Ukumbi wa CCM Wilaya ya Manyoni,  Ngwigula Shigela.
Afisa Maendeleo ya Jamii, Wilaya ya Manyoni, Flavia Kiwango (kulia) akisoma taarifa ya miradi ya maendeleo ya Vijana wilayani humo mbele ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi (kushoto), Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Elias Mollel na wa pili kulia ni Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani.
Mwenyekiti wa kikundi cha vijana cha St.Vidicon Manyoni Computer Workshop, Fidel Timoth (kulia) akisoma taarifa ya kikundi hicho kwa Naibu Waziri Katambi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akikagua vifaa vinavyotengenezwa kwa chuma na kikundi cha vijana cha St.Vidicon Manyoni Computer Workshop, 
   Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akiwa amekaa na msafara wake na maofisa kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Singida kwenye sofa zilizotengenezwa na kikundi cha Vijana cha St.Vidicon Manyoni Computer Workshop wakati wa ukaguzi wa shughuli za vijana waliopata mkopo kutoka halmashauri. 

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akielekeza jambo baada ya kuangalia majiko yaliyotekenezwa na vijana wa kikundi cha St.Vidicon Manyoni.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akisalimiana na mmoja wa WanaKikundi cha Vijana cha Chapakazi cha Wilaya ya Ikungi, Ashura Abubakari baada ya kuwasili wilayani hapo juzi katika ziara yake hiyo ya kikazi.
Vijana wa Kikundi cha Chapa Kazi cha Ikungi, wakinyoosha mikono mbele ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha nyingi kwa ajili ya kuendesha miradiya maendeleo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akikagua matofali yanayofyatuliwa na Vijana wa Kikundi cha Chapakazi cha Wilaya ya Ikungi. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mwanahamisi Omari. Na kushoto ni Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi katika shughuli hiyo, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Dijovson Ntangeki.


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi (kulia)  akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Ikungi na Vijana wa Kikundi cha Chapakazi wakati akikagua Shamba la Kitalu Nyumba lililopo nje ya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi,  Richard Rwehumbiza
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu cha Sabasaba, Fatuma Malenga baada ya kufika chuoni hapo wakati wa ziara yake hiyo ya kikazi. Katikati ni Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Ally Mwendo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akizungumza na mwanafunzi wa fani ya ushonaji nguo wa chuo hicho.Janeth Lucas.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akiangalia nguo za CCM zilizoshonwa na wanafunzi wa chuo hicho.
Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, akimlisha keki mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho wakati wa ziara ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, 
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Patrobas Katambi, akizungumza na Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana na Wanagenzi cha Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ilongero, Frida Dastan, baada ya kutembelea Shamba Kitatu cha zao la nyanya zinazilimwa na vijana hao baada ya kupatiwa mkopo wa Sh.Milioni 10.