Sunday, April 30, 2023

BOHARI YA DAWA (MSD) KANDA YA KATI YAKUTANA NA WADAU WAKE KATIKA KIKAO KAZI

Meneja wa Bohari ya Dawa (MSD)  Kanda ya Kati, John Sipendi, akizungumza na wadau wa MSD katika kikao kazi kilichofanyika wilayani Kondoa mkoani humo Aprili, 29, 2023.

.............................................................

 Na Mwandishi Wetu, Dodoma

 BOHARI ya Dawa (MSD) Kanda ya Kati Dodoma imekutana na wadau na wateja wake wakiwemo waganga wakuu, wafamasia na watendaji wa halmshauri kuhakikisha wanajadili uboreshaji wa huduma za afya na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa uhakika ili kupunguza kero kwa wananchi. 

Katika mkutano huo wadau hao wamekubaliana kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za maboresho sekta ya afya kwa vitendo kwa kutumia taaluma zao kutoa huduma stahiki. 

Akizungumza jana wilayani Kondoa mkoani Dodoma Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi alisema, lengo la MSD kurejesha mikutano hiyo ya pamoja na wadau ni kukubali kukoselewa, kujenga mazingira ya kupunguza changamoto za pande zote mbili, kubadilisha uzoefu na kukubaliana kufanya kazi kwa pamoja bila kutafuta mshindi kwa kuwa wote wanamuhudumia mwananchi wa Tanzania. 

“Kwa kutambua umuhimu wa ushirikiano kati yetu na wadau wa afya mkutano huu umeazimia kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia za amboresho sekta ya afya kwa vitendo kwa kutumia taaluma zetu kutoa huduma stahiki na kwa wakati,”alisema. 

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu, alisema katika kikao hicho kikichoshirikisha watendaji wenye ngazi ya maamuzi wa Mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani ikiwemo Singida na Manyara kwa pamoja wamejadili maboresho ya ufikishaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma na namna ya kushirikiana katika kumpatia mtanzania huduma bora za afya. 

Alisema, wamebaini zipo changamoto zinazoweza kutatuliwa kwa pamoja ikiwemo eneo la maoteo, bajeti za vituo na mahitaji ya bidhaa hizo kulingana na wakati uliopo ili kupunguza uharibu wa dawa zinazoteketezwa na kuiingizia serikali hasara. 

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Best Magoma, alisem watahakikisha kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dk. Samia inaonekana kwa kutimiza wajibu wao kwa walengwa ambao ni wananchi kufikiwa na huduma bora za afya.

Ivon Mwingie ambaye ni Mfamasia Mkuu wa Hospitali  ya Taifa ya Afya ya Akili ya Milembe iliyopo Dodoma, alisema kikao kazi hicho ni muhimu na kina afya kwa watendaji katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, kuliko mihimili ya serikali yenye jukumu moja kubaki kunyosheana vidole.

Saturday, April 29, 2023

TAASISI YA PROFESSOR MWERA FOUNDATION YAWAOMBA WALIMU SINGIDA KUANZISHA MFUKO WA ELIMU



Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera, akizungumza na wadau wa sekta ya elimu na walimu katika mkutano wa wadau wa elimu 2023 Mkoa wa Singida uliofanyika Aprili 27, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKURUGENZI  wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara, Hezbon Mwera amewaomba walimu Mkoa wa Singida kuanzisha mfuko wa elimu ambao utasaidia kwa shughuli mbalimbali katika sekta ya elimu.

Mwera alitoa ombi hilo jana wakati akizungumza na walimu hao kwenye mkutano wa wadau wa elimu mkoa wa Singida  wa mwaka 2023 uliofanyika Aprili 27, 2023, Ukumbi wa Social Mission mjini hapa.

“Nashauri kila halmshauri za mkoa wa Singida kwa kuwashirikisha wadau wengine anzisheni mfuko wa elimu ambao utakuwa ukisaidia kuboresha masualayote yanayohusu elimu katika maeneo hayo na mkoa wa Singida kwa ujumla,” alisema Mwera.

