Tuesday, January 31, 2023

KATIBU TAWALA SINGIDA: WAANDISHI WA HABARI KUWENI WAZALENDO KWA KUANDIKA HABARI ZENYE TIJA

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko (kushoto) akifungua mkutano wa Uhamasishaji wa Program ya Shule Bora kwa Wasimamizi wa vyombo vya habari na Wahariri Mkoa wa Singida uliofanyika leo Januari 31, 2023 wilayani Manyoni mkoani hapa.

Na Dotto Mwaibale, Manyoni

WAANDISHI wa Habari Mkoa wa Singida wametakiwa kuwa wazalendo kwa kuandika habari zenye tija kwa mkoa na Taifa kwa ujumla .

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko  wakati akifungua mkutano wa uhamasishaji wa program ya Shule Bora kwa Wasimamizi wa vyombo vya habari na Wahariri Mkoa wa Singida uliofanyika leo Januari 31, 2023 wilayani Manyoni mkoani hapa.

“Waandishi wa habari mnatakiwa muwe wazalendo kwa kuandika habari nyingi za maendeleo ili kuutangaza mkoa wetu na si kuandika zile zinazohusu mabaya tu japo hazikatazwi” alisema Mwaluko.

Aidha Mwaluko aliwataka wanahabari kwenda vijiji kuandika habari za uchunguzi ambazo zitasaidia kuibua changamoto za wananchi, watumishi wa afya na kada zingine na kwenye shule ili ziweze kufahamika na kupatiwa ufumbuzi.

Katika hatua nyingine Mwaluko alisema licha ya waandishi wa habari kuwa wengi mkoani hapa haridhishwi na utendaji wao na badala yake amewataka wabadilike ili wawe chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Singida.

Mwaluko alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wanahabri hao kuwa mwaka huu Mkoa wa Singida utafanya maadhimisho ya miaka 60 tangu uanzishwe mwka 1963 hivyo aliwaomba waandike habari mbalimbali njema zitakazoutangaza mkoa kuelekea kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika Oktoba mwaka huu.

Meneja Mawasiliano wa Shule Bora,Raymond Kanyambo akizungumzia program hiyo ya shule bora alisema ni program ya Serikali unaofadhiliwa na UKAID wenye lengo la kukuza na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji mashuleni ili kuboresha elimu na kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wa kike na wa kiume wanapata elimu bora.

‘Program hii ya miaka sita inatekelezwa katika Mikoa Tisa Tanzania Bara yaani Katavi, Rukwa, Dodoma, Singida, Mara, Simiyu, Pwani, Tanga na Kigoma. Mkoa wa Singida ni moja mojawapo ya mikoa ambayo program hiyo ya Shule bora inatekelezwa kwenye shule mbalimbali,"alisema Kanyambo.

Kanyambo aliongeza kuwa program hiyo imefadhiliwa na Uingereza kwa Paundi milioni Tisa ,ambapo unaifikia mikoa hiyo ili kuhakikisha watoto wote hata wale wenye changamoto mbalimbali wanapata fursa ya kusoma.

Alisema, program hiyo itaweza kuwaendeleza walimu kufundisha kwa ufanisi ili kuinua kiwango cha taaluma mashuleni na kuwa na mazingira bora ya ufundishaji na kuwa imelenga kuiunga mkono Serikali katika kuinua kiwango cha elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote.

Aidha, Kanyambo alisema mkutano huo umewashirikisha waandishi wa habari ili kushirikiana nao kutokana na umuhimu wao wa kupasha habari jamii na jinsi ya kuandika habari zinazohusu elimu na changamoto zake na kufanya uhamasishaji wa jamii, wazazi umuhimu wa masuala ya elimu kwa watoto .

“Tunahitaji ninyi waandishi wa habari mliopo kwenye halmashauri zote za wilaya kutuunga mkono katika jambo ili muhimu kwani sisi tunafanya kazi na vyombo vyote vya habari bila ya kuvibagua” alisema Kanyambo.

Mada kubwa iliyotolewa katika mafunzo hayo ni Mawasiliano ya program na ushiriki wa vyombo vya habari katika kufanikisha malengo ya program hiyo.

