Thursday, December 24, 2020

KANISA LA ABC LAWAKUMBUKA WAJANE, WAGANE KRISMAS

Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila (katikati) akikabidhi juzi msaada wa chakula na vitu vingine kwa Wagane na Wajane.
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila akikabidhi juzi msaada wa vifaa vya shule kwa watoto wenye uhitaji.Kulia ni mke wake Janeth Ndabila.
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila akikabidhi juzi msaada wa vifaa vya shule kwa watoto wenye uhitaji.Kulia ni Mke wake Janeth Ndabila.
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila akikabidhi juzi msaada wa chakula kwa Nasaba  Seifu.
Mgane Hussein Libe akishukuru baada ya kupokea msaada huo.
umbe wa Serikali ya mtaa wa Mandela, Leonard  Chalema na Tabrisa Bushiri 
Wajane wakiondoka katika kanisa hilo baada ya kupokea msaada huo.
Mjumbe wa Serikali ya mtaa wa Mandela, Leonard  Chalema akizungumza baada ya kupokea msaada huo.
Wajane wakiwa katika kanisa hilo wakati wakisubiri kupokea msaada wa chakula.
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila, akizungumza na Wajane kabla ya kuwakabidhi msaada huo.
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mtaa wa Tabata Mandela na watoto wenye uhitaji baada ya kuwakabidhi juzi msaada wa vifaa vya shule
 

Na Dotto Mwaibale.


KANISA la Abundant Blessing Centre (ABC) la Mtaa wa Mandela jijini Dar es Salaam limetoa msaada wa chakula na vitu vingine kwa ajili ya kuwasaidia Wagane na Wajane 50 wanaoishi kwenye mtaa huo.

Mbali na kutoa msaada pia kanisa hilo limetoa msaada wa vifaa vya shuleni kama madaftari na kalamu kwa watoto 20 wenye uhitaji ikiwa ni maandalizi ya masomo watakayoanza Januari 2021.

Akizungumza juzi wakati wa kukabidhi msaada huo Askofu Kiongozi wa kanisa hilo Flaston  Ndabila alisema wamekuwa wakiguswa na changamoto mbalimbali za Wajane na wagane pamoja na wanafunzi wanaoishi mtaa huo na ndio maana  kama kanisa wameweka utaratibu kila mwaka kutoa msaada huo.

"Huu ni mwaka wetu wa tano tumekuwa tukifanya hivi  hasa kipindi hiki cha Sikukuu za mwishoni mwa mwaka za Krismas na mwaka mpya kuelekea mwezi wa kwanza ambapo watoto hawa wenye uhitaji wanakuwa wanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya shule" alisema Ndabila. 

Aidha Ndabila alisema wanatoa msaada huo kwa wanafunzi hao ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli ambayo inatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. 

Wajumbe wa Serikali ya mtaa wa Mandela, Leonard  Chalema na Tabrisa Bushiri kwa niaba ya Mwenyekiti wa mtaa huo, Yusufu  Nyumbi wakipokea msaada huo wamelishukuru kanisa hilo kwa utaratibu wao wa kila mwaka wa kuwajali wenye uhitaji.

Mgane Hussein Libe ambaye huu ni  mwaka wake  wa tatu kupata msaada huo alisema kanisa hilo ni mfano wa kuigwa na akashauri makanisa mengine kuiga mfano huo wa kusaidia jamii badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya hivyo. 

Hosiana Mkono ambaye ni mjane amelishukuru kanisa hilo kwa kutoa msaada huo na kugusa maisha ya wenye uhitaji.

Monday, December 21, 2020

NDAHANI AWATAKA WAZAZI KUWAPA WATOTO WAO MLO KAMILI

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, akikabidhi vyeti  katika Mahafali ya Elimu ya Awali ambapo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi jana.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, akikabidhi vyeti.
Mtoto akionesha cheti baada ya kukabidhiwa.
Mkuu wa Shule hiyo Sister Malietha, akisoma risara katika mahafali hayo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, akihutubia katika mahafali hayo.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida


KAIMU Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amewataka wazazi na walezi kujenga tabia ya kuwapa watoto wao mlo kamili  badala ya chipsi.

