Friday, July 28, 2023

DC SINGIDA : WAFANYABIASHARA VIPODOZI SHIRIKIANENI NA SERIKALI KATIKA KUDHIBITHI VIPODOZI VYENYE SUMU

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, akizungumza na Wafanyabiashara wa Vipodozi Mkoa wa Singida Julai 27, 2023, wakati akifungua kikao cha TBS na wafanyabiashara hao cha kutoa elimu juu ya uelewa kuhusu vipodozi vyenye viambata sumu.

.......................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili amewataka wafanyabiashara wa vipodozi mkoani hapa kushirikiana na Serikali pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kudhibiti bidhaa zenye viambata vyenye sumu.

Mragili alitoa ombi hilo wakati akifungua kikao cha TBS na wafanyabiashara cha kutoa elimu juu ya uelewa kuhusu vipodozi vyenye viambata sumu Mkoa wa Singida.

Hatua ya TBS kutoe elimu hiyo ilifuatia maombi yaliyotolewa na wafanyabiashara hao kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwezi Mei, 2023 wakati maafisa wa TBS walipoanzisha operesheni ya kupita katika maduka ya vipodozi kwa lengo ya kuondoa bidhaa hizo katika soko ambazo zinaathari kwa binadamu.

“Mwezi Mei mliniletea malalamiko kuwa maafisa wa TBS wamefika kwenye maduka yenu na kuanza kuondoa vipodozi ambavyo havikubaliki kwa matumizi ya binadamu mkidai operesheni hiyo ilikuwa ikifanyika bila ya kupewa uelewa wa matumizi ya bidhaa hizo, niliona mlikuwa na hoja ya msingi licha ya TBS kutangaza jambo hilo tangu mapema ndipo nilichukua uamuzi wa kuwazuia maafisa hao ili mpate mafunzo hayo na twende pamoja,´alisema Mragili.

Alisema anawapongeza sana TBS kwani baada ya kuwazuia kutokana na uungwana wao licha ya kuwa walikuwa wakitekeleza wajibu wao kisheria Mwezi Juni 2023 walirudi tena Singida na kufanya kikao na wafanyabiashara hao na kuwapa elimu na sasa wamerudi tena kwa mara nyingine kwa lengo lilelile.

Alisema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ndio limepewa jukumu la kusimamia vipodozi hivyo kupitia Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019 ambapo limekuja na mkakati  wa kuelimisha wananchi juu aina ya vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku kwenye soko la Tanzania ikiwa ni pamoja na kuendesha ukaguzi wa kushtukiza kwenye soko kwa lengo la kuviondoa , kutoa elimu kwa umma na kuvisajili.

Mragili alisema kuendelea kuviuza na kuvitumia vipodozi hivyo ni hatari kwani wanaliangamiza taifa jambo ambalo ni hatari na halikubaliki na kwamba baada ya mafunzo hayo hategemei kuona bidhaa hizo zikiendelea kuwepo kwenye soko ambapo alitoa tahadhari kwa wafanyabiashara hao kuviondoa mara moja kabla havijakutwa na maafisa wa TBS na kuvikamata.

“ Baada ya mafunzo haya hatutakuwa na huruma na mfanyabiashara yeyote atakayekamatwa akiendelea kuwa na vipodozi hivyo kwenye soko na hasije akatuambia ni bahati mbaya ninyi mnamtandao mkubwa nendeni mkawaambie na wenzenu kwani wanaoathirika navyo si wale tu mnaowauzia bali na ndugu zenu pia,” alisema Mragili.

Aliwataka wafanyabiashara hao waache kuangalia upande mmoja tu wa kuwa watakosa fedha bali wawe na dhamira ya kulinda afya za watanzania.

Awali akitoa mafunzo hayo Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka alisema matumizi ya vipodozi hivyo vyenye viambata vyenye sumu ni hatari kwa afya ya binadamu na vimekuwa vikiwaathiri watu wengi na kuliongezea taifa gharama kubwa ya kuwatibu waathirika na kupunguza nguvu kazi ya taifa.

