Wednesday, February 28, 2024

KUNA UMUHIMU WA MIFUKO YA KUHIFADHIA DAMU KUDUMU KWA MUDA WA MIEZI 5 MPAKA 9

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai

........................

Na Mwandishi Wetu.

 BOHARI ya Dawa (Msd), imesema kuna haja ya kuwa na akiba ya mifuko ya kuhifadhia damu itakayodumu kwa kipindi cha kuanzia miezi mitano hadi tisa, kuepuka kuadimika kwa bidhaa hizo. 

Kauli hiyo ya MSD inakuja katika kipindi ambacho, akiba ya mifuko hiyo kwa sasa ni miezi mitatu, jambo linalopaswa kuongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ya damu linalosababishwa na ajali. 

Akizungumza jana Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai  wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wataalamu wa Maabara, alisema MSD inaona kuna haja ya kutafuta mbinu thabiti itakayowezesha kuwa na akiba kubwa ya mifuko na hivyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa damu salama kwa wananchi. 

Alisisitiza kuwa, damu ni suala linaloamua maisha ya watu na mahitaji yake ni muhimu hasa kwa wajawazito, hivyo kuna haja ya kuhakikisha inapatikana kwa uhakika. 

Katika kufanikisha hilo, alisema kuna haja ya kuwa na akiba ya mifuko ya kuhifadhia damu itakayodumu kwa miezi mitano hadi tisa, badala ya mitatu ya sasa. 

“Serikali imejitahidi katika kuhakikisha kunakuwa na mifuko ya kuhifadhia damu. Kwa sasa akiba inaweza kudumu kwa miezi mitatu, lakini kunahitajika collective approach (mbinu za pamoja) kukabiliana na hilo,” alisema. 

Alieleza  kwa kutumia mbinu hizo za pamoja taifa litakuwa na uwezo wa akiba ya mifuko kwa zaidi ya miezi mitano na kuwezesha uhakika wa upatikanaji wa damu kwa wananchi. 

“Kuna eneo bado tunaweza tukafanya vizuri zaidi ili taifa liwe na mifuko isiyopungua miezi mitano hadi tisa,” amesema. 

Alisema, akiba ya mifuko iliyopo sasa ni miezi mitatu na kwamba kuna haja ya kutafuta mbinu za kuongeza akiba hiyo. 

Tukai alisisitiza kuwa kikao hicho kinalenga tathmini ya utendaji katika maabara ili kuhakikisha kunakuwa na ubora wa huduma. 

“Tunachotaka ni kuwa na uratibu wa pamoja na uwazi nje ya kufanya hivyo kuna watu hawataelewa kama bidhaa fulani ipo eneo fulani,” alisema. 

Lakini hatua hiyo, alisema itawezesha kupunguza kuisha muda wa baadhi ya vifaa kabla ya kutumika, ilhali kuna taasisi zinazohitajika. 

“Tunataka kupunguza ile hali ya vitendanishi kuisha muda wake kabla ya kutumika ilhali kuna maeneo vilikuwa vinahitajika ila tu hawakuwa wanajua,” alisema. 

Naye Kaimu Mfamasia Mkuu wa serikali, Msafiri Chiwanga, alisema  serikali imeendelea kuwekeza katika mashine za kiuchunguzi ili kuhakikisha mgonjwa anapatiwa tiba sahihi kulingana na ugonjwa unaomsumbua kupitia kwa wataalamu wa maabara. 

Aliwataka wataalamu hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria kulingana na miongozo iliyowekwa ili huduma inayotolewa iweze kuwa na ubora unaokubalika katika sekta ya afya. 

Alisema, kufuatia kuwepo kwa changamoto za usugu wa vimelea vya magonjwa katika baadhi ya dawa, wataalamu wa maabara wanatajwa kuwa msaada katika kuhakikisha tiba inayotolewa kwa mgonjwa inaendana na ugonjwa husika na hii ni baada ya matokeo ya vipimo  kupitia mashine za kiuchunguzi.                  

·          

Sunday, February 11, 2024

KAMPUNI YA BIVAC YAHIMIZA WAKULIMA SINGIDA KUCHANGAMKIA KILIMO CHA MAHARAGE LISHE

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akionesha maharage Lishe yanayouzwa na kampuni hiyo.