Ndahani alitoa ombi hilo jana katika mahafali ya Elimu ya Awali ambapo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi.

"Nawaombeni wazazi na walezi waleeni watoto katika maadili mema, mkizingatia mlo kamili  kuliko kuwapa chipsi" alisema Ndahani.

Aidha Ndahani aliwaambia wazazi hao wajenge tabia ya kuwashirikisha watoto hao katika michezo mbalimbali kwani inawajenga kiakili na kiafya.

Akizungumza suala la matumizi ya TV kwa watoto aliwaambia wazazi hao wawe wakiwatafutia vipindi vya kuwajenga watoto badala ya kuangalia  katuni zinazofundisha tabia mbaya ikiwemo wizi,ukorofi,ugaidi, uchoyo na hata ngono.

" Kuweni makini na hizi katuni ambazo hazina maadili kwa watoto ni bora watoto waangalie katuni zetu za kitanzania zilizodhibitishwa na  Taasisi ya Elimu Tanzania na si hizo za nje ambazo hazina maadili ya kwetu" alisema Ndahani.

Ndahani aliwaomba wazazi hao kuwajenga watoto wao katika uzalendo na kupenda Taifa na wazazi wao.

 Akizungumzia tabia za  watoto waliokosa maadili alisema katika baadhi ya familia  wamekuwa wakiwaendesha wazazi wao kwa kupanga kila kitu na kipi akifanye na kipi asikifanye huku wazazi wakiwaangalia tu.

Mkuu wa Shule hiyo Sister Malietha aliwaomba wazazi hasa wakina baba kujenga tabia ya kukagua kazi za shuleni za watoto wao badala ya kuwaachia wakina mama pekee kwani malezi ya mtoto lazima yawashirikishe wazazi wote.

GEKUL AONYA WANAOJIHUSISHA UVUVI HARAMU, UKWEPAJI KODI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti alipomtembelea ofisini kwake jana.Waziri Gekul yupo mkoani Manyara kwa ziara ya Kikazi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Ukuzaji Viumbe Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Imani Kapinga alipokuwa akimpa maelekezo Mwakilishi wa Kampuni ya XIN SI LU,  Suvi Zeng (katikati) alipotembelea eneo la ufugaji wa Samaki katika Mabwawa la Kampuni hiyo jana.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kulia) akipokea samaki aina Sato kutoka kwa Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi alipotembelea  eneo la  Kampuni ya XIN SI LU kutoka China iliyowekeza katika ufugaji wa Samaki kwenye Mabwawa Mkoani Manyara jana.

 

Na Mbaraka Kambona, Manyara

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewataka wale wote wanaojihusisha na uvuvi usiozingatia sheria na taratibu kuacha mara moja kwani Serikali haitakuwa na huruma kwa watakaokamatwa. 

Gekul alitoa onyo hilo alipokuwa akiongea na Wavuvi wa Mkoa wa Manyara alipofanya ziara mkoani humo jana. 

Kwa mujibu wa Waziri Gekul katika operesheni ya kupambana na uvuvi haramu iliyopita ilitumika karibu bilioni 1. 2 jambo ambalo alisema halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa serikali ili kukomesha vitendo hivyo. 

“Hatutavumilia jambo hili liendelee, Sisi kama Wizara tumesema ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi haramu lakini na nyinyi wavuvi muwe tayari kutoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu ukomeshwe mara moja,” alisema Gekul.

Aliongeza kwa kusema kuwa uvuvi haramu ukikomeshwa itasaidia kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi ya samaki katika maziwa na maeneo mengine. 

