Monday, November 30, 2020

KANISA LA MORAVIAN WATAKIWA KUTORIDHIKA NA MAENDELEO WALIONAYO

Mwenyekiti na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Mchungaji, Yona Mwambeta, akihubiri Jumapili wakati akiongoza harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Moraviani Usharika wa Kijichi jijini Dar es Salaam.
Waumini wa kanisa hilo wakiwa katika ibada hiyo.
Ibada ikiendelea.
Ibada ikiendelea.
Mwenyekiti na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Mchungaji, Yona Mwambeta (kushoto) na Mchungaji wa kanisa hilo Usharika wa Kijichi, Raphael Mwampagatwa wakiwa kwenye ibada hiyo.
Maombi yakiendelea.
Harambee ikiendelea. Kushoto ni mke wa Mwenyekiti na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Mchungaji, Yona Mwambeta, Mchungaji Lilian Mwambeta akihesabu sh.550.000 walizotoa kama mchango wao wa ujenzi wa kanisa hilo.
Mchungaji Lilian Mwambeta, akimkabidhi fedha hizo Mwenyekiti wa harambe hiyo, Subilaga Mwambeta.
Waumini wa kanisa hilo na wachungaji wao wakiwa nje baada ya kuhitimisha harambee hiyo.


Na Dotto Mwaibale


MWENYEKITI na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini,  Mchungaji, Yona Mwambeta amelitaka kanisa hilo kutoridhika na badala yake waige makanisa mengine yaliyopiga hatua ya maendeleo kwa kujenga makanisa makubwa na kuanzisha miradi ya maendeleo nchini.

Mwambeta aliyasema hayo Jumapili wakati akiongoza harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Moraviani Usharika wa Kijichi jijini Dar es Salaam.

"Wamoravian tangu siku nyingi wao ni watu wa kuridhika na vitu vidogo nawaambieni badilikeni na kuiga wanavyofanya wenzetu wa makanisa mengine ambao wapo mbali kimaendeleo" alisema Mwambeta.

Alisema kazi ya ujenzi wa kanisa hilo si ya waumini wa kanisa hilo pekee bali ni ya Mungu hivyo uchache wao usiwakatishe tamaa ya kupata fedha za kujenga kanisa hilo.

Akitolea mfano kanisa la Itungi lililopo wilaya ya Kyela mkoani Mbeya alisema lilianza kujengwa na watu wachache lakini leo hii limekuwa ni kanisa la mfano.

Mwambeta aliwataka waumini hao wa Kanisa la Moravian Kijichi kujenga kanisa kubwa litakalo akisi miaka  100 ijayo bila kujali litachukua muda gani kukamilika ujenzi wake.

Aidha Mwambeta aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwashirikisha watu mbalimbali bila ya kujali dini zao na madhehebu wanayotoka ili kulijenga kanisa la usharika huo.

Mwenyekiti wa ujenzi wa kanisa hilo Jackson Mwaisemba alisema harambee hiyo ni ya pili  na kuwa wataendelea kufanya nyingine ili kufikia malengo ya kupata sh.milioni 100 zitakazo saidia kuanza ujenzi wa kanisa  hilo.

Mchungaji wa kanisa hilo Usharika wa Kijichi, Raphael Mwampagatwa alimshukuru Mwambeta kwa kuendesha harambee na kuwapa ari na moto mpya waumini wa kuchangia ujenzi huo.

Mchungaji Mwampagatwa alitumia harambee hiyo kutoa namba ya Voda 5312023 na Tigo 0679-607003 kwa ajili ya makanisa mbalimbali, taasisi, mashirika, wafanya biashara na mtu yeyote ambaye atapenda kuchangia ujenzi wa kanisa hilo kiasi chochote cha fedha awe Dar es Salaam na maeneo mengine ndani na nje ya Tanzania na Mungu atawabariki.

Katika harambee hiyo fedha taslimu zilizopatikana zilikuwa ni sh.3,717,000, ahadi sh.4,685,000 na jumla ikiwa ni sh. 8,402,000.

Saturday, November 28, 2020

MTATURU AANZA KUTEKELEZA AHADI ZA WANANCHI KWA KASI YA 4G

Wachungaji na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kiaskofu Msalaba Mrefu mjini Singida, wakiwa na pikipiki walizokabidhiwa hivi karibuni na Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu kwa ajili ya kazi za kanisa hilo,
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akimkabidhi pikipiki, Mkuu wa Jimbo la Kusini Usharika wa Issuna, Mchungaji, Obedi Msele.
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akimkabidhi pikipiki, Mchungaji Joyce Madadi wa Usharika wa Ikungi.

 Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akimkabidhi pikipiki, Mchungaji, Felix Kibiriti.


Na Dotto Mwaibale, Singida.


MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameanza kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kwa kasi ya 4G.

Mtaturu ametekeleza ahadi yake  kwa kutoa pikipiki tano kwa Usharika wa Kiaskofu Msalaba Mrefu mjini Singida ambazo alimkabidhi Mchungaji Felix Kibiriti kwa niaba ya Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati Dkt. Alex Mkumbo kwa ajili ya matumizi ya shughuli mbalimbali za kanisa hilo mkoani Singida.