..................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

KAMPUNI ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha imewaomba wakulima Mkoa wa Singida kuchangamkia fursa ya kuanzisha kilimo cha maharage lishe na kuwa itawasaidia kuwatafutia soko.

Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo , Beatrice Alban hivi karibuni mjini Singida wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kilimo cha maharage hayo ambayo ni muhimu kwa masuala ya lishe.

Alban alisema wamefika Mkoa wa Singida kupeleka   fursa yenye faida zaidi ya tatu ya kwanza ikiwa inahusu masuala ya lishe ambayo imekuwa ni changamoto kubwa kuanzia ngazi ya familia hadi jamii ambapo Seikali imeiona na ya pili ni uchumi hasa kwa mkulima ambaye kila siku amekuwa hapigi hatua na badala yake amekuwa akirudi nyuma.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa kuiona changamoto hiyo kampuni hiyo inatamani kuona mkulima akipiga hatua kubwa katika masuala ya kilimo na sio kurudi nyuma.

Alban alizungumzia fursa nyingine kuwa ni ile inayohusu afya ya watoto ambayo inakwenda na usemi usemao ‘afya ya mtoto ni furaha ya mzazi’ kwani mtoto akiwa na afya bora mzazi atafanya kazi vizuri na kutunza kila kitu anachokipata na kujumuika na jamii katika shughuli mbalimbali.

Alisema katika nchi yetu kumekuwa na changamoto ya lishe hasa kwenye mikoa mingi hasa ile inayofanya vizuri kwenye masuala ya kilimo,

Alisema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Siliani Arusha waligundua maharage yenye virutubisho vingi ambayo yanaweza kuufanya mwili kukua na kupokea matokeo kwa haraka na kuwa maharahe hayo yanaitwa maharage lishe.

Alisema maharage hayo ni ya kawaida na yanapikwa kama yanavyopikwa mengine lakini hayo yamerubishwa kwa kutumia teknolojia ya udongo na kuongezwa madini ya zinki na chuma ambayo ni muhimu na kuwa kama mwili wa binadamu utakosa madini hayo utakuwa ukinyemelewa na magonjwa mengi na mgonjwa akipelekwa hospitali kutokana na mwili wake kukosa madini hayo hata dawa atakayopewa haitaweza kufanya kazi.

“Mwili wetu unahitaji kuwa na madini ya zinki na chuma kwa wingi ili tuweze kuwa na afya bora,” alisema Alban.

Mkurugenzi huyo alitoa maelezo hayo ili kuonesha umuhimu wa maharage hayo ambapo alisema kampuni hiyo ipo tayari kutoa ushauri na maafisa ugani kwa ajili ya kilimo cha maharage hayo ikiwa ni pamoja na kuwatafutia soko.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akionesha maharage Lishe yanayouzwa na kampuni hiyo.

Muonekano wa maharage lishe yakiwa sokoni
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban (kushoto) akiwa katika moja ya maonesho ya vyakula.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bivac Company Ltd Lishe yenye makao makuu yake Arusha, Beatrice Alban akiwa Uwanja wa Ndege wa Songwe jijini Mbeya wakati wa safari za kuhamasisha kilimo cha maharage hayo.
 

Friday, February 9, 2024

MSD MBEYA YATAMBUA USHIRIKIANO WA WADAU

    Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa (katikati) akimkabidhi cheti Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Enock Mwambalaswa (kulia) kwa niaba ya  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera iliyotunukiwa halmashauri hiyo baada ya kuwa ya kwanza kufuatia vituo vyake vya afya kutokuwa na madeni inayodaiwa na MSD pamoja na  kutumia vyanzo vingine vya fedha mbali ya zile zinazo tolewa na Serikali kama ruzuku kwa ajili ya kununua bidhaa za afya. Hafla ya makabidhiano ya tuzo na vyeti hivyo ilifanyika Februari 9, 2024 sanjari na mkutano wa wadau na MSD. Kusshoto ni Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya Marco Masala.

........................................................         

Na Dotto Mwaibale, Mbeya

BOHARI ya Dawa (MSD)  imewatambua na kuwapongeza wadau wake wa Kanda ya Mbeya kwa ushirikiano na umahiri wao kwenye suala zima la kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye maeneo yao.