Mratibu wa Program hiyo Mkoa wa Singida, Samwel Daniel alisema program hiyo inawahusu wanafunzi wa shule za awali na msingi na kuwa walitoa mafunzo endelevu kwa walimu wakuu, mahiri na taaluma ambapo walimu 1774 wamenufaika nayo.

Meneja Mawasiliano wa Shule Bora,Raymond Kanyambo akizungumzia program hiyo.

Mkutano ukiendelea.

Kaimu Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Luganuzi Muwelu akichangia jambo kwenye mkutano huo.

Afisa Habari Manispaa ya Singida, Petronella Msechu akichangia jambo kwenye mkutano huo.

AfisaHabari Mwandamizi, Idara Habari Maelezo Ridhiwan Msisiri akizungumza kwenye mkutano huo.

Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.

Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Maria Lyimo akizungumza kwenye mafunzo hayo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi yaRais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ntenghenjwa Hosseah. na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko.
Mratibu wa Program ya Shule Bora Mkoa wa Singida, Samwel Daniel akitoa mada kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo.
Waandishi wa habari Elisante Mkumbo (kushoto) na Thobias Mwanakatwe wakiwa kwenye mkutano huo.
Maafisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Hadija Missanga (kushoto) na Rachel Japhet kutoka Mkalama wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakiwa kwenyemkutano huo. Kutoka kulia ni Nathaniel Limu, SeifTakaza na Elisante John.
Mkutano ukiendelea.
Taswira ya mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea..
Mkutanoukiendelea.
Mwanahabari Seif Takaza akizungumza kwenye mkutano huo.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja. 


Saturday, January 28, 2023

KATIBU MKUU JUMUIYA YA WAZAZI : WAZAZI TUJIKITE KUTOA ELIMU YA MAADILI KWA JAMII

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima akizungumza  na wananchi, Wana CCM na viongozi wa chama hicho wa Wilaya ya Singida katika mkutano uliofanyika Ofisi ya CCM  Mkoa wa Singida ikiwa ni moja ya matukio katika mfululizo wa ziara yake.

Na Dotto Mwaibale, Singida

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima, ametoa rai kwa wazazi kujikita katika jukumu la kutoa elimu kwa jamii kuhusu suala la maadili kutokana  na hivi sasa kuanza kujitokeza mfululizo wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia hapa nchini.

Akizungumza leo na wananchi,wanachama na viongozi wa CCM Wilaya ya Singida, amesema suala la malezi ya watoto ni jukumu la Jumuiya ya Wazazi kwani hivi sasa kumeanza kujitokeza mwenendo usiofaa kwa jamii katika nchi yetu.

"Kila tukikaa ndani ya siku mbili ukisikiliza vyombo vya habari wanakwambia kuna unyanyasaji wa kijinsia, mara utasikia baba kamuua mama,mara mama kauawa na mtoto au mama kaua mtoto au baba kampiga mama kipigo kikubwa,yote haya ni ukiukwaji wa maadili ambayo Jumuiya ya Wazazi inayakemea," amesema Kalima.

Kalima amesema Jumuiya ya Wazazi imeanza programu na msisitizo katika mambo mawili ambayo ni mafunzo na suala la kuimarisha uchumi wa jumuiya.

Amesema mafunzo ya kutosha yakifanyika viongozi watajua wao wa nini wanapaswa kulifanya badala ya hivi sasa ambapo inawezekana viongozi wanaochaguliwa wanakuwa hawafahamu majukumu yao.

"Leo hivi inawezekana Katibu wa Tawi amechaguliwa lakini hajui Kamati ya Utekelezaji inatakiwa ikutane mara ngapi kwa mwaka lakini baada ya mafunzo kufanyika kila kitu kitakwenda vizuri," amesema.

Kalima amesema Jumuiya ya Wazazi ikiwa imara maana yake chama, Jumuiya ya Vijana na Jumuiya ya Wanawake nayo itakuwa imara kwasababu Jumuiya ya Wazazi ni jumuishi na ni kiongozi wa jumuiya zote.