Alivitaja vipodozi visivyo salama ni vile ambavyo vina kemikali zinazoweza kuudhuru mwili na kuusababishia matatizo, ambavyo havijasajiliwa na TBS, vipodozi vyenye viambata (kemikali) vya sumu na vilivyopigwa marufuku, ambavyo muda wake wa matumizi umeisha, vipodozi ambavyo havioneshi tarehe ya kuharibika  (Expire-date).

Vingine ni vile ambavyo maelezo yake hayajaandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza ambavyo vinaweza vikawa ni mafuta, losheni, krimu, pafyumu, poda na kadhalika.

Mwabuka alitumia nafasi hiyo kuwataka wafanyabiashara wa vipodozi hivyo kupeleka taarifa za vipodozi wanavyouza ikiwa ni pamoja na kuvisajili kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wake., hatua itakayowasaidia kujua ni vipodozi vipi vimepigwa marufuku na vile vinavyoruhusiwa kwenye soko la Tanzania.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wauzaji wa Vipodozi Mkoa wa Singida, Pili Hussein akizungumza kwa niaba ya wenzake aliomba Serikali kuwadhibiti wafanyabiashara wakubwa wa bidhaa hizo ambao wamekuwa wakiwauzia.

“Tunashindwa kuelewa kuna vyombo husika vya ukaguzi katika bandari, viwanja vya Ndege na mipakani ambako bidhaa hizi zinapitishwa na wafanyabiashara wakubwa na kusajiliwa ambao wanafahamika lakini wanaacha kuwadhibiti hadi zikifika kwetu ndio wanakuja kuzikamata jambo hili sio zuri kwani linaturudisha nyuma na kufilisi mitaji yetu,” alisema Hussein.

Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka, akitoa mada kuhusu uelewa wa vipodozi na madhara yake kwa wafanyabiashara hao.
Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango, akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili kufungua mafunzo hayo ya siku moja.
Wafanyabiashara wa vipodozi Mkoa wa Singida wakiwa kwenye mafunzo hayo
Washiriki wa mafunzo wakifuatilia mada iliyokuwa kuwa ikitolewa na Meneja wa TBS Kanda ya Kati, Nickonia Mwabuka.

Taswira ya mafunzo hayo.
 

Wednesday, July 26, 2023

RC SINGIDA: NIT- KIFANYENI CHUO CHENU KUWA MAHALI SAHIHI PA KUPATIA MAFUNZO STAHIKI

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa, akimkabidhi zawadi Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kozi ya Maafisa Usafirishaji na Madereva Wakuu wa Taasisi za Umma na Halmashauri zote hapa nchini uliofanyika Julai 26, 2023 katika Ukumbi wa RC Misheni mjini hapa. Kulia ni Mkuu wa Kituo cha Mafunzo Endelevu cha NIT, Bahati Mabina.

........................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida 

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ametoa wito kwa Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuendelea kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili kukifanya chuo hicho kuwa mahali sahihi pa kupatia mafunzo stahiki. 

Wito huo umetolewa na Serukamba kwa niaba yake na Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango wakati akizindua kozi ya Maafisa Usafirishaji na Madereva Wakuu wa Taasisi za Umma na Halmashauri zote hapa nchini uliofanyika Julai 26, 2023 katika Ukumbi wa RC Misheni mjini hapa.

 

“Nimeisikia hotuba ya Mkuu wa Chuo, Profesa Zacharia Mganilwa  kuhusu umuhimu wa mafunzo haya kwenu binafsi na serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan naamini baada ya mafunzo haya mtakuwa mabalozi wazuri wa chuo chetu hiki  kwenye utoaji wa mafunzo mbalimbali ya operesheni za usafirishaji pamoja na Taasisi zenu mnazofanyia kazi,”alisema Mwangomango.

 

Alisema kuwepo kwa mafunzo hayo ni matokeo ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia waliowezesha kuwepo kwa Mradi huo wa East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambao ni mkopo wa Serikali.