Akizungumzia suala la upatikanaji wa chakula mashuleni alisema jambo hilo linawezekana kwa kuwashirikisha wazazi na kuwa maeneo mengine wameanza kwa kutoa uji na kueleza watoto wanapopata chakula wanafanya vizuri katika masomo yao.

Alisema iwapo wataona wazazi hawatoi ushirikiano katika jambo hilo ni vema siku moja wakaitisha kikao  na wawashindishe njaa kuanzia asubuhi hadi jioni hapo ndipo watakapoona umuhimu wa watoto kupata chakula wakiwa shuleni kwani wapo ambao hawalielewi wakidhani linafanywa na Serikali.

.Aidha, Mwera alisema ili kukabiliana na upungufu wa madarasa na nyumba za walimu aliwaomba  walimu hao kwa kuwashirikisha wadau wengine kuanzisha benki za matofali na kuwa hatua hiyo itakwenda kupunguza changamoto hiyo kwani kuna baadhi ya halmashauri zimefanikiwa kwa kununua mashine za kufyatulia matofali na zimefanya vizuri.

Pia Mwera aliomba walimu kutoka vyuo vya ualimu Mkoa wa Singida wanapo kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo ni vizuri wakafanya mafunzo hayo kwenye  shule za mkoani hapa na hata wakati wa likizo wawe wanafanya hivyo na kuwa itaongeza ufaulu kwa wanafunzi kutokana na walimu hao kuwa na moto wa kufundisha..

Halikadharika, Mwera alisema ili kusaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na kuongeza ufaulu ni kuanzishwa vituo vya vijana kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji,  kata hadi Tarafa ambavyo vitakuwa na mashine zitakazo tumika kudurufu mitihani itakayotumika kwa ajili ya kujifunza vijana hao.

Katika mkutano huo Mwera alipata fursa ya kuelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo kuwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya ufundi bure  kwa vijana ambapo kwa Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara zaidi ya Sh.Bilioni 3 taasisi hiyo ingezipata iwapo kama ingehitaji kutoa mafunzo hayo kwa kutoza fedha na kuwa vijana 3500 wamenufaika.

Alitaja kazi nyingine ni kuhamasisha vijana wa shule za msingi na sekondari kujiunga na vyuo vya ufundi baada ya kuhitimu, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya hoteli na utalii kwa kuhamasisha utalii wa ndani pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana na wanawake na kuhamasisha watoto wa kike juu ya umuhimu wa shule.

 Pia Mwera alisema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia watoto Yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kupata masomo kuanzia shule ya msingi, Sekondari hadi vyuo vya ufundi. 

Alisema taasisi hiyo awali ilikuwa ikifanya kazi katika mikoa 10 lakini kutokana na kufanya vizuri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa kibali kuendelea kufanya kazi katika  mikoa yote ya Tanzania Bara ambapo ameomba maofisa wao watakapokuwa wakipita mikoani  wapewe ushirikiano.

Hivi karibuni taasisi hiyo ya Mkoa wa Mara inayojishughulisha na masuala ya elimu ili mtunuku tuzo ya heshima Rais Dk.. Samia Suluhu Hassan kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini, tuzo aliyokabidhiwa  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa niaba yake.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (kushoto) akimkabidhi cheti Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera, baada ya taasisi hiyo kutoa baadhi ya tuzo za heshima kwa washindi.
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera (kulia) akiwa meza kuu na viongozi waliohudhuria mkutano huo. Kutoka kushoto ni Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dk.Baganda Elpidius, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili, Katibu Tawala Tawala, Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Lucy Boniface na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, Lucia Mwiru.
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera, akiwa na Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dk.Baganda Elpidius baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Professor Mwera Foundation ya mkoani Mara,Hezbon Mwera (kulia) akiwa kwenye mkutano huo.


Wadau wa sekta ya elimu na walimu wakiwa kwenye mkutano huo.
Taswira ya makutano huo.
 

Friday, April 7, 2023

TANESCO SINGIDA YATOA FUTARI KWA MAKUNDI MBALIMBALI KWA AJILI YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

Viongozi mbalimbali wa Ofisi ya Sheikh Mkoa wa Singida, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) baada ya kupokea msaada wa futari  kutoka shirika hilo kwa ajili ya kuwasaidia watu mbalimbali wakiwepo wenye mahitaji maalum.