Amesemasema CCM ni chama imara ambacho kina muundo mzuri wa kiuongozi na ndio maana hivi karibuni vyama vya ukombozi Afrika ambavyo CCM ilivisaidia vilifika hapa nchini kujifunza kwasababu vinatambua CCM ni mwalimu wao kimuundo.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amesema serikali ihakikishe inaweka mkazo mabasi ya shule wahudumu wawe wanawake badala ya wanaume kwani imebainika nako kumekuwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto.

Kuhusu mpango wa Bima ya Afya kwa wote, alisema CCM na serikali yake ina nina ya kuhakikisha kila ila mwananchi anapata huduma za afya hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki katika mpango huo.

Kalima aliitaka Serikali kukataa misaada inayotolewa na wafadhili yenye masharti ya kutaka serikali kuruhusu vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.

" Tunaiomba serikali yetu tunajua,tumeshaona na tumesikia kuna baadhi ya misaada inayotolewa yenye masharti magumu masharti ambayo yanataka kuelekeza nchi ijikite kwenye mapenzi ya jinsia moja Jumuiya ya Wazazi inashauri ikibaini misaada yenye masharti kama hayo ikatae sababu siyo mipango ya Mungu bali ni laana," alisema.

Kalima alisema hivi karibuni alisoma mahali fulani wanajiandaa kutengeneza mitaala katika shule za swali na msingi kuanza kuwafundisha watoto masuala ya ushoga.

Vijana wa Itifaki wa CCM Mkoa wa Singida wakimvika Shada maalumu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima, baada ya kuwasili Ofisi ya CCM Mkoa wa Singida kuzungumza na wananchi, Wana CCM pamoja na viongozi wa chama hicho wa Wilaya ya Singida.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, akizungumza kwenye mkutano huo.

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Lucy Boniface akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Singida, Bertha Nakomolwa, akizungumza kwenye mkutano huo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru akizungumza.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Mkoa wa Singida, Tatu Daghau akizungumza kwenye mkutano huo.
Waendesha bodaboda wakiongoza msafara wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima wakati alipokuwa akiwasili Ofisi ya CCM Mkoa wa CCM kwa ajili ya kufanya mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali wa CCM baada ya kuwasili Ofisi ya CCM Mkoa wa Singida.
Mapokezi yakiendelea.

Taswira ya mkutano huo.
Wazee wa CCM Wilaya ya Singida wakimpa heshima ya kumkabidhi Ngao Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima mara baada ya kuwasiliOfisi ya CCM Mkoa wa Singida.
Viongozi mbalimbali wa CCM wakiwa kwenye mkutano huo.
Wajumbe wa idara mbalimbali wa CCM wakiwa kwenye mkutano huo.
    Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima (katikati) na viongozi wengine meza kuu wakiongoza kula kiapo baada ya kupokelewa kwa wananchi waliojiunga na CCM.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima akionesha furaha wakati akiagana na Wana CCM baada ya kumaliza kuzungumza nao katika mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Gilbert Kalima akiwaaga Wana CCM baada ya kumaliza kuzungumza nao.
 

Wednesday, January 25, 2023

NHC YATOA SARUJI MIFUKO 75 KUSAIDIA UJENZI WA HOSTELI SINGIDA

Meneja wa Shirika la Nyumb la Taifa (NHC) Mkoa wa Singida, Judith Mwalongo (kulia) kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Fadhili Chimsala, moja ya mfuko wa saruji kati ya 75 yenye thamani ya Sh. Milioni 1.5 iliyotolewa na shirika hilo kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa hosteli ya wasichana katika Sekondari ya Kintinku iliyopo wilayani Manyoni mkoani Singida leo hii Januari, 25, 2023. Wengine katikati ni dereva wa shirika hilo, Hassan Njiku na Afisa wa shirika hilo, Renalda Mlambo.

Na Dotto Mwaibale, Manyoni

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa mifuko 75 ya saruji yenye thamani ya Sh. Milioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya wasichana katika Sekondari ya Kintinku iliyopo wilayani Manyoni mkoani Singida.

Akizungumza wakati akikabidhi saruji hiyo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Fadhili Chimsala kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo,  Meneja wa NHC Mkoa wa Singida, Judith Mwalongo alisema saruji hiyo ina kwenda kusaidia kukamilisha ujenzi wa hosteli hiyo na kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi wa shule hiyo wakati wa kwenda shuleni.