 

‘Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kimepewa jukumu kubwa la kuwaandaa wataalamu waliobobea katika nyanja tano za Usafirishaji. Lakini leo nimejikita kwenye usafiri wa barabarani ambapo mmekuwa mkituzalishia maafisa usafirishaji na madereva wenye weledi mkubwa. Ombi langu kwa chuo ni kuhakikisha kinatoa mafunzo haya mara kwa mara ili wataalamu hawa waendane na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia," alisema Mwangomango.  

Alisema ubunifu si jambo la kufumbia macho hata kidogo hasa katika ukuaji huu mkubwa wa teknolojia ambapo aliwaomba washiriki wa mafunzo hayo kuwa wabunifu na kusoma kwa bidii ili watakapomaliza waweze kuongeza tija katika vituo vyao vya kazi.

 

Mwangomango alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa chuo, wanataaluma na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanafanyika katika Mkoa wa Singida kwa kanda ya kati na kueleza kuwa wangeweza kuamua yakafanyike mikoa mingine. 

Awali akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua mafunzo hayo, Mkuu wa chuo hicho, Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa alianza kwa kutoa historia fupi ya chuo hicho kuwa kilianzishwa mwaka 1975 ili kuwaandaa wataalamu watakaoziba pengo lilosababishwa na kuondoka kwa Wataalamu na kisha kuunda Makampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA), Kamata,Usafiri wa mabasi ya mikoani, Uchukuzi wa Mizingo , Usafiri wa Maji mwambao wa Pwani  (TACOSHILI ) na kuwa makampuni hayo yalianzishwa na Shirika la Taifa la Uchukuzi (NTC) kwa niaba ya Serikali ili kuziba pengo la Wataalam wa Usafirishaji nchini.

Alisema chuo hicho kwa sasa kipo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kinaendesha Mradi wa Kikanda wa East AfricaSkills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kueleza kuwa mradi huo unatekelezwa katika nchi tatu yaani Tanzania, Kenya na Ethiopia ili kuwezesha muingiliano wa kijamii katika nchi za ukanda wa Afrika.

Alisema ndani ya nchi hizo kuna vituo vya umahiri 16 ambapo kwa hapa nchini kinaitwa Kituo cha Umahiri cha Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji.

Alisema kituo hicho kwa upande mmoja kimelenga kufundisha wataalam wa usafiri wa Anga Marubani, wahandisi wa Ndege, Wahudumu ndani ya Ndege ambapo kwa upande wa wataalam wa usafirishaji walengwa ni wataalam wa usafiri wa njia ya reli,maji na kwa kozi hiyo walengwa ni wataalam wa njia ya barabara. 

Alisema katika kufikia malengo ya mradi, chuo kinajukumu la kuandaa mitaala inayokidhi matakwa ya soko la Ajira, kuongeza ushirikiano na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi kwa kuwa na mikataba ya ushirikiano, Kuboresha Miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, kuzifikia Taasisi zingine ambazo ziko nje ya Mradi na kutoa mafunzo.

Alisema katika kulifikia lengo namba nne la utekelezaji wa mradi huo , chuo kimeandaa mafunzo ya siku tano kwa ajili ya Maafisa Usafirishaji na Madereva Wakuu kwa lengo la kuwajengea, Ujuzi wa Usimamizi,Uendeshaji na Matengenezo ya Magari. 

Aidha, Mganilwa alisema mafunzo hayo yatafanyika katika Kanda mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani kuanzia Julai 10, 2023 hadi Januari 26,

 2024. 

Alizitaja Kanda saba ambazo yatafanyika mafunzo hayo kuwa ni Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kusini, na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar na kuwa mshiriki kutoka serikalini alipaswa kuchangia ada ya kiasi cha Sh.500,000 hata hivyo gharama hizo za ada atalipiwa kupitia fedha za mradi ambapo washiriki wanaotoka sekta binafsi chuo kilipunguza ada kutoka Sh. 500,000  mpaka Sh.250,000 ili kuhakikisha wataalamu hao wanapata ujuzi unaotakiwa.  

