Friday, February 24, 2023

WANANCHI IBOFWE WAMBEBA MBUNGE NYAMOGA WAKISHUKURU KWA UJENZI WA ZAHANATI, BARABARA

Wananchi wa Kijiji cha Ibofwe, Kata ya Irole wilayani Kilolo mkoani Iringa wakiwa wamembeba Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga ikiwa ni kuonesha shukurani zao baada ya mbunge huyo kufanikisha ujenzi wa Zahanati na Barabara katika kijiji hicho. Mbunge Nyamoga alibebwa leo wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika kijiji hicho.

Na Mwandishi Wetu, Kilolo, Iringa

Awali, wananchi wa Kijiji cha Ibofwe, Kata ya Irole Wilayani Kilolo walimuomba Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga  ashuke kwenye gari kisha wakampakia kwenye bodaboda.

Ilipobaki umbali wa kama kilometa moja hadi kufika eneo la mkutano, wananchi hao wakamuomba ashuke kwenye bodaboda ili wambebe.

Haikuwa rahisi kwake kukubali kubebwa lakini kwa sababu yalikuwa ndiyo mapokezi ya wanakijiji, hakuwa na budu kukubali.

"Mbunge wetu, kikosi cha mapokezi kipo tayari kukubeba, sisi wananchi tumeamua kukubeba na usihofi hatutakuangusha," alisema mmoja wao huku akipiga saluti.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho amesema hawana zawadi kubwa ya kumpa mbunge wao kama.shukrani zao kwa ujenzi wa zahanati ya Kijiji na barabara.

"Tangu kuumbwa kwa dunia hii ndio mara ya kwanza barabara yetu inapitika. Asante Mbunge wetu  Nyamoga," amesema.

Mbunge Nyamoga ameshukuru kwa mapokezi huku akiahidi kutekeleza ahadi zilizobaki ikiwemo umeme na maji.

"Asanteni sana, mapokezi haya ni yataendekea kunikumbusha kila siku, vijiji hivi vyote ni vyangu," amesema.

Wananchi wakiwa wamembeba mbunge wao kuonesha furaha ya kujengewa Zahanati na barabara.
Mbunge Nyamoga akiwa amebebwa na wananchi hao.
Mbunge Nyamoga akiwa amebebwa baada ya wananchi kumuomba ashuke kwenye gari ili apakiwe kwenye bodaboda.

SOKO LA BIDHAA TANZANIA LAPANDISHA BEI YA MAZAO YA WAKULIMA NCHINI

Meneja Uendeshaji Biashara wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Augustino Mbulumi akizungumza katika mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa waandishi wa habari wa mikoa ya  Dodoma na Singida juzi Februari 22, 2023 (hawapo pichani) kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo iliyochini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

MFUMO wa ununuzi wa mazao kwa njia ya mtandao unaoendeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) umesaidia kupandisha bei ya mazao ya wakulima ambayo uuzwa kwa mnada.

Hayo yamebainishwa na Afisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasilino (TEHAMA) kutoka TMX, Goodluck Luhanjo wakati akizungumza katika mafunzo yaliyokuwa yakitolewa kwa waandishi wa habari wa mikoa ya  Dodoma na Singida kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo iliyo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2022  TMX imefanikiwa kuuzwa kwa tani 107,056,619 za bidhaa mbalimbali zenye thamani ya Sh. Bilioni 223.26 na kati ya fedha hizo Sh. Bilioni 212.09 sawa na asilimia 95 zililipwa kwa wakulima na kutaja mazao yaliyouzwa  kuwa ni ufuta, choroko, korosho, kakao, kahawa na dengu.

Akitolea mfano alisema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo  wakulima walikuwa wakiuza choroka kwa Sh.400 hadi 900 lakini baada ya kuanza kuuza kwa kutumia mfumo huo bei imepanda hadi kufikia Sh.1340,huku zao la kokoa katika mikoa ya Tanga, Mbeya na Morogoro iliyokuwa ikiuzwa kwa Sh.1200 ikipaa hadi kufikia Sh.4500 hadi 5000 kwa kilo baada ya kuuzwa kwa mfumo huo.

"Tulivyofanya tathmini kwenye mnyororo wa thamani wa zao la ufuta wilayani Kondoa mkoani Dodoma na Babati mkoani Manyara ulikuwa ukiuzwa kati ya Sh. 1200 hadi 1500 lakini baada ya kuingia kwenye mfumo bei ilipanda hadi kufikia Sh.3,195 kwa kilo moja" alisema Luhanjo.

Akizungumzia zao la kahawa mkoani Kagera alisema kwa msimu wa mwaka jana kahawa aina ya robosta ambayo ilikuwa haijabanguliwa maganda ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh.900 hadi 1200 lakini baada ya kuuzwa kwa njia ya mfumo bei ilipanda hadi kufikia Sh.2000 hadi 2500 kwa kilo.

