TRA YAFAFANUA MADAI YA MFANYABIASHARA EMMANUEL GADI
........................................
Na: Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) haina mfumo
wowote mwingine inaouendesha wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo wa Forodha
wa TANCIS ambao unatumika kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja
wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Stephen Kauzeni kwa waandishi wa habari
wakati akitoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii
kuhusu malalamiko ya Bw. Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech
Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini
nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha.
“Bw. Emmanuel Gadi alifikisha malalamiko yake kwa
njia ya barua tarehe 27 Februari, 2023 akidai kupewa uthibitisho na TRA wa
kuingiza mzigo wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kampuni ya Tosh
Logistics Ltd.
TRA ilifanya Uchunguzi wa kutosha na kuthibitisha
kwamba hapakuwa na mzigo wowote ulioingizwa nchini kwa jina la Wintech Tanzania
Ltd wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kadhia yenye namba TZDL –
22-1382193 ya tarehe 18 Agosti 2022 kama anavyodai,” amesema Bw. Kauzeni.
Ameongeza kuwa, TRA ilimjibu mhusika kupitia
barua yenye kumbukumbu namba CF 8/92/01 ya tarehe 25 Julai 2023 ikimjulisha
kuwa, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa House Bill of Lading na
kutoonekana kwa mzigo huo kwenye kadhia iliyowasilishwa na kampuni ya Tosh
Logistics Ltd, TRA isingeweza kuthibitisha kuingizwa kwa mzigo huo nchini.
“Kupitia taarifa ya Bw. Emmanuel Gadi aliyoitoa
kwenye vyombo vya habari, tumebaini kuwepo kwa viashiria vya ukwepaji kodi
kwani ni dhahiri kuwa mzigo wake uliingizwa kwa njia za magendo,” ameeleza
Meneja Kauzeni.
Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amemtaka
mlalamikaji kuwasilisha nyaraka na uthibitisho wa Kampuni yake kuingiza mzigo
huo nchini mara moja ili hatua stahiki zichukuliwe.
.jpg)
Comments
Post a Comment