Dotto Mwaibale na Hamis Hussein - Singida

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO )  Mkoa wa Singida limetoa Sadaka ya Futari kwa  Wajane, Yatima, Wazee na watu wengine wenye mahitaji maalum mkoani hapa.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Tanesco  Mkoa wa Singida Afisa Usafirishaji wa shirika hilo, Juma Omary alisema shirika hilo limeitikia wito wa Ofisi ya Sheikh wa Mkoa wa Singida ambayo ambaye alitoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia makundi mbalimbali yenye uhitaji katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Leo tupo katika tukio  muhimu la kuwasaidia wenzetu wenye mahitaji,  Sheikh wa Mkoa alitupa ujumbe ili tusaidie jambo hilo  kwa kuwa shirika letu linashughulika na kuhudumia jamii tukaona tuitikie wito huo kwa kuwa ni wajibu wetu kurudisha faida kidogo tunayoipata kwa jamii,"  alisema Omary.

Omary alipongeza Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kuwa kiunganishi na Jamii na kuwa shirika hilo linaunga  jitihada za Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Subeiry Bin Ali na Sheikh wa  Mkoa wa Singida, Issa Nasoro za kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali wakiwepo Yatima na Wajane.

Afisa Uhusino na Huduma kwa wateja wa shirika hilo Mkoa wa Singida,  Rehema Mwaipopo alisema Tanesco imekuwa ikihudumia jamii hivyo inaungana  na watu wenye uhitaji katika kipindi hiki cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo alitumia nafasi hiyo  kuiomba ofisi ya Sheikh wa mkoa kuliombea shirika hilo ili liendelee kuwahudumia wananchi.

 Sheikh wa Mkoa wa Singida  Issa Nassoro amelishukuru shirika hilo  kwa kuwaajali wenye uhitaji ambapo ametumia nafasi hiyo kuyataka mashirika na taasisi zingine kuiga mfano kutoka Tanesco wa kusaidia jamii badala ya kusubiri wadau kutoka nje ya nchi.

 Nassoro alisema kuwa wajane na Yatima ni watu wa karibu na jamii kwa historia ya ukoo na dini pamoja na utanzania ambapo aliwataka wadau wengine kuwa na moyo wa huruma wa  kusaidia jamii.

“ Nawashukuru sana Tanesco Mkoa wa Singida kwa kuwajali wenye uhitaji na nitowe wito kwa mashirika mengine kama vile viwanda vya mafuta, na taasisi zingine kuiga mfano wa huo  kwa kuwasaidia wajane, Watoto yatima, wafungwa wa magereza ni aibu kuona  watu kutoka Uturuki na Misri  kuwasaidia ndugu zetu” . Alisema Sheikh  Nassoro.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kitengo cha Kusaidia jamii yenye Uhitaji kama vile Wajane, Yatima na Wazee ambao hawajiwezi cha Nusrati Al Ummati,  Ally Amani aliishukuru Tanesco Mkoa wa Singida kwa kutoa Futari hiyo pamoja na Taasisi ya Sheikh Arfu ambayo imetoa Tende.

“Mashallah wapendwa kaka zetu, Wapendwa shirika letu la Tanesco tunashukuru sana kwa msaada mliotoa kwetu  tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi na kuwatimilizia mahitaji yenu karibuni tena kwenye ofisi ya Sheikh wa Mkoa wa Singida. 

Aidha, Amani alimshukuru Sheikh Arfu na kampuni yake kwa kuwapelekea  tende boksi 20  kwa ajili ya kusaidia makundi hayo.
Picha ya pamoja wakati wa hafla yakupokea msaada huo toka Tanesco.
Afisa Usafirishaji wa shirika hilo, Juma Omary (wa nne kutoka kulia) akizungumza na viongozi wa ofisi ya Sheikh wa Mkoa wa Singida wakati wa kukabidhi msaada huo.
Afisa Usafirishaji wa shirika hilo, Juma Omary (katikati) akimkabidhi msaada huo mmoja wa wahitaji. Kulia ni Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro. Zawadi zikiwa zibeshikwa tayari kwa kutolewa kwa wahusika.
Msaada huo ukitolewa kwa wahusika.
Msaada huoukipokelewa.
Wakina mama wakisubiri kupokea msaada huo.

