Sunday, December 10, 2023

SERIKALI YATOA MIL. 114/- KITUO CHA AFYA MTAE, MSD YAKIKABIDHI VIFAA TIBA

Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tanga, Mary Isango, akimpatia nyaraka mbalimbali, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtae kilichopo Lushoto mkoani Tanga, Shafii Makamba (kulia), wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba vyenye thamani ya Sh.Milioni 114 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kununulia vifaa hivyo kupitia MSD kwenye tukio la makabidhiano lililofanyika Disemba 9, 2023. Wengine wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kushoto ni Dereva wa MSD, Rashidi Msambo na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtae, Andrew Kilama. 

.........................................................

Na Dotto Mwaibale, Lushoto

SERIKALI imetoa Sh.Milioni 114 kwa Kituo cha Afya  Mtae kilichopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambazo zimetumika kununulia vifaa tiba kupitia Bohari ya Dawa (MSD) na hivyo kinatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji mwishoni mwa mwezi Disemba 2023.

Hatua ya kituo hicho kuanza  kutoa huduma hiyo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya kuibadilisha zahanati ya kijiji cha Mtae kuwa Kituo cha  Afya ili wananchi waweze kupata huduma bora na karibu.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho,  Shafii Makamba akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo kutoka MSD alianza kwa kuishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani kupitia MSD kwa kuwezesha kutoa vifaa hivyo vya dharura kwa ajili ya kufanya huduma ya dharura kwa wakina mama na watoto.

"Vifaa hivi tulivyovipokea leo kutoka MSD Kanda ya Tanga  vitasaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kwa sababu kabla ya hapo walikuwa wakilazimika kutembea umbali usiopungua kilometa 65 kwenda Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kupata huduma za dharura hasa za upasuaji na kuwa wataachana na adha hiyo na kupata huduma hii hapa hapa katika kituo chetu," alisema Makamba.

Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Tanga, Mary Isango akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Meneja wa MSD wa kanda hiyo, Sitti Abdulrahman, alisema wamepeleka vifaa hivyo baada ya kituo hicho cha afya kujengwa jengo la upasuaji na kupelekewa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh.Milioni 114 ambavyo vinaenda kuondoa changamoto waliyokuwa wakiipata wananchi kwenda kupata huduma hiyo mbali.

"Huduma za upasuaji sasa zitafanyika katika kituo hiki baada ya kupata vifaa hivi ambavyo ni muhimu sana sisi kama bohari ya dawa wito wetu kwa watendaji wa kituo hiki ni kuvitunza ili viweze kudumu muda mrefu na kuleta tija kwa wananchi kadri watakavyokuwa wakiendelea kuvitumia kwa kuzingatia kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua," alisema Isango.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mtae, Beatrice Alphonce, Disifa Mdoe na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Andrew Kilama waliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vitaondoa kabisa madhira waliyokuwa wakiyapata na wakati mwingine kusababisha vifo.

"Tulikuwa na changamoto kubwa baadhi ya wajawazito walikuwa wakijifungulia njiani kutokana na umbali mrefu wa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kupata huduma lakini sasa tutakuwa tunaipata hapahapa nyumbani kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu mama Samia kwa kutuona na kutuonea huruma wanawake wenzake na kama ingewezekana tungemuomba siku moja aje hayaone kwa macho maendeleo haya aliyotuletea," alisema Alphonce.

Alphonce alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia, Mbunge wa jimbo hilo, Rashid Shangazi na viongozi wa wilaya hiyo kwa jitihada kubwa wanayoifanya ya kuwaletea maendeleo hayo ambapo aliwaombea kwa Mungu awape afya na maisha marefu.Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tanga, Mary Isango na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtae, Shafii Makamba wakizipitia nyaraka hizo kabla ya kukabidhiana vifaa hivyo.Mapitio ya nyaraka hizo yakifanyika kwa pamoja kabla ya makabidhiano. Kutoka kushoto ni Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tanga, Mary Isango, Dereva wa MSD, Rashidi Msambo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtae, Andrew Kilama na  Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtae, Shafii Makamba,Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtae, Andrew Kilama akishukuru Serikali kwa kuwapelekea vifaa hivyo kupitia MSD,Muonekano wa Zahanati ya Kijiji cha Mtae kabla ya kubadilishwa kuwa Kituo cha AfyaMuonekano wa jengo la upasuaji lililojengwa na Serikali na kuipandisha hadhi zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya.Vifaa tiba hivyo vikitolewa kwenye gari tayari kwa makabidhiano.Vifaa tiba vikipelekwa kwenye jengo la upasuaji.Watoto wa Kijiji hicho wakishiriki kubeba vifaa hivyo.Kazi ya ubebaji wa vifaa hivyo ikiendelea.Vifaa vikibebwa.Wananchi wa kijiji hicho wakishiriki kubeba vifaa hivyo.Mkazi wa kijiji hicho, Beatrice Alphonce akiishukuru Serikali na MSD kwa kufanikisha kupatikana kwa vifaa hivyo.Mkazi wa kijiji hicho, Disifa Mdoe akipipongeza Serikali na MSD kwa kuwapelekea vifaa hivyo.Gari la MSD likiwa safarini kupeleka vifaa hivyo.

Monday, December 4, 2023

REA YAWASHA MRADI WA BILIONI 25 KUPOZA, KUSAMBAZA UMEME IFAKARA MOROGORO

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya, akizungumza baada ya kuwasha  Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara    (Ifakara Substation), Desemba 3, 2023 Ifakara, Morogoro. Kituo kimejengwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya Shilingi bilioni 25.

...........................................................................

Na Mwandishi Wetu, Ifakara-Morogoro

SERIKALI  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imewasha Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha  Ifakara ambacho kimegharimu shilling bilioni 25.

Akiwasha kituo hicho ambacho kimelenga kuongeza uwekezaji na uanzishaji wa viwanda kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero , Mh Dunstan Kyobya ameshauri kituo hicho kiitwe Samia Ifakara Substation.

Ameipongeza REA na EU kwa kuhakikisha kituo kimekamilika na kuwashwa kwani kinaenda kumaliza matatizo ya umeme katika wilaya ya Kilombero, Malinyi na Ulanga ambayo ni maeneo ya kimkakati ya kilimo na viwanda.

“Tunategemea kuongeza uwekezaji kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na vile vya kuchakata madini” amesema Mh Kyobya.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira na vyanzo vya maji ili kujihakikishia umeme wa uhakika katika mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi na Kidatu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwashwa kwa kituo hicho kunaongeza upatikanaji wa umeme na hivyo kuwawezesha wananchi  kukuza na kuboresha hali zao za kiuchumi kwa kufungua biashara mbalimbali kwa uwepo wa umeme wa uhakika katika maeneo hayo.

“Wananchi watumie upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kujiongezea kipato kwa kuwekeza na kuanzisha viwanda vya mazao ya kilimo na madini ambayo yanapatikana kwa wingi Kilombero, Ifakara, Ulanga na Malinyi,” amesema Mhandisi Olotu.

Naye Mbunge wa Kilombero, Aboubakar Asenga amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa kuzalisha kwa wingi na kuanzisha viwanda vikubwa.

“Tunaishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yake, ni wajibu wetu wananchi kutumia fursa hii ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa kuwa na viwanda vya kukausha na kukoboa mpunga, uzalishaji wa matofali kwa kisasa na uongezaji thamani wa madini ili kujiongezea kipato, ” amesema Mh Asenga.

Meneja wa Mradi huo kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza 2020 ambapo kinazalisha kV 220 za umeme baada ya wananchi wa maeneo hayo kuwa wanapata umeme mdogo wa kV 33 uliokuwa unasababisha kukatika mara kwa mara.

Na baada ya kuwashwa kwa kituo hicho, kutawezesha kuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za kilimo.

Meneja Miradi ya Nishati wa EU, Mhandisi Francis Songela amesema katika Mradi huo wamechangia shilingi bilioni 18 na Serikali ya Tanzania imetoa shilingi bilioni 7.

Amesema kituo hicho kipo katika eneo la  kimkakati la  Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania , SAGCOT ambapo Mradi huo unaenda kuleta mapinduzi ya kilimo na viwanda.

“Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ni maeneo ya kimkakati ya SAGCOT kwani yana rutuba kwa kilimo na shughuli nyingi za kiuchumi ambapo umeme wa uhakika ilikuwa changamoto  na kwa kuwashwa kwa kituo hiki tunategemea mapinduzi ya kilimo na viwanda, ” amesema Mhandisi Songela.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu akizungumza.
. Mbunge wa Kilombero, Mhe. Aboubakar Asenga akizungumza.
 Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara (Ifakara Substation) kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwena akitoa maelezo kuhusu Kituo hicho kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya na Viongozi wengine mbalimbali wakati wa tukio la kuwasha Kituo hicho kilichojengwa na Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) kwa lengo la kuimarisha huduma ya upatikanaji umeme kwa wananchi wa wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.
Taswira ya Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara (Ifakara Substation). Taswira hii ilichukuliwa Desemba 3, 2023 wakati wa tukio la kuwasha rasmi Kituo hicho baada ya ujenzi wake kukamilika.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya (katikati)  akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali na wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), TANESCO na Umoja wa Ulaya (EU) wakifurahi baada ya tukio la kuwasha rasmi Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara (Ifakara Substation), Desemba 03, 2023.

Sunday, November 26, 2023

BOHARI YA DAWA (MSD) YATWAA TUZO YA MLIPA KODI BORA 2023

 Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai (kushoto) akipokea tuzo ya mlipa kodi bora.

MSD Yatwaa Tuzo Ya Mlipakodi Bora 2023

..............................................

 

Na Mwandishi Wetu


BOHARI ya Dawa (MSD), imetwaa tuzo ya Mlipakodi Bora kwa mwaka 2023 ya Mamlaka ya Kodi Tanzania.

Tuzo hizo zimetolewa  usiku wa Novemba 24, 2023 katika hafla maalum ya wiki ya Mlipakodi zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijiini Dar es Salaam ambako Bohari hiyo imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha WalipakodiWalipakodi wa Kati kwa Mkoa wa Kikodi wa Temeke.

Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema ushindi huo una maana kubwa kwa Bohari hiyo na Watanzania.

Amesema MSD ambayo ni moja ya Taasisi za kimkakati za Serikali inayohusika na kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali nchini inafuata taratibu, sheria na miongozose ikiwa ni pamoja na kulipa kodi stahiki.

"Maendeleo yoyote ya nchi yanategemea kodi zinazolipwa hivyo ni vyema kila mlipa kodi akalipa kodi stahiki ili kuwezesha muendelezo wa biashara na  kuimarisha maendeleo kwa mustakali wa ustawi wa jamii, " ameongeza Tukai katika hafla hiyo ambako mgeni Rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Tukai, MSD sasa iko katika mkakati wa kujiendesha kibiashara hivyo hatua ya kulipa kodi kwa utaratibu uliowekwa hadi kutambuliwa ni fursa ya kuaminika kwa wadau wetu katika huduma tunazotoa.

Awali Mkurugenzi wa Elimu wa Mlipakodi na Mawasiliano, Richard Kayombo alisema vigezo vilivyotumika kupata washindi ni kulipa kiasi kikubwa cha kodi na hiari pamoja na kutunza kumbukumbu vizuri

Tuzo hiyo ya mlipa kodi bora ikioneshwa.
 

Tuesday, November 21, 2023

SERIKALI YAMWAGA VIFAA TIBA VYA SH. MILIONI 222.472 SINGIDA

 

  Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akipeana mkono na Mbunge wa Jimbo la Singida, Mashariki, Miraji Mtaturu  ikiwa ni ishara ya kumkabidhi jenereta na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD kwenye hafla iliyofanyika Novemba 20,2023 katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

.................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

SERIKALI  ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa tiba Mkoa wa Singida vyenye jumla ya takribani Sh.Milioni 222.472.

Vifaa hivyo ni pamoja na majenereta, sambamba na vifaa vitakavyotumika kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya muda na huduma nyinginezo ambavyo vimekabidhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kituo cha Afya Sepuka na Hospitali ya Wilaya ya Singida, Ilongero.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambayo ilishuhudiwa na wabunge, watendaji wa idara mbalimbali za sekta ya afya, wananchi pamoja na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Meneja  wa MSD Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa alisema kazi hiyo ya usambazaji wa vifaa hivyo ni jukumu lao walilopewa na Serikali.

" Kazi yetu kubwa sisi MSD ni Uzalishaji, Ununuzi,  Uhifadhi na Usambazaji wa  bidhaa za afya na vitendanishi hapa nchini ambayo tunaifanya kwa mamlaka ya kisheria," alisema Jumaa.

“MSD leo tupo hapa Ikungi kwa ajili ya kukabidhi jenereta, kitanda cha kufanyia upasuaji, Ultra-Sound mashine pamoja na mashine ya kuasaidia kuwapatia joto watoto wachanga na waliozaliwa kabla ya wakati.(njiti-Infant Radlant warmer) vyenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 72

Jumaa alisema lengo kubwa la kupelekwa kwa vifaa hivyo ni kuhakikisha huduma za uzazi zinaboreshwa na kuwa katika wilaya hiyo MSD ilikuwa inakamilisha vifaa ambavyo ilikuwa imepokea fedha zaidi ya Sh. Milioni 300 ili kukamilisha usambaji wake.

Alisema MSD Kanda ya Dodoma imepokea maombi  ya vifaa  tiba zaidi ya  700  Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ajili ya vituo  vya Afya  na Zahanati.

"Ukiangalia muda tuliopokea fedha hizi na utekelezaji wa kupeleka vifaa hivyo ni muda mfupi sana na hiyo imetokana na Serikali kuboresha huduma za MSD na kufikia hatua hii ya kukamilisha vifaa ambavyo hatukuvipeleka awali na kuvipeleka sasa baada ya fedha zake kuzipokea muda mfupi uliopita," alisema Jumaa.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha na MSD imekuwa ikinunua na kusambaza vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya kote nchini ambapo aliishukuru kwa hatua hiyo na kueleza kuwa inajenga morali kwa watumishi wa sekta ya afya na kuipenda kazi wanayoifanya.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu  aliishuru Serikali na MSD kwa kupeleka vifaa hivyo na kueleza kuwa sekta ya afya ni uhai na kuwa watu wakiwa na afya njema ndipo wataweza kufanya kazi zao vizuri.

"Leo hii tunashuhudia vifaa hivi vilivyo letwa na Serikali kupitia MSD na kukabidhi hospitali yetu ya Ikungi maana yake ni utekelezaji wetu wa kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo tuliiomba kwa muda mrefu," alisema Mtaturu.

Alisema kujenga majengo tu ya hospitali haitoshi na kuwa inahitaji na vitu vya ziada vikiwemo vifaa na kuwa madaktari na wataalamu wengine wamesomeshwa kwa lengo la kuwasaidia watu kutibu maradhi mbalimbali na kwa kuvitumia vifaa hivyo ndio wanaweza kufanya kazi yao kwa urahisi iwe kwa kupima na kufanya upasuaji.

Mtaturu alisema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya afya hapa nchini hivyo kila mtu mpenda maendeleo anapaswa kumshukuru kwa jinsi anavyo iendesha nchi kwenye sekta mbalimbali.

Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu akipokea vifaa hivyo kwa ajili ya Kituo cha Afya cha  Sepuka alisema miongoni mwa vifaa alivyo pokea kutoka MSD ni jenereta lenye ukubwa wa KVA 60 na vifaa vingine 11 ambavyo baadhi ni toroli la kuwekea vifaa wakati madaktari na wauguzi wanapokwenda kutoa huduma, vifaa vinavyotumika kumsaidia mtoto baada ya kuzaliwa aweze kupumua vizuri na kuwa vifaa vyote alivyovipokea vinatumika kupingana na uzazi pingamizi na lengo lake ni kumuokoa mama wala mtoto wasife wakati wa kujifungua.

Alitaja vifaa vingine alivyopokea ni mashine kwa ajili ya hewa, mashine ya kupimia uzito, kifaa cha kutundikia dripu ya maji, kifaa cha kuwapa joto watoto waliozaliwa kabla ya muda, kifaa cha kuvuta uchafu kwenye njia ya hewa baada ya mtoto kuzaliwa, saa ya ukutani, kifaa kinachobeba vifaa vya kumuhudumia mtu aliyepata majeraha na pampu inayotumika kumnyonya mtoto kwa ajili ya kuondoa kitu kilichokwama kooni au kupoteza fahamu baada ya kupaliwa na kuwa vifaa hivyo vyote vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 82.

Kingu aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha na akapongeza maboresho makubwa yaliyofanywa ndani ya MSD na kueleza kuwa MSD ya leo ni ya kisasa na mkombozi kwa wananchi katika kazi ya kutoa huduma za afya si kwa Mkoa wa Singida pekee bali kwa nchi nzima kazi ambazo zimekuwa zikionekana kupitia vyombo vya habari.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea jenereta na gari la kuwabebea wagonjwa na wajawazito ambao wengi wao walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa umeme wa uhakika wakati wakipata huduma hasa za upasuaji na kukosekana kwa gari la kuwapeleka hosptali wanapokuwa wagonjwa.

Ighondo alisema pamoja na kupelekewa gari hilo pia Serikali kupitia MSD imewapelekea kifaa kinachotumika kwa ajili ya kuwaongezea joto watoto wanaozaliwa chini ya muda.

Alisema mbali ya gari hilo la wagonjwa vifaa walivyopokea vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 62.7

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dorisila Mlenga, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Grace Ntogwisangu pamoja na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel waliishukuru Serikali kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vinakwenda kuwarahisishia utendaji wa kazi za kutoa huduma kwa wananchi ambapo walisema watavisimamia na kuvitunza ili viweze kudumu kwa muda mrefu wakizingatia Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.

Wananchi Elesisia Mlenga, Asha Salim, Asha Musa, Mwalimu Tatu Njoka, Ashura Iddi na Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Seketoure, Getruda Yona waliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapekea jenereta na gari la wagonjwa na kueleza kuwa vifaa hivyo vinakwenda kuwasaidia katika kupata huduma bora za afya.

Mwanafunzi Getruda Yona alimshukuru Rais Samia kwa kuwajengea shule na kuwapunguzia umbali mrefu ambapo walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 10 kwenda shuleni kabla ya kujengewa kwa shule hiyo ya Seketoure.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akipeana mkono na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu  ikiwa ni ishara ya kumkabidhi jenereta na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD kwenye hafla iliyofanyika Novemba 20,2023 katika Kituo cha Afya cha Sepuka Wilaya ya Ikungi. Kutoka kushoto ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel , Diwani wa Kata ya Sepuka Halima Ng'imba, Afisa Huduma Mwandamizi kwa Wateja MSD Kanda ya Kati, Juliana Mbogo na  Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.


Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kushoto) akipeana mkono na Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo ikiwa ni ishara ya kumkabidhi jenereta na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD kwenye hafla iliyofanyika Novemba 20,2023 katika Hospitali ya Wilaya ya Singida.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akisisitiza jambo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa Mbunge wa Jimbo la Singida, Magharibi Elibariki Kingu (kushoto) Kulia ni Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa MSD Kanda ya Kati, Juliana Mbogo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akipeana mkono na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Sepuka Kesia Daniel baada ya kukabidhi vifaa hivyo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa MSD na wakituo cha Afya cha Sepuka baada ya kukabidhi vifaa tiba hivyo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Singida wakati wa kukabidhi vifaa hivyo
Mbunge Ramadhani Ighondo akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo.

Mganga wa Wilaya ya Singida, Grace Ntogwisangu, akizungumza na wananchi kwenye hafla hiyo.
Gari la MSD , likiwa tayari kushusha vifaa hivyo.
Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati) na Afisa Huduma Mwandamizi kwa Wateja wa NSD, Juliana Mbogo wakiwajibika wakati wa kukabidhi vifaa hivyo.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, akizungumza na wananchi wa Kata ya Sepuka wakati wa kupokea vifaa hivyo.

Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu,Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa na Afisa Huduma Mwandamizi kwa Wateja wa MSD, Juliana Mbogo wakiwa na zawadi zao za kuku walizopewa na Wanawake wa Kata ya Sepuka.
Wananchi wa Kata ya Sepuka wakiwa kwenye hafla ya kupokea vifaa hivyo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akiwa katika picha ya pamoja na wanawake waliohudhuria kliniki wakati wa makabidhiano ya vifaa hvyo Kata ya Sepuka.

Muonekana wa moja ya magenereta yaliyo kabidhiwa na MSD katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Singida na Kituo cha Afya cha Sepuka.
Wanawake wakiwa kwenye hafla ya kukabidhiwa vifaa hivyo Hospitali ya Wilaya ya Singida, Ilongero. 


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Seketoure wakiwa kwenye hafla hiyo.

Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo.

Gari la wagonjwa lililotolewa na SAerikali kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida likioneshwa kwa wananchi (hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo ya kupokea vifaa tiba.

Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Ilongero, Mwanamoshi Bakari, akizungumza kwenye hafla hiyo.

Muonekano wa baadhi ya majengo ya Hosptali ya Wilaya ya Ikungi.

Muonekano wa moja la jengo la Kituo cha Afya cha Sepuka.

Muonekano wa moja ya jengo la Hospitali ya Wilaya ya Singida Ilongero.
Jenereta likiwa limebebwa kwa jeki tayari ya kuhifadhi katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi wakati ikisubiriwa kujenga kibanda litakalo wekwa.


Sunday, November 19, 2023

TIA KUJENGA JENGO LA GHOROFA TANO KAMPASI YA SINGIDA, LENGO NI KUSOGEZA HUDUMA PAMOJA

 

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo, akihutubia katika Mahafali ya 21 ya taasisi hiyo yaliyofanyika Novemba 17, 2023 Kampasi ya Singida.

.............................................................


Na Dotto Mwaibale, Singida

TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA) inatarajia kujenga jengo la ghorofa tano katika Kampasi ya Singida  ambalo licha ya kuupendezesha mji wa Singida lakini pia litaweka huduma za taaluma sehemu moja na hivyo kupunguza wingi wa majengo.

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa taasisi hiyo, Profesa William Pallangyo amesema hayo kwenye mahafali ya 12 katika kamapsi ya Singida yaliyofanyika Novemba 17, 2023 mjini hapa.

Amesema ujenzi huo unatokana na mradi wa magezi ya kiuchumi wa vyuo vya elimu ya juu ambao ni matokeo ya mkopo wa masharti nafuu unaotekelezwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamo jana na Wizara ya Fedha ambapo Singida kupia TIA Kampasi ya Singida ni miongoni mwa mikoa nchini iliyonufaika na mpango huo kwa kupata Sh.Bilioni 18.

Profesa  Pallangyo amesema, jengo hilo litakuwa na ghorofa tano likiwa na kumbi za mihadhara,madarasa kumbi za mikutano pamoja na ofisi linatarajia kuanza kujengwa Februari mwaka 2024.

" Hadi kukamilika kwa ujenzi huo zitatumika Sh. Bilioni  16  na kwa sasa kinachofanyika ni uandaaji wa tathimini ya mazingira," aliseama Prof. Pallangyo.

Ujenzi huo umekuja hasa kwa kipindi hiki ambapo Kampasi ya Singida imepiga hatua katika uendeshaji wa mafunzo, huduma za ushauri wa kitaalam, rasimali watu pamoja na miundo mbinu ya kufundishia na kujifunzia.

Profesa Pallangyo amesema idadi ya wanaojiunga kwa mwaka imekuwa ikiongezeka huku akigusia kuwa kwa mwaka wa masomo 2023/2024 TIA Singida imepokea wanafunzi 1443 lengo likiwa ni kufikia 2600 ikilinganishwa na wanafunzi 1556 kwa mwaka wa masomo ya 2022/23.

Amesema ongezeko la wanafunzi kwa kiasi kikubwa limetokana na ubora wa elimu unaotolewa na taasisi hiyo na kuwajengea umahiri unaowawezesha kupata ajira sambamba na kujiajiri.

Amesema Sababu ya pili ni utaratibu wa serikali kuwapangia vyuo wahitimu wa kidato cha nne waliofaulu na kukidhi vigezo huku akifafanua kuwa kwa mwaka wa masomo 2023/24 jumla ya wanafunzi 1170 kutokana maeneo mbalimbali ya nchi wamejiunga na fani mbalimbali katika chuo hicho.

Ametaja sababu ya tatu kuwa pamoja na ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya Shahada na kwa mwaka huu pekee jumla ya wanafunzi 810 watanufaika na mikokopo katika kampasi ya Singida hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 15.9 ikilinganishwa na wachuo 699 waliopata mikopo kwa mwaka 2022/23.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Iramba, Mh. Suleimani Mwenda ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mh. Peter Serukamba katika mahafali hayo amesema mafunzo wanayoyatoa kuhusu uhasibu ununuzi na ugavi, usimamizi wa biashara na uongozi wa rasimali watu unaendana na mtazamo wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hasani wa kutengeneza Diplomasia ya Uchumi.

Amesema mafunzo wanayoendelea kuyatoa yameendelea kuboresha ubora wa elimu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia hususani Tehama.

Hata hivyo amesema licha ya kufundishwa kuhusu Tehama lakini matumizi yake bado ni ya kiwango cha chini hasa katika masula ya kuongeza maarifa kwa mtu mmoja mmoja hasa kwa kundi la vijana.

Ameshauri kuongeza juhudi katika kuwaelekeza vijana kuhusu matumizi sahihi ya Tehama na kuwa kwa Afrika Mashariki Tanzania inaongoza katika matumizi ya Tehama lakini watumiaji  wakubwa ambao ni vijana chini ya miaka 35 wanaitumia kwa mambo yasiyokuwa na tija.

Akizungumzia kuhusu ajira amewataka wahitimu kujiongezea thamani kwa kuwa wabunifu kwenye kazi ili wawe na mawanda mapana ya kupata ajira zisizo kuwa na shaka..

Viongozi wakiwa meza kuu wakishiriki kuimba wimbo wa Taifa. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha, Thabiti Dokodoko, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Wakili Said Chiguma, Mgeni rasmi wa Mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Afisa Mtendaji wa TIA, Profesa, William Pallangyo na Mkurugenzi wa TIA, Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema.
Waadhiri wakiwa kwenye mahafali hayo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Machapisho TIA, Dkt.Abdallah Gora, Mhadhiri Shibalyandumi Ulomi na Mhadhiri Dkt. CrispinRyakitimbo.
Wazazi na Walezi wa Wahitimu hao wakiwa kwenye mahafali hayo.

Viongozi wa TIA wakishiriki mahafali hayo. Kutoka kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Ushauri, Mystica Ngongi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo (NDC) ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Ushauri Nicolaus Shombe Mjumbe wa Bodi ya Ushauri na Mhadhiri Mwandamizi-Chuo Kikuu cha Mzumbe, Leonada Mwagike na Mkurugenzi wa Utawala, Menejiment na Usimamizi wa Rasilimaliwatu-Ofisi ya Rais TAMISEMI, Emma Lyimo.

Mshereheshaji wa mahafali hayo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya mpango wa ukuzaji na uendelezaji wa wanafunzi kitaaluma na kitaalamu yaani(Career Development Program), TIA,  Imani Matonya akiwajibika. 

Muonekano wa viongozi mbalimbali na Waadhiri Jukwaa kuu.
Wasanii wa kikundi cha utamaduni cha Kabila la Wanyaturu wakitoa burudani kwenye mahafali hayo.


Mshereheshaji wa mahafali hayo Daud Mashauri akiwajibika.

Wahitimu wa Shahada ya Uhasibu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakirusha kofia juu kuonesha furaha zao katika mahafali ya 21 ya taasisi hiyo.


Picha za matukio mbalimbali ya mahafali hayo zikichukuliwa.

Mgeni rasmi wa mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleimani Mwenda (katikati) akiahirisha mahafali hayo ya 21 kwa mwaka 2023. Kushoto ni Wakili Said Chuguma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa wizara na kulia ni  Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Profesa. William Pallangyo.