Friday, June 30, 2023

MADEREVA MSD WAJENGEWA UWEZO ILI KUTOA HUDUMA KWA UFANISI KATIKA UTENDAJI KAZI WAO

Watumishi wa Kada ya Udereva wa Bohari ya Dawa (MSD) kutoka Makao Makuu na Kanda zote 10 wakiwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo yalioandaliwa na MSD yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WATUMISHI wa Kada ya Udereva wa Bohari ya Dawa (MSD)  wamepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo iliwaweze kutoa huduma bora kwa wateja wakati wa usambazi wa bidhaa za afya.

Mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Morogoro yamewahusisha madereva wote wa MSD kutoka Makao Makuu na Kanda zote 10 ambazo ni Dodoma, Mtwara, Kilimanjaro, Kagera, Dar es Salaam, Iringa, Tanga, Tabora, Mbeya na Mwanza.

Mkufunzi wa mafunzo hayo Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu , Adolar Duwe, amesema kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa Wataalamu wa usambazaji bidhaa za afya kwani yatawawezesha kuongeza uelewa juu ya huduma kwa wateja na namna ya kuhudumia wateja wa MSD.

Akizumgumza kwa niaba ya Maderava wa MSD Bw. Erick Kaaya, amesema mafunzo hayo yamewaongezea ujuzi, kujiamini na uelewa wa masuala mbalimbali ya muhimu katika kuhudumia wateja.

 Aidha ameiomba Menejimenti ya MSD, kuratibu mafunzo hayo mara kwa mara, ili kuwajengea uwezo na kuongeza tija katika utekelezaji wa shughuli za taasisi.

Madereva wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mmoja wa madereva akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakitolewa.
Taswira ya mafunzo hayo.
 

Saturday, June 24, 2023

MADINI CHUMVI YALIYOPATIKANA WILAYA YA MANYONI KUWA CHANZO KIPYA CHA MAPATO

 Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota akizungumzia  Madini Chumvi yaliyopatikana Kata ya Majiri Kijiji cha Mpandagani  wilayani humo katika kikao kilichofanyika ofisini kwake jana Juni 23,2023 kuwa ni chanzo kipya cha mapato katika Halmashauri ya wilaya hiyo. 

Na Dotto Mwaibale, Manyoni

MKUU wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota amesema kuwa Madini Chumvi katika Kata ya Majiri Kijiji cha Mpandagani  yatakuwa chanzo cha mapato katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.

DC Kemirembe ameyasema haya leo Juni 23,2023 katika kikao cha Kuwasilisha ripoti ya Utafti wa madini hayo uliofanywa na Wataalam kutoka Wizara ya Madini.

"Tunawashukuru sana kwa utafiti wenu mliofanya na kutuhakikishia kuwa madini chumvi yanayopatikana ni mazuri na yanafaa kwa kiwango kikubwa kwa matumizi ya binadamu, sisi kama wawakilishi wa Serikali tutahakikisha tunakitumia vizuri chanzo hiki cha mapato kwa manufaa ya jamii lakini pia ili kukuza mapato ya halmashauri YETU”. alisema Kemirembe.

Akiwasilisha ripoti hiyo Mjiolojia Mwandamizi, Charles Moye  amethibitisha kuwa chumvi inayopatikana katika eneo hilo wilayani humo ni nzuri  kwa matumizi ya binadamu na kuwa ni tofauti kabisa kwaubora na ile inayopatikana  maeneo mengine.

"Manyoni mmebahatika kupata chumvi ambayo ni bora na ya viwango vya juu hivyo mnakila sababu ya kukilinda chanzo hiki kipya cha mapato katika wilayani yenu'" alisema Moye.

Mjiolojia Mwandamizi, Charles Moye  amethibitisha kuwa chumvi inayopatikana katika eneo hilo wilayani humo ni nzuri  kwa matumizi ya binadamu.

Kikao hicho kikiendelea. 

SERIKALI YATAKA WASHAURI WA WANAFUNZI KUWAJENGA WANAFUNZI KATIKA MAADILI MEMA NA UZALENDO

Mkuu waWilaya ya Ikungi,  Mhe. Thomas Apson (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chama cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa Wanafunzi Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TACOGA 1984), baada ya kufunga mafunzo yaliyohusu namna bora ya kukuza utendaji katika kuwapa ushauri wanafunzi yalioanza Juni, 21, 2023 na kufikia tamati Juni 23,2023 katika Ukumbi wa TIA Kampasi ya Singida.