WAZIRI ULEGA AKABIDHI MADUME YA NG'OMBE KWA VIKUNDI VYA WAFUGAJI WILAYA YA MKALAMA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akiswaga ng'ombe katika hafla ya kukabidhi madume bora 40 ya ng'ombe  kwa vikundi vya wafugaji wilayani Mkalama mkoani Singida Aprili, 6, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Mkalama 

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amekabidhi madume bora 40 ya ng'ombe kwa vikundi vya wafugaji wilayani Mkalama mkoani Singida ukiwa ni mkakati wa serikali wa kufanya mabadiliko ya sekta mifugo wenye lengo la kuboresha mbari za mifugo ili kuwa na mifugo yenye tija zaidi.

Akikabidhi ng'ombe hao jana katika hafla iliyofanyika Kijiji Cha Iguguno wilayani hapa, alisema serikali imenunua madume ya ng'ombe 366 kwa thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 878.4 ambao watagawiwa wafugaji kwenye halmashauri nane nchini.

Ulega alisema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufungua milango, nchi nyingi zimekuwa zikihitaji nyama kutoka Tanzania lakini bahati mbaya ng'ombe za asili zinazofugwa na wafugaji hapa nchini hazina uzito nyingi zinakuwa kati ya kilo 80 hadi 120 tu.

Alisema madume bora ng'ombe ambayo yamenunuliwa na serikali watoto watakaozaliwa wa Zebra na Boran watakuwa na uzito wa kati ya kilo 150 hadi 200 na ubora unaotakiwa.

Aidha, Ulega aliwataka wafugaji nchini kuachana na fikra za kuwa na makundi makubwa ya mifugo ambayo mingi inaishia kufa kwa ukame na badala yake wawe na utaratibu wa kuivuna na kuiuza ili kuimarisha kipato chao na kuepukana na hasara zinazoweza kuzuilika.

Alisema wafugaji wabadilike waachane na ufugaji kama wa enzi  za mababu zetu wa kuwa na makundi mengi ya ng'ombe ambao inapotokea ukame wanakufa na kusababisha hasara kwa mfugaji.

Aliongeza kuwa wafugaji waanze kumiliki maeneo yao kwa ajili ya malisho na Halmashauri za Wilaya zihakikishe wafugaji ambao wana maeneo ya malisho wanapimiwa na kupewa hati ili kuepusha migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza kati ya wakulima na wafugaji.

 Mkurugenzi Msaidizi Uzalishaji Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Simon Lyimo alisema serikali imenunua madume bora ya ng'ombe ambayo yamesambazwa kwenye halmashauri za  Mkalama ambayo imepewa madume 40,Msalala 50,Chato 50,Maswali 50, Chamwino 50,Buchosa 46,Mvomero 40 na Halmashauri ya Wilaya ya Mkulanga ambayo imepewa madume 50.

Lyimo alisema serikali imenunua madume hayo ikiwa ni mpango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika  mabadiliko ya sekta mifugo ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuboresha mbari za mifugo ili kuwa na mifugo yenye tija zaidi.

Afisa Mifugo Wilaya ya Mkalama, Joseph Michael, alisema madume hayo 40 yatagawiwa kwa kila kikundi dume mmoja na atatumika kwa wanakikundi wote ambapo kikundi kitawajibika kumtunza,kumlisha na matibabu ili kumlinda ubora na ufanisi wake.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama,  Moses Machali ameahidi kuwa wao kama wilaya watahakikisha Madume hayo ya ng'ombe yanazalisha ng'ombe bora kama serikali ilivyokusudiwa.

Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Isack , ameomba serikali kuongeza kujenga majosho ya ng'ombe ili wilaya hiyo isikumbwe na magonjwa mbalimbali ya mifugo.