Mbali ya kukabidhi pikipiki hizo zenye thamani ya sh.milioni 11, Mtaturu pia alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo pikipiki mbili zenye thamani ya sh.milioni 4.6 kwa ajili ya Kituo cha Polisi cha Wilaya hiyo ili ziweze kusaidia kwa kazi.

Akizungumza hivi karibuni katika hafla ya kukabidhi pikipiki hizo Mtaturu alisema utoaji wa pikipiki hizo ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa kusaidia kanisa hilo kupata usafiri wa uhakika kwa watumishi wake wanapo kwenda kuhubiri neno la Mungu.

 "Nitaendelea kutimiza ahadi zangu na kushirikiana na wananchi kwa kasi ili kuunga mkono jitihada ya Rais Dkt. John Magufuli ya kutekeleza miradi ya maendeleo" alisema Mtaturu.

Aidha Mtaturu alisema kuwa pikipiki hizo zitatumika katika sharika za Mang'onyi, Issuna, Mungaa na Ikungi zilizopo Jimbo la Singida Mashariki.

 Mtaturu alitoa ahadi hiyo Novemba 8, 2020 wakati akizindua kitabu cha Misemo na Methali za Wanyaturu kilichoandikwa na Mchungaji Dkt.Syprian Yohana Hilinti (PhD) kilichozinduliwa katika Kanisa Kuu la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT) Singida mjini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi huko mshereheshaji katika hafla ya  uzinduzi wa kitabu hicho akiwa ni Mbunge wa Iramba  Mwigulu Nchemba.

Friday, November 27, 2020

KAMATI YA USALAMA WILAYA YA IKUNGI SINGIDA YAKAGUA MIRADI YA ELIMU NA AFYA



Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wakijadiliana wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Elimu na Afya wilayani humo. Kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo.
Moja ya chumba cha darasa kilicho kaguliwa na kamati hiyo.
Baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa.
Muonekano wa vyoo vya Shule ya Msingi vilivyo kaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Muonekano wa baadhi ya madarasa yaliyokaguliwa na kamati hiyo.
Ukaguzi ukiendelea. 

Wajumbe wa kamati hiyo wakikagua ujenzi wa Chuo cha Veta. Kushoto mbele ni  Mwenyekiti wa kamati hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo.


Muonekano wa ndani wa baadhi ya madarasa ya shule za sekondari yaliyokaguliwa na kamati hiyo.


Muonekano wa ndani wa baadhi ya madarasa ya shule za sekondari yaliyokaguliwa na kamati hiyo.


Moja ya chumba cha darasa cha shule ya sekondari kilicho kaguliwa na kamati hiyo.


Jengo la Maabara lililokaguliwa na kamati hiyo.


Muonekano wa vyoo vilivyo kaguliwa na kamati hiyo.



Na  Mwandishi Wetu, Ikungi


KAMATI ya Usalama ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya Elimu na Afya ambapo mbali na kupongeza usimamizi wa fedha zilizoletwa na Serikali juu ya miradi hiyo, iliwataka baadhi ya wasimamizi wa miradi hiyo kukamilisha kwa wakati ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wa miradi ya Elimu, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,  Edward Mpogolo, alisema ni lazima madarasa na vyoo vikamilike kwa wakati ili yaanze kutumika mapema mwakani na kuondoa changamoto ya vyumba vya madarasa iliyokuwepo kwenye shule hizo .

Aidha pamoja na mapungufu machache yaliyobainishwa na kamati wakati wa ukaguzi, kamati iliridhishwa na miradi hiyo kwa kuwa thamani ya fedha za serikali katika miradi inaonekana ambapo pia ilimtaka Mhandisi wa Halmashauri kuhakikisha anasimamia  maboresho na mapungufu yaliyojitokeza na kutoa msaada wa kitaalamu kwa kila mradi uliokutwa na dosari. 

Kwa shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi, Mpogolo alizielekeza Serikali za vijiji na Kamati za Maendeleo ya Kata kuanza mchakato wa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hizo na kuongeza kuwa serikali itaunga mkono katika ukamilishwaji wa majengo ya shule hizo huku akiagiza afisa Mipango Miji na Mhandisi wa wilaya kukagua na kupima maeneo yote yenye shule shikizi na kupeleka mapendekezo  katika vikao vya halmashauri juu ya ukamilishwaji wa shule hizo.

Katika mradi wa ujenzi wa  Hospitali ya Wilaya, Mpogolo, aliitaka kamati ya ujenzi iliyoteuliwa na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya usimamizi wa mradi ambao unaendeshwa kwa mfumo wa  “Force Account” kuhakikisha wanakuwepo  eneo la mradi kila siku kwa ajili kushauri kitaalamu na kusikiliza changamoto ambazo mafundi wanakumbana nazo wakati wa ujenzi. 