Profesa Mganilwa alisema kozi hiyo ya muda mfupi itawaongezea umahiri katika kutumia ipasavyo vipuli vya magari na vilainishi, kufanya ukaguzi wa magari, kuhakikisha matumizi sahihi ya mafuta, kuratibu matumizi sahihi ya matairi na kuboresha uendeshaji wa magari kwa ujumla na kuwa matumaini yake washiriki hao watakua mabalozi wazuri wa mafunzo hayo kwa kuzingatia kuwa wamebahatika kuwa kanda ya pili kati ya kanda nane za Tanzania. 

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Mafunzo Endelevu cha NIT, Bahati Mabina alisema washiriki waliobahatika kupata mafunzo hayo ni 42, madereva wakiwa ni 16 na maafisa Usafirishaji 26 na kuwa ni ya siku tano. 

Imani Octavian mshiriki wa mafunzo hayo kutoka makampuni binafsi akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake alisema wamejifunza mengi kupitia mafunzo hayo na kuwa wanaenda kuwa mabalozi kwa wenzao.

Alisema mafunzo hayo yamelenga kuwaepusha na uingiaji wa gharama kubwa ya uendeshaji wa kazi zao kwa kutumia magari kama vile matumizi ya mafuta, matairi na matengenezo na kuwa maeneo yote hayo matatu yameguswa na wakufunzi wa mafunzo hayo.

Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Goodluck Mwangomango akizindua kozi hiyo.
Mkuu wa Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa, akitoa historia fupi ya chuo hicho na malengo ya kozi hiyo.
Mkuu wa Kituo cha Mafunzo Endelevu cha NIT, Bahati Mabina, akizungumzia washiriki wa mafunzo hayo.
Afisa Uhusiano Mkuu wa chuo hicho, Tulizo Chusi, akizungumza kabla ya kuzinduliwa kozi hiyo.
Washiriki wakiwa kwenye uzinduzi wa kozi hiyo.
Kozi ikizinduliwa.
Washiriki wakiwa kwenye kozi hiyo.
Uzinduzi wa kozi hiyo ukiendelea.
Wakufunzi wa kozi hiyo wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Kozi ikizinduliwa.
Taswira ya kozi hiyo.
Picha ya pamoja na amgeni rasmi.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi. 

Sunday, July 16, 2023

MBUNGE GEKUL: WANANCHI KUWENI WATULIVU SERIKALI IPO KWENYE MCHAKATOTO WA KUANDAA FIDIA ZENU

Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul, akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika ziara yake aliyoianza hivi karibuni jimboni humo.

......................................................

Na Mwandishi Wetu, Babati

MBUNGE wa Jimbo la Babati Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul amewataka wananchi ambao nyumba zao zitapitiwa na ujenzi wa njia ya ‘Bypass’ kuwa watulivu kwani Serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa fidia zao.

Gekul ameyataja  maeneo yatakayo athirika na ujenzi huo ni pamoja na Mitaa ya Hangoni,Kwere,Mrara na Wang'waray.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi ambayo ameianza baada ya vikao vya bunge la bajeti kumalizika hivi karibuni Gekul amesema kuanzia mwezi wa Septemba waathiriwa wa kupisha ujenzi huo ambao tayari wamekwisha tambuliwa baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufanya tathimini na kupima ujenzi wa barabara hiyo wataanza kulipwa.

Ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika utaongeza pato la ndani la Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwani pia itapita kwenye geti la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Wakati huo huo Mbunge Gekul amewasisitiza wazazi na walezi kuwapelekea watoto wao shuleni ili baadae waje kuwa watu muhimu katika familia na Taifa kwa ujumla.

Gekul ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika Shule ya Msingi Ayabadiney iliyopo Kata ya Bonga wilayani Babati.