.................................................. 

Na Dotto Mwaibale, Singida

SERIKALI imewataka washauri wa wanafunzi na viongozi wa serikali za wanafunzi kuendelea kuwajenga wanafunzi katika maadili mema na uzalendo, umoja wa kitaifa ili wawe wabunifu ndani ya mazingira ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amesema hayo Juni 23, 2023 wakati wa kufunga mafunzo ya washauri wa wanafunzi na viongozi wa serikali za wanafuzi yaliyoandaliwa na Chama cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa Wanafunzi Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (TACOGA 1984) ambayo ilisomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Thomas Apson.

“Ninyi  washauri    wa  wanafunzi  ndio mtakaoweza kuleta mabadiliko, nawaomba muendelee kuwajenga wanafunzi katika maadili mema na uzalendo, umoja na utaifa, nanyi  viongozi  wa wanafunzi  shirikianeni  vizuri  na  washauri  wenu  ili  msaidie  kuokoa maisha ya wenzenu,’’ alisema.

Apson aliwaomba washauri hao waendelee kuwashauri wanafunzi ili  kuunga  mkono  juhudi  za  Serikali  za  kuhakikisha wanasoma  katika  mazingira  mazuri  na  kupatiwa  misaada  stahiki kama  vile  mikopo  kutoka  Bodi  ya  Mikopo  HESLB  na  ZHELB.

Alisema jitihada ziongezwe katika kuwaelekeza  kushiriki  kikamilifu  katika  ukuzaji  na uendelezaji wa vipaji na taaluma kwa lengo la kuimarisha moyo wa uvumbuzi  miongoni  mwa  jamii  ya  vijana  wasomi  ili  waweze kujitegemea baadaye. 

“Waelekezeni  kukuza  uhusiano  na  ushirikiano  baina  ya  Vyuo  vya Elimu ya Juu, Vyuo vya Kati, Vyuo vya Ufundi pamoja na Taasisi za hiari  zinazojishughulisha  na  masuala  ya  elimu,  sayansi,  tamaduni na  maadili  ya  kitanzania,  ili  kuondokana  na  tabia  za  kuiga  na kujiingiza  kwenye  masuala ya ushoga,  madawa ya kulevya na bhangi,” alisema.

Aidha, aliwataka washauri  watumieni  na  kuwashirikisha  wanafunzi kufanya  tafiti  zinazohusu changamoto mbalimbali  zinazowakabili  ili  kupata  usahihi  wa  yale yanayowasumbua zaidi  na hatimaye kuyakabili kwa urahisi.

“Niwashauri muendelee  kutumia  mbinu  za  kisomi  na  kisayansi  ili  TACOGA1984  ije ijulikane kama ‘Association’ ya wataalamu na wabobevu wa masuala ya ushauri  nasaha  (ASSOCIATION  OF  PROFESSIONAL COUNSELLORS),” alisema.

Mwenyekitiwa TACOGA1984, Bi Sophia Nchimbi, alisema chama hicho kilianzishwa rasmi mwaka 1984 na kuwa vyuo vilivyoshiriki kwenye mafunzo hayo ni 39 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kati ya kazi ambazo wanazifanya ni kutoa ushauri na unasihi katika ofisi zao na nje wadau wao wakubwa wakiwa ni wanafunzi, wafanyakazi na wengine kutoka nje ya ofisi zao na pia wanatoa mafunzo ya namna hiyo kwa Serikali za wanafunzi wa vyuo binafsi na shule za sekondari na kuwafundisha shughuli za mapambano ya kutokomeza ukatili.

Alitaja kazi nyingine wanazozifanya ni kufanya utafiti na pindi wanapokutana katika mikutano yao ya kila mwaka huwa wanabadilishana uzoefu kwani mara nyingi wanapoifanya peke yao inakuwa ngumu.

Alisema mafunzo yaliyotolewa ni kudhibiti migogoro ya wanafunzi katika vyuo, uongozi wa wanafunzi na usimamizi wa mabadiliko, ukatili wa kijinsia, kupunguza ukeketaji wa kijinsia vyuoni na kwa wanafunzi kwa ujumla, matatizo ya afya ya akili, ustawi miongoni mwa wanafunzi, VVU na Ukimwi na masuala mtambuka, usimamizi wa fedha za wanafunzi, bajeti, utunzaji wa fedha na ukaguzi, huduma kwa wateja, umuhimu, majukumu changamoto, pamoja na kusimamia na kuboresha miongozo ya ushauri nasaha.