Akizungumza Februri 9, 2024 katika mkutano huo wa wadau na MSD, Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya, Marco Masala alisema mkutano kazi huo umelenga kuweka mkakati wa pamoja wa kudumu na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya katika mikoa hiyo unaboreshwa na unaimarika.

Akisistiza katika mkutano huo ulioambatana na tukio hilo la utoaji vyeti kwa wateja wote na utambuzi wa wadau waliofanya vizuri kwenye maeneo kadhaa kwa kuwapatia tuzo maalumu kutoka mikoa ya Mbeya, Rukwa, Songwe na Halmashauri ya makete iliyopo mkoani Njombe, Masala alisema lengo la mkutano huo ni kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza majukumu yao na kutatua changamoto zinapojitokeza kwa pamoja.

Akizungumzia tukio la kuwatambua na kuwapongeza wadau hao mahiri alisema hatua hiyo ilifikiwa kutokana  namna wanavyotoa ushirikiano dhabiti katika kufanikisha kazi mbalimbali na MSD.

"Wadau hawa tunaowatambua leo ni pamoja na vituo ambavyo havina madeni ndani ya MSD,  vinatumia vyanzo vyao vingine kununua bidhaa za afya kutoka MSD, lakini zaidi wanatimiza wajibu ipasanyo wa kuwezesha usambazaji wa vifaa tiba kwa wakati," alisema Masala.

Aidha Meneja huyo aliongeza kwamba kwa sasa MSD inaendelea kujipambanua kwa ufanisi wa utoaji wa huduma zake kwa kuzingatia mahitaji halisi kuzunguka kanda yote ya Mbeya hivyo kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu kupata vifaa tiba na dawa.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa aliwaomba wadau kutambua kuwa jukumu kubwa walilo nalo ni kuvisimamia vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yanayotokana na uchangiaji wa huduma za afya ili viweze kununua bidhaa za afya, sambamba na kusimamia mnyororo wa ugavi wa bidhaa hizo.

“Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongeza fedha inayotengwa kwa ajili ya bajeti ya kununulia bidhaa za afya ili kuboresha utoaji wa huduma za afya. Hivyo, kila mmoja ana jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya ili kuleta tija kwa wananchi,” alisema Malisa.

Aidha, Malisa aliwataka wadau hao kuhakikisha wananchi watapata huduma bora zaidi katika vituo vya kutolea huduma za Afya bila manung’uniko na kupitia mkutano huo aliwakumbusha wadau wa MSD kupitia Wizara ya Afya, kufanya maoteo ya bidhaa za afya kwa usahihi na kwa wakati.

Alisema kwa kufanya hivyo itaiwezesha MSD kuwa na takwimu sahihi katika kuagiza kutoka kwa wazalishaji na washitiri hivyo kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.

Malisa aliwakumbusha wadau hao kusimamia matumizi sahihi ya takwimu za mnyororo wa ugavi ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi juu ya bidhaa za afya katika maeneo yao.

Meneja Huduma kwa Wateja wa MSD, Dkt. Pamella Sawa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai alisema lengo lingine la kikao kazi hicho ni kupeana maelekezo au kutatua changamoto zilizopo baina ya wadau wao na MSD na kuelimishana namna bora ya kufanya kazi kwa kushirikiana na pale watakapo zibaini watafute njia bora ya kuboresha.

Alisema kikao hicho kinahusisha wadau wa mikoa ya Mbeya, Rukwa, Songwe na Halmashauri ya Makete wanaohudumiwa na MSD wakiwemo viongozi mbalimbali wa sekta ya afya na Serikali.

“Sasa hivi kuna mabadiliko na maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ndani ya MSD na ninyi wateja wetu ni mashahidi hasa katika majukumu yetu kwenye eneo la usambazi kutoka mara nne hadi mara sita ya mzunguko na upatikanaji wa bidhaa za afya unakuja kwa wakati,” alisema Dkt. Sawa.

Kwa upande wake Dkt. Enock Mwambalaswa ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma ambayo imepata cheti cha pongezi na tuzo tatu ambazo Halmashauri hiyo imepata ikiwa ni Halsmashauri pekee iliyopata tuzo zote tatu.

Alisema kuwa pia Halmashauri hiyo imeibuka kidedea kwa kupata tuzo kwa kutumia vyanzo vingine vya mapato tofauti na vyanzo vinavyotolewa na Serikali kama ruzuku kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba.