 Meneja Uendeshaji Biashara wa TMX, Augustino Mbulumi, akizungumzia faida kadhaa za soko la bidhaa Tanzania alisema ni kuimarisha bei kwenye soko,kupunguza hatari ya upotoshaji wa soko, upatikanaji wa taarifa za Soko na uhakika wa malipo kwa wakulima.

Alitaja faida nyingine kuwa ni kupunguza gharama muda na fedha, kupunguza athari mbalimbali kwenye ubora na wizi, uwezo wa kupata mazao mengi na yenye ubora kwa wakati mmoja na imesaidia biashara ya kimataifa kwa gharama nafuu.

Aidha,  Mbulumi alisema kwa upande wa Serikali inasaidia upatikanaji wa taarifa ya kuaminika, njia rahisi za kukusanya mapato, bodi za mazao zinaweze kujikita katika uzalishaji wa mazao na kuhamasisha kampeni ya uchumi wa viwanda.

Alitaja baadhi ya changamoto kuwa ni zile za kimiundombinu kuwepo kwa maghala machache yanayozingatia viwango vya kuhifadhi mazao hasa nafaka, vifaa vichache au kukosekana kabisa kwenye baadhi ya maeneo ya minada ya mifugo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni upinzani kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwawakinufaika sana na biashara isiyo rasmi, kuwepo kwa mgongano wa maslahi na  wakati mwingine husababisha upinzani wa mabadiliko, vyama vya ushirika kuzoea kutumia 'sanduku la zabuni’ na njia zisizo za kidijitali hivyo kuwepo na upinzani wa kutumia mfumo waKielektroniki wa Soko la Bidha.

"Baadhi ya hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizi ni kupitia Wizara ya Kilimo, na kufanya kazi na Bodi ya Stakabadhi za Ghala, kuna mipango ya kuwa na ghala katika ngazi ya wilaya kwenye maeneo ya uzalishaji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari imeanza mchakato wa kuhuisha vifaa hivyo hasa mashine za kupimia mifugo uzito na kupata vifaa vinavyohitajika katika maeneo ya minada kuboresha utendaji kazi."  alisema Mbulumi.

Meneja Uendeshaji Biashara wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Augustino Mbulumi, akisisitiza jambo kwenye mafunzo hayo.
Afisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasilino (TEHAMA) kutoka TMX, Goodluck Luhanjo akizungumza katika mafunzo hayo. Kulia Meneja Uendeshaji Biashara wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Augustino Mbulumi.
Mwanahabari Mussa Yusuph kutoka gazeti la Uhuru akichangia jambo kwenye mafunzo hayo. Kulia ni Mwanahabari Thobias Mwanakatwe wa Gazeti la Nipashe Mkoa wa Singida.
Waandishi wa habari wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa. katika mafunzo hayo.
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mafunzo hayo. Kutoka kulia ni Mwandishi wa Habari Hamisi Hussein kutoka Wazo Huru Media Mkoa wa Singida na Claudia Kayombo kutoka Gazeti la Uhuru Mkoa wa Singida
Mwanahabari Hamisi Hussein akiwajibika ipasavyo katika mafunzo hayo.
Taswira ya mafunzo hayo.

Monday, February 20, 2023

RC SERUKAMBA AWATAKA WARATIBU KUONGEZA BIDII UTOAJI ELIMU YA VVU

p>
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na waratibu wa UKIMWI wa Wizara,Mikoa na Halmashauri wakati wa kikao  cha usambazaji wa taarifa ya mapitio ya fedha za UKIMWI kwenye sekta za umma na sekta binafsi ya mwaka 2022. Kutoka kulia ni  Mkurugenzi wa fedha na Utawala wa TACAIDS, Yasin Abasi na kushoto ni Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Singida, Patrick Kasango.
 

Na Mwandishi Wetu, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida,  Peter Serukamba amewaagiza waratibu wa UKIMWI nchini  kuzungumza na jamii kwa uwazi kuhusu mabadiliko ya tabia katika kujikinga na maambukizi ya VVU ifikapo 2030 kuwe na Tanzania isiyokuwa na UKIMWI.

Akizungumza leo Februari 20,2023 wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa taarifa ya mapitio ya fedha za UKIMWI kwenye sekta za umma na sekta binafsi ya mwaka 2022 iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana aalisema iwapo jamii itaelewa vizuri na ikakubali kubadili tabia Tanzania itafikia malengo ya Dunia ya 2030 ya  kumaliza UKIMWI.

Serukamba alisema kuwa Serikali imekua ikipambana kudhibiti maambukizi ya VVU pamoja na madhara yake kwa zaidi ya miaka thelathini, ambapo kwa kiasi kikubwa mapambano haya yanategemea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za UKIMWi,ambapo amefafanua kuwa kwa mahitaji kwa mwaka ni takribani Sh. Trilini 1.3.

Aidha, aliongeza kuwa utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI umekua ukipata fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali hivyo ni muhimu kufanya mapitio ya fedha zinazotumika kwenye afua hizo ili kubaini mchango wa taasisi za sekta ya umma na mchango wa taasisi za sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kutambua Maeneo ambayo mchango huo unapelekwa kulingana na afua za VVU na UKIMWI lakini muhimu zaidi kutambua upungufu uliopo wa fedha katika kutekeleza afua za VVU na UKIMWI hapa ili Kuhakikisha utekelezaji wenye tija kwa Taifa, Jamii na mtu mmoja mmoja.