Amesema kuwa endapo kutakuwa na majosho mengi mifugo itakuwa haina magonjwa na hivyo kuzalisha nyama bora ambayo inakidhi masoko ya nje.

Baadhi ya wafugaji waliokabidhiwa Madume hayo ya ng'ombe kwa ajili ya mbegu wameishukuru serikali kwa kutoa Madume hayo ambayo kwa sasa yatawasaidia kuzalisha g'ombe bora.

Wamesema kupitia madume hayo watakuwa na mifugo bora itakayokuwa na mazao bora yanayotokana na mifugo, na hatimaye watainuka kiuchumi katika kaya zao.

wa Iramba Mashariki, Francis Isack, akizungumza katika hafla hiyo.
Wananchi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Muonekano wa ng'ombe hao waliokabidhiwa katika vikundi hivyo.
 

Tuesday, April 4, 2023

MSD YAANDAA SEMINA KWA WAHARIRI VYOMBO VYA HABARI, KUFANYIKA JIJINI DODOMA

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai
 

Na Dotto Mwaibale, Babati

BOHARI ya Dawa (MSD) imeandaa Semina maalum kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini itakayofanyika kwa siku mbili mkoani Dodoma.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai imeeleza kuwa semina hiyo itaanza kesho Aprili 5, 2023 na kufikia tamati kesho kutwa Aprili 6, 2023 na kuwa itafanyika katika Ukumbi wa Tume ya Uchaguzi  mkoani humo.

"Lengo la semina hii ni kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya MSD ambayo ni manne ya kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya nchini sambamba na maboresho mbalimbali yanayofanywa na taasisi hiyo kupitia mpangomkakati wake wa muda mfupi na mrefu" alisema Tukai.

Tukai alisema mbali na kuwajengea uelewa Wahariri juu ya majukumu na maboresho ya MSD, semina hiyo pia itatoa fursa kwa MSD kutoa ufafanuzi juu ya masuala kadhaa ambayo yamekuwa yakijitokeza kwenye jamii, kufanya ziara naokwenye maghala ya MSD kuangalia mfumo mzima wa mnyororo wa ugavi unavyofanya kazi na kisha kutembelea baadhi ya wateja wa MSD.

Sunday, April 2, 2023

KAMATI YA BUNGE PIC YAIPA KONGOLE REA KWA KASI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Public Investment Committee PIC), Augustino Vulu, akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembea mradi huo wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (R3R2) katika vijiji vya Irisya, Masutianga na Munyu vilivyopo Wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida, Aprili Mosi, 2023. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

Na Dotto Mwaibale, Singida

KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Public Investment Committee PIC) imewapongeza  Wakala wa Nishati Vijijini (REA)  kwa mradi wa usambaji wa a umeme katika vijiji vitatu vilivyopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida..

Vijiji vilivyonufaika katika mradi huo ni Munyu, Irisya na Masutianga vyote vikiwa Kata ya Irisya wilayani humo.

Wajumbe hao wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa PIC, Augustino Vulu wametoa pongezi hizo Aprili 1, 2023 baada kutembelea mradi huo wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (R3R2) ambao umeonesha kuleta tija kwa wananchi.

Vulu alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh. bilioni 50 kwa ajili ya kukamilisha miradi minne inayotekelezwa mkoani humo miradi ambayo ikikamilika itakuwa chachu kubwa ya maendeleo kwa wananchi.

“Leo tupo hapa Shule ya Sekondari ya Irisya ambapo tumeshuhudia jinsi wanafunzi na wananchi wanaoishi katika kijiji hicho jinsi walivyoanza kunufaika baada ya kupata umeme ambao umewekwa kwenye madarasa na wanafunzi kuanza kujisomea hadi usiku.” alisema Vulu.

Vulu alisema wanatarajia kuona ufaulu ukiongezeka kwa wanafunzi wanaochukua masomo ya sayansi kwani hivi sasa watakuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo baada ya kupata umeme.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene alisema mradi huo umeanza kuleta faida katika Shule ya Sekondari ya Irisya na vijiji hivyo vitatu vinavyopakana na shule hiyo na lengo likiwa nikuona umeme huo unawasaidia, kiuchumi, maendeleo kwa maana ya elimu na mambo mengine.