Alisema pamoja na kazi hizo nzuri wanazozifanya kunachangamoto kadhaa zikiwemo za ushiriki mdogo wa wadau wao na vyuo kutoka wizara ya elimu, vyuo vya kati na vyuo vya VETA ambapo wakizungumza nao moja kwa moja wanataka kwanza wazungumze na wizara husika kwa ajili ya kupata kibali.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, ambapo yamefanyika mafunzo hayo Dk. James Mrema alishukuru ushirikiano uliopo baina ya TACOGA na TIA na akaomba udumishwe kwani wote wanajenga nyumba moja hawapaswi kuwa na utengano.

Dk. Mrema alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya juu kwani imewafanya wanafunzi wengi kuendelea na masomo ukilinganisha na siku za nyuma.

Mshauri wa Wanafunzi wa Sheria kutoka Chuo cha Sheria Zanzibar, Bi. Sabra Balyan Suheil  akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo alisema yamewapa mwanga wa vitu vingi ambavyo walikuwa hawavijui hasa namna ya kumuhudumia mteja ambapo sasa wamepata mbinu hata za kwenda kuwahudumia waume zao na jamii kwa ujumla.

Mwenyekiti wa TACOGA 1984, Bi. Sophia Nchimbi ambaye pia ni Mshauri wa Wanafunzi (OUT), akitoa taarifa ya chama hicho wakati wa kufunga mafunzo hayo.

Makamu Mwenyekiti TACOGA 1984, Ndugu Augustine Matemu, akizungumza wakati wakufunga mafunzo hayo

Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Dk.James Mrema (katikati waliokaa), ambaye alimuwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi hiyo, Tanzania, Profesa William Pallangyo akizungumza wakati wakufunga mafunzo hayo.

   Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa katika ufungaji wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Thomas Apson, akimkabidhi cheti,  Naibu Mshauri wa Wanafunzi MUDCC na Katibu Mwenezi wa TACOGA 1984, Bi Zitta Victoria Mnyanyi,  

Mshauri wa Wanafunzi wa Sheria kutoka Chuo cha Sheria Zanzibar, Bi. Sabra Balyan Suheil  akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo wakibadilishana mawazo wakati wa ufungaji wa mafunzo.
Mafunzo yakifungwa.
Mafunzo yakifungwa.

Mafunzo hayo yakifungwa.

Furaha ikitamalaki wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.

Washiriki wakiwa kwenye hafla ya kufunga mafuzo hayo
Mafunzo hayo yakifungwa.
Mafunzo yakifungwa.
Mafunzo ya siku tatu yakifungwa.
Taswira ya ufungaji wa mafunzo hayo.
Mlezi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Mhandisi Saad Hassan  ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa TACOGA 1984 (kulia) akiwa na Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo cha KCMUCo na Mjumbe wa TACOGA 1984, Anza-Amen Lema wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.
Mwangalizi wa Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania(TIA) Kampasi ya Singida, Madamu Ambwene Kajula (kushoto) akikabidhiwa chti na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa katika ufungaji wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Thomas Apson.
Mhazini wa TACOGA, Bi. Ruth Kitundu, Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo cha MUHAS , akikabidhiwa cheti na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Thomas Apson.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.

Tuesday, June 20, 2023

TPHPA KUENDELEA KUBORESHA MIUNDOMBINU NA HUDUMA KWA WANANCHI

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof Joseph Ndunguru (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mamlaka hiyo Mkoa wa Shinyanga baada ya kuzungumza na Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo katika ziara yake ya kikazi aliyoianza leo mkoani humo. Wa kwanza kutoka kushoto ni  Msimamizi wa Kituo cha TPHPA Mkoa wa Shinyanga, Jesca Ndomba,  na wa tatu ni Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Prof. Siza Tumbo


Na Mwandishi, Wetu,Shinyanga

MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imesema itaendela kuboresha miundombinu yake na huduma kwa wananchi hili waweze kupata tija katika sekta ya kilimo kama ilivyo dira na dhima ya Wizara ya Kilimo.


 Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Prof Joseph Ndunguru wakati
 akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo Mkoa wa  Shinyanga na kuwataka kufanya kazi kwa weledi na kufuata maadili ya kazi zao. 