Dkt. Mwambalaswa alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali kwa kutoa kipaumbele kwenye mgawanyo wa mapato ambao unaelekeza halmashauri kutoa msukumo kwa kutenga kila asilimia 50 ya mapato yake na kuyapeleka kwenye huduma za afya.

Halmashauri tatu zilizoibuka kidedea kwa kutumia vyanzo vingine vya fedha mbali ya zile zinazo tolewa na Serikali kwa ajili ya kununua bidhaa za afya ni Mbeya mji,  halmashauri ya mji wa Tunduma  na Halmashauri Mbeya.

Halmashauri tatu za kwanza ambazo vituo vyake vya afya havina madeni au madeni yake kidogo ni Ileje, halmashauri ya mji Tunduma na Busokelo na zote hizi zimetunukiwa tuzo za umahiri.Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje , Joyce Wilson akipokea cheti.cha umahiri.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Beno Malisa akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.
Meneja Huduma kwa Wateja wa MSD, Dkt. Pamella Sawa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai 
Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya Marco Masala, akizungumza kwenye mkutano huo.
Meneja Uhusiano wa MSD, Etty Kusiluka akiongoza mkutano huo.
Picha ya pamoja
Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano huo ukiendelea.
Mgeni rasmi wa mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa (katikati) ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huoakiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa MSD.
Baadhi ya Wafanyakazi wa MSD, wakiwajibika kwenye mkutano huo. Kutoka kushoto ni  Afisa Huduma kwa wateja Mwandamizi wa MSD Kanda ya Dodoma, Juliana Mbogo, Afisa Manunuzi wa MSD kutoka makao makuu, Renatha Nicolaus, Afisa Huduma kwa wateja kutoka MSD Makao makuu Joaniruth Msanga na Fundi Sanifu Vifaa tiba MSD Mkoa wa Mbeya Mbeya, Sabrina Lucas. 
Wafanyakazi wa MSD wakiwa kwenye mkutano huo. Kutoka kushoto ni Caroline Cornelius Mfamasia kutoka Wilaya ya Kondoa, Afisa Huduma kwa Wateja Frank Apolinary na Afisa Mauzo Rhoda Joseph.
Mkutano ukiende;ea.
Wafanyakazi wa MSD wakiwa kwenye mkutano huo.
Taswira ya mkutano huo.

 Wadau wa sekta ya afya wakiwa kwenye mkutano huo

Thursday, February 8, 2024

KITUO CHA AFYA MSANGE CHAKUMBUKWA, MSD YAPELEKA VIFAA TIBA VYA SH.MIL- 150

Afisa Mauzo  wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi akizungumza kwa niaba Meneja wa MSD wa kanda hiyo,  Mwanashehe Jumaa wakati akikabidhi jenereta la dharura litakalotumika katika Kituo cha Afya Msange kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida Februari 7, 2024 

.................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekikumbuka Kituo cha Afya cha Msange kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa kutoa fedha jumla ya Sh.Milioni 150 kwa ajili ya kununua vifaa tiba.

Afisa Mauzo  wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi akizungumza kwa niaba Meneja wa MSD wa kanda hiyo,  Mwanashehe Jumaa wakati wa kukabidhi jenereta la dharura litakalotumika katika kituo hicho lenye thamani ya Sh.Milioni 65.7 alisema kati ya fedha hizo zilizotolewa tayari wamekwisha peleka vifaa vyenye thamani ya Sh.Milioni 98.3.

"Vifaa vingine vilivyobaki vitaendelea kupelekwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu MSD itahakikisha vinafika na vinatumika kutoa huduma za matibabu kwa wananchi," alisema Mosi.

Alisema katika zoezi la kupeleka vifaa tiba hivyo kwenye vituo vya afya Ofisi ya Rais TAMISEMI imetenga jumla ya Sh.Milioni 700 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa hivyo na kuwa Kituo cha Afya Msange kimenufaika na fedha hizo.

Alisema katika Halmashauri hiyo vituo sita vimetengewa fedha kwa ajili ya vifaa hivyo ambavyo vinaendelea kupokelewa.

Mosi alisema jukumu kubwa la MSD ni kununua, kutunza, kuzalisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara katika vituo vyote vya Serikali vilivyopo nchini na kueleza kuwa MSD wamedhamiria kuokoa maisha ya watu.