Akifafanua umuhimu wa kufanyika kwa zoezi la Mapitio ya Fedha za UKIMWI kwenye Sekta ya Umma na Binafsi (Public and Private Expenditure Review) ni kuwa zinaisaidia serikali kufahamu kiwango cha matumizi ya fedha za UKIMWI kinachopangwa na Sekta ya Umma na Binafsi.

Pia kufahamu maeneo ambayo fedha hizo zinaelekezwa, kujua kiwango cha utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI ili kubaini mchango wa sekta ya umma na binafsi katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI. Aidha, mapitio ya fedha za UKIMWI husaidia kubaini changamoto katika utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI nchini na kuweka mikakati ya kuzitatua.

Serukamba ameyataja mafanikio ya mafanikio yaliyotakana na zoezi hilo kuwa ni pamoja na kuboresha ugawaji wa rasilimali fedha za UKIMWI kulingana na afua zinazotekelezwa hapa nchini, kuimarisha mikakati ya kuhamasisha sekta binafsi na sekta za umma kupanga na kutekeleza shughuli za VVU na UKIMWI kwenye maeneo yao pamoja na kukuza mchango wa sekta ya umma na sekta binafsi katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI hapa nchini.

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TACAIDS, Yasini Abasi alisema kuwa uhitaji wa fedha za UKIMWI bado ni mkubwa kwani kwa sasa wafadhili wanaendelea kupungua na hivyo kuitaka jamii kuendelea kuchangia mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI ili hata pale itakapo tokea waansitisha basi Mfuko  uwe na fedha za kutosha kwa ajili ya huduma za UKIMWI.

Kikao hicho kiliwashirikisha waratibu wa UKIMWI kutoka baadhi ya Wizarani,Halmashauri na Mikoa.

Waratib wa UKIMWI kutoka Wizarani, Halmashauri na Mikoa walioshiriki  Kikao cha usambazaji wa taarifa ya mapitio ya fedha za UKIMWI kwenye sekta za umma na sekta binafsi ya mwaka 2022 kilichoandaliwa na Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) wakiwa katika kikaohicho.

Mkuu wa MKoa wa Singida  Peter Serukamba (aliyekaa katikati)  akiwa katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wa zoezi la kukusanya taarifa za fedha za UKIMWI kwenye sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na waratibu wa UKIMWI (aliyekaa kulia kwake)  ni Mkurugenzi wa fedha na Utawala wa TACAIDS, Yasin Abasi  na kushoto ni Mratibu wa wa UKIMWI MKoa wa Singida, Patrick Kasengo.. Picha hii imepigwa mara baada ya uzinduzi wa kikao cha usambazaji wa taarifa ya mapitio ya fedha za UKIMWI kwenye sekta za umma na sekta binafsi ya mwaka 2022

Mkuu wa MKoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi  (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na waratibu wa UKIMWI kutoka wizarani na  baadhi ya Waratibu wa Halmashauri nchini mara baada ya ufunguzi wa kikao cha uzinduzi wa kikao cha usambazaji wa taarifa ya mapitio ya fedha za UKIMWI kwenye sekta za umma na sekta binafsi ya mwaka 2022 kilichofanyika leo Februari 20,2023  mkoani Singida. Kulia kwake Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TACAIDS, Yasin Abasi na kushoto ni Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Singida, Patrick Kasango.

Mkuu wa MKoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi  akiwa katika picha ya pamoja na waratibu wa UKIMWI kutoka wizarani na  baadhi ya Waratibu wa Halmashauri nchini mara baada ya ufunguzi wa kikao cha uzinduzi wa kikao cha usambazaji wa taarifa ya mapitio ya fedha za UKIMWI kwenye sekta za umma na sekta binafsi ya mwaka 2022 kilichofanyika leo Februari 20,2023  mkoani Singida. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TACAIDS, Yasin Abasi na kushoto ni Mratibu wa UKIMWI Mkoa wa Singida, Patrick Kasango.


Saturday, February 18, 2023

MSD YATOA UFAFANUZI DAWA ZILIZOMALIZA MUDA


 Na Mwandishi Wetu

BOHARI ya Dawa (MSD) imesema bidhaa za afya, hususani dawa zina utaratibu maalumu wa utunzaji na matumizi yake, ambapo dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi haziruhusiwi kusambazwa, wala kutumika ndani ya bohari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na MSD na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano MSD Etty Kusiluka ilisema bohari imesikitishwa na taarifa iliyotolewa juzi February 18, 2023 Gazeti la Nipashe toleo Na. 0581225 yenye kichwa cha habari “Wagonjwa wapewa dawa zilizoisha muda wa matumizi” katika ukurasa wake wa kwanza na wa pili.