Alisisitiza mradi huo, ambao ulitengewa kiasi cha sh. Bilioni 1.5 unatakiwa ukamilike kwa wakati na kwa thamani halisi kama ambavyo iliagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, katika ziara yake ya kampeni, ambapo alitoa siku 60 ili kukamilika kwa mradi huo na kuahidi kufika kwa ajili ya uzinduzi.

Katika ziara hiyo ya siku tatu, kamati pamoja na wataalamu wa halmashauri walitembelea na kukagua miradi yote ya Afya na Elimu inayotekelezwa katika Wilaya ya Ikungi katika mwaka wa fedha 2019/2020  na  yote ikiwa na thamani ya zaidi ya  sh. Bilioni 4.5.

Wakati huo huo, mkuu wilaya hiyo amemuagiza Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kuchunguza taratibu zote za ujenzi wa Madarasa Matatu na vyoo vya Shule ya Msingi Matongo baada ya kubainika ukiukwaji wa taratibu mbalimbali za ujenzi. 

Ukiukwaji huo ulibainika baada ya kamati ya usalama kufika katika shule hiyo kukagua ujenzi unaoendelea wa madarasa na vyoo hivyo na kubaini mapungufu mengi na hivyo, Mpogolo kuagiza kufanyika kwa uchunguzi na ikibainika hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wahusika wote wa usimamizi wa mradi huo na katika kipindi hicho cha uchunguzi Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo amtafute mwalimu atakaekaimu nafasi ya mwalimu mkuu.

Hata hivyo, Kamati ya Usalama ilimshukuru Rais Magufuli kwa kuleta fedha nyingi zaidi ya 4.5 bilioni za maendeleo kwa muda mfupi. Pia imempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Justice Kijazi, kwa kuendelea kusimamia vizuri fedha ya serikali katika miradi inayoletwa katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. 

Miradi iliyokaguliwa na kamati hiyo ni ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari na msingi, mabweni, mabwalo, ununuzi wa madawati, ujenzi wa vyoo, maabara na ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha Veta.


SEKTA YA MISITU IKISIMAMIWA VIZURI INAWEZA KULETA MAPINDUZI MAKUBWA YA MAENDELEO KWENYE VIJIJI

Muwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Nanjita Nzunda  akifungua Warsha na Mkutano Mkuu wa 20 wa Mwaka wa MJUMITA mkoani Morogoro.

Mwenyekiti wa MJUMITA, Revocatus Njau akitoa nasaha zake mbele ya wajumbe kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kufungua mkutano huo.


Mkurugenzi wa MJUMITA, Rahma Njaidi  akieleza malengo ya Warsha na Mkutano huo Mkuu wa 20 wa Mwaka wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.



 Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo, akitoa salamu za Shirika lake mbele ya wajumbe wa mkutano huo wa Mwaka wa MJUMITA.

Wajumbe wa Mkutano huo Mkuu wa 20 wa Mwaka wa MJUMITA kutoka Kanda zote sita wakifuatilia hotuba na nasaha za ufunguzi wa mkutano huo.
Wajumbe wa Mkutano huo Mkuu wa 20 wa Mwaka wa MJUMITA kutoka Kanda zote sita wakifuatilia hotuba na nasaha za ufunguzi wa mkutano huo.
Wajumbe wa Mkutano huo Mkuu wa 20 wa Mwaka wa MJUMITA kutoka Kanda zote sita wakifuatilia hotuba na nasaha za ufunguzi wa mkutano huo.
Wajumbe wa Mkutano huo Mkuu wa 20 wa Mwaka wa MJUMITA kutoka Kanda zote sita wakifuatilia hotuba na nasaha za ufunguzi wa mkutano huo.



 Na Calvin  Gwabara, Morogoro.


IMEELEZWA kuwa Sekta ya Misitu ikisimamiwa vizuri na kwa uendelevu italeta mchango chanya katika sekta zinazotegemea mifumo ikolojia ya Misitu ya asili kama vile Kilimo, Maji,Wanyamapori, na nishati.

Hayo yalisemwa na  Nanjita Nzunda Muwakilishi wa KatibuTawala wa Mkoa wa Morogoro kwenye ufunguzi wa Warsha na mkutano Mkuu wa 20 wa mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misiti Tanzania MJUMITA uliofanyika Mkoani Morogoro.

Alisema  kuwa sera na sheria ziko wazi na zinawezesha vijiji kuanzisha na kurasimisha misitu yao na kuandaa mipango yao ya usimamizi, sheria ndogondogo na mipango ya uvunaji.

“Kwa kurasimisha Misitu yao ya hifadhi, vijiji vinakuwa na mamlaka ya kusimamia na kunufaika kwa asilimia Mia moja na Misitu huo lakini pia kunatoa fursa kwa Kijiji husika kuusimamia huo Msitu kwa manufaa ya Wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa Misitu” alisema  Nzunda.

Aliongeza kuwa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya Jamii ni nyenzo kuu ya uhifadhi wa Misitu kwani wananchi wanakuwa na na mamlaka ya kuusimamia Msitu husika kulingana na Mipango yao ya Usimamizi na sheria ndogo walizojiwekea.