 Prof. Ndunguru amesema Serikali inamategemeo makubwa na mamlaka hiyo katika utatuzi wa changamoto zinazowasumbua wakulima hususan katika udibiti wa wadudu waharibifu wa mazao pamoja na visumbufu .

 Akitoa taarifa ya utendaji kazi msimamizi wa kituo cha TPHPA Mkoa wa Shinyanga, Jesca Ndomba amesema wameweza kudhibiti visumbufu katika wilaya za Shinyanga ,mkoa wa Tabora ,Simiyu na Kigoma.

Wafanyakazi wa TPHPA wakichukua wakiandika maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Prof. Ndunguru.
Wafanyakazi wa TPHPA wakiwa katika picha ya pamoja na Prof. Ndunguru (wa tatu kutoka kushoto)
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof Joseph Ndunguru (kulia) na Msimamizi wa Kituo cha TPHPA Mkoa wa Shinyanga, Jesca Ndomba wakipitia taarifa mbalimbali wakati wa mkutano huo na wafanyakazi.
 

BOHARI YA DAWA (MSD) YAANZA RASMI ZOEZI LA KUHESABU MALI

Wafanyakazi wa Bohari ya Dawa (MSD) wakiendelea na zoezi la kuhesabu malikatika maghara yao. 

Na Dotto Mwaibale,  

BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza rasmi zoezi la kuhesabu mali kwa mujibu wa sheria. Zoezi hilo la kuhesabu mali  linategemewa kukamilika  mwishoni  mwa mwezi Juni 2023 ili kuanza mwaka mpya wa fedha. 

Katika kipindi hiki maghala yote ya MSD Makao Makuu pamoja na Kanda zote  yatakuwa yamefungwa kupisha zoezi hilo. 

Awali kabla ya kuanza kwa zoezi hilo Bohari ya Dawa (MSD) iliwaarifu wateja wake wote wa Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati kuwa  kuanzia Juni 15, 2023 mpaka Juni 30, 2023 litafanyika zoezi la kuhesabu mali kwa mujibu wa sheria na kuwa kutokana na zoezi hilo la kuhesabu mali, maghala yote ya MSD yatafungwa kwa kipindi cha wiki mbili kuanzia Juni, 15, 2023.

Maombi yote ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara yawasilishwe MSD kabla ya Juni 7, 2023, ili kukidhi mahitaji wakati wote maghala hayo yatakapokuwa yamefungwa na kuwa  huduma ya dharura ya kupata mahitaji itatolewa, pale tu itakapothibitika uhitaji.

Zoezi la kuhesabu mali likiendelea.
Mali za MSD zikihesabiwa.
Umakini ukifanyika wakati wa kuhesabu mali hizo
 

Tuesday, June 13, 2023

MEJA JENERALI MBUGE “TUIMARISHE USHIRIKIANO KUKABILI MAJANGA”

Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja  Jenerali  Charles Mbuge  akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida. 

Na Mwandishi Wetu- Singida 

Serikali  kupitia  Ofisi  ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta mbalimbali katika kukabiliana na maafa ili kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama.

Kauli hiyo imetolewa   mkoani Singida na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja  Jenerali  Charles Mbuge  wakati akifungua kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja.

Meja Jenerali Mbuge amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la mwingiliano wa binadamu, wanyama na mazingira ambao  husababisha  kutokea kwa magonjwa mbalimbali yanayotoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu hivyo ipo haja ya   kuwepo kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana  na majanga hayo.

“Tunahuisha mwongozo huu kwa sababu ya mabadiliko ya sheria na kanuni za usimamizi wa Maafa.   Mwongozo huu ni muhimu katika kurahisisha ushirikiano wa kisekta ili kujenga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya milipuko ya magonjwa na dharura zingine zenye madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa husisitiza yakiwemo  Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO),  Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Wanyama (WOAH) na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa pamoja husisitiza ushirikiano wa sekta mbalimbali ili  kuwa na mikakati na sera za  pamoja katika kuimarisha afya ya wanadamu, wanyama na mazingira.

“Ili kutekeleza dhana ya Afya moja, ni muhimu kuwa na miongozo mbalimbali ili kurahishisha uratibu na utendaji katika ngazi zote. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru FAO ambao walianzisha mchakato wa kutengeneza mwongozo huu ambao katika kikao hiki utauhuishwa na kutafsiriwa,” ameeleza. 