“Bohari ya Dawa (MSD) imesikitishwa na taarifa iliyoripotiwa na gazeti hilo ambapo kichwa cha habari cha taarifa hiyo na kile kilichoripotiwa ndani ya taarifa husika haviendani hivyo kusababisha taharuki kwa wananchi, vituo vya kutolea huduma za afya nchini, Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla. Taarifa hii pia imeharibu taswira ya MSD,alisema.

Alisema uongozi wa MSD umesikitishwa na upotoshaji huo ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 36 kifungu kidogo cha (1-3) cha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016;taarifa hiyo, imeharibu taswira ya MSD na hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 50 (1) (a) (i) na (ii) cha Sheria ya Habari, kitendo hicho ni kosa la jinai.  

“Kutokana na hilo, MSD, inalitaka gazeti la Nipashe kukanusha taarifa hii na kuomba radhi kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti lake, kama ilivyoripotiwa tarifa hii tarehe 18 Februari, 2023 kwa siku tatu mfululizo,”alisema.

Tungependa umma utambue kwamba bidhaa za afya, hususani dawa zina utaratibu maalumu wa utunzaji na matumizi yake, ambapo dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi haziruhusiwi kusambazwa, wala kutumika. MSD inafuata utaratibu wa usimamizi wa bidhaa za afya ambao upo kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Dawa na Vifaa Tiba Na. 219 ya mwaka 2021 na Sheria ya Utunzaji wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004, chini ya Wizara ya Afya,”alisema.

Alisistiza kuwa MSD ina utaratibu wa ndani unaozuia dawa zilizobakiza miezi mitatu kuisha muda wa matumizi (expiry) kutoka katika maghala yake kote nchini. Dawa zinazoisha muda wake wa matumizi katika maghala ya MSD hutengwa kwenye sehemu maalumu zikisubiri hatua za uteketezaji kwa kufuata taratibu na sheria zinazosimamia uteketezaji wa dawa.

Aidha, ieleweke kuwa, MSD inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya na si mwananchi mmoja mmoja (mgonjwa), na hivyo kuondoa uwezekano wa dawa zilizoisha muda wake kumfikia mgonjwa kama ilivyoripotiwa kwenye kichwa cha habari cha taarifa hiyo.

Etty alisema MSD itaendelea kuwa na  mawasiliano na MSD badala ya kuandika taarifa za upande mmoja.

“ MSD iko tayari kutoa ushirikiano kwa mwandishi yeyote anayehitaji taarifa za majukumu ya MSD, ama ufafanuzi wa suala lolote kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazosimamia utoaji habari,”alisema.

Tuesday, February 14, 2023

VETA KANDA YA KATI YATOA MAFUNZO YA UFUGAJI KUKU KWA WAJASIRIAMALI WILAYA YA IKUNGI


Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza leo Februari 14,2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wajasiriamali wa kata za Ikungi na Unyahati wilayani Ikungi mkoani Singida. Kutoka kulia ni Afisa Masoko na Utafiti Veta Kanda ya Kati, Sadan Komungoma na Afisa Maendeleo  ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe.


............................................................

Na Dotto MwaibaleIkungi

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati imeanza kutoa  mafunzo ya ufugaji wa kuku kisasa kwa wajasiriamali ili kuwawezesha wananchi kuondokane na ufugaji wa mazoea kwenda ufugaji wenye tija utakaowakwamue kiuchumi.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza leo Februari 14,2023 wakati wa mafunzo hayo kwa wajasiriamali wa kata za Ikungi na Unyahati wilayani Ikungi mkoani Singida ili kuwawezesha wananchi  kufanya ufugaji wenye tija utakaowaongezea kipato.

"Mafunzo haya ambayo ni ya kwanza kutolewa katika Chuo cha VETA Ikungi tangu kilipozinduliwa mwaka jana yanalenga kuboresha biashara za wananchi ili wafuge kuku kwa ubora ambao utaongeza thamani ya nyama na mayai," alisema.

Naye Afisa Masoko na Utafiti VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma,alisema VETA imeanza kutoa kozi ambayo inahusiana na ufugaji wa kuku kutokana na Mkoa wa Singida kusifika kwa ufugaji wa kuku na kilimo cha alizeti ambao unafanyika lakini sio kwa tija hivyo VETA inawaongezea ujuzi na maarifa wananchi katika ufugaji.

Alisema mafunzo haya ya muda mfupi yanatolewa kwa wajasiriamali kwenye mikoa ya kanda ya kati ambayo ni Dodoma,Singida na Manyara ili kuwawezesha wananchi kunufaika na uwepo wa vyuo vya VETA vilivyoanzishwa kila wilaya ili wajikwamue kiuchumi kupitia ujasiriamali.

Naye ya Afisa Maendeleo ya Jamii Wila ya Ikungi, Haika Masawe, alisema ifike wakati wananchi wabadilike kwa kuachana na ufugaji wa mazoea na badala yake wafuge kibiashara.

Haika ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi,Justice Kijazi, alisema VETA pamoja na kutoa mafunzo haya wasaidie kuwatafutia masoko wajasiriamali.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekuwa ikiwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ambapo hivi karibuni ilitoa mikopo ya Sh.milioni 141 kwa vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na ujasiriamali.