“Kwa kuwa mmeonesha nia ya kutoa ushirikiano katika hili, shirikianeni na viongozi wenu kuanzia leo hizo nyavu haramu zikatupwe, tusisikie tena kuhusu nyavu haramu iwe mwanzo na mwisho ,” aliongeza Gekul. 

Aidha, Waziri Gekul alisema kuwa kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia Vizimba na Mabwawa jambo ambalo anasema likisimamiwa vizuri litaongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umasikini na kuchochea uchumi wa taifa letu. 

“Niwaombe Wakurugenzi na Viongozi wengine wa Halmashauri waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa na Serikali kwa Vijana, Wanawake na Walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye utafiti ili kujua ujenzi wa mabwawa unagharimu kiasi gani ili wawajengee mabwawa ya kufugia samaki na tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira,” alisisitiza Gekul. 

Katika hatua nyingine, Gekul aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa uvuvi kuwafikia wavuvi wote na kuhakikisha wanalipia leseni za uvuvi ili kuzuia upotevu wa mapato na kukuza pato la Serikali. 

“Hili litekelezwe haraka, kila mtu ajisikie vizuri kulipa kodi ya serikali, lipeni kodi na mpatiwe risiti za mashine za elekroniki kwa kufanya hivyo kutazuia upotevu wa mapato ya serikali,” alifafanua. 

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange alisema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wameyapokea na watayafanyia kazi kama ilivyoelekezwa ili sekta ya uvuvi mkoani humo iweze kupiga hatua inayotarajiwa. 

“Tutahakikisha wavuvi wote tunawafikia kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili lakini vile vile wale ambao hawana leseni waweze kukata leseni ili serikali iweze kuwatambua na kupata mapato kupitia shughuli za uvuvi,” alisema Twange. 

Mwenyekiti wa Wavuvi, Halmashauri ya Babati, Iddi Hassani alisema kuwa watafanyia kazi maelekezo na watahakikisha wanashirikiana na serikali ili wavuvi wote wawe na leseni za uvuvi na wataendelea kupambana na uvuvi haramu ili kunusuru viumbe maji na kuendelea kufanya uvuvi endelevu.

TAKUKURU SINGIDA YAZIDI KUWABANA WAKOPESHAJI HARAMU, NDANI YA MIEZI MITATU YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 80

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, akimbidhi Sh.milioni 8,600,000, Esther Pununta (wa pili kushoto) mbele ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida, mkoani hapa juzi, akiwa ni mmoja wa waathirika waliopitiwa na wimbi  la  ‘Mikopo Umiza,’ ambazo ziliokolewa na Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Singida. Kushoto ni mtoto wake Naomy Geuza. Wa tatu kutoka kulia ni Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, Wengine ni Mstahiki Meya Yagi Kiaratu na Naibu Meya, Hassan Mkata.

Muathirika wa Mikopo Umiza  Mwalimu Mstaafu Seleman Haji, akimkabidhi shilingi milioni 46 mke wake Magdalena Gunda baada ya kukabidhiwa na  Mkuu wa Mkoa wa Singida  Dk .Rehema Nchimbi,

 Mkuu wa Mkoa wa Singida  Dk. Rehema Nchimbi, akizungumza na Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida (hawapo pichani) baada ya kukabidhi fedha hizo.

Muathirika wa Mikopo Umiza  Loth Mwangu,  akiwa na fedha zake baada ya kukabidhiwa.

Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida wakishuhudia waathirika wa Mikopo Umiza walivyo kuwa wakirudishiwa fedha zao.


Baadhi ya waathirika wa mikopo hiyo wakiwa na maafisa wa Takukuru wakati wa kurudishiwa fedha zao.
Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida wakishuhudia waathirika wa Mikopo Umiza walivyo kuwa wakirudishiwa fedha zao.
Wajumbe  wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida wakishuhudia waathirika wa Mikopo Umiza walivyo kuwa wakirudishiwa fedha zao.