Mbunge Gekul (katikati) akiwa kwenye mkutano huo.
Wananchi wakimsikiliza mbunge wao (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
 

WATAALAM SEKTA YA AFYA BABATI WATOA CHANGAMOTO ZAO KWA MBUNGE GEKUL, WANUFAIKA WA TASAF NAO WAIBUKA

Mmoja wa Wataalam wa Sekta ya Afya Hospitali ya Mji Babati mkoani Manyara akielezea changamoto walizonazo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi.

...............................................

Na Mwandishi Wetu, Babati

WATAALAM wa Afya wa Hospital ya Mji Babati mkoani Manyara wametoa malalamiko yao kwa Mbunge wa Jimbo la Babati Mji Pauline Gekul kutokana na changamoto wanazozipitia kwenye masuala  ya kiutumishi.

Wataalam hao wametoa malalamiko hayo baada ya kukutana na mbunge huyo katika ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, ziara ambayo anaifanya jimbo jimbo lote baada ya kumalizika kwa vikao vya bunge la bajeti hivi karibuni.

Baadhi ya malalamiko waliolalamikia ni ufinyu wa kikokoteo baada ya kustaafu, kutopandishiwa mishahara baada ya kumaliza masomo Yao pindi wakiwa Kazini pamoja na kucheleweshewa kwa pindi wanapohamishwa vituo vya kazi.

Hivyo wamemuomba Mbunge huyo kupelekea malalamiko yao Bungeni ama kwa Waziri husika ili wajue namna ya kutatua changamoto zao.

"Nilikuwa sijui kuhusu changamoto hii nitazifikisha kwa wahusika naamini ndani ya muda zitafanyiwa kazi kwani ni jambo la kitaifa," alisema Gekul.

Wakati huo huo wakazi wa Mtaa wa Dawari Kata ya Bonga wameilalamikia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kutowalipa fidia zao ndani ya miezi mitatu baada ya kufanya kazi walizopangiwa kufanya ili kujikimu na kimaisha.

Malalamiko hayo yamekuja mara baada ya Mbunge wa Jimbo la Babati Mji Pauline Gekul kufanya ziara katika Kata hiyo ikiwa na lengo la kusikiliza na kutatua Kero za wananchi

Akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo Mkuu wa Idara ya TASAF wa Halmashauri ya Mji Babati, Esther alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo lakini malipo yao yameshindwa kukamilika kutokana na baadhi yao kufanya kazi nje na utaratibu na kuwa fedha za ruzuki ziko pale pale kwa wale ambao wamekithi vigezo  vya kufanya kazi za kijamii.

Watumishi hao wa Sekta ya Afya wakiwa kwenye mkutano huo wa Mbunge wa kusikiliza kero.
Kero zikiendelea kusikilizwa.
Kero zikitolewa. 

Friday, July 14, 2023

BOHARI YA DAWA (MSD) MFANO WA KUIGWA JUMUIYA YA NCHI ZA KUSINI MWA AFRIKA (SADC)

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD)  Mavere Tukai, akizungumza na wakuu  wa Taasisi za Bohari ya Dawa pamoja na viongozi wanaosimamia manunuzi ya bidhaa za afya katika  Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), baada ya kufanyika kwa mkutano wa siku mbili kwa viongozi hao uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 10, 2023 na kufikia tamati Julai 12, 2023 kwa wakuu hao kutembelea MSD kujionea shughuli mbalimbali zinavyofanyika zikiwamo za kuhifadhi Dawa na Vifaa Tiba.  

.................................................

Na Mwandishi Wetu 

WAKUU wa Taasisi za Bohari ya Dawa pamoja na viongozi wanaosimamia manunuzi ya bidhaa za afya katika  Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wameeleza kuwa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) imekuwa mfano wa kuigwa katika nchi za jumuiya hiyo.

Aidha wamesema MSD itakuwa chachu ya kuunganisha maendeleo na kukuza uchumi wa Afrika kutokana na ufanisi wake katika  upatikanaji wa uhakika wa dawa na bidhaa za afya.