“Kuletwa umeme katika vijiji hivi sisi kwetu ni furaha na tunajua sasa tumetimiza wajibu wetu kuhakikisha kuwa yale malengo tuliojiwekea yanatimia” alisema Ndeme.

Ndeme aliwataka wananchi kuitumia fursa hiyo ya kuwekewa umeme kwa kujiunganisha kwenye maeneo yao ya makazi na biashara na wabuni biashara ambazo zinatumia umeme kwa ajili ya kujinufaisha kwa kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja, vijiji, wilaya nzima na mkoa kwa ujumla.

Aidha Ndeme amewaomba wananchi wa maeneo hayo yaliyopata umeme kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao wanayolima kwa kuyachakata na kuyaongezea thamani na kujikuta wakikua kiuchumi. 

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Singida kwa Kamati, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ameeleza kuwa Serikali kupitia Wakala hiyo imetoa jumla ya shilingi bilioni 73.1 na Dola za Marekani 988,707.60 ili kuhakikisha miradi minne inayotekelezwa mkoani humo inakamilika na wananchi wanapatiwa huduma ya nishati hiyo ili kujipatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 

Aidha, ameeleza zaidi kuwa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Wilaya za Ikungi na Singida unatekelezwa na Mkandarasi M/s Central Electricals International Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 26.3 na katika Wilaya za Iramba, Manyoni na Mkalama, unatekelezwa na M/s CRJE – CTCE Consortium kwa gharama ya shilingi bilioni 31.6 

Amesema kuwa, maendeleo ya Mradi kwa wastani yamefikia asilimia 70.21 ambapo kwa Wilaya za Ikungi na Singida, Mkandarasi amefikia asilimia 77.54 na Wilaya za Iramba, Manyoni na Mkalama, Mkandarasi amefikia asilimia 62.87. 

Mkoa wa Singida una jumla ya vijiji 441 ambapo vijiji 287 vimekwishapatiwa umeme kupitia miradi ya umeme vijijini iliyotekelezwa awali. Vijiji 169 vilivyobaki vinaendelea.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na REA katika kazi hiyo ya kutoa huduma kwa wananchi na ndio maana ilipo REA na TANESCO ipo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene, akizungumzia manufaa ya mradi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza kwenye ziara hiyo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga akizungumza kwenye ziara hiyo.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye ziara hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakiwa kwenye ziara hiyo.
Wajumbe wa Bodi ya REA wakiwa kwenye mkutano huo uliofanyika Kijiji cha Irisya. Kulia ni Osward Urassa na Francis Songela.
Wakurugenzi na Mameneja kutoka  REA wakiwa kwenye mkutano huo.
Wananchi na viongozi wa Wilaya ya Ikungi wakiwa kwenye mkutano uliofanywa na PIC katika Kijiji cha Irisya.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Irisya wakitoa burudani.
Taswira ya mkutano huo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Public Investment Committee PIC), Augustino Vulu, akionesha umahiri wa kucheza ngoma sanjari na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Irisya.
Wanafunzi wa Sekondari ya Irisya wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza kwenye mkutano huo.


Wajumbe wa Kamati PIC (mstari wa mbele) wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, REA, Jones Olotu akizungumza kwenye mkutano huo.

Mkandarasi wa mradi huo (katikati) wa Kampuni ya M/s Central Electricals International Ltd akijitambulisha pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Wananchi wa Kata ya Irisya wakiwa kwenye mkutano huo.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Mhandisi Florence Mwakasege, akizungumza.
Safari ya ukaguzi wa maabara ya Shule ya Sekondari ya Irisya ikifanyika kujionea matunda baada ya kupata umeme.
Wanafunzi wakielezea shughuli wanazozifanya kwa vitendo katika maabara yao baada ya kupata umeme
Baadhi ya viongozi wa REA wakiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene (katikati) baada ya kukagua maabara hiyo.
Mafunzo kwa vitendo yakioneshwa katika ziara hiyo ya PIC. Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Public Investment Committee PIC), Augustino Vulu, wakiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Sekondari ya Irisya.