Na Godwin Myovela, Singida


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),  kwa kasi na mwendelezo ule ule imeendelea kuwafuta machozi wananchi wanyonge mkoani hapa, kwa kuokoa na hatimaye kuwakabidhi fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 80 walizokuwa wametapeliwa kupitia Kampuni za Mikopo zinazoendesha shughuli zake kinyume na utaratibu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, amewakabidhi kiasi hicho cha fedha waathirika wote waliopitiwa na wimbi hilo, maarufu ‘Mikopo Umiza,’ mbele ya Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida, mkoani hapa juzi.

“Ni Serikali hii ya Magufuli ndio iliyofanikisha kuwabana hawa wakopeshaji haramu na hatimaye leo mnakabidhiwa haki yenu iliyokuwa imeporwa, tuendelee kumshukuru Rais kwa mema haya anayoendelea kutufanyia,” alisema Nchimbi.

Zoezi la urejeshaji wa fedha hizo kwa waathirika limefanyika mbele ya madiwani hao ili kuhamasisha umuhimu wa ushirikiano na utendaji wa pamoja baina yake na Taasisi hiyo katika kupiga vita vitendo vyote vya rushwa, ikizingatiwa madiwani ni miongoni mwa viongozi wanaowajibika kwa karibu zaidi na wananchi.

 Akiwasilisha taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza katika kipindi cha Oktoba na Disemba mwaka huu, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema takribani shilingi milioni 88.8 zimeokolewa na kurejeshwa kwa wahusika. 

Mathalani, mbele ya Mkuu wa Mkoa na Madiwani wa Baraza la Manispaa, Elinipenda alieleza kwamba miongoni mwa matukio yaliyodhibitiwa na Taasisi hiyo katika kipindi cha miezi 3 iliyopita ni pamoja na tukio la kusisimua la mkopeshaji mmoja asiye na vibali vya kufanya biashara hiyo ya ukopeshaji alimkopesha Mwalimu Mstaafu Seleman Haji shilingi milioni 6.5 na baada ya mwalimu huyo kupokea pensheni yake mkopeshaji alimtaka amlipe shilingi milioni 46.

“Takukuru iliingilia kati makubaliano hayo ya kikandamizaji kwa kumtaka mkopeshaji huyo arejeshe shilingi milioni 39.5 na amefanya hivyo. Tunaomba Mkuu wa Mkoa umkabidhi leo hii mstaafu huyu fedha yake iliyookolewa,” alisema Elinipenda.

Hata hivyo matokeo ya ufuatiliaji na udhibiti huo umebaini kuwa baadhi ya wakopeshaji binafsi wanafanya shughuli hiyo bila ya vibali halali, hali inayosababisha kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato na kujipatia fedha isivyo halali.

Aidha, udhibiti umebaini kuwepo kwa utozaji mkubwa wa riba zisizovumilika za zaidi ya asilimia 100 kinyume na viwango vilivyowekwa na kuainishwa na Benki Kuu. 

Aidha, kupitia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Takukuru, imeelezwa baadhi ya wakopeshaji hawaandai mikataba ya ukopeshaji, hivyo wakopeshwaji hawana nakala za mikataba, na hata iliyopo kwa baadhi ya kampuni hizo haikidhi sifa na vigezo.

Imeelezwa, baadhi ya kampuni hizi za mikopo hazina hata wataalamu wa mahesabu hali inayowafanya kutoza riba zenye mkanganyiko, na hivyo kujikuta wakimbambikiza riba kubwa mkopeshwaji.

Pamoja na mambo mengine imebainika kuwa kuna uvujishaji mkubwa wa taarifa za watumishi wanaostaafu. Mathalani taratibu za malipo ya mafao ya mstaafu yanapokuwa yamekamilika wakopeshaji wanakuwa wa kwanza kupata taarifa kabla ya mhusika mwenyewe. 