Nzunda alibainisha kuwa pamoja na faida hizo lakini kila Mwaka Tanzania inapoteza hekta zaidi ya 460,000 za Misitu kiasi ambacho ni kikubwa sana hivyo kila Mtanzania anapaswa kuchukua za makusudi kunusuru Misitu.

“ Nawapongeza sana MJUMITA na TFCG kwa kuwezesha vijiji kuanzisha misitu ya hifadhi ya vijiji Kilosa,Mvomero,Morogoro,Kilwa,Lindi, Liwale,Tunduru, Nachingwea, Handeni na Kipindi ambako zaidi ya vijiji 100 vimewezeshwa na nimefurahi kusikia kwamba mashirika haya mawili yamewezesha Misitu ya Hifadhi zaidi ya 50 kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali (Gazettment).

Aliongeza kuwa Misitu hiyo ina jumla ya Hekta 168,331.38, na kwamba hayo ni mageuzi makubwa katika sekta ya Misitu na nu Misitu ya mfano kufikia hatua hiyo.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi huyo kufungua warsha na mkutano huo Mkuu Mwenyekiti wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania MJUMITA, Revocatus Njau  alisema kuwa MJUMITA ni chombo cha Kitaifa ambacho kinaunganisha Jamii zinazoishi kandokando ya misitu ya asili na kuwa na sauti ya pamoja juu ya usimamizi wa Misitu na utawala Bora.

Mwenyekiti huyo alisema mtandao huo ulianzishwa Mwaka 2000 na ilisajiliwa Kama NGO Mwaka 2017 na mtapa sasa ina mitandao 100 katika Kanda sita za Tanzania na kwamba ina wanachama katika vijiji 452 kwenye mikoa 30 ya Tanzania bara.

“ Kupitia jitihada hizo kubwa za TFCG na MJUMITA zinewwzesha kuboresha maisha ya jamii kupitia shughuli mbalimbali kama vile ufugaji wa Nyuki,Kilimo,Kilimo hifadhi,miradi ya maji,ufugaji vipepeo, uzalishaji wa Mkaa Endelevu na uanzishwaji wa ViCOBA” alibainisha Njau.

Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa MJUMITA ineweza kuwaleta Pamoja takribani Wanachama 15,000 katika usimamizi wa Misitu ya asili vijijini wakisimamia Misitu zaidi ya hekta 1,800,000 katika vijiji viwili.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa MJUMITA, Rahma Njaidi alisema kuwa Warsha na Mkutano huo Mkuu wa Mwaka hufanyika kila Mwaka na kuwakutanisha wajumbe kutoka nchi nzima ili kujadili changamoto na mafanikio yanayopatikana kila Mwaka na kuyatafutia ufumbuzi wa pamoja.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa misitu bado inaangamia kutoakana na kazi mbalimbali za kibinadamu hivyo kuna kila sababu ya kurasimisha Misitu hiyo iliyo kwenye vijiji nchi nzima ili kupunguza uharibifu unaofanyika kiholela ili itunzwe na kutumika kwa njia endelevu kwa maslahi ya vijiji na Taifa kwa ujumla.

“ Tukiacha uharibifu huu uendelee tutaifanya nchi yetu kuwa jangwa na sisi hatuwezi kuruhusu Hilo litokee hivyo tuisaidie Serikali maana sisi ndio tupo huku chini tunajua kinachoendelea” alisisitiza, Njaidi.

Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa NAFOMA uliofanyika Mwaka 2017 ulionyesha zaidi ya hekta 4069 inapotea kutokana na uharibifu wa aina mbalimbali za misitu.

“ Ni wajibu wetu wananchi kuhakikisha tunatunza misitu yetu nchi nzima kwa kupanga namna bora  ya kusimamia lakini pia mapato yanayopatikana kutokana na mazao ya misitu hiyo yatumike kwenye vijiji kwenye miradi ya maendeleo kama motisha ya usimamizi huo” alisema Lyimo.

Lyimo aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutambua kuwa wakati umefika jamii na serikali iwekeze kwenye Misitu ili itangazwe kwenye gazeti la Serikali ili kuvipa vijiji nguvu za kuisimamia vizuri kisheria na kuongeza misitu ya hifadhi ya jamii inayosimamiwa kutoka hekta milioni mbili kwa sasa na kuifikia misitu hekta milioni 22 ambayo haijaifadhiwa kwa sasa.

Mashirika ya MJUMITA na TFCG wanatekeleza Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ) chini ya Mradi wa kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) na mradi wa kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoFOREAT) kwa ufadhili wa Shirika la  Maendeleo la Uswis (SDC).


Thursday, November 26, 2020

SINGIDA YAWANOA WANAUSHIRIKA

 

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba akiongea na Waandishi wa Habari.

                  

Mwenyekiti wa   Chama Kikuu Cha Ushirika  cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani  akiongea na Waandishi wa Habari


 Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa   Vyama vya Ushirika  katika  Mkoa Singida  wakipewa mafunzo

                            ......................................