Diwani wa Kata ya Msange ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali watanzania hususani wananchi wa halmashauri hiyo na Kata ya Msange.

Alisema kituo hicho kimejengwa kwa fedha za Serikali jumla ya Sh.Milioni 500 na kuwa wametumia Sh.Milioni 200 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa tiba.

Digha aliishukuru Serikali na MSD kwa kuwapelekea jenereta hilo la dharura ambalo linakwenda kusaidia wakati umeme utakapokuwa unakatika.

Wakazi wa Kata hiyo Hamisi Ramadhani na Greta Nyonyi waliishukuru Serikali na MSD kwa kuwapelekea jenereta hilo ambalo litakuwa mkombozi kwao.

"Tulikuwa na changamoto kubwa baada ya umeme wa kawaida kukatika hasa kwa upande wa wajawazito ambao walikuwa wakitakiwa kufanyiwa upasuaji lakini kwa jenereta ili tuliloletewa na MSD tuna kila sababu ya kutoa shukurani zetu kwa viongozi wetu," alisema Nyonyi.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau alisema jenereta hilo litawafanya kuwa na umeme wa uhakika na kuweza kutoa huduma za matibabu kwa urahisi na haraka kwa masaa 24.Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau akizungumza wakati wa mapokezi hayo.

Diwani wa Kata ya Msange ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo.
Mkazi wa Kata hiyo Greta Nyonyi akiishukuru Serikali na MSD kwa niaba ya wanawake wa Kata hiyo kwa kuwapelekea jenereta katika kituo hicho cha afya.
Mapokezi ya jenereta hilo yakifanyika. Kutoka kushoto ni Afisa Mauzo  wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi, Mfamasia wa kituo hicho cha afya, Isengwa Mathias na Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Noel Mchau
Afisa Mauzo  wa MSD Kanda ya Dodoma, Omari Mosi, akimkabidhi jenereta hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Eliya Digha (kulia) Katikati ni Mwakilishi wa Mbunge wa Jimbo hilo, Amina Senge.
Wananchi wa Kata ya Msange na viongozi wao wakionesha furaha yao wakati wakipokea jenereta hilo.
Gari la MSD likishusha jenereta hilo.

ANGALIA VIDEO 
Attachments area Preview YouTube video KITUO CHA AFYA MSANGE CHAKUMBUKWA

Sunday, February 4, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA AFYA YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA MSD

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai, akitoa taarifa  ya hali ya utendaji na majukumu ya MSD kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI jijini Dodoma., 

..............................................

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imesema imeridhishwa na hali ya utendaji wa Bohari ya Dawa(MSD) na mipango ya utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo uzalishaji wa dawa ili kupunguza kununua dawa nje ya nchi.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya hali ya utendaji na majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD), ambapo ameichagiza MSD kuongeza ufanisi, ubunifu wa hali ya juu kwa kuhakikisha bidhaa za afya zinakuwa toshelevu na kusambazwa.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti ameshauri MSD kufuatilia na kukusanya madeni ili kuhakikisha inajiendesha vizuri bila kuathiri mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya na kuongeza kuwa wataendelea kuishauri serikali kuiwezesha MSD kupata mtaji ili iweze kujiendesha.

_“Bohari ya dawa sasa imeongezewa jukumu moja la kuzalisha bidhaa za afya na kuifanya sasa kutekeleza majukumu manne ambayo ni kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya katika vituo vya vyote vya umma vya kutolea huduma za afya nchini”_ ameeleza Mhe. Nyongo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai kwa uongozi imara katika taasisi hiyo na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za afya kuongezeka na kufikisha vituoni kwa wakati.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai ameeleza kuwa tayari wameanzisha kampuni Tanzu ambayo itaingia mikataba na makampuni binafsi ya ndani na nje kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za afya nchini, na wajumbe wanne wa Bodi wa kampuni hiyo tanzu wameshateuliwa.Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai kwa uongozi imara katika taasisi hiyo na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za afya kuongezeka na kufikisha vituoni kwa wakati.

Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel, akichangia jambo kwenye kikao hicho.Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo akizungumza kwenye kikao hicho.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwa kwenye kikao hicho.

Kikao kikiendelea

 Mkutano ukiendelea.