KATIBU WA TAMUFO STELLA JOEL ATOA WIMBO KUHAMASISHA MAENDELEO


Mwimbaji wa Muziki wa Injili Nchini Tanzania na Katibu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Stella Joel akiwa katika muonekano wa picha tofauti baada ya kuachia wimbo wa kuhamasisha maendeleo unaoitwa Tanzania ya Maendeleo.


 Stella Joel akiwa katika pozi.

 Stella Joel akitafakari ukuu wa Mungu baada ya kutoa wimbo huo ambao unabamba hivi sasa hapa nchini.


Na Dotto Mwaibale


BAADA ya kimya cha muda mrefu, Mwimbaji wa Muziki wa Injili Nchini Tanzania, Stella Joel ameachia wimbo wa kuhamasisha maendeleo unaoitwa Tanzania ya Maendeleo.

Mara ya mwisho Stella aliachia wimbo wa Hakuna Mwanamke mbaya alioshirikiana na malkia wa muziki wa Injili, Rose Muhando.

Stella ambaye ni Katibu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) alisema, imefika hatua kwa wasanii kuhamasisha nyimbo zinazochochea maendeleo na kuisaidia jamii kutatua changamoto zake.

“Baada ya Tanzania kufikia uchumi wa kati nikaona ni vyema niweke hilo kwenye muziki, nyimbo za aina hii zinachangia sana kupiga hatua za kimaendeleo zaidi,” alisema Stella.

Stella aliwashauri wanamuziki nchini kubadilisha mtizamo wao, kutojikita kwenye  jumbe za mapenzi peke yake badala yake waangalie changamoto nyingi za kijamii kama masuala ya lishe, ukatili wa kijinsia na mengine.

Sunday, December 20, 2020

BAKWATA SINGIDA YAPONGEZA UJENZI WA SHULE

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Buruan Mlau akihutubia  kwenye Mahafali ya Shule ya Awali ya Al Wafaa inayo milikiwa na Taasisi ya Dhi Nureyn iliyopo eneo la Mandewa yaliyofanyika jana mkoani hapa.

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Buruan Mlau akikabidhi vyeti kwenye Mahafali ya Shule ya Awali ya Al Wafaa inayo milikiwa na Taasisi ya Dhi Nureyn iliyopo eneo la Mandewa yaliyofanyika jana mkoani hapa. Kutoka kulia ni Sheikh wa Wilaya ya Singida, Issa  Simba, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mikidadi Abrahman na kushoto ni mmiliki wa shule hiyo, Hamisi Ntandu,

Wanafunzi wakiwa kwenye mahafali hayo.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Buruan Mlau akikabidhi vitabu kwenye Mahafali hayo.

Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Buruan Mlau akikabidhi vitabu kwenye Mahafali hayo.


Wanafunzi wakiwa na vitabu walivyo kabidhiwa baada ya kufanya vizuri kwenye masomo ya dini.


Wanafunzi wakiwa na vitabu walivyo kabidhiwa baada ya kufanya vizuri kwenye masomo ya dini.

Mmiliki wa shule hiyo, Hamisi Ntandu, akiwa kwenye Mahafali hayo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Msingi na Awali  Mikidadi Abrahman, akisoma risala kwenye mahafali hayo.



Na Dotto Mwaibale, Singida.


KATIBU wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Buruan Mlau anewapongeza Waislamu mkoani hapa kwa kuwa na muamko wa kujenga shule kwa ajili ya watoto wao.

Mlau ambaye alikuwa mgeni rasmi alitoa pongezi hizo kwenye mahafali ya Shule ya Awali ya Al Wafaa inayo milikiwa na Taasisi ya Dhi Nureyn iliyopo eneo la Mandewa yaliyofanyika jana mkoani hapa.

"Katika Mkoa wa Singida hivi sasa tuna shule za kiislamu sita tunakila sababu ya kumshukuru mwenyezi Mungu kwani hapo zamani hatukuwa na shule hata moja tulikuwa nazo katika mikoa ya Mwanza, Arusha , Dar es Salaam na mikoa mingine." alisema Mlau.