 

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Mkoa wa Singida umeandaa  mafunzo  ya siku  tatu ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa   Vyama vya Ushirika  katika  Mkoa ili kuwasaidia  kuacha  kufanya kazi kwa  mazoea  badala yake wafanye  kazi  kwa weledi na kwa kuzingatia sheria  huku wakitanguliza mbele maslahi ya wakulima. 

 

Akifungua mafunzo hayo leo mjini Singida kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia eneo la Uchumi Beatus Choaji amesema Mkoa umeamua kufanya  mafunzo hayo kutokana na kupata taarifa  ya ukaguzi uliofanywa kwenye vyama vya ushirika  kushindwa kufanya vizuri.

 

Choaji amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho kwa viongozi wa Vyama Vya Ushirika na maafisa wengine wa Serikali ambao wamekuwa wakishirikiana na walanguzi kuwanyonya wakulima ambapo amesema hili ni  kosa kisheria  na  kuwaonya kwamba  katika kipindi cha sasa Sheria kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwatia hatiani kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi.

 

 “Nawaagiza Watumishi wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake fanyeni kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria huku mkitanguliza mbele maslahi ya wakulima”aliongeza Choaji

 

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Singida, Thomas Nyamba amesema lengo la  kuandaa mafunzo hayo ni kutoa elimu  ya kuwawezesha Watendaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

 

Nyamba amesema kumekuwa na makosa mbambali ya kiuzembe  na kitaaluma katika utendaji wa kazi lakini kupitia mafunzo haya watendaji wote watabadilika.

 

Mwenyekiti wa   Chama Kikuu Cha Ushirika  cha Wakulima Mkoa wa Singida (SIFACU LTD) Yahaya Ramadhani  amesema pamoja na mambo mengine wajumbe wa kikao hicho watafundishwa masomo ya uandishi wa vitabu vya mwanzo na vitabu vikuu,uaandaaji wa taarifa za fedha,uongozi na utawala pia na Sheria ya Vyama Vya Ushirika Na.6. ya Mwaka 2013

 

Ameyataja masomo mengine yatakayo fundishwa kuwa ni uandaaji wamakisio ya mapato na matuminzi,uandaaji wa mpango mkakati, utatuzi wa migogoro na usimamizi wa fedha na udhibiti wa rushwa katika vyama vya ushirika.

 

Baadhi ya washiriki katika wa mafunzo hayo wamepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Tano kutoa mafunzo na kusema kwamba yataongeza tija katika utendaji wao wa kazi.

 

Mwenyekiti wa AMCOS wa Wilaya ya Ikungi Mnang’ana Rukia Jumanne amesema mafunzo hayo yamewasaidia kutambua majukumu ya kila mmoja kwenye vyama vya ushirika hivyo yatawawezesha kufanya kazi bila kuingiliana nakwa weledi tofauti na kipindi cha awali.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi amesisitiza kwamba   kwa sasa Serikali imeweka  mikakati madhubuti ya kuufanya Mkoa wa Singida  kuwa miongoni mikoa itakayozalisha kwa  wingi mazao na  kuilisha Tanzania na nchi  mbalimbali za Afrika  na dunia kwa ujumla na hivyo kuwa na  Vyama vya Ushirika  makini ni jambo  lisiloepukika  kwenye Mkoa wa Singida.

“Tumeanza vizuri kwenye zao la Korosho na Alizeti sasa tunaongeza nguvu kufufua na kuanzisha mazao ya Mkonge na Parachichi” aliongeza Mhe. Nchimbi

Wednesday, November 25, 2020

VIJIJI VYA LIWALE MKOANI LINDI VYANEEMEKA NA UHIFADHI WA MISTU

Katibu Tawala wa Wilaya  ya Liwale mkoani Lindi, Rajabu Kambangwa  akizungumza na wandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini kuhusu mchango wa sekta ya misitu kwenye wilaya hiyo.
Afisa Sera na Majadiliano  wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) Elida Fundi   akizungumza na waandishi wa habari walipokuwa kwenye ziara ya kuona namna Vijiji vya Darajani, Mihumo na Mtawatama zilivyofanikiwa katika jitihada za utunzaji shirikishi wa misitu.
Afisa Misitu wa Wilaya ya Liwale Nassoro Ali Mzui akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jitihada wanazozifanya kwa kushirikiana na Serikali za vijiji na wadau wengine wa misitu kwenye ulizi shirikishi wa misitu.
Afisa Sera na Majadiliano  wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) Elida Fundi akiwa kwenye picha ya pamoja na kamati ya maliasili ya kijiji cha Mtawatawa Wilayani Liwale.
 

Na Calvin  Gwabara, Liwale.


ZAIDI ya shilingi milioni 957 zimepatikana kwenye vijiji kutokana sekta ya misitu katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi na hivyo kuchangia katika kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya na maji.

Hayo yamebainishwa na KatibuTawala wa Wilaya  hiyo,  Rajabu Kambangwa wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mchango wa sekta ya misitu na ushiriki wa wilaya hiyo kwenye uhifadhi shirikishi wa misitu ya vijiji.

