REA YAWASHA MRADI WA BILIONI 25 KUPOZA, KUSAMBAZA UMEME IFAKARA MOROGORO
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya, akizungumza baada ya kuwasha Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara (Ifakara Substation), Desemba 3, 2023 Ifakara, Morogoro. Kituo kimejengwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya Shilingi bilioni 25.Na Mwandishi Wetu, Ifakara-Morogoro
SERIKALI
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imewasha Kituo cha Kupoza na
Kusambaza Umeme cha Ifakara ambacho
kimegharimu shilling bilioni 25.
Akiwasha kituo hicho ambacho kimelenga kuongeza
uwekezaji na uanzishaji wa viwanda kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika, Mkuu wa
Wilaya ya Kilombero , Mh Dunstan Kyobya ameshauri kituo hicho kiitwe Samia
Ifakara Substation.
Ameipongeza REA na EU kwa kuhakikisha kituo
kimekamilika na kuwashwa kwani kinaenda kumaliza matatizo ya umeme katika
wilaya ya Kilombero, Malinyi na Ulanga ambayo ni maeneo ya kimkakati ya kilimo
na viwanda.
“Tunategemea kuongeza uwekezaji kwa kuanzisha
viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na vile vya kuchakata madini”
amesema Mh Kyobya.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza
mazingira na vyanzo vya maji ili kujihakikishia umeme wa uhakika katika mabwawa
ya kuzalisha umeme ya Kihansi na Kidatu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA,
Mhandisi Jones Olotu amesema kuwashwa kwa kituo hicho kunaongeza upatikanaji wa
umeme na hivyo kuwawezesha wananchi
kukuza na kuboresha hali zao za kiuchumi kwa kufungua biashara
mbalimbali kwa uwepo wa umeme wa uhakika katika maeneo hayo.
“Wananchi watumie upatikanaji wa umeme wa uhakika
kwa kujiongezea kipato kwa kuwekeza na kuanzisha viwanda vya mazao ya kilimo na
madini ambayo yanapatikana kwa wingi Kilombero, Ifakara, Ulanga na Malinyi,”
amesema Mhandisi Olotu.
Naye Mbunge wa Kilombero, Aboubakar Asenga
amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa umeme
mkubwa kwa kuzalisha kwa wingi na kuanzisha viwanda vikubwa.
“Tunaishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yake,
ni wajibu wetu wananchi kutumia fursa hii ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa
kuwa na viwanda vya kukausha na kukoboa mpunga, uzalishaji wa matofali kwa
kisasa na uongezaji thamani wa madini ili kujiongezea kipato, ” amesema Mh
Asenga.
Meneja wa Mradi huo kutoka REA, Mhandisi Romanus
Lwena amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza 2020 ambapo kinazalisha kV 220 za
umeme baada ya wananchi wa maeneo hayo kuwa wanapata umeme mdogo wa kV 33
uliokuwa unasababisha kukatika mara kwa mara.
Na baada ya kuwashwa kwa kituo hicho, kutawezesha
kuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za kilimo.
Meneja Miradi ya Nishati wa EU, Mhandisi Francis
Songela amesema katika Mradi huo wamechangia shilingi bilioni 18 na Serikali ya
Tanzania imetoa shilingi bilioni 7.
Amesema kituo hicho kipo katika eneo la kimkakati la
Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania , SAGCOT ambapo
Mradi huo unaenda kuleta mapinduzi ya kilimo na viwanda.
“Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ni maeneo ya kimkakati ya SAGCOT kwani yana rutuba kwa kilimo na shughuli nyingi za kiuchumi ambapo umeme wa uhakika ilikuwa changamoto na kwa kuwashwa kwa kituo hiki tunategemea mapinduzi ya kilimo na viwanda, ” amesema Mhandisi Songela.





Comments
Post a Comment