Mlau aliwapongeza sana waislamu hao  kwa ushirikiano mzuri wanaoufanya wa kujenga shule ili watoto wao waweze kupata elimu zote mbili kwa maana ya dini na elimu ya dunia.

Aidha Mlau aliwataka waislamu hao kuendelea kushirikiana na kuziboresha shule hizo kwa ajili ya manufaa ya watoto wao.

Akizungumza katika mahafali hayo Sheikh wa Wilaya ya Singida, Issa  Simba alisema hata Mtume Muhammad aliwahi kuzungumza kuwa mwanadamu yeyote akitaka kuishi maisha mazuri duniani na peponi ni lazima awe na elimu na si vinginevyo.

Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ya Msingi na Awali  Mikidadi Abrahman alisema ilisajiliwa mwaka Januari 21, 2018 kwa namba ya usajili EL17536 kuwa shule ya mchanganyiko ya wavulana na wasichana na kuwa Januari 6, 2018 walipatiwa kibali kwa ajili ya shule ya bweni na kuwa sasa wanatoa elimu kuanzia ya awali hadi darasa la saba.

Alisema kwa sasa wana jumla ya wanafunzi 335 wakiwemo wavulana 173 na wasichana 162 na walimu 20, walimu 13 wakiume na saba wa kike.

Abrahman alisema kati ya walimu hao sita wanafundisha masomo ya dini na 14 masomo ya kawaida kwa maana elimu ya mazingira.

Alisema baadhi ya malengo ya kuanzisha shule hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya elimu kwa kutoa elimu bora yenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla. 
 

Friday, December 18, 2020

WADAU WAKUTANA KUTATHIMINI UTEKELEZAJI WA MRADI WA SWIOFish

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah  akitoa maelezo ya tathmini ya maendeleo ya Mradi wa SWIOFish kwa Uongozi wa Benki ya Dunia kupitia njia ya mtandao katika kikao cha kufanya tathmini kilichofanyika jana mjini Dodoma.
Afisa Uvuvi Mwandamizi, Upendo Hamidu akifafanua jambo katika kikao hicho.
Sehemu ya Wajumbe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Taasisi zinazotekeleza Mradi wa SWIOFish Tanzania Bara na Visiwani pamoja na Mamlaka ya Bahari Kuu wakiwa katika majadiliano na viongozi wa Benki ya Dunia kwa njia ya mtandao kuhusu kufanya tathmini ya mradi huo, Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma.


TAASISI zinazohusika na utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) wamekutana kujadili na kufanya tathimini ya utekelezaji wa mradi huo wa miaka sita (6) ili kupima mafanikio na mapungufu yaliyojitokeza kabla ya kufanya maamuzi ya kuendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wake.

Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa Mradi huo kwa wadau waliohudhuria kikao hicho kwa njia ya mawasiliano ya kimtandao (Web conference) kutokea jijini Dodoma Disemba 16, 2020, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema kuwa kikao hicho cha tathimini ni moja ya taratatibu walizoziweka kuwa kila baada ya miezi sita timu ya wataalamu kutoka taasisi za utekelezaji pamoja na wafadhili wa mradi huo Benki ya Dunia wanakaa pamoja kutathimini maendeleo ya mradi huo ili kusaidia kusukuma utekelezaji pale ambapo pataonekana kuna mkwamo.