Alisema kuwa wilaya ya Liwale misitu ni chanzo kikubwa cha mapato ya wilaya kwani katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 iliingizia serikali kiasi cha shilingi bilioni 2.6 ikifuatiwa na sekta ya kilimo na hivyo kuifanya sekta ya misitu kuwa sekta muhimu kwauchumi.

” Sisi kama wilaya tunanufaika sana na uwepo wa rasilimali hizi kwa hiyo tunafarijika sana ujio wa miradi kama huu ya Uhifadhi shirikishi wa misitu kwani inasaidia kuwajengea uwezo wananchi kwenye vijiji vyetu kuona umuhimu wa misitu na uhifadhi wake kwa maendeleo endelevu lakini kubwa zaidi kuona misitusi ya serikali bali ni mali yao” alisema  Kambangwa.

Katibu Tawala huyo alisema kwenye Kijiji cha Likombola pekee kiliingiza kiasi cha shilingi milioni 253 huku Kijiji cha Mtawatawa wakiingiza kiasi cha shilingi milioni 122 ambazo zimetumika kufanya shunguli mbalimbali za maendeleo kwenye vijiji hivyo ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa, Zahanati, Nyumba ya Mtendaji wa Kijiji Pamoja naTrekta la Kijiji ambalo linawasaidia kwenye kilimo kwa kukodishiana  kwa gharama za chini na kwa wakati.

Alisema pamoja na mafanikio hayo makubwa lakini swala la uhifadhi bado linahitaji elimu kwa jamii maana Wananchi wasipoona faida za moja kwa moja kwenye vijiji vyao hawawezi kuitunza wala kuilinda na hivyo kusababisha misitu kupotea wakidhani ni mali ya Serikali.

Kwa upande wake Afisa Sera na Majadiliano wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)Elida Fundi alisema kuwa vijiji vinafanyakazi kubwa na nzuri katika kuhifadhi misitu ya vijiji na hii inatokana na elimu na motisha wanayoipata kwenye vijiji vyao baada ya kuvuna misitu hiyo kwa uendelevu.

Alisema MJUMITA kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo na misitu wataendelea kushiriki kikamilifu kwenye kuzisaidia Halmashauri na vijiji katika awamu hii ya tatu ya mradi kuweka mipango bora yamatumizi ya ardhi na utengaji wa maeneo ya misitu ya hifadhi za vijiji ili itunzwe na kuvunwa kwa njia endelevu ambazo zitatunza misitu hiyo.

Kwa upande wake Afisa Misitu wa wilaya hiyo, Nassoro Ali Mzui alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo kwenye uhifadhi wa misitu hiyo ni vitendea kazi hasa vyombo vya usafiri kama pikipiki na zana zingine kwani misitu mingine inaukubwa wa zaidi ya hekta elfu 13 hivyo kuwawia vigumu kufanya doria na kuizunguka kwa miguu.

Alisema kwa kuwa vijiji vinachangia asilimia kumi ya mapato yatokanayo namisitu kwenda kwenye halmashauri wamekuwa wakifanya doria za pamoja na wanavijiji na kamati zao za maliasili za kijiji pamoja na maafisa wa maliasili na askari ili kusaidia kuongeza nguvu na kurahisha zoezi la ulinzi kwenye misitu hiyo.

AFISA VIJANA SINGIDA AWATAKA VIJANA KUTUMIA FURSA YA MSIMU HUU WA MVUA KWA KILIMO

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani. 
 


Na Mwandishi Wetu, Singida

KAIMU Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amehamasisha vijana mkoani hapa na kwingineko nchini kuhakikisha wanatumia fursa ya msimu huu wa mvua kujikita katika kilimo cha kibiashara ili kujiongezea kipato.

Akizungumza mkoani hapa jana, Ndahani alisema anaamini kijana yeyote atakayethubutu kujiingiza katika kilimo kamwe hatajutia kutokana na faida kubwa atakayoipata.

"Nawahamasisha vijana wenzangu tujitokeze tukalime, tusiiache mvua hii ikapita bure. Kwa wasio na mashamba wasisite kwenda kukodi...shamba la kukodisha gharama yake ni wastani wa kati ya shilingi elfu 25 na 30 kwa ekari moja," alisema.

Alisema wakati serikali ikipambana kuhamasisha mageuzi ya kilimo ni jukumu la vijana kuhakikisha wanaunga mkono juhudi hizo kwa kutambua kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.

Ndahani alisema takribani asilimia 60 za malighafi ya viwanda vilivyopo nchini hutegemea kilimo hivyo ni jukumu la vijana kuhakikisha wanakwenda na kasi ya mheshimiwa Rais John Magufuli katika kulifanya taifa hili kuendelea kustawi kiuchumi.

"Niwaombe sana tusiwaachie wazee na wanawake peke yao bali vijana tuingie rasmi shambani tusiache mvua hizi zikapita hivi hivi,"alisema afisa huyo wa vijana.

Alisisitiza mathalani kwa vijana wa mkoa wa singida, wana kila sababu ya kuchangamkia fursa ya kilimo chenye tija kutokana na uwepo wa viwanda vingi vinavyohitaji malighafi, hususan zao la alizeti ambalo ndio zao kuu mkoani humo.