"Wanafunzi wa shule hii wanatembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku wakati kwenda na kurudi nyumbani hali inayowafanya washindwe kupata masomo yao vizuri na sisi baada ya kuiona changamoto hiyo tukaamua kuchangia ujenzi wa hosteli hii" alisema Mwalongo.

Mwalongo alisema shirika hilo lina utaratibu wa kushiriki shughuli za kijamii kwa kusaidia katika  mambo ya maendeleo kama walivyofanya katika shule hiyo.

"Shirika letu lina utaratibu wa kurudisha faida tunayoipata kwa jamii kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo (Cooperate Social Responsibility) na leo tumekuja hapa Manyoni kushiriki ujenzi wa Hosteli katika Shule ya  Sekondari ya Kintinku kwa mara nyingine tena kwani tulishawahi kutoa msaada kama huu na yote hii ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kusaidia shughuli za maendeleo" alisema Mwalongo.

Mwalongo alitoa ahadi ya kuendelea kusaidia ujenzi huo pindi watakapopata nafasi ya kufanya hivyo lengo likiwa ni kuhakikisha ujenzi wa hosteli hiyo unakamilika na wanafunzi wanaitumia.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Fadhili Chimsala akipokea msaada huo alilishukuru shirika hilo kwa msaada ambao wamekuwa wakiutoa mara kwa mara katika halmashauri hiyo na kuwa wamekuwa wadau wao wakubwa wa maendeleo.

"Kweli NHC mnafanya kazi kubwa katika halmashauri yetu hatuna maneno mengi zaidi ya kuwashukuru tunaomba hizi salamu zetu mtufikishie kwa mkurugenzi wenu mkuu Nehemia Mchechu na msichoke kutusaidia" alisema Chimsala. 

Meneja wa Shirika la Nyumb la Taifa (NHC) Mkoa wa Singida, Judith Mwalongo (kulia) na Afisa wa shirika hilo, Renalda Mlambo wakisaini fomu ya makabidhiano ya saruji hiyo.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Saida Moshi, akisaini fomu za makabidhiano ya saruji hiyo.
Picha ya pamoja baada ya makabidhiano ya saruji hiyo.

Sunday, January 22, 2023

MATUKIO YA MAUAJI WILAYA YA MANYONI WANANCHI WAMLILIA RC SERUKAMBA AWASAIDIE

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyoni na Itigi katika kikao cha kusikiliza kero kilichofanyika juzi wilayani humo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

UTARATIBU wa ziara aliounzisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba  kwenda kusikiliza kero za wananchi katika wilaya zote mkoani hapa zimekuwa na tija kubwa  kwani zimeibua mambo mengi yakiwemo matukio ya mfululizo ya kuuawa kwa watu wilayani Manyoni.

Mauaji ya mfululizo ya watu ambao maiti zao zinaokotwa kila wiki maeneo tofauti ya Wilaya ya Manyoni yamewashtua wananchi wa wilaya hiyo ambao wamelazimika kupaza sauti kumweleza Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba, kumuomba aingilie kati na kuwasaidia kuliondoa jambo hilo.

Katika hali ya kushangaza,wananchi hao wamesema mauji ya watu ambayo yameibua hofu kubwa kwa jamii baadhi ya pikipiki zinazomilikiwa na askari polisi wa Manyoni kwa ajili kuendesha biashara zao ndizo zinatumika kwenye mauaji hayo.

Wananchi wa Manyoni walimweleza juzi hayo Mkuu wa Mkoa wa Singida,Serukamba  ambaye alikwenda katika wilaya hiyo kusikiliza kero mbalimbali ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake zakusikiliza kero.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hapa Manyoni vifo vimekithiri sana kila wiki lazima tuokote maiti mahala fulani lakini sio kwamba wananchi wa Manyoni hawawafahamu wahalifu bali wanawafahamu ," alisema Prisca Maleta.

Maleta ambaye wakati akizungumzia suala hilo mamia ya wananchi waliokuwa kwenye kikao hicho walikuwa wakimshangilia, alisema wananchi wanashindwa kutoa taarifa polisi kutaja wanaohusika na uhalifu huo kwasababu baadhi ya polisi sio waaminifu wanaficha siri za watoa taarifa.