Aidha amebainisha kuwa   Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa ina  wajibu wa kuratibu utekelezaji wa dhana ya  Afya Moja kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya 2004, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na Mkakati wa Afya Moja 2022-2027.

Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Valentina Sanga akiwasilisha Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja . 

Mtaalam wa Afya ya Jamii kutoka Shirika la Afya Duniani Bi. Pelagia Muchuruza akieleza jambo wakati wa kikao hicho. 

Afisa Kiungo wa Afya Moja kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Justine Assenga akifafanua jambo katika kikao hicho.

 Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja  Jenerali  Charles Mbuge  (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.

Baadhi ya Wataalam kutoka sekta mbalimbali wakifuatilia kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.


Saturday, June 10, 2023

TMDA KANDA YA KATI YATOA ELIMU YA UTOAJI TAARIFA YA MADHARA YA DAWA MKOANI SINGIDA

Zoezi la Uelimishaji na uhamasishaji wa utoaji wa taarifa za madhara ya dawa ukifanyika Hospitali ya Kiomboi wilayani Iramba mkoani Singida.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kati imefanya uelimishaji na uhamasishaji wa utoaji wa taarifa za madhara yanayohisiwa kusababishwa na dawa katika Halmashauri za Wilaya ya Iramba na Manyoni mkoani Singida.

Akizungumza wakati wa zoezi la uelimishaji lililofanyika kwa nyakati tofauti wiki hii, Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA, Seraphina Omolo alisema lengo kubwa ilikuwa ni kutoa uelimishaji na uhamasishaji wa utoaji wa taarifa za madhara yanayohisiwa kusababishwa na dawa,chanjo na vifaa tiba katika maeneo ya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali, vituo vya afya na zahanati.

‘”Zoezi hili liliwalenga watoa huduma za afya kuhusu utoaji wa  taarifa za madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba ili kuendelea kulinda afya ya jamii,” alisema Omolo.

Omolo alisema katika mafunzo hayo, watoa huduma hao walisisitizwa kutoa taarifa mara moja endapo watakutana na bidhaa duni za dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Aidha, Omolo alisema utoaji wa taarifa za madhara hayo pamoja na kutoa taarifa za bidhaa duni hurahisisha katika udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa na hivyo jamii kulindwa kutokana na athari ambazo zingeweza kutokea.

Omolo alitaja moja ya jukumu kubwa  la TMDA kuwa ni kulinda afya ya jamii kwa kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Kwa upande wake Mkaguzi wa Dawa,  Octavian Ngoda alisema kutoa taarifa za madhara ni jukumu ambalo lipo kisheria ambapo  watoa huduma  wanapaswa kuzitoa hata kama ni maudhi madogo madogo ya kupata homa au kusikia kichefu chefu na sio yale madhara makubwa ambayo yanaweza kusababisha  mgonjwa kulazwa, kupata ulemavu au kufariki

Zoezi hilo likifanyika Kituo cha Afya cha Ndago wilayani Iramba.
Uelimishaji huo ukifanyika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.
Ulimishaji huo ukiendelea,  Hospitali ya Kilimatinde wilayani Manyoni.
Uelimishaji ukiendelea.
 

Thursday, June 8, 2023

DIWANI ITIGI ADAIWA KUZUIA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akipokea taarifa ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Isanjandugu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya Juni 7, 2023. Katikati ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ilimbato Japhet,  aliotoa taarifa hiyo na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota. 

Na Dotto Mwaibale, Itigi

UONGOZI wa Wilaya ya Itigi mkoani Singida, umemlalamikia Diwani wa Kata ya Mitundu, Patrick Masanja  kwa madai ya kukwamisha utekelezwaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Kemirembe Lwota alisema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba katika mfululizo wa ziara yake ya kukagua na kuhamasisha ukamilishaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali wilayani humo Juni 7, 2023.

Kemirembe alisema kuwa diwani huyo Patrick Masanja amekuwa akiwazuia wananchi kutokushiriki shughuli za maendeleo mbalimbali zinapofanyika katika kata hiyo.

"Mheshimiwa mkuu wa mkoa katika kata hii kikwazo kikubwa ni diwani wa kata ya Mitundu kuwa na tabia ya kuwazuia wananchi wasishiriki kwa kutoa nguvu kazi wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendele," alisema Kemirembe.

