Thursday, April 18, 2024
Tuesday, April 9, 2024
MSD YAKUTANA NA WADAU WAKE KANDA YA IRINGA, RC RUVUMA ATAKA WELEDI SEKTA YA AFYA
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali. Ahmed Abbas Ahmed (kushoto) akipokea tuzo maalumu kutoka kwa Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa Bohari ya Dawa (MSD), Victor Sungusia wakati wa mkutano mkuu wa MSD na wadau wake wa Mkoa wa Ruvuma uliofanyika Aprili 8, 2024,
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali. Ahmed Abbas Ahmed, amewataka watumishi wa sekta ya afya Mkoani Ruvuma, kuzingatia weledi na kutoa huduma bora kwa wananchi, ili kuakisi maboresho na uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye sekta ya afya, chini ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita.
Kanali Ahmed amesisitiza kuwa, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya maboresho na ujenzi wa miundombinu ya afya mathalani majengo, ununuzi wa bidhaa za afya
na kuwezesha ajira za kutosha, lengo likiwa kuinua hadhi ya huduma zinazotolewa nchini, hasa zinazomgusa mtanzania wa kawaida.
Kanali Ahmed ametoa rai hiyo hii leo, wakati wa akifungua kikao kazi baina ya MSD Kanda ya Iringa na wadau wake kutoka halmashauri saba za mkoa wa Ruvuma (Madaba Tc, Madaba Dc, Songea MC, Songea DC, Nyasa DC, Mbinga TC na Mbinga DC), kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ruwiko, ulioko Manispaa ya mji wa Songea.
Mkuu huyo wa Mkoa amewakumbusha viongozi hao wa sekta ya afya Mkoani humo, kufanya maoteo yao ya bidhaa za afya kwa usahihi, umakini na kwa wakati ili kuiwezesha Bohari ya Dawa (MSD) kutekeleza majukumu yake ya ugavi wa bidhaa za afya kwa weledi.
Mhe. Ahmed amewataka pia watendaji hao kusimamia ukusanyaji wa mapato, na kutumia vyema vyanzo vyao vingine vya mapato katika kulipa madeni ya MSD, huku akiwakumbusha pia kuhakiki taarifa sahihihi za utunzaji na utoaji wa bidhaa za afya, ili kuepuka upotevu wa bidhaa hizo.
Katika hatua nyigine, Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza MSD kwa utendaji wake katika kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya, huku akiwapongeza kwa kuitisha mkutano huo wa wadau kwani utasaidia kuboresha mahusiano na mawasiliano.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ugavi na uendeshaji wa MSD Victor Sungusia, amebainisha maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanywa na MSD katika nyanja mbalimbali kupitia majukumu yake makuu ya uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji.
Bw. Sungusia amebainisha jinsi MSD ilivyojizatiti katika utekelezaji wa majukumu yake kupitia mifumo ya kisasa ya kidigitali, ugatuzi wa majukumu ya Kanda, ujenzi wa viwanda mbalimbali vya dawa na vifaa tiba, maboresho ya mfumo wa usambazaji wa bidhaa, upanuzi wa maeneo ya uhifadhi na kuwajengea uwezo watumishi wake.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Iringa Bw. Robert Lugembe akiwakiribisha wajumbe wa kikao hicho, alibainnisha kuongezeka kwa uwezo wa MSD kuwahudumia wateja wake na kukidhi mahitaji, sambamba na maboresho ya upatikanaji wa bidhaa za afya mathalani vifaa tiba, mkoani humo.Meneja wa MSD Kanda ya Iringa Bw. Robert Lugembe akizungumza kwenye mkutano huo.
Thursday, April 4, 2024
WANANCHI ITIGI WAMSHUKURU RAIS , KITUO CHA AFYA KUANZA UPASUAJI
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida, Hussein Simba, akizungumza wakati akiongoza kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Aprili 3, 2024. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ayubu Kambi na na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jonathan Hemed.
..................................
Na Mwandishi Wetu, Itigi
WANANCHI wa Kata ya Rungwa iliyopo wilayani Itigi mkoani Singida wamemshuru
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea Kituo cha Afya ambapo sasa wajawazito
wameanza kupata huduma ya upasuaji na kuondokana na changamoto waliokuwa nayo
ya kufuata huduma hiyo Hospitali ya St. Gasper iliyopo Itigi.