Pia aliwakumbusha vijana kuwa mbali ya alizeti tayari serikali imekwishafungua dirisha lingine kwa kilimo cha korosho kwenye mikoa yote ya Kanda ya Kati ikiwemo Singida, zao ambalo lina usalama zaidi na soko la uhakika ndani na nje ya nchi...na kwamba wasichelewe kuchangamkia fursa hiyo ili kuondokana na umasikini na kuinua kipato.

Ndahani ambaye ameshawahi kushiriki kwenye timu maalumu ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru miaka ya hivi karibuni, alisema anaamini misingi bora ya taifa lolote lenye amani, utulivu na usalama hutokana na watu wake hususan vijana kujikita ipasavyo katika  uwajibikaji kwenye nyanja mbalimbali-ikiwemo shughuli za kilimo.


Sunday, November 22, 2020

MEYA SINGIDA AJIVUNIA KUIACHA MANISPAA IKIWA NA HATI SAFI

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida aliyemaliza muda wake, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mtamaa mkoani hapa, Gwae Chima Mbua (katikati), akiongoza moja ya vikao vya baraza la madiwani.


Na Godwin Myovela, Singida


MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Singida aliyemaliza muda wake, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mtamaa mkoani hapa, Gwae Chima Mbua, amesema mpaka sasa anajivunia kuiacha manispaa hiyo ikiwa inashikilia cheti cha hati safi kutokana na usimamizi madhubuti uliojengwa katika misingi ya nidhamu, hususan kwenye eneo la makusanyo na matumizi ya fedha za umma.

Akizungumza na vyombo vya habari mkoani hapa leo, vilivyomtaka aeleze kwanini anastahili tena kupewa dhamana ya nafasi ya umeya na si diwani mwingine, alijibu kila mgombea hupimwa kwa uwajibikaji wake na sio kimitazamo wala mihemko.

Alisema mpaka alipokabidhi ofisi hiyo hivi karibuni, aliacha manispaa hiyo ikiwa kwenye makusanyo ya takribani asilimia 83, sambamba na kufanikiwa kuwaunganisha madiwani na watumishi katika kuendelea kuijenga Singida kwa kasi na muktadha unaoendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

“Nawashukuru madiwani na serikali walinipa ushirikiano mkubwa sana, lakini nidhamu, uadilifu na kasi tuliyokwenda nayo vilichochea kasi ya maendeleo yetu hadi kuzivutia hata halmashauri nyingine zipatazo 19 kutoka maeneo tofauti nchini kuja kujifunza- hasa kupitia umahiri wa mradi wa stendi ya misuna,” alisema Mbua.

Alisema mpango uliopo kama atapata ridhaa ya kuchaguliwa tena, ni kuchagiza kwa kuharakisha mchakato wa maboresho ya soko la vitunguu kwa kuhakikisha linawekewa miundombinu ya kisasa ikiwemo zege na lami kwenye barabara zinazolizunguka ili kuondoa kero ya tope na mazingira yasiyo rafiki hasa wakati wa mvua.

Alisema tayari manispaa hiyo imefanikiwa kufungua akaunti maalumu ya mikopo ya akina-mama, hivyo jukumu lililo mbele yake kama atapata ridhaa ni kuimarisha fursa hiyo kwa ustawi wa maisha ya wanawake wa singida, lakini shabaha kubwa ni kuhakikisha makusanyo yanapanda kwa zaidi ya asilimia 83.

Mbua alisisitiza kama atachaguliwa tena ataendelea kuhamasisha nidhamu ya matumizi ya fedha kama alivyofanikiwa kwa miradi mbalimbali iliyotangulia, ikiwemo ule wa fedha zilizotolewa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

“Tunakwenda vizuri na kwa kasi ya aina yake, natamani kuiona singida ikiwa jiji…kwa sasa kuna maeneo fulani tayari yameshaanza kuitwa Ubungo, naitamani singida isiyo na rushwa, singida ya maendeleo ya kweli,” alisema Diwani huyo wa Mtamaa na kuongeza:

“Bado kuna mambo mengi ya kuweka sawa mathalani pale stendi bado tunahitaji kufunga CCTV Camera, lakini tunahitaji kukamilisha mchakato wa kutenga maeneo ya viwanda, kupima viwanja zaidi, kujenga machinjio ya kisasa, kuboresha mifumo ya ukusanyaji taka, pamoja na kuboresha soko letu la vitunguu.”

Mipango mingine iliyopo kama atapata ridhaa ni kuhakikisha anasukuma kwa kasi ujenzi wa soko la kisasa litakalojengwa eneo la Mandewa nje kidogo ya manispaa hiyo, sambamba na kuboresha ‘High Schools’ za Mungu Maji na Mandewa, juhudi ambazo anashukuru kwamba zinaungwa mkono na serikali.