Aliongeza kuwa suala hilo wameliongelea katika vikao mbalimbali lakini bado diwani huyo anaendelea kuwakwamisha.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, John Mgalula akiomuongelea diwani huyo mbele ya mkuu wa mkoa alisema hata walipokuwa wakitekeleza ujenzi wa kituo cha afya cha  kata hiyo pia alikuwa akiwazuia wananchi kufanya kazi.

Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Laila Sawe alisema kabla ya diwani huyo alikuwepo mtangulizi wake ambapo kazi za maendeleo zilikuwa zikifanyika bila ya vikwazo vya aina yoyote ambapo alimtaka Masanja abadilike.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Manyoni, Barnaba Mushi alisema chama hicho kinazifahamu vizuri changamoto na misuguano iliyopo baina ya diwani huyo dhidi ya viongozi wa wilaya hiyo na kuwa wanazifanyia kazi.

Diwani Patrick Masanja akijitetea mbele ya mkuu wa mkoa mara baada ya shutuma hizo kuelekezwa kwake alisema sio kweli kuwa yeye ana wazuia wananchi  kutokushiriki kwenye miradi ya maendeleo, bali shutuma hizo zinatokana na chuki binafsi na hata baadhi ya viongozi wa kata hiyo wanalielewa jambo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alimtaka diwani huyo abadilike kwani haiwezekani kila mtu amnyoshee kidole na kuwa jambo hilo halimjengi kisiasa.

Aidha Serukamba ameridhishwa na usimamizi mzuri na ukamilishwaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo na kuwapongeza viongozi wote kwa ukamilishaji wa miradi hiyo kwa kiwango cha juu.

Pia Serukamba amewapongeza wataalam na wananchi kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuchangia utalaam na nguvu kazi katika kutekeleza miradi hiyo ambayo imegharimu fedha nyingi.

"Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hii na jambo kubwa tunalopaswa kulifanya ni kuikamilisha kwa thamani halisi ya fedha alizozitoa na kwa wakati uliopangwa," alisema.

Miradi aliyoitembelea na kuikagua ni mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi, Isanjandugu,, Kituo cha Afya Kata ya Mitundu, ujenzi wa madarasa Shule ya Msingi Makale, ujenzi wa madarasa ya mikondo miwili Shule ya Msingi Mlowo ambao ujenzi wake utagharimu Sh. Milioni 493.4, ujenzi wa bweni la Wasichana katika Shule ya Sekondari ya Mgandu, ujenzi wa Zahanati ya Kijijij cha Lulanga na Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Itigi inayojengwa eneo la Kitalaka.

Mazungumzo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo yakifanyika.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati) akiwa kwenye ukaguzi wa ujenzi wa shule hiyo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, John Mgalula na kulia ni Mkuu wa Wilayaya Manyoni, Kemirembe Lwota.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akiagana na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Isanjandugu, Ilimbato Japhet.
Muonekano wa moja ya madarasa katika shule hiyo.
Muonekano wa baadhi ya majendo ya Kituo cha Afya cha Kata ya Mitundu.
Ukaguzi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya ukiendelea.
Muonekano wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi, Makale.
Mazungumzo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi ya Makale.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota, akizungumzia kuhusu Diwani wa Kata ya Mitundu, Patrick Masanja anayedaiwa kuzuia wananchi wasishiriki kutekeleza miradi ya maendeleo.
Muonekano wa bweni la wasichana ambalo limejengwa Shule ya Sekondari ya Mgandu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni , Kemirembe Lwota wakitoka kukagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Lulanga.
Muonekano wa ujenzi wa madarasa ya mikondo miwili yanayojengwa Shule ya Msingi, Mlowo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza na viongozi mbalimbali wakati wa ujenzi wa madarasa hayo.
Ukaguzi wa ujenzi wa madarasa hayo ukifanyika.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akiongoza ukaguzi wa ujenzi wa madarasa hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akielekeza jambo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Itigi.
Mhandisi wa Wilaya ya Itigi, Peter Shayo (kushoto) akielekeza jambo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa hospitali hiyo.

Diwani wa Kata ya Mitundu, Patrick Masanja ambaye anadaiwa kuzuia wananchi wasitekeleze miradi ya maendeleo.

Muonekano wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Itigi.
Ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali hiyo ukiendelea.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya hospitali hiyo.