Diwani wa Kata hiyo Said Sudi akitoa shukurani hizo kwa niaba ya wananchi
wake wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Aprili 3, 2024 alisema
hawana cha kumlipa Rais Samia zaidi ya kumpa kura zote katika uchanguzi mkuuu
utakaofanyika mwakani.
"Kata yetu tutampa kura asilimia 100 mama yetu kwa kazi kubwa
aliyotufanyia si kwa kituo cha afya pekee bali na miradi mingine mingi iliyotekelezwa.
wajawazito walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 194 pale walipohitaji
kupata huduma ya upasuaji lakini sasa wanaipata hapahapa nyumbani ni jambo la
kumshuruku sana Mungu kupitia Rais wetu," alisema Sudi.
Sudi alisema Rais Samia aliwapa Sh. Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa
kituo hicho cha afya ambacho kimeanza kutoa huduma hiyo Februari 27, 2024
ambapo wajawazito watano wamenufaika na huduma.
Alisema wajawazito walionufaika na huduma hiyo ni kutoka vitongoji vya
Mkora A na B na kata za jirani za Kiloli
na Kambikatoto.
Sudi alitumia nafasi hiyo kuomba wasaidiwe kupata gari la kubebea wagonjwa,
mashine ya kufulia na kunyoshea nguo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Simba alisema ukusanyaji
wa mapato katika halmashauri hiyo upo vizuri hadi kufikia mwezi februari
walikuwa wamefikia asilimia 95 ya mapato ya Serikali mapato huru na mapato
lindwa ilikuwa ni asilimia 35 na kuwa
wanaamini kwa kasi hiyo hadi mwezi machi ambao bado hawajaujadili watafikia
asilimia 100.
Simba alisema kupitia fedha za Serikali kuu na wahisani wamefikia asilimia
77 ya lengo ambapo zaidi ya Sh.Bilioni 4.9 halmashauri hiyo imekwishapewa ili
kukamilisha miradi mbalimbali na kuwa asilimia iliyobaki ni ndogo ambapo amewahimiza
madiwani kuisimamia miradi hiyo kwa kufanya kazi kwa vitendo zaidi badala ya
maneno ili kufikia malengo ya wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota, aliomba miradi
yote inayotekelezwa ikikamilike ifikapo
Aprili 30, 2024 ambapo pia aliwaomba madiwani kuhimiza kampeni ya kupata
madawati kufuatia kuwepo kwa changamoto ya kukosekana kwa madawati katika shule zote wilayani humo.
Aidha, Lwota alihimiza mazao yote kuuzwa kwa njia ya stakabadhi gharani
badala ya kuuzwa kiholela jambo linalosababisha Serikali kukosa mapato ambapo
utaratibu wa kuyauza mazo hayo unafanyika.
Katika hatua nyingine Lwota amewataka madiwani hao na watumishi wengine
katika wilaya hiyo kuanza maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru ambao
unatarajiwa kuanza kukimbizwa wilayani humo mwanzoni mwa mwezi wa Julai, 2024.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni, Jumanne
Ismail alishukuru mshikamano uliopo baina ya chama na Serikali ambao unaendelea
kuifanya halmashauri hiyo kusonga mbele.
Ismail alisema Aprili 15, 2024 wanatarajia kuanza kufanya mikutano ya
hadhara katika kata zote wakianzia wilayani Manyoni na kisha Itigi na lengo la
mikutano hiyo ni kuzungumza na wananchi kuhusu miradi yote iliyotekelezwa
katika maeneo yao na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa
CCM.
Katika kikao hicho cha baraza la madiwani ambacho kilikuwa na ajenda nane Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Hussein Simba aliweza kumkaribisha Mkurugenzi mpya wa halmashauri hiyo, Ayubu Kambi na kutoa taarifa fupi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa lengo la kumpa picha halisi ya miradi hiyo ili aielewe na atakapoanza kazi ajue pa kuanzia.
Katibu wa CCM Wilaya ya Manyoni Maimuna Likunguni, akichangia jambo kwenye kikao hicho.