“Nina nia njema ya kuwatendea haki watu wa manispaa ya Singida kwa nafasi ya Meya, suala kubwa ni kuleta maendeleo na faraja,..lakini pia kuunga mkono kwa vitendo kasi ya mheshimiwa Rais katika kuifanya manispaa yetu kuendelea kuwa njema tena njema sana,” alisema Gwae Mbua.

SPRF INAVYOSHIRIKISHA WANAFUNZI KUTOKOMEZA UKATILI

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Munkinya, Yoden Ngogo akiwakaribisha Maafisa wa Shirika lisilo la Kiserikali la Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) la mkoani Singida mwishoni mwa wiki,  kuzungumza  na wanafunzi wa shule hiyo, kuhusiana na masuala yahusuyo athari za ukatili wa kijinsia.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Munkinya wakisikiliza mafunzo ya ukatili wa kijinsia yalikuwa yakiwasilishwa na watendaji wa SPRF (hawapo pichani)
Wanafunzi wa Munkinya Sekondari wakiwasilisha mpango kazi wa utekelezaji majukumu yao kuhusiana na vita iliyopo dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia.

Mafunzo yakiendelea.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Siuyu wakifuatilia mafunzo hayo.

Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ikungi, Paul Mgelwa akifuatilia mafunzo hayo, kulia ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Siuyu.

Mratibu wa Mradi kutoka SPRF, Mwalimu Bernard Maira akizungumza na wanafunzi wa sekondari ya Siuyu (hawapo pichani)

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Siuyu wakifuatilia mafunzo hayo.

Mratibu wa Mradi kutoka SPRF, Mwalimu Bernard Maira akizungumza na wanafunzi wa sekondari ya Siuyu wakati wa mafunzo hayo.

 


Na Godwin Myovela, Singida


MATUKIO ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wasichana wenye umri mdogo, ikiwemo mimba na ndoa za utotoni, vitendo vya ukeketaji na ubakaji yameendelea kupungua katika wilaya ya Ikungi mkoani hapa- huku sababu kubwa ikitajwa kuwa ni matokeo ya ushirikishaji wa makundi rika katika kupambana na vita hiyo ndani ya jamii, imeelezwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) nchini, Dkt Suleiman Muttani, aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya shirika hilo kutembelea na kufanya mijadala ya pamoja kwa kushirikisha shule za sekondari Munkinya na Siuyu zilizopo wilaya ya Ikungi, mkoani hapa.

“Tumeunda ‘Clubs’ za wanafunzi mashuleni ambao pamoja na mambo mengine tunawapa fursa ya kuchagua viongozi, tunawajengea uwezo na kuwasimamia kutengeneza mpango kazi ambao unawasaidia katika kuwawezesha kufichua na kupeana elimu ya matukio ya kutokomeza ukatili, mimba na ndoa za utotoni wao kwa wao,” alisema Muttani. 

Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa shirika hilo, Mwedinuu Beleko, akiwasilisha mada kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wanafunzi wa shule hizo, aliitaka jamii kujitokeza haraka na kutoa taarifa yenye ushahidi pindi matukio ya ukatili yanapojitokeza ili kurahisisha mwenendo wa shauri.

“Nawaomba wanafunzi msiogope, wala msitishwe na mtu yeyote tukio lolote la ukatili linapojitokeza basi hakikisheni aliyefanyiwa ukatili huo anashiriki mara moja katika kutoa taarifa yenye ushahidi…na msipoteze huo ushahidi na vielelezo vyote ili kuharakisha mchakato wa kesi kuendelea kwa wakati,” alisema Beleko.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wilayani hapa, Paul Mgelwa aliwasihi wanafunzi kuwa makini na kutodanganyika ili kukabiliana na mimba zisizotarajiwa ambazo hufifisha ndoto na matarajio yao-na kusisitiza kuwa daima wanapaswa kuweka kipaumbele cha elimu kwanza kwa kuzingatia elimu ndio ukombozi wa maisha katika kupambana na umasikini.

Katibu wa Shirika hilo, Dkt Mwajuma Mikidadi alisema malengo ya SPRF, ambayo miradi yake ipo chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS), ni kukuza ushirikiano miongoni mwa wadau na jamii, taasisi za kitaifa na kimataifa katika kutokomeza umaskini wa kipato, sambamba na kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kukua na kutekeleza programu endelevu.

“SPRF na jamii ndio moto wetu kwa sasa, programu hii imesaidia kumfanya kila mwanafunzi wa kike kutambua haki zake, lakini madhara ya mila zilizopitwa na wakati na kandamizi, masuala ya ukeketaji na mimba na ndoa utotoni ndani ya jamii,” alisema Mikidadi.

Mratibu wa mradi huo, Mwalimu Bernard Maira, alisema hata hivyo shirika hilo limefanikiwa kuanzisha Kamati za MTAKUWWA kwenye vijiji 8 zinazopinga Ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto huku wakihamasisha uanzishwaji wa vikundi mathalani Sauti ya Mwanamke na Sauti ya Mwanafunzi, ambavyo vimekuwa chachu ya mageuzi ya kifikra dhidi ya mila potofu na masuala ya ukatili ndani ya jamii zao.