KANISA KATOLIKI JIMBO LA SINGIDA LAPATA PIGO VILIO MAJONZI VYATAWALA KANISANI
Na Dotto Mwaibale, Singida
JUMUIYA ya Waumini na Wafanyakazi wa Jimbo Katoliki Singida imepata pigo na kusababisha vilio na majonzi baada ya kumpoteza mmoja wa Wafanyakazi wake mahiri Ibrahimu Hussein ambaye amefariki dunia mwanzoni mwa wiki wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Misheni ya Makiungu mkoani Singida.
Akiongoza ibada ya Misa Takatifu ya kuaga mwili wa marehemu Askofu wa Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda alisema Jumuiya ya Wakatoliki Singida itamkumbuka na kuendelea kumuombea kwa namna alivyojitoa kutekeleza matendo mema katika kipindi cha uhai wake.
"Tuendelee kumuombea.Kifo cha kimwili sawa...lakini kifo cha kiroho ni kibaya zaidi sababu ni chukizo mbele ya Mungu. Kifo cha kijana huyu ni cha baraka, neema na ni mlango wa kuingia mbinguni.. kumuona Mungu," alisema Askofu Mapunda.
Baadhi ya walioguswa na msiba huo walisema Ibrahimu alikuwa ni kijana wa aina yake kwani hata alipokuwa akitumwa hakuonesha kukataa wakati wote alikuwa akitabasamu.
Mazishi ya marehemu Ibrahimu Hussein yalifanyika jana nyumbani kwao Mang'onyi wilayani Ikungi mkoani hapa.






Comments
Post a Comment