“Kwa ujumla niseme tangu mradi huu uanze hatujawahi kupata taarifa isiyoridhisha kutoka kwa wafadhili wa mradi, wamefurahishwa na utekelezaji unavyoendelea  kwenye maeneo yote ikiwemo matumizi ya pesa, na ujenzi wa majengo mbalimbali na inatupa faraja kuona kwamba tunatekeleza mradi huu kama tulivyokubaliana,” alisema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah alisema kuwa wameshawasilisha ombi kwa Wizara ya Fedha kuongeza muda wa utekelezaji wa Mradi huo kwa mwaka mmoja zaidi badala ya kuisha mwaka 2021 uendelee mpaka 2022 ili kufidia mapungufu yaliyojitokeza kufuatia  athari za  mlipuko wa ugonjwa wa Korona ulioikumba Dunia mwanzoni mwa mwaka huu huku akisema Benki ya Dunia imeridhia ongezeko hilo la muda ili mradi huo uweze kutimiza adhma yake.

Aliendelea kusema kuwa kufuatia vikwazo vya kusafiri vilivyoweka katika baadhi ya maeneo ya nchi duniani kutokana na maradhi ya Korona wameamua kufanya vikao kupitia mawasiliano ya kimtandao na vikao hivyo vilianza tangu Disemba 14, 2020 ambapo wadau wamekuwa wakikutana kujadili maendeleo ya mradi huo na Disemba 18, 2020 ndio ilikuwa hitimisho kwa wadau wote kupitia taarifa ya utekelezaji na kukubaliana mambo ya msingi ya kufanya kabla kuendelea na utekelezaji kwa muda ulioongezwa.

Aidha, Dkt. Tamatamah aliongeza kwa kusema kuwa Benki ya Dunia imeahidi kuisaidia Tanzania kufanikisha mpango wake wa kutekeleza agenda yake ya uchumi wa Bluu huku akisema kuwa Wizara ipo tayari kuendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kulinda rasilimali za uvuvi na kuleta maendeleo ya sekta ya uvuvi kwa ujumla.

Taasisi zinazotekeleza mradi huo ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania Bara, Wizara Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu zote kutoka Zanzibar.

Mradi huo wa SWIOFish tangu uanze kazi mwaka 2015 umekuwa ukitekeleza shughuli mbalimbali zinazohamasisha ulinzi wa rasilimali za bahari ikiwemo usafi wa fukwe za bahari, ujenzi wa majengo ya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari (BMU) pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali kama vile Boti ambazo zimesaidia kukomesha uvuvi haramu katika maeneo mbalimbali  na kusaidia kutoa huduma kwa watalii nchini.


Thursday, December 17, 2020

RC NCHIMBI: WAZAZI MSIWE MBALI NA VIJANA KIPINDI HIKI BAADA YA MITIHANI

Kaimu Afisa Vijana wa Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akihutubia mahafali ya 10 ya Shule ya Sekondari Utaho iliyopo wilaya ya Ikungi, mkoani Singida jana.



Mwonekano wa kisima hicho ambacho hakijaanza kufanya kazi kutokana na kukosa mabomba ya kusambazia maji
Mkuu wa shule ya Sekondari Utaho, Mwavita Malagila, akizungumza kwenye mahafali hayo.

Wanafunzi wakiingia kwenye viwanja vya shule hiyo kabla ya kuanza mahafali hayo

Maandamano kuelekea kwenye viwanja kabla ya kuanza kwa sherehe za mahafali hayo. Kulia ni Mkuu wa shule ya Sekondari Utaho, Mwavita Malagila

Meza kuu ikishiriki kuimba wimbo wa Taifa

Wanafunzi wakiimba wimbo wa uzalendo kabla ya mahafali hayo

Wahitimu wakiingia kwenye viwanja vya shule hiyo kabla ya kuanza mahafali hayo.

Ndahani akikagua moja ya visima vilivyochimbwa kwa umahiri mkubwa ndani ya shamba la mwekezaji huyo kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa maji kwa jamii inayozunguka maeneo hayo.

Embe zilizotokana na shamba hilo lililopo eneo la Utaho

Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya sekondari Utaho, Idd Siph, (kushoto) akimwelekeza jambo mgeni rasmi wa mahafali ya 10 ya shule hiyo Frederick Ndahani (wa pili kulia). Wengine ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Utaho ‘A’ Shaban Daghau, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Utaho, Yasini Juma, Mwenyekiti wa Kijiji cha Utaho ‘B’ Omari Chima, na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Samamba iliyojengwa kwa nguvu ya wananchi, Japhet Pwiti. 

Sherehe za mahafali hayo zikiendelea.

Ndahani akikagua shamba bora la zao la embe ambalo limelimwa kwa tija kubwa na kuonyesha matokeo makubwa ndani ya muda mfupi, kulia ni mwekezaji mzawa wa shamba hilo, Aqlan Gharib maarufu Turu Best, eneo la Utaho, Ikungi, Singida

Mwonekano wa shamba hilo ambalo kama litatumika kama shamba darasa kwa makundi rika mbalimbali ndani ya jamii litainua tija ya kilimo ndani ya mkoa wa Singida.



Na Godwin Myovela, Singida 


WITO umetolewa kwa wazazi na walezi wote nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika kuwapa uangalizi wa karibu vijana wanaomaliza kidato cha nne ili kuwanusuru kutumbukia kwenye majanga yanayoweza kuhatarisha mustakabali mzuri wa ndoto zao. 

Akihutubia sherehe za mahafali ya 10 ya Shule ya Sekondari Utaho, iliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana, Kaimu Afisa Vijana mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Dkt Rehema Nchimbi, alisema ni jukumu la mzazi kupokea kijiti kile kile cha mwendelezo wa maadili mema kutoka kwa walimu wao, pindi vijana wawapo majumbani. 

"Wazazi msiwe mbali na vijana hawa, tushirikiane kuhakikisha kile walichojifunza shuleni hata wakiwa nyumbani wanaendelea kukiishi katika misingi ya uzalendo," alisema Ndahani.

Alisema mustakabali chanya wa maendeleo ya Tanzania katika muktadha wa ustawi wa kiuchumi, amani na usalama wa nchi upo mikononi mwa vijana hao, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwatupia jicho la karibu katika kipindi hiki wanapoandaliwa kimasomo. 

Pamoja na mambo mengine, aliwasisitiza wazazi katika kipindi hiki kuwa makini dhidi ya genge baya la wasafirishaji haramu wa binadamu wanaopita-pita kuwarubuni vijana, hususani watoto wa kike mkoani hapa kwa kigezo cha kwenda kuwatafutia ajira zenye maslahi makubwa jambo ambalo sio la kweli. 

“Katika hili wazazi tuchukue tahadhari kubwa…hali siyo ya kuridhisha kutokana na mabinti wengi kuendelea kusafirishwa nje ya nchi kwa siri, kwa ahadi za kutafutiwa ajira zenye mshahara mnono jambo ambalo sio kweli, na kinyume chake hugeuzwa watumwa kwa kufanyishwa biashara za ngono na madawa ya kulevya kwa maslahi ya waliowasafirisha” alisema Ndahani. 

Aidha, akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa Nchimbi kwa vijana hao, Ndahani alisema Rais John Magufuli anaipenda sana Singida, na ndio maana hivi karibuni amekabidhi shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa sekondari hiyo ya Utaho. 

Alisema juhudi za kukabiliana na changamoto nyingine zilizopo, ikiwemo uhaba wa nyumba za walimu na maabara vitaendelea kuzingatiwa na kushughulikiwa ipasavyo, ili kuhakikisha Utaho naendelea kuwa kitovu cha elimu ndani ya mkoa. 

Awali, Ndahani akiwa kwenye eneo hilo la Utaho, alipata fursa ya kutembelea na kukagua mradi wa aina yake wa shamba bora la zao la embe linalomilikiwa na mwekezaji mzawa, Aqlan Gharib maarufu "Turu Best" na aliwasihi wana-singida kwenda kujifunza teknolojia za kilimo hicho chenye tija kwa ustawi wa lishe na ongezeko la kipato.

Mail Delivery Subsystem