"Tatizo linakuja kwa Jeshi la Polisi mimi kama Prisca ninapokwenda kutoa taarifa polisi kabla mtuhumiwa hajaenda kukamatwa wanampa taarifa kuwa fulani amekuja kukuripoti huku,vitengo hivi ndio vinasababisha vifo kuongezeka kwasababu kunakuwa na visa na visa," alisema.

Maleta alimweleza Mkuu wa Mkoa  kuwa kuna baadhi ya askari ambao anawajua kwa sura na majina ambao wanamiliki pikipiki zao ambazo ndizo zinazoshiriki kwenye uhalifu wa mauji ya watu.

"Kuna baadhi ya askari kwa sura na majina ila siwezi kuwataja hapa ila ukihitaji nitakutajia wana pikipiki zao ambazo ndizo zinashiriki kwenye uhalifu," alisema.

Mwananchi mwingine Khalfan Zuberi  Paloto alilalamikia jeshi hilo kitengo cha upelelezi kuwa mtu anapopeleka mashitaka kituoni na kufunguliwa jadala, badala ya kukutanishwa na askari mpelelezi wa kesi yake hupewa namba ya simu na kila ikipigwa muhusika husema yupo nje ya wilaya.

“Mimi nilipeleka kesi ya wizi nikapewa namba ya simu ya mpelelezi nilipompigia akataka nimpe namba ya simu ya mshukiwa, alipigiwa simu akimuita kituoni lakini mshukiwa alipofika hakumkuta ayelimuita,” alisema.

Paloto alisema  tatizo hilo limekuwa sugu kwenye idara ya upelelezi ya polisi wilayani humo, hali inayowafanya waamini huduma haziwezi kuwa na ubora unaotakiwa kutokana na unyeti wa idara hiyo.

Mkuu wa Polisi  Wilaya ya Manyoni (OCD), Ahmad Makele akijibu madai hayo alikiri kuwepo kwa mauaji hayo ya mara kwa mara wilayani humo.

"Vifo vinavyotokea sio vya kisasi wala kuwania mali sababu mtu akiuawa vinachukuliwa viungo vya mwili wake kama vile sehemu za siri," alisema.

Makele alisema Jeshi la Polisi limeanza kuchukua hatua za kukabiliana na mauaji hayo na watu kadhaa wamekwisha kamatwa na misako zaidi bado inaendelea kufanyika ili kukomesha vitendo hivyo.

Kufuatia malalamiko hayo ya wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Serukamba amemwagiza Afisa wa Usalama wa Taifa wa Wilaya ya Manyoni (DSO), kuunda kamati itakayoshirikisha vyombo vyote vya usalama kuchunguza mauaji hayo.

Serukamba ambaye alionekana kuchukizwa na suala hilo alisema mkoa anaoungoza hawezi kukubali kuwa na askari wanaoshirikiana na wahalifu.

"Haiwezekani watu wanauawa kirahisi rahisi na serikali ipo, vinginevyo tumwambie IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini) awaondoe Manyoni,pia hatuwezi kuwazuia na polisi wanaoshirikiana na wahalifu, hatuwezi kuwafukuza kazi lakini tunaomba wapelekwe mikoa mingine hapa tunahitaji kuona polisi wema ambao wanalinda wananchi na mali zao," alisema.

Alisema Jeshi la Polisi linao uwezo wa kuwajua wahalifu,washirikina na wanaofukua makaburi hivyo wote wafahamike wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa akizungumza katika kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Jumanne Mlagaza, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mkazi wa Manyoni Prisca Maleta.akitoa kero yake mbele ya mkuu wa mkoa.
Mkazi wa Manyoni Khalfani Zuberi akinyoosha kidole kuomba apewe nafasi ya kutoa kero zake.
Mkazi wa Manyoni Khalfan Zuberi akitoa kero zake.
Meneja wa Tanesco Wilaya ya Manyoni Mhandisi James Mushi akizungumza katikakikao hicho wakati akitoaufafanuzi kufuatia kero zilizokuwa zikiwasilishwa na wananchi.
Kero zikitolewa mbele ya mkuu wa mkoa.
Kikao cha kero kikiendelea.