Akizungumza leo Julai 12, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kufanyika kwa mkutano wa siku mbili kwa viongozi hao uliofanyika nchini Tanzania  Mwenyekiti wa wakuu hao Richard Biayi amesema wameona shughuli zinazofanywa na MSD na wameridhishwa nayo na wanaamini siku chache zijazo Afrika itashikamana hasa katika eneo la uagizaji bidhaa za afya.

Ameongeza  wakiwa MSD wametembelea ghala la kuhifadhi dawa na bidhaa za afya sambamba na kushuhudia uzalishaji wa barakoa kwenye kiwanda cha MSD kilichopo kwenye bohari hiyo na walichojifunza Tanzania imepiga hatua kwenye eneo hilo kupitia MSD.

Viongozi hao wapo nchini tangu Julai 10 kwa ajili ya kikao cha kujadili na kuboresha namna ya kununua dawa kinachotarajiwa kumalizika leo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameeleza kuwa uwepo wa viongozi hao kutoka jumuiya ya SADC imelenga kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu maboresho ya kimifumo katika uendeshaji bohari ya dawa.

"Ni kama tunabadilishana uzoefu na kila mmoja anajifunza, mfano wenzetu Zambia ni wazuri sana kwenye nishati mbadala kwa hiyo ni vema kujifunza ili nasi siku zijazo tupunguze gharama," alisema.

Ameongeza  mkutano wao wa mkakati wa manunuzi dhidi ya viongozi hao wa SADC ulihudhuriwa na nchi zote za Jumuia hiyo na ambao hawakuwepo walishiriki kwa njia ya mtandao na wametoka na mapendekezo kadhaa.

"MSD na secretarieti ya SADC tumejadili namna ya kuboresha manunuzi na tumetoa mapendekezo ta muda mfupi, wakati na mrefu.” amesema.

Aidha amesema  wamependekeza namna ya kuboresha mfumo wa manunuzi na kuboresha bidhaa za afya, usimamizi, rasilimali watu na fedha, malipo na mawasiliano.

“Mfano mfumo unatakiwa wa kidigitali maana tuko nchi mbalimbali hatuwezi kuwasiliana kwenye makaratasi… mapendekezo yakikubaliwa, vipaumbele vitawekwa na tutakwenda kwenye utekelezaji,” amesema Tukai.

Wakuu wa Taasisi za Bohari ya Dawa pamoja na viongozi wanaosimamia manunuzi ya bidhaa za afya katika  Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wakipata maelezo walipotembelea Bohari ya Dawa (MSD) Keko jijini Dar es Salaam.
Kazi ikiendelea.
Maelezo yakiendelea kutolewa kwa wakuu hao walipokuwa MSD.
Mmoja wa Wafanyakazi wa MSD akiendelea na kazi wakati wakuu hao kutoka SADC walipotembelea Bohari hiyo.
Wakuu hao kutoka SADC wakiwa katika ziara hiyo MSD.
 Wakuu wa Taasisi za Bohari ya Dawa pamoja na viongozi wanaosimamia manunuzi ya bidhaa za afya katika  Jumuia ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wakipatiwa maelekezo walipokuwa kwenye ziara hiyo ya kutembelea MSD.

Ziara ikiendelea.

Wakuu hao wakiwa kwenye ziara hiyo.

Ziara hiyo ikiendelea Bohari ya Dawa (MSD)

Wakuu hao wakiwa kwenye ziara hiyo.

Ziara ikiendelea.

 

AFISA VIJANA SINGIDA AWAPONGEZA WAZAZI KWA UTOAJI WA CHAKULA SHULENI

Afisa Vijana Mkoa wa Singida  Frederick Ndahani (wa pili kushoto) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Lishe wa Shule ya Msingi Nkalankala na Shule ya Sekondari ya Set Benjamin wakati akikagua chakula kilichopatikana kwa ajili ya wanafunzi wa shule hizo. 

Na Mwandishi Wetu, Singida 

AFISA Vijana Mkoa wa Singida  Frederick Ndahani ameupongeza Uongozi wa Shule ya Msingi Nkalankala na Shule ya Sekondari ya Set Benjamin pamoja na wazazi  wa Kata ya Nkalankala kwa kuamua kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni.

Ndahani ameyasema hayo wakati akifuatilia Ufundishaji na hali ya utoaji wa chakula shuleni katika Shule za Msingi na Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida.

Ndahani amewapongeza wazazi waliounda kamati ya Lishe ya shule na kusimamia ,utoaji wa elimu ya umuhumu wa chakula,ukusanyaji,utunzaji na upishi ambapo hadi sasa Shule ya Msingi Nkalankala imekusanya jumla ya magunia 90 ya Mahindi, maharage gunia 20 na mafuta ya chakula lita 350 na Shule ya Sekondari Set Benjamin tayari imekusanya magunia 33 ya mahindi,maharage gunia 12 ,mafuta ya chakula lita 150 na sukari kilogramu 25 hatua ambayo imesaidia wanafunzi wote katika shule hizo kupata chakula shuleni.

Nawashauri viongozi na wazazi kuiga mfano wa wazazi wa Nkalankala katika utoaji wa chakula shuleni na tukiamua tunaweza kuleta mapinduzi ya elimu mkoani Singida kwa sababu watoto sasa watapata chakula na kuwa watulivu darasani.

Kwa upende wake Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe katika Shule ya Sekondari Set Benjamin Abduli Silimu amesema wazazi baada ya kushirikishwa jambo hilo la uchangiaji wa chakula wamekubali  kutoa chakula cha kutosha ambacho kitatumika hadi msimu ujao wa chakula wa Juni 2024.

Katibu wa Kamati ya Lishe katika Shule ya Msingi Nkalankala,  Elizabeth Yona amesema wajibu wa wazazi ni kutoa huduma bora kwa watoto.

" Serikali ina wajibu wake, walimu na Sisi wazazi tunaowajibu wetu na moja ya wajibu ni kuwapatia chakula wanafunzi wakiwa shuleni na nje ya shule," alisema Yona.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Set Benjamin Jackiline Molel na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nkalankala iliyopo Mkalama wamesema wataendelea kusimamia utoaji wa Chakula Shuleni Kwa kushirikiana na Wazazi wa Kata ya Nkalankala.

Afisa Vijana Mkoa wa Singida  Frederick Ndahani na wajumbe wa kamati hiyo ya Lishe ya shule hizo wakikagua chakula hicho.
 

Tuesday, July 11, 2023

MBUNGE NGASSA: WANANCHI MSITETELEKE MPO SALAMA KWENYE MIKONO YA CHAMA CHA MAPINDUZI

Wakina mama wakimlaki Mbunge wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora, Nicholaus Ngassa wakati wa ziara yake aliyoifanya jimboni humo mara baada ya vikao vya Bunge la Bajeti kumalizika hivi karibuni, ambayo ilikwenda sanjari na mikutano ya hadhara. 

Na Mwandishi Wetu, Igunga 

MBUNGE wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora Mhe. Nicholaus Ngassa amewaomba wananchi wa jimbo hilo kutoteteleka  kwa kauli mbalimbali za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya watu, kuhusu maendeleo na kuwahakikishia kuwa chini ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Samoa Suluhu Hassan  wapo kwenye mikono salama na waendele kupokea miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa kupitia Ilani ya Chaka hicho.

 Ngassa ametoa kauli  hiyo wakati akizungumza na Wananchi kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara aliyofanya katika Vijiji na Vitongoji vya Kata ya Kinungu.

"Kinungu tumeleta umeme, barabara, maji ya visima  ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwa shule zote za sekondari na msingi na sasa mjiandae kupokea maji ya Ziwa Victoria kupitia mradi unaotekelezwa kwa thamani ya Sh. Bilioni 20  kutoka kwenye tenki linalojengwa Mlima wa Bulenya.

 Watoto wanasoma elimu bure bila malipo,tumeongeza upatikanaji wa madawa na vifaa tiba kwenye vituo vya afya na zahanati za vijijini, haya ndio maendeleo tuliyoahidi mwaka 2020 kwenye kampeni na tunaendelea kutekeleza, " alisema Ngassa.

Ngassa alisema hayo yote yanatekelezwa chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye anatoa fedha nyingi nchi mzima kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

" Binafsi nichukue nafasi ya kipekee kumshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi hii kubwa anayoifanya kwenye jimbo letu, mkoa wetu na Taifa kwa ujumla nawaomba ndugu zangu kwa iman zetu tuendelee kumuombea kwa Mungu ampe  afya na maisha marefu," alisema Ngassa.

Katika mikutano hiyo Mbunge Ngassa alipata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali na zile zilizokuwa ndani ya uwezo wake alizitafutia ufumbuzi wa papo kwa papo kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya  Igunga na zile zilizokuwa nje ya uwezo wake alisema ataziwasilisha kwa wahusika

Wananchi wa Kitongoji cha Migunga  Kata ya Igunga wakimpokea kwa shangwe Mbunge wao kipenzi  Nicholaus Ngassa wakati wa ziara yake jimboni humo.
Mbunge Ngassa (kushoto) akitoa maelekezo ya ukarabati wa Zahanati ya Mwamapuli kwa Muuguzi Afya wa zahanati hiyo.
Mbunge Ngassa akiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza  wa Shule ya Msingi Mwamapuli Kata ya Kinungu, aliowavalisha sare ikiwa ni utekelezaji  wa programu ya kugawa sare kwa wanafunzi wa darasa hilo jimboni humo 
Wananchi wa Kitongoji cha Mwanunili Kijiji cha Mwamapuli Kata ya Kinungu wakimsikiliza Mbunge wao Ngassa alipokuwa akihutubia kwenye mkutano wa hadhara.
 

WAKUU WA TAASISI ZINAZOSIMAMIA MANUNUZI BIDHAA ZA AFYA NCHI ZA SADC WAKUTANA JIJINI DAR ES SALAAM, KESHO KUTEMBELEA MSD

Wakuu wa Taasisi zinazosimamia Manunuzi ya Bidhaa za Afya kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukutana jijini Dar es Salaam jana Julai 10, 2023 katika mkutano wa siku tatu.

Na Mwandishi Wetu

WAKUU wa Taasisi zinazosimamia Manunuzi ya Bidhaa za Afya kwa nchi za SADC wamekutana jana Julai 10, 2023 jijini Dar es Salaam, kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha mpango wa manunuzi ya pamoja ya bidhaa za afya kwa nchi za ukanda wa Kusini mwa Africa-SADC (SPPS).

Washiriki hao pamoja na mambo mengine watajadili namna bora ya kutekeleza mpango wa manunuzi ya pamoja ili kuweza kutekeleza mpango huo kwa ufanisi zaidi na kujadili mapendekezo yaliyotolewa na mshauri mwelekezi.

Nchi 16 Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo  ni wanachama wa mpango huo wa manunuzi ya bidhaa hizo za afya ni   Angola, Boswana, Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Seychellers,  Msumbiji, Namibia, Afrika ya Kusini, Eswatini, Tanzania , Zambia, Comoros, na Zimbabwe. 

Mkutano huo wa siku tatu ulianza jana Julai 10, 2023 na  utafikia tamati kesho Julai 12, 2023 kwa wakuu wa taasisi hizo  kutembelea Bohari ya Dawa (MSD) Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika zikiwamo za uhifadhi wa dawa na vifaa tiba.

Mshiriki wa mkutano huo kutoka Zambia akiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea
Washiriki wa mkutano huo wakibadilishana mawazo
Washiriki wa mkutano huo kutoka Eswatini wakiwa kwenye mkuano huo.
Washiriki wa mkutano huo wakibadilishana mawazo
Mkutano huo ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
Washiriki wakifuatilia mawasilisho yaliyokuwa yakitolewa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Washiriki kutoka Angola wakiwa kwenye mkutano huo.