Baadhi ya washiriki wamafunzo hayo akiwepo Fatma Said na Hadija Nassoro walisema mafunzo hayo yatawaongezea maarifa na mbigu za ufugaji wa kuku  na kukuza uchumi wao kutokana na kuuza mayai na nyama ya kuku ambapo walitumia nafasi hiyo kupongeza Veta kwa kuwapa mafunzo hayo ambayo ni muhimu kwao


 Afisa Masoko na Utafiti Veta Kanda ya Kati, Sadan Komungoma akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe, akizungumza kwenye ufunguzi huo.

Mwalimu wa ufugaji wa wanyama Veta Mkoa wa Singida, Hamisi Msangi, akitoa maelekezo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo.
Mafunzo yakiendelea.
Wajasiriamali wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Maafisa Watendaji  Mariam Edward kutoka Kata ya Muungano akiteta jambo na Anifa Swalehe (kushoto) kutoka Kata ya Kinyamwandyo, wakati wa mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Mafunzo yakiendelea.

Monday, February 13, 2023

MWENYEKITI MPYA BODI YA REA AANZA KAZI RASMI NA KUSISITIZA UCHAPAKAZI, UADILIFU

Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Nishati Vijijini, Janet Mbene akizungumza na Wajumbe wa Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), juzi Februari 11, 2023 jijini Dar es Salaam.

Na Veronica Simba, REA 

MWENYEKITI mpya wa Bodi ya Nishati Vijijini, Janet Mbene ameanza kazi rasmi kwa kukutana na kuzungumza na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambapo amesisitiza uchapakazi, weledi, uadilifu na ushirikiano katika kazi.

Katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam leo, Februari 11, 2023 na kuhudhuriwa pia na Wajumbe wa Bodi, Mwenyekiti amehamasisha kufanya kazi kwa ufanisi ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa katika kuwasaidia wananchi hususan wa vijijini kupata maendeleo.

“Tujitahidi sana kufanya kazi vizuri, kwa weledi na kwa wakati huku tukisimamia maeneo ambayo tunapaswa kuyasimamia kwa karibu sana hasa wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali,” amesisitiza Mwenyekiti.

Akizungumza zaidi, Mbene ameeleza kuwa maendeleo ya kiuchumi yanategemea sana nishati za aina zote, hivyo akatoa hamasa kwa wafanyakazi wa REA kupitia Menejimenti kutumia vizuri rasilimali kidogo zinazopatikana ili tija yake ionekane.

Amesema REA ni Taasisi yenye umuhimu mkubwa kwa Taifa kutokana na mchango wake katika maendeleo hususani ya wananchi wa vijijini. “Na kwa hali hiyo hii kazi tuliyopewa siyo ndogo,” amesisitiza.

Zaidi, Mwenyekiti amewataka wote kuhakikisha wanafanya kazi inayoacha alama na kwa namna hiyo kuzitendea haki nafasi walizopewa kuwatumikia Watanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti na Wafanyakazi wote wa REA, Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Hassan Saidy amemhakikishia Mwenyekiti ushirikiano na kwamba watatekeleza yote aliyoyaagiza.

Awali, Wajumbe wa Menejimenti walipata fursa ya kujitambulisha kwa Mwenyekiti na kila mmoja kueleza majukumu yanayotekelezwa katika Idara/Kitengo anachosimamia.

Janeth Mbene aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Februari Mosi, 2023 na kutangazwa Februari 3, mwaka huu kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini baada ya Mtangulizi wake kumaliza muda wake. 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy akieleza majukumu ya Wakala hiyo kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Nishati Vijijini, Janet Mbene (katikati) katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, juzi Februari 11, 2023.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy akieleza majukumu ya Wakala hiyo kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Nishati Vijijini, Janet Mbene (katikati) katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, juzi Februari 11, 2023.

Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Janet Mbene (hayupo pichani) wakati wa kikao baina ya Mwenyekiti na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kilichofanyika jijini Dar es Salaam, juzi Februari 11, 2023.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy akieleza majukumu ya Wakala hiyo kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Nishati Vijijini, Janet Mbene (katikati) katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Februari 11, 2023.

Friday, February 10, 2023

KAMISAA WA SENSA ANNE MAKINDA: REDIO ZINA UMUHIMU MKUBWA WA KUTOA TAARIFA SAHII ZA MATOKEO YA SENSA

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Anne Makinda, ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wahariri wa habari wa redio jamii yanyayohusu matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yanayofanyika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali mkoani hapa ambayo  yameanza leo Februari 10, 2023 na yatafikia tamati kesho.

Na Dotto MwaibaleSingida

KAMISAA wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Anne Makinda amesema redio zinategemewa sana na wananchi kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na taasisi zingine zikiwemo za idara ya takwimu.

Makinda ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo leo Februari 10, 2023 wakati akifungua mafunzo ya wahariri wa habari wa redio jamii yanyayohusu matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yanayofanyika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali mkoani hapa ambayo yatafikia tamati kesho..

Alisema redio jamii pamoja na zile za mikoa zimekuwa redio pendwa kwa wananchi wa mikoa husika kwa kuwa zinatangaza habari nyingi zinazohusu na kugusa maendeleo ya kiuchumi, kijamii.mazingira na utamaduni wa watu na kwa kufanya hivyo zimejiweka karibu na wananchi wa maeneo yao.

“Redio jamii zinaelezwa ni chombo muhimu katika kujenga jamii zenye mwamko, kuwajengea uwezowananchi kuwasilisha mahitaji yao kwa mamlaka husika kwa urahisi na zaidi zinaaminika na jamii” alisema Makinda.

Aidha Makinda alisema wameanza kutoa mafunzo hayo kwa wahariri wa redio  na wala sio magazeti na televisheni kwasababu redio ni chombo kinachowafikia wananchi kwa urahisi na katika njia rafiki wakati wote tofauti na njia nyingine za upashanaji habari kama vile magazeti na televisheni, hivi sasa Tanzania Bara kila mkoa una vituo vya redio kati ya viwili hadi vitano ukiachia mikoa kama Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Mwanza ambayo ina utitiri wa vituo hivyo.

Alisema sababu kuu ya kuanza mafunzo haya kwa redio ni kutokana na uwezo wa redio kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi kama ilivyo katika nchi nyingi zinazoendelea kama Tanzania, redio ndio chombo kikuu kinachotegemewa na wananchi wengi kupata habari na kuwa hapa nchini hivi sasa, redio zimejipambanua kwa kuwa na vituo vya redio zaidi ya 200.

Aidha, Makinda alisema kutokana na maendeleo ya teknolojia, siku hizi huhitaji tena kuwa na redio ili uweze kupata matangazo ya redio bali yamerahisishwa hadi mwananchi anaweza kupata matangazo ya redio kiganjani yaani kupitia simu ya mkononi ikiwemo simu za bei nafuu maarufu humu nchini kama Vitochi au kiswaswadu.

“ Matangazo ya redio yanapatikana pia kwa njia ya mtandao yaani intaneti. Katika hali hiyo, nidhahiri kuwa redio ndio chombo pekee ambacho watanzania wengi wanakitegemea kupata taarifa. Mathalan, hata tafiti ambazo tulizifanya wakati wa kupima uwelewa wa wananchi kuhusu Sensa, asilimia 49.0 walisema wamepata taarifa za Sensa kupitia redio ikifuatiwa na asilimia 47kupitia ujumbe mfupi kupitia simu za kiganjani. Hivyo, mafunzo haya kwetu ni muhimu sana kwa kuwa tuna uhakika kuwa yakifanikiwa wananchi wetu wataweza kupata matokeo ya Sensa kwa urahisi zaidi na kusaidia utekelezaji wa mpango kazi wa usambazaji wa mafunzo ya matokeo ya Sensa” alisema Makinda. 

Akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Singida,  Naing'oya Kipuyo, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuviwezesha vyombo vya habari kuwa na uelewa mpana wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ili viweze kutimiza wajibu wao wa kusambaza, kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutumia matokeo ya Sensa na vikifanya hivyo, vitakuwa vimetimiza wajibu wao kwa taifa hususan kufanikisha malengo ya sensa.

“ NBS imekuwa ikiandaa mafunzo ya aina hii kwa vyombo vya habari mara kwa mara kwa kuwa jukumu letu la uzalishaji na usambazaji takwimu linakuwa rahisi kama tutakuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na vyombo hivi” alisema Kipuyo.

 Aidha, Kipuyo alisema kwa kawaida kabla ofisi yao haijafanya mazoezi makubwa ya ukusanyaji takwimu ikiwemo Sensa ya Watu na Makazi wana utaratibu wa kuvifanyia mafunzo maalum vyombo vya habarikuwawezesha kuwa na ufahamu mpana wa tafiti ili viweze kuielewesha jamii kuhusu mazoezi hayo na inafanya hivyo hivyo, hata baada ya matokeo kutolewa  ili kuwaelewesha nini kimejiri katika tafiti hizo kwa kuwafundisha na kuwafafanulia matokeo hayo kwa kina iliviweze kuyasambaza kwa wadau wote ipaswavyo.

Alisema katika mnasaba huo, NBS imejenga uhusiano na ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari nchini na kama ilivyo kuwa wakati wa Sensa kwani havikuwaangusha kabisavilifanya kazi nzuri na matokeo yake yameonekana.

“Vyombo vya habari ni sehemu ya mafanikio tuliyoyapata katika utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ambayo ilikuwa ya kihistoria. Hivyo, sina shaka yoyote kuwa vyombo vya habari vitaendelea na mwenendo ule ule wa kuzipa umuhimu habari za Sensa ambapo kwa sasa ni matokeo ambayo yanapaswa kuwafikia wananchi popote walipo hivyo naomba nichukue fursa hii kuvishukuru kwa dhati” alisema Kipuyo.

Mratibu wa Mtandao wa Redio za Kijamii nchini (TADIO)  Cosmas Lupoja alisema mtandao huo umekuwa ukifanya kazi kwa karibu na Serikali na taasisi mbalimbali na kuwa unajumuisha redio wanachama 42 Zanzibar zikiwa tano 5na Tanzania Bara 37.

“Wanachama wetu wengine ni Chama cha Waandishi wa Habari Pemba (Pemba Press Club) Dodoma TV na Dodoma FM ambapo kwa ujumla tuna kuwa 44” alisema Lupoja.

Lupoja alitumia nafasi hiyo kuwashukuru sana Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa ushirikiano mkubwa wanao wapa kwa kuwashirikisha kuanzia mwanzo wa mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 hadi mwisho wake na kueleza kuwa redio za kijamii zimekuwa na mchango mkubwa kutokana na kuwafikia watu wengi zaidi ambapo aliomba ushirikiano huo uendelee kudumu.

Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Singida,  Naing'oya Kipuyo (kushoto) akitoataarifa kwa niaba ya  Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa.
Mratibu wa Mtandao wa Redio za Kijamii nchini (TADIO)  Cosmas Lupoja akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mratibu wa Mafunzo hayo, Said Ameir akifanya utambulisho kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Anne Makinda, akisalimiana na washiriki wa mafunzo hayo.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Anne Makinda, akisalimiana na washiriki wa mafunzo hayo muda mfupi baada ya kupiga nao picha.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Anne Makinda, akisalimiana na mshiriki wa mafunzo hayo Mhariri wa RedioMwangaza, Godfrey Lutego.
Washiriki wakiwa kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
Ufunguzi wa mafunzo hayo ukiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo, Godfrey Lutego kutoka Dar es Salaam na Meneja Redio Unyanja FM Patrick Kosima (kulia) kutoka Nyasa mkoani Ruvuma wakiteta jambo wakati wa mafunzo hayo.



Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa busy.
Taswiraya washiriki wa mafunzo hayo.
 Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Tanzania Bara, Anne Makinda (katikati waliosimamam mbele) , ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.

Thursday, February 9, 2023

SUA, TAASISI ZOTE ZA WIZARA YA KILIMO WASAINI MKATABA WA KUINUA KILIMO NCHINI


Wakuu wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo zinazojishughulisha na undelezaji wa pembejeo za Kilimo Utafiti na uzalishaji na wawakilishi wao wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano kati ya Taasisi hizo na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katikaafla iliyofanyika Februari 9, 2023 mkoani Morogoro.

Na Calvin Gwabara, Morogoro.

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo zinazojishughulisha na undelezaji wa pembejeo za Kilimo Utafiti na uzalishaji zimesaini mkataba wa mashirikiano ujulikano 'MoU. ambao utasaidia kuongeza ushirikiano katika utendaji wa Taasisi hizo na kuongeza ufanisi na tija katika kilimo nchini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof.  Maulid  Mwatawala kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda alisema awali SUA ilikuwa iingie makubaliano hayo na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na Taasisi ya Uthibiti ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kwa ajili ya kupokea wanafunzi kwenye mafunzo kwa vitendo lakini baadae Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akaagiza ziongezeke na Tasisi zingine zote zilizo chini ya wizara yake.

“MoU hii haina lengo la kuhamisha majukumu ya Taasisi fulani ya kisheria kwenda kwenye Taasisi nyingine bali ni kusaidiana katika utekeelzaji wa majukumu ili kupunguza mzigo ambao ungewezwa fanywa na Taasisi mbili ukafanywa na Taasisi moja na kuielemea na kupelekea kuchelewesha matokeo tarajiwa kwa Jamii na Taifa”alisema Prof. Mwatawala.

Mwatawala amewataka wakuu wa Taasisi hizo kuteua kila Taasisi mtu ambaye atakuwa ni mratibu katika utekelezaji wa makubaliano hayo ili wasaidie yale ambayo watakubaliana kuyafanya kati ya Taasisi na Taasisi yaweze kufanyika kwa ufanisi na kupendekeza kuwepo kwa vikao mara mbili kwa mwaka kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa makubaliano hayo ili kuchochea ufanisi wake.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru alisema ushirikiano huo utasaidia sana katika kuweka mipango ya pamoja ambayo itasaidia kutoa matokeo yenye mchango mkubwa kwa Taifa na kutafuta fedha na rasiliamali zingine za kuendeshea Taasisi hizo.

“Tunachokifanya leo ni kitu kizuri sana maana kwa mchanganyiko wetu katika fani mbalimbali na majukumu yetu ya kitaasisi tunaweza kuanzisha miradi ya pamoja ambayo italeta tija kwenye kilimo kwa kutumia Sayansi Teknolojia na Ubunifu tukaweza kutoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo na uchumi wa Taifa”alisema Ndunguru.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo wa TPHPA ameahidi kuhakikisha yale yote watakayokuwa wamekubaliana kuyetekeleza kupitia Taasisi yake watayatimiza kwa ufanisi na kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha makubaliano hayo yanafanikiwa na kuleta tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo amesema Taasisi yake imekuwa ikishirikiana na baadhi ya Taasisi hizo kwenye nyanja mbalimbali lakini kwa makubaliano hayo mapya yanaongeza wigo wa ushirikiano na tija.

“Ushirikiano huu lengo letu kubwa la mwisho na kumfikia mtu wa mwisho ambaye ni Mkulima ambaye anaweza kuwa mdogo,wa kati au mkubwa na lengo la Waziri ni tija na kwa kufanya kazi kwa pamoja kwani  kutasaidia kuondoa kazi moja kufanywa na Taasisi nyingi (duplication) na kupunguza gharama kwa kuwa kazi hiyo ingeweza kufanya na tasisi moja na wote tukapata matokeo” alibainisha Dkt. Ngailo.

Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Stanford Chijenga alisema  kama wadau wa mbegu wamekuwa wakifanya kazi na Taasisi hizo kwa nyakati tofauti ikiwemo kupokea Wanafunzi wa SUA na katika masuala ya Mbegu kutoka (TARI) na (ASA) lakini sasa umefunguliwa mlango mkubwa zaidi wa ushirikiano ambao anaamini utasaidia kuinua kilimo.

“Kama walivyobainisha wakuu wengine wa Taasisi, sisi kama TOSCI tunaamini sasakwa kuunganisha Taasisi hizi zote zinazohusiana na kilimo kunakuwa na nguvu ngine ya ziada inaongezeka katika kuisaidia jamii. Maana huko nyuma wengi kwa kutofahamu taratibu za uthibiti wa ubora wa mbegu, walidhani kuthibiti ubora wa mbegu ni jukumu linalowachelewesha, na hii ni kutokana na kutokuwa na uelewa sana wa namna shughuli zinavyofanyika. Lakini kupitia ushirikiano huu naamini tutafanya kazi kwa karibu zaidi kusaidia wakulima wa nchi yetu kupata mbegu bora” alisema Chijenga. 

Akitoa salamu za Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) Dkt. Sophia Kashenge alisema wamefarijika sana kuwa sehemu ya mashirikiano hayo kwakuwa wamekuwa wakifanya kazi na Taasisi hizo kwa nyakati tofauti kabla ya makubaliano hayo lakini sasa baada ya makubaliano hayo anaamini ni mwanzo mwingine mzuri wa kuendelea kufanya kazi zaidi kwa umoja.

“Kwanza nitumie nafasi hii kuishukuru SUA kwa sababu sisi kama wazalishaji wa mbegu kuna maeneo mengi ambayo tumekuwa tukiona tunaweza kufanya kazi nao vizuri hasa katika uzalishaji wa mbegu kwani tunaamini SUA wanazo mbegu nyingi ambazo wamezitoa na bado hazijafika kwa wakulima kwahiyo kwa ushirikiano huu tunaweza kuzalisha mbegu kwa pamoja” alisema Kashenge.

Kashenge amewapongeza SUA kwa kuanzisha kozi ya kuzalisha wataalamu wa mbegu nchini kwakuwa awali walikuwa wakiwatumia watu kwanza kwa kuwajenga lakini baada ya ujuio wa kozi hiyo na Wahitimu wa fani hiyo kutaongeza ufanisi kwakuwa kulikuwa na pengo kubwa la wataalamu wa mbegu nchini.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Upande wa Utawala Fedha na Mipango Prof. Amandus Muhairwa amewaomba wakuu wa Taasisi hizo kushikamana kwa pamoja kutetea hoja na mambo mbalimbali yanayohusu Sayansi nchini badala ya kuwa na kauli za kupingana kwenye mambo yaliyo wazi kisayasi kwa maslahi binafsi au ya Taasisi zao.

“Naiona hii kama nafasi nzuri sana maana kwa sasa tunaogelea kwenye Bahari mbaya sana yani Sayansi inapingwa na watu walioshiba ambao wanaweza kutukataza kutumia Viuatilifu ( Dawa za kuua wadudu) lakini kwa jinsi tunavyozidi kuongezeka hatutaweza kuviepuka hivyo vitu na ikafikia wakitushinda watasema hata tusitumie mbolea lakini kwa umoja wetu tukisimama tutaifikisha nchi yetu mahali pazuri” alieleza Prof. Muhairwa.

Makubaliano hayo yamesainiwa kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo ambazo ni Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Taasisi ya Uthibiti wa Mbegu Tanzania (TOSCI),Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu (TPHPA) na Vyuo vya mafunzo ya Kilimo (MATI).


    Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala (kulia) akitoa salamu za SUA na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Stanford Chijenga ambao ndio waratibu wa ushirikiano huo.

   Wakuu wa Taasisi hizo,  wakisaini mkataba huo wa mashirikiano (MoU)
Wakuu wa taasisi hizo na wawakilishi wao wakifuatilia maelezo na uwekaji saini wa mkataba huo.

Hafla ya kusaini mktaba huo ikiendelea.
Uwekaji saini wa mkataba huo ukiendelea
H
Hafla